Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, November 15, 2017

Niliyoshuhudia Kipindupindu cha Mbarali.

 Na Joachim Nyambo.

KAMA kuna msukosuko Wakazi wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya hawatokuja kuusahau kwenye historia ya mwaka 2017 ni Ugonjwa wa kipindupindu.Kwa hakika ugonjwa huu umeacha historia kubwa wilayani hapa.Na hakika wakazi wa wilaya hii wamepata shida.

Agosti  2 mwaka huu ndipo Ugonjwa wa Kipindupindu uliripotiwa kulipuka katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya Mbarali.Kibaya zaidi ni kuwa maeneo ya awali hakukuwa na wataalamu wa kubaini kuwa wagonjwa waliopatikana walikuwa na dalili za ugonjwa huo hivyo waliendelea kuachwa majumbani wakipata tiba za kubahatisha.Hawakuamini kipindupindu kinaweza kutokea kiangazi cha jua kali.
Baada ya Agost 2,ugonjwa ulipobainika ndipo heka heka zilikolea.Jambo la kwanza ilikuwa ni maamuzi ya Kamati ya ulinzi na usalama kupiga marufuku utoaji holela wa huduma za vyakula na vinywaji.Hapo ililazimu Hoteli,Migahawa na Mamalishe zote kufungwa.Vivyo hivyo kwa vilabu hususani vya pombe za kienyeji.

Kufungwa kwa maeneo haya muhimu kukaleta adha si tu kwa wafanyabiashara wa vyakula na vinywaji kushindwa kujiingizia kipato.Walaji nao walipata wakati mgumu.Wageni ndiyo walikuwa katika wakati mgumu zaidi kwani wakati wenyeji walipokwenda majumbani mwao kula chakula,wao walilazimika kushinda njaa au kuponea biskuti na soda.

Kwakuwa katazo hili lilidumu kwa siku kadhaa,wauzaji na wateja wa vyakula na pombe walibuni mbinu.Mbinu hizi zilikuwa za hatari zaidi na huenda ndizo zilisababisha ugonjwa kusambaa kwa kasi.Ilikuwa ni kupika na kuuza vyakula majumbani kwa uficho.Huku usafi haukuzingatiwa kwakuwa kila kitu kilifanyia kwa siri.Hata vyombo vilivyotumika havikukaushwa juani kwani vingeonekana machoni pa watawala waliopiga marufuku.

Uuzaji pombe za kienyeji ulikuwa wa hatari zaidi.Wauzaji waliozinunua kutoka kwa waliozitengeneza kwa kificho walikwenda kuziuzia kwenya maeneo yaliyojificha na wanywaji kuyatumia maeneo hayo pasipo kujali hali ya usafi.Wapo inaosemekana walinywea pombe chooni.Hivyo walikaa nje ya nyumba ya mtu kama wanajamii wanaojadiliana mambo ya msingi lakini walipeana muda wa kuingia msalani kunywa pombe kwani vilabuni hazikuwekwa.

Naikumbuka Agost 4 niliposhuhudia mama mmoja anaeuza Supu ya Ng’ombe katika vibanda vilivyopo jirani na ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbarali alipokimbia na Sufuria ya Supu baada ya kuona kundi la wanahabari tukielekea nyumbani kwake.Tukiwa wanne tulikuwa wilayani hapa kikazi na tulipowauliza wenyeji walituonesha sehemu tunayoweza kupata kifungua kinywa kwakuwa tulitoka jijini Mbeya alfajiri.

Pasipo kujua kama mama huyo alikuwa anauza kificho kwani hatukuwa tumefika mjini Rujewa wala kukutana na uongozi ili kujua kilichokuwa kinaendelea juu ya masuala ya chakula tulikwenda moja kwa mwa mama huyo,lakini tukashangazw3a baada ya kuona anatoka mbio na sufuria lake na kulificha nyuma ya nyumba yake.Tulipoulizia supu wakati amerudi tulijibiwa hawakupika siku hiyo.

Tulilazimika kurudi katika jengo la Ofisi ya mkuu wa wilaya lakini kabla hatujafika tukaitwa na mwenyeji ambaye kimsingi alikuwa ametutambua.Ndipo tulisimama na alipotufikia kwa sauti ya chini akasema…

“Sikilizeni Yule mama alijua ninyi ni askari.Unajua huku kwetu wamepiga marufuku kuuza vyakula kutokana na kipindupindu.Sasa huyu anauza kwa kificho na kwakuwa huku hakuna ni mbali na majumbani sisi tunalazimika kula hapa japo tunamsimamia.Hivyo ninyi nendeni kwani nimekwisha mwelekeza ni nyi ni akina nani.”alituambia mwenyeji yule.

Hatukuwa na namna zaidi ya kurudi na kupata kifungua kinywa.Japo ilikuwa kwa mashaka makubwa lakini hatukuwa na chaguo kwakuwa njaa nayo ilikuwa inauma na hatukujua kazi tuliyoendea itaanza saa ngapi na itatuchukua muda gani.Tulipokwenda mjini Rujewa ndipo tukashuhudia vibanda vyote vya vyakula kufungwa.

Agost hiyo 4 katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Serikali ya wilaya  ikawataka wananchi  wa maeneo yote wilayani hapa kuchukua Tahadhari.Hadi tarehe hiyo watu wanne walikuwa wamekufa na 55 kulazwa katika kambi maalumu kutokana na ugonjwa huo.

Hadi wakati huo maeneo yaliyokuwa yamekumbwa na Kipindupindu ni ugonjwa huo ni Kata tatu za Ubaruku,Rujewa na Lugelele huku chanzo cha mlipuko kikitajwa kuwa ni kuchafuliwa kwa maji ya Mto Mbarali maarufu kwa jina la Mfereji wa Wachina ambao huriririsha maji yake katika kata hizo.

Akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashau ya wilaya ya Mbarali,Mkuu wa wilaya hiyo Reuben Mfune aliwataka madiwani kuhamasisha wananchi kwenye kata zao kuchukua tahadhari badala ya kubaki wakiamini kipindupindi kitaishia tu kwenye maeneo kiliporipotiwa kwa sasa.

“Tuwaambie wananchi tuwahimize usafi,wasio na vyoo tuhakikishe wanakuwa navyo.Tusijione took salama kwakuwa maeneo yetu hajagundulika mgonjwa.Ni muhimu tukachukua tahadhari mapema kabla hakijasambaa zaidi”alisisitiza Mfune.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Kivuma Msangi aliwataka wakazi wilayani hapa kuchukua hatua za haraka kuwafikisha kwenye kambi maalumu iliyopo katika uwanja wa Barafu mjini Rujewa wagonjwa wanaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo badala ