Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, October 23, 2014

Walio na kazi wana ichezea wakati wasionayo wanaililia.






Na Joachim Nyambo,Mbeya.

UPO usemi usemao “Nilitafuta kazi nikapata kazi,Sintoona kazi kufanya kazi”.Ni nyingi kati ya ofisi za umma utakapoingia utakutana na mabango yaliyoandikwa sentesi hii kwenye kuta kabla haujaingia kukutana na mtu uliye na shida naye.

Maneno haya mazuri na yenye kuonesha watu wa oifisi husika wamekikaa kimkakati wa kiutendaji zaidi umekuwa ukionekana zaidi katika ofisi za umma.Ni faraja kubwa kuingia katika ofisi yoyote na kukutana na maneno kama haya.

Lakini kwa baadhi ya watumishi wa umma kauli hii haina uzito wowote.Wao Badala ya Bilitaka kazi nikapata kazi,sintoona kazi kufanya kazi wao ni Nilipewa kazi bila kazi sintoona kazi kutofanya kazi.Ni kutokana na mtazamo huu wao hufanya kile wanachokiona badala ya kile walichoagizwa.

Mantiki hii ya kutoona umuhimu wa kufanya kazi imejidhihirisha hivi karibuni huko mkoani Kagera ndani ya jeshi la polisi.Kupitia Vyombo mbalimbali vya habari juma lililopita tulimsikia na kumsoma kamanda wa Polisi mkoani Kagera,Hennry Mwaibambe akitangaza hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na jeshi hilo kwa askari walionekana kupigwa picha ya mahaba na kuiweka mitandaoni.

Siku chache kabla ya maamuzi hayo ya jeshi askari wawili walioonekana kuvalia sare za kikosi cha usalama barabarani mmoja akiwa wa kiume na mwingine wa kike walionekana katika picha ya pamoja wakiwa wamekumbatiana na kupigana busu.

Picha hii iliyosambaa katika mitandamo mingi ya kijamii ndani na nje ya nchi ilionesha dhahiri wawili hawa walifanya tukio hili wakati wakiwa katika majukumu yao ya kikazi waliyopangiwa na mkubwa wao.Kwakuwa na askari wa kikosi cha usalama barabara,licha ya kuwa picha haikuonesha barabara lakini ni imani ya walio wengi kuwa walikuwa kando kando ya barabara waliyopangiwa kufanyia kazi siku hiyo.

Picha hiyo ilionesha askari wa kiume akiwa amempakata wa kike wakiendelea kupigana busu.Picha hiyo ilipigwa mwaka 2012 wakati askari hao wakiwa kazini.


Katika kikao chake na waandishi wa habari,kamanda Mwaibambe alisema jeshi hilo limechukua maamuzi ya kuwafukuza kazi askari hao walioonekana katika mkao wa uhusiano wa kimapenzi.

Lakini rungu la jeshi halikuiishia kwa wawili hawa walioonekana kwenye picha.Askari mwenzao pia anaedaiwa kupiga picha hiyo mwaka 2012 na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.Kamanda Mwaibambe anasema polisi hao watatu wamefukuzwa kwa kukosa maadili mema ya jeshi hilo.

Mwaibambe anawataja polisi walio kwenye picha ya mahaba kuwa ni mwenye namba F.7788 PC Mpaji Mwamsumbi na WP 8898 PC Veronica Mdeme wote wa wilaya ya Missenyi.Aliyewapiga picha ni askari mwenye namba G.2122 PC Fadhil Linga.

Kamanda alisema picha hiyo inakwenda kinyume na maadili mema ya jeshi kwakuwa walipiga picha wakiwa kazini na wamevaa sare za kazi.Kwa upande wa Fadhili kamanda alisema anakabiliwa na kosa la kuwapiga picha wenzake hao kwa kutumia simu yake ya kiganjani na kutuma kwenye mitandao mbalimbali wakati akijua ni kinyume cha maadili ya jeshi la Polisi.Kosa la pili ni kutuma picha hiyo kwenye mtandao.

Kamanda anasema picha iliyoonekana kwenye mtandao ni picha halisi ambayo haijachakachuliwa ama kufanyiwa uhariri wa aina yoyote mpaka iweze kupoteza uhalisia wake.

Kamanda huyo pia anasisitiza kuwa maadili ya jeshi yapo kisheria na askario wao wote wanatambua.Wanapokwenda vyuoni wanafundishwa namna ya kuishi katika maisha ya utumishi wa jeshi la polisi.

Msisitizo huu wa kamanda Mwaibambe ndio unaodhihirisha kuwa askari hawa watatu hawakuona umuhimu wa kufanya kazi,kwasababu hawakufanya kazi kuipata kazi.Wangekuwa wanathamini kazi waliyopewa ni lazima wangesimamia maadili waliyofundishwa chuoni na kuheshimu pia maagizo ya bosi aliyewapangia kazi siku hiyo.

Ni jambo la kusikitisha sana katika dunia ya sasa ambayo kilio kikubwa ni ukosefu wa ajira.Tanzania kama nchi inayoendelea ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na wimbi kubwa na ukosefu wa ajira wa wananchi wake.

Vijana ni ndiyo jamii kubwa nchini ambayo kila kukicha kilio chake kikubwa na uhaba wa ajira.Vijana walio na elimu na wasio na elimu wote maisha kwa kiasi kikubwa yamekuwa sawa kwakuwa wote wanaangukia katika kilio kile kile cha kukosa ajira.

Ni hivi karibuni tu hapa nchini ilionekana kituko cha mwaka baada ya wizara ya Mambo ya ndani kupitia idara ya Uhamiaji kuita watu kwenye usahili.Idara hiyo ilikuwa ikihitaji kutoa nafasi za ajira kwa watu wapatao 70 pekee,Ajabu ni kuwa waliitwa kwenye usaili kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaama walikuwa zaidi ya 10,000.Tunaambiwa hao 10,000 walioitwa Dar es salaam ni wale waliochujwa katika mchujo wa awali.

Kwa uwiano huu wa mahitaji ya Idara ya uhamiaji katika usaili huu na watu waliopeleka maombo ni jibu tosha la kuwezesha kujua mahitaji ya ajira yalivyo makubwa nchini.Wapo waliosafiri umbali mrefu kutoka mikoa ya Katavi,Rukwa,Kagera na Kigoma kwenda kwenye usaili na walikosa nafasi licha ya kutumia gharama kubwa.Hii leo watu walioko kwenye ajira kama askari hawa watatu wanachezea ajira yao.

Lakini hii si mara ya kwanza kwa askari wa jeshi la polisi kuchezea ajira zao.Wapo wengine pia ambao katika kipindi cha hivi karibuni tumekuwa tukisikiwa wamewajibishwa kwa kukiuka matakwa ya ajira yao.Wapo wanaojihusisha na rushwa,Ujambazi na hata wizi wa watoto.

Aprili mwaka huu askari wawili mmoja wa jeshi la polisi mkoani Mbeya na mwingine wa magereza walikuwa miongoni mwa washitakiwa watano waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Askari hawa ni EX-F 8302 PC James(32) wa polisi na B 500 Sajent Juma Musa(37) wa Magereza.Askari hawa walihukumiwa na washitakiwa wenzao watatu na mahakama ya mkoa wa Mbeya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali Basilius
Namkambe na Achileus Mulisa mbele ya hakimu mkaazi mfawidhi wa
mahakama hiyo Michael Mteite kuwa washitakiwa wote kwa pamoja
walitenda kosa la unyang’anyi wa kutumia Silaha kinyume cha Sheria
kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mawakili hao waliieleza mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda kosa
hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima
Kawetere barabara ya Mbeya/Chunya.

Walisema washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kulizuia
gari lenye namba T 756 ABL aina ya Toyota Pick Up lililokuwa
likiendeshwa na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya
ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar
Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo mawili
ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari lingine ambalo
lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 aina ya  Grand Mark II.

Walisema ghafla washitakiwa hao waliokuwa na pingu na panga moja
waliwateka wafanyabiashara na kuwapora fedha taslimu kiasi cha
shilingi milioni tatu,mabegi matatu yaliyokuwa na nguo,Kompyuta
mpakato moja aina ya Sumsang,simu ya kiganjani aina ya Sumsang pia na
mablanketi mawili.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo ja, Hakimu mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Michael Mteite alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wanatiwa
hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili.

Alisema ushahidi uliotolewa na shahidi wa kwanza ambaye alikuwa dereva
Ezekia Matatira (34) na shahidi wa pili  Sreedhar Pasupelet(38) mwenye
asili ya Kiasia kwamba haukuacha shaka yoyote na ulishabihiana.

Kama vile haitoshi mwezi huo huo afisa mmoja wa jeshi la polisi akakamatwa na jeshi hilo na kufukuzwa kazi kwa tuhuma za kuiba mmtoto mchanga wa siku saba

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Ahmed Msangi alimtaja jaskari
anayeshikiliwa kuwa ni Detactive Constable Priscar Kilwai mwenye namba
WP 5367 ambae eneo lake la kazi ni mkoa maalumu wa kipolisi wa Ilala
katika kanda maalumu ya Dar es salaam.

Kamanda Msangi alisema WP Priscar alikamatwa April 17 majira ya
kati ya saa nne na saa tano asubuhi akiwa katika eneo la Meta jijini
Mbeya alikokutwa akiwa na kichanga alichoiba.

Akizungumzia kisa cha wizi huo,kamanda msangi alisema mtoto mchanga
aliyeibwa alifahamika kwa jina la Goodlack Salehe ambaye alizaliwa
April 6 mwaka huu huko mjini Kyela.

Aliwataja wazazi wa mtoto aliyeibwa kuwa ni Mboka Mwakibabile makazi
wa eneo la Njiapanda mjini Kyela ambaye ni mama wa mtoto na Salehe Isa
Mwangosi mkazi wa Kasumulu ambaye ni baba wa mtoto huyo na ambaye pia
anashikiliwa.

Alisema siku moja kabla ya siku ya tukio baba wa mtoto huyo
alimjulisha mzazi mwenzie kuwa kuna shangazi yake ambaye kesho yake
angefika nyumbani kwa mama wa mtoto kwa lengo la kumwona mtoto na pia
aweze kumsindikiza kumpeleka mtoto huyo kliniki.

Alisema siku iliyofuaata yaani April 6 mwaka huu majira ya kati ya saa
sita na saa saba mchana shangazi huyo ambaye ni WP Priscar alifika
nyumbani kwa mkwewe na baada ya kumsalimia mtoto huyo waliongozana
wote wawili kukipeleka kichanga kliniki kama mzazi mwenza alivyokuwa
amependekeza.

Alisema baada ya kufika kliniki walitakiwa kuwa na daftari na kwakuwa
hawakwenda nalo ikalazimu jitihada za kwenda dukani kununua daftari
hilo zifanyike.

Kamanda huyo alisema shangazi huyo bandia alitoa kiasi cha shilingi
2000 na kumpa mama wa mtoto aliyekwenda moja kwa moja dukani huku
akimwacha mwanaye kwa WP Priscar akijua kamwacha sehemu salama kwani
alijua ni bibi yake yaani shangazi wa mzazi mwenzie.

Ajabu ni kuwa mama huyo aliporudi na daftari lake hakumwona mkwewe
wala mtoto hali iliyolazimu aanze kuuliza watu waliokuwepo jirani
ambao baadaye walimwambia kuwa walimwona mtu aliyemwachia mtoto
akipanda pikipiki na kutokomea kusikojulikana.

“Baada ya hapo mama huyu akalazimika kutoa taarifa kituo kidogo cha
polisi kilichopo pale Kyela na jitighada za kutafuta zilianza mara
moja.Hatua ya kwanza ilikuwa ni kumkamata baba wa mtoto kwakuwa moja
kwa moja alionekana kuhusika katika njama za wizi huo” alisema.

Alisema baada ya kumkamata baba wa mtoto jitihada ziliendelea hadi
April 17 alipokamatwa maeneo ya Meta jijini Mbeya akiwa na
kichanga hicho.

“Baada ya kumkamata na kupata tetesi kuwa ni afisa wa jeshi tulianza
kupeleleza na ndipo tukabaini ukweli na kuwa anatokea mkoa maalumu wa
kipolisi wa Ilala Dar es salaam”

Alisema uchunguzi wa awali unaonesha hakuna mahusiano yoyote ya
undugu kati ya askari huyo na baba wa mtoto isipokuwa mahusiano
yaliyopo ni ya kibiashara ambapo ilionekana kuna biashara ambazo
wamekuwa wakifanya kwa kushirikiana.

Matukio haya na mengine mengi yanaonyesha wazi ni kwa namna gani baadhi ya askari hawaoni uchungu wa ajira zao.Wanaziona ajira zao kama kido kisicho cha msingi wakati wasio na ajira wanalia usiku na mchana kusaka.Wapo wanaolazimika hata kwenda hata kwa waganga wa jadi wakiamini huenda wanaweza kusaidiwa kupata ajira.

Ni vema askari wetu wakajitathmini iwapo wanmaitaka kazi au la.Kama wameichoka wanaweza kuweka wazi wakawaachia wanaoihitaji wakalitumikia jeshi kwa uadirifu badala ya kuendelea kulipaka matope jeshi letu.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment