Na Joachim Nyambo
HATIMAYE mgogoro wa kimpaka uliodumu
kwa zaidi ya miaka 10 kati ya mwekezaji katika shamba la Kapunga kampuni ya Expot
Trading na wakazi wa kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali umemalizika.Ukomo wa
mgogoro huu umefikiwa kwa mwekezaji kuridhia kiasi cha hekta 1,870 za ardhi
kurejeshwa kwa kijiji hicho.
Mapema mwezi Januari mwaka huu,Waziri
wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Willium Lukuvi alitangaza kurejeshwa kwa
hekta hizo za ardhi kwa nyakati tofauti alipozungumza na wakazi wa kijiji cha
Kapunga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo na pia alipokuwa
kwenye kikao na madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.
Lakini nini kilikuwa kiini cha
mgogoro huu na yapi yaliyojiri wakati wa msuguano baina ya wakazi wa kijiji cha
Kapunga na mwekezaji.Maisha ya pande hizi mbili yamekuwaje katika kipindi chote
cha mgogoro.Hapa ndipo ninapoamua kukupitisha katika maisha ya miaka hii kumi
kupitia makala haya mfululizo niliyoamua kuyaiya Maisha ya mateso Kijijini Kapunga.
Mwaka 1985
wakazi wa kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali waliombwa na serikali kutoa eneo chepe
chepe lenye ukubwa wa hekta 5500.Ombi hilo lililenga serikali kupata eneo hilo
kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.Ni hasa ilikuwa ni kuboresha kilimo nchini
kutoka kile cha matumizi ya maji ya mvua ambacho ni cha msimu.
Inasemekana Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyeomba
eneo hilo baada ya kupita katita vijiji vilivyopo pembezoni mwa barabara kuu na
kukuta wakazi wakiuza mahindi mabichi na mbogamboga.Vijiji hivi ni pamoja na Chimala,Mswiswi
na Igurusi.Kwakuwa ilikuwa msimu wa kiangazi ilimshangaza Mwalimu.
Baada ya kuuliza wenyeji na kuambiwa kulikuwa na bonde
lililo na maji mengi aliomba apelekwe kulitembelea na ndipo akawaomba wakazi wa
kijiji cha Kapunga watoe eneo hilo kwa serikali.
Mwaka 2012 nilizungumza na aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji
cha Kapunga Ramadhan Nyoni aliyesema wanaKapunga walikubaliana na ombi hilo
hasa baada ya kuelezwa manufaa ambayo wangenufaika kwa serikali kuliboresha
eneo hilo kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.Zao lililopendekezwa kulimwa
kwenye bonde hilo ni mpunga.
Jitihada za kujenga miundombinu ndani ya shamba hilo
lenye hekta 5,500 zilianza kwa serikali kuomba mkopo Benki ya Dunia(WB).Lakini
WB ilitoa sharti kwa serikali kuhakikisha pia inaboresha eneo la hekta 800 kwa
wakulima wadogo waliotoa ardhi yao.
“Hapo ndipo ukafikiwa uamuzi wa hekta 5,500 za
serikali ziwe mashariki na hekta 800 za wakulima wadogo ziwe magharibi na
katikati eneo la kijiji cha Kapunga lenye hekta 1070.”alisema Nyoni na
kuendelea
“Savei iliyofanyika ilihusisha maeneo yote matatu kwa
maana ya eneo lililo na jumla ya hekta 7,370.Na katika mambo tuliyokuwa
tumeahidiwa ni pamoja na serikali kukijenga kijiji chetu na kuwa cha mfano
nchini”
“Serikali katika kujenga mradi kwenye eneo lake
kupitia shirika la Nafco haikumaliza wote.Hekta 500 ndizo ziliandaliwa kwaajili
ya kilimo.500 zilitumika kwa ujenzi wa makazi ya Nafco,kiwanda na karakana na
2000 zikaachwa”
Baadaye Nafco ilishindwa kuliendesha shamba hilo na
hatimaye serikali ikaamua kuliuza kwa mwekezaji.Matangazo ya kuuza shamba hilo
yalionesha hekta 5500.
Baadaye serikali ilimpata mwekezaji na kumkabidhi
shamba hilo.Kinyume na matangazo ya kumtafuta mwekezaji mkataba uliongiwa kati
ya serikali na kampuni ya Expot Trading Limited unaonesha jummla ya hekta 7,370.
Mkataba huo ulisainiwa agosti 17 mwaka 2006.Katika
mkataba huo,inaonekana serikali iliwakilishwa na mhandisi mkazi wa wizara
ya Kilimo,Chakula na Ushirika Rosemary Tesha na kampuni ya Expot Trading
Limited ikawakilishwa na Sunil Kumar kutia sahihi.
“Maswali tunayojiuliza wana Kapunga ni kwamba kama
serikali ilituomba hekta 5,500 za ardhi,tukaipa hekta hizo na matangazo ya
kutafuta mwekezaji yakamaanisha hekta hizo huo mkataba ulioingiwa kati ya
serikali na mwekezaji unaoonesha hekta 7370 unatoka wapi?”
“Ina maana serikali iliamua kuuza mpaka ardhi ya
wananchi walioikaribisha na kuipa eneo.Hili limekuwa mgogoro wa muda mrefu kati
yetu na mwekezaji kwakuwa madai yake anasimamia mkataba hivyo uwepo wetu sisi
na shamba letu la wakulima wadogo hautambui”
Mwenyekiti huyo wa kijiji cha Kapunga wakati huo
alisema umefika wakati wakazi wa kijiji hicho wanajuta kwa kukubali ombi la
mwalimu Nyerere la kumpa ardhi.Anasema badala ya matarajio waliyokuwa nayo
wakati huo sasa wanavuna mateso na adhabu ambazo kama wasingetoa ardhi yao
wangeendelea kuishi maisha ya furaha siku zote za maisha yao.
