Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, May 31, 2016

SABABU 10 WAZEE MBEYA KUMUUNGA MKONO JPM

Na Joachim Nyambo.

 
“Kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu inatukumbusha kaulimbiu za huko nyuma kama vile Uhuru na kazi,Uhuru ni kazi na Heshima ya mtu kazi”  Ni kauli ya Mwenyekiti wa wazee wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mbeya,Isakwisa Mwambulukutu wakati wazee hao walipotoa tamko la kupongeza utendaji kazi wa rais John Magufuli.

Tamko hilo liliungwa mkono na wazee wengine wanachama wa umoja huo wakiwemo Edward Ndonde,Daniel Fussi,Kikeke A Kikeke,Rogate Masuba,John Mushi,Bujo Mwakatumbula,Joji Nyirenda,Boniface Kasyunguti,Philimon Mwansasu na mmoja wa waasisi wa TANU mkoani Mbeya,Helena Mwaipasi.

“Sisi wazee tunaounda umoja wa Wazee wa CCM tunaoishi jijini Mbeya kwa niaba ya wazee wenzetu tunapenda kutoa tamko rasmi la kumpongeza rais John Magufuli kwa utekelezaji wake mzuri wa Ilani yetu ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015 na utendaji wake mzuri wa kazi katika awamu hii ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”alisema Mzee Mwambulukutu.
 
“Tunapotoa tamko la kumpongeza Dk.Magufuli isieleweke kuwa tunaziona awamu nyingine zilizotangulia hazikufanya mazuri,lahasha.Kama alivyosema aliyekuwa rais wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuwa Kila zama na Kitabu chake,viongozi wa awamu zilizotangulia kila mmoja alifanya mambo kwa kadiri ya karama aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kulingana na hali halisi ya wakati wake huo.Hara Dk Magufuli ni moja ya matunda ya awamu hizo zilizotangulia”anasema.

Mwenyekiti huyu anasema ni Ukweli usiopingika kuwa maendeleo ya mtu au Taifa kwa ujumla hayawezi kupatikana kama watu hawataki kufanya kazi.Ni jambo la kumpongeza rais kwa kuhimiza hilo na anapaswa alisimamie kwa nguvu zote ili nchi iweze kujikwamua kutokana na lindi la umasikini.

Wazee hawa wanasema sababu ya pili ya kumpongeza rais ni Kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma.Watumishi wengi wa umma walifikia mahali ambapo walifanya kazi kwa kadiri ya matakwa yao bila kujali taratibu na kanuni za kazi.

“Walisahau ile kauli mbiu aliyotoa rais Ally Hassan Mwinyi isemayo,Usipowajibuka,Ole Wako,Utakumbana na Fagio la Chuma.Sisi wazee tunaamini Magufuli ni fagio la Chuma,kwani matokeo tumeanza kuyaona kwenye sehemu ambazo huduma hutolewa kama vile hospitali,ofisi za serikali na sehemu nyinginezo.”

Sababu ya Tatu ni Kupambana na rushwa,ukwepaji kodi na ubadhirifu wa mali za Umma.Anasema Kwa kwa Kutumbua Majipu,Dk.Magufuli anawakumbusha enzi za Hayati Edward Moringe Sokoine alipopambana na Wahujumu Uchumi.

“Sisi wazee tunamwombea rais Magufuli Mungu amlinde,ili atumbue majipu yote,vipele,chunusi na kukwangua kabisa ukurutu ili Tanzania yetu ibaki safi na yenye afya njema kiuchumi na kiustawi wa jamii”

Kuboresha huduma za jamii ili kuleta hali nafuu ya maisha ya watanzania ni sababu ya nne wanayoitaja wazee hawa kuwasukuma kutoa pongezi zao.Hii ni pamoja na kuboresha huduma hospitalini,kutoa elimu bure toka chekechea hadi kidato cha nne na kuhakikisha mikopo inapatikana kirahisi kwa vijana  wa elimu ya juu.

“Kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara,reli,umeme,maji na mingine mingi hapa anatukumbusha usemi wa It can be done play your part.Hivyo tunatoa wito kwa watanzania wenzetu kutimiza wajibu wao pale walipo ili huduma za kijamii ziweze kuwa bora na kutufanya wote tuwe na maisha nafuu”.

Kufufua na kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kuongeza ajira,kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na Kilimo,uvuvi na Ufugaji na kuinua uchumi wa Taifa pia limewakosha wazee hawa.Wanasema wameanza kuona matunda kwani mkoni Mbeya tayari kiwanda cha Zana Za Kilimo(ZZK) kimeanza kufanya kazi na baadhi ya vijana wamepata ajira.

