HABARI KAMILI
BALOZI
wa Japan nchini Kazuyoshi Matsunaga ameitabiria makubwa Tanzania iwapo wasomi
wa nchi hii watachukua hatua mathubuti
za kitaaluma na kizalendo katika kulitoa taifa kwenye umaskini na kulipeleka mbele
kimaendeleo.
Matsunaga
ameyasema hayo wilayani Ileje wakati wa hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya
mkataba wa ujenzi wa chuo cha ufundi(VETA) kati ya balozi huyo na na
viongozi wa serikali wilayani hapa ambapo Japan itachangia kiasi cha shilingi milioni 160.
Amesema
kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo wasomi wakizitumia vizuri fani zao
nchi yao itakwenda mbele na kuwa taifa lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi .
Akitumia
picha za mji mkuu wa Japan Tokyo alionyesha mwonekano ulivyokuwa mara baada ya
vita kuu ya pili ya Dunia ukionekana
kuharibiwa vibaya huku kukiwa hakuna miundombinu yoyote kama vile majengo na
umeme.
Aliongeza
kuwa walioifikisha Japan ilipo sasa kimaendeleo ni wasomi ambao walitanguliza
uzalendo kwa taifa lao huku nchi hiyo ikiwa haina rasilimali kama ilivyo kwa
Tanzania ambayo ina utajiri mkubwa wa madini kama vile dhahabu na almasi lakini
iko nyuma kimaendeleo.
Matsunaga
alisisitiza kuwa wahitimu wa vyuo vyote vinavyoanzishwa nchini wanapaswa wawe
chachu ya maendeleo katika maeneo yao na taifa kwa ujumla.
Naye
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Janet Mbene alitoa wito kwa wasomi waishio
nje ya Ileje kuwekeza wilayani kwao hatua aliyosema itaongeza kasi ya
maendeleo hususani kwa wilaya zilizopo pembezoni.
No comments:
Post a Comment