“Wakati tunaombwa shamba tuliahidiwa mambo mengi sana
yaliyotuvutia.Tuliambiwa kijiji chetu kitakuwa cha mfano maana tungejengewa
shule ya kisasa,kuletewa umeme na pia watoto wetu wangepata ajira kutoka katika
shamba tulilotoa”
“Wakati wa Nafco tulianza kuona mwelekeo wa
kutekelezwa kwa ahadi tulizopewa.Maana tuliletewa maji kijijini kwetu na tukawa
tunayatumia kwa matumizi yote.Badaa ya kuingia mwekezaji alikata huduma hiyo na
kutoa sababu nyingi”
“Ndoto ya kuwa na kijiji cha mfano iliondoka mara tu
baada ya mwekezaji kuuziwa shamba.Hapo usemi wa baadhi ya viongozi akiwemo Juma
Ngasongwa na mwenzake Joseph Mungai waliosema mkae mkao wa kula walipokuwa
wanamkabidhi shamba mwekezaji tukaona ulimaanisha mkae mkao wa kufa.Maana
badala ya kutujengewa shule ya kisasa alithubutu hata kuleta kijiko kikavunja
tofali za tanuli mbili tulizokuwa tumechoma tukilenga kujenga shule yetu
wenyewe.”
Baada ya kuvunja tanuli hizo mwekezaji huyo
alizigeukia baadhi ya nyumba za wakazi na kuzichoma kisha akajenga uwanja wa
ndege kwenye eneo hilo.Anasema alianza kwa kuweka mabango kwenye makazi ya kaya
18 kabla ya kuzichoma moto na wakazi hao wakalazimika kuishi chini ya
miti.Badaye aling’oa madaraja na kukataza wakijiji kukatisha ndani ya eneo laki
wanapokwenda mashambani mwao.
Anasema badala ya ushirikiano kati ya watumishi wa
Nafco na wakazi kijijini hapo ikaonekana sasa viendo vya
unyanyasaji,udhalilishaji na kukomoana.Vitendo hivyo ni pamoja na mifugo
kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi 20,000 kila mmoja walipokutwa ndani ya
eneo la mwekezaji.Na wafugaji walipoomba stakabadhi ya malipo hayo wakapewa ya
Nafco na si kampuni ya sasa.
Nyoni anafafanua kuwa matukio ya mwekezaji huyo yapo
mengi yanayowanyiam raha wakazi hao lakini tatizo ni kutofahamika kwa mpaka
halisi.Lipo pia tukio la Julai 10,2011 ambapo mfanyakazi wa kampuni hiyo
alimgonga kwa gari mfugaji Mwiguru Nguru na kumchana msamba kabla ya kumpiga
ng’ombe mmoja risasi.
Mzee Willium Joram Kasekwa (72) ni miongoni mwa wakazi
wa kijiji hicho walioshiriki mchakato wa kuikabidhi serikali eneo la shamba la
Kapunga.Anaikumbuka sana siku alipokuja mwalimu Nyerere kuja kutia baraka
katika shamba hilo.
“Akimaanisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi
alizindua shamba la wakulima wadogo kwa kupanda miche kadhaa ya mpunga katika
shamba langu.Ulikuwa mwaka 1966 alipokuja na aliongozana na mkewe mama Maria
pamoja na mwanamke mwingine aliitwa Bibi Titi”
Wazee wengine Zebrone Gaone Mbila na Elbaut Mwinuka
pia nilipozungumza nao mwaka 2012 walionesha kukumbuka busara za Mwalimu Nyerere
alizozionesha na kuwahakikisha maisha bora kwa kutoa kwao shamba kwa serikali.
Lakini wakasema wema wao umewasababishia sasa familia
zao kuishi kama mkimbizini.Baada matukio ya mwekezaji katika shamba hilo
hayaishi na kila kukicha anasisitiza kuwa kijiji cha Kapunga pamoja na mashamba
ya wakulima wadogo ni eneo lake hivyo wakazi wanapaswa kuondoka.
Jitihada mbalimbali zilifanywa na wakazi wa kijiji
hicho wakati huo lakini mara kadhaa ziligonga mwamba.Moja ya jitihada hizo ni
pamoja na barua ya Februari 5 mwaka 2007 waliyomwandikia rais Jakaya Kikwete
kuomba awasaidie kutatua mgogoro wa mpaka kati ya kijiji na mwekezaji lakini walise
haikujibiwa.
Walisema maendeleo katika kijiji hicho yalikwama tangu
mwaka 2006 kwakuwa walibakia kuishi mguu mmoja nje mguu mwingine ndani.Wanailalamikia
sera ya ubinafsishaji wakisema imeleta mateso makubwa kwao na kutamani Mwalimu
Nyerere kurudi duniani ili awarejeshee ardhi yao.
Kwa wakati huo,Uongozi wa wilaya ya Mbarali kupitia
ofisi ya mkuu wa wilaya ulikiri kuwa mgogoro wa kimpaka kati ya kijiji cha
Kapunga na mwekezaji ni pasua kichwa unakwamisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya
kijiji hicho.
.........................ITAENDELEA KESHO ........................
No comments:
Post a Comment