Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, July 23, 2014

MHASIBU WA HALMASHAURI MBEYA APANDISHWA KIZIMBANI NA TAKUKURU.

MHASIBU wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Gerishon Bwile amefikishwa katika mahakama ya mkoa wa Mbeya akikabiliwa na makosa matatu tofauti. Mhasibu huyo alipandishwa kizimbani juzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa na kusomewa mashitaka matatu ambayo ni Kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake,ubadhirifu na kuisababishia mamlaka hasara. Mbele ya Hakimu Mkazi James Mhanusi,ilielezwa na mwendesha mashitaka wa Takukuru Nimrod Mafwele kuwa mtumishi huyo wa umma alifanya makosa hayo Mei 2013. Mafwele alisema kosa la kwanza alilofanya mhasibu huyo ni kutumia Nyaraka za Serikali kumdanganya mwajiri ambaye ni halmashauri ya wilaya ya Mbeya na kisha kujipatia fedha kinyume cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007. Alisema katika kosa hilo mshitakiwa akiwa ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alitumia risiti yenye namba 0009 iliyoandikwa jina la Rich & Mrs Mufat Decoration na kuidhinisha malipo ya mapambo yenye thamani ya shilingi 1,350,000 wakati sio kweli. Mwendesha mashtaka huyo alilitaja kosa jingine kuwa ni Ubadhilifu kinyume cha kifungu cha 28(1) namba 11 cha mwaka 2007 ambapo mhasibu huyo alijipatia kiasi cha shilingi 1,350,000 alichokabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Mafwele alilitaja kosa la tatu kuwa ni kuisababishia hasara mamlaka kinyume cha vifungu namba 10(1),(i),57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi namba 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo Halmashauri ilipata hasara ya shilingi 1,350,000 mali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka yote mshitakiwa aliyakana huku upande wa walalamikaji ukibainisha kuwa upelelezi umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali. Baada ya Hakimu Mhanusi kupanga tarehe ya Julai 25 kuwa ya kusikiliza maelezo ya awali alimwachia huru mshitakiwa kwa dhamana baada ya masharti kukamilishwa ikiwa ni pamoja na mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili walio watumishi wa serikali wakiwa na barua wakiwa na barua za mwajiri na mali kauli ya shilingi milioni moja kila mmoja. Aidha pia hakimu Mhanusi aliyataja masharti mengine ya dhamana aliyopewa mshitakiwa kulingana na kifungu namba cha 148 kifungu kidogo namba 6 ambapo mshitakiwa harusiwi kutoka nje ya mkoa wa Mbeya bila ruhusa ya mahakama huku pia akimtaka awasilishe hati ya kusafiria kwenye kituo cha polisi. Hii ni kesi ya pili kwa Takukuru kuwafikisha mahakamani watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya baada ya hivi karibuni taasisi hiyo kuwaburuza mahakamani Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Upendo Sanga na wenzake wane kwa kosa la kuhujumu uchumi ambayo bado inaendelea.

No comments:

Post a Comment