“Hapa tukizingatia ile kaulimbiu ya Kupanga ni Kuchagua hakuna kitakachoshindikana.Hivyo tunaomba juhudi ziendelee ili kufufua viwanda vingine kama vile HISoap,kiwanda cha nguo na kiwanda cha kusindika nyama”

Jambo jingine ni Kuboresha na maslahi ya wafanyakazi kwa kuanza na kupunguza kodi itokanayo na mishahara yao kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa.Wanasema wanaamini kutokana na Kutumbua Majipu,kudhibiti wafanyakazi hewa na madeni hewa hali ya kiuchumi itakuwa bora na hivyo kuwezesha kuongezeka kwa mishahara ya wafanyakazi na huduma bora kwa umma zitapatikana.

“Jambo ji ngine ni kuhimiza ujenzi wa Taifa linalojitegemea.Ile kauli ya rais Magufuli ya Bora kushindia mihogo,kuliko mkate wa Siagi wa masimango unatukumbusha kauli ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere ya Heri kuwa masikini na Huru,Kuliko kuwa Tajiri na Mtumwa”

“Sisi wazee tunamwomba rais wetu akaze uzi wala asijali vitisho vya wafadhili wanafiki na maneno ya Wanasiasa Uchwara.Tunaamini pia kwa kubana matumizi ya serikali kwa kupunguza safari za nje ya nchi,posho za vikao visivyo na tija kwa taifa letu na kupunguza sherehe zinazomaliza fedha nyingi nchi yetu itaweza kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuweza kujitegemea”

Wazee hawa wanasema unyenyekevu aliouonyesha Dk.Magufuli wakati wa kuzindua Daraja la Kigamboni ni wa kipekee.Pamoja na kwamba usimamizi wa ujenzi wa daraja hilo ulikuwa chini yake tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi,alikataa daraja hilo kuitwa jina lake na badala yake aliamua liitwe Daraja la Nyerere,kwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuimarisha umoja wa Kitaifa na kupigania Uhuru wa Bara la Africa.

Mzee Mwambulukutu anasema Kudhibiti uagizwaji holela wa sukari toka nje ya nchi ili kuhakikisha watanzania wanapata sukari iliyo salama na kwa bei nafuu na pia kukuza viwanda vya sukari vya hapa nchini,inastahili pongezi.Pamoja na purukushani za hapa na pale zinazofanywa na wafanyabiashara wasio na Uzalendo wanaamini juhudi za Rais zitashinda kwakuwa Palipo na Mwanga,giza hujitenga.

“Jambo la mwisho ni kudhibiti hali ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar na hivyo kufanikisha uchaguzi wa marudio bila fujo.Akiwa Amirijeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,aliweza kuhakikisha ulinzi na usalamakatika visiwa vya Zanzibar unakuwepo na hivyo kuwezesha uchaguzi wa marudio kufanyika hapo Machi 20 mwaka hu bila vurugu zozote.”

“Sisi wazee tunampongeza kwa hilo na tunapongeza ushindi wa kishindo wa CCM katika uchaguzi huo,uliofanyika kwa amani na utulivu”alisema Mzee Mwambulukutu.

Wazee wengine akiwemo Kikeke A Kikeke,wanasema juhudi na ushirikiano wa pamoja baina ya watanzania wote pasipokujali nafasi waliyonayo ndiyo utakaowezesha mikakati mbalimbali ya Dk.Magufuli kufanikiwa.iwapo kutakuwepo na makundi ya watu wanayojitenga na kukwamisha itakuwa vigumu kwake kuwezesha watanzania kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wa katibu wa umoja huo Philimon Mwansasu,alisema watanzania wanapaswa kutambua kuwa maisha bora hayawezi kupatikana kama taifa litabakia mikononi mwa matajiri wachache wenye kupenda kulimbikiza mali kwaajili yao na familia zao na kuwaacha masikini wakiwa watumwa ndani ya taifa lao.

“Tunachopaswa kufanya watanzania wote ni kushirikia katika mipango ya rais kuhakikisha tunafichua maovu yote yanayofanywa na watendaji wabovu.Kuchukuliwa kwao hatua ndiyo mwanzo wa walalahoi kupata unafuu wa ugumu wa maisha.Tukisema tushirikiane na wahalifu kwa madai kuwa tunawaonea huruma tutakuwa tunazidi kujikwamisha wenyewe”anasema Mwansasu.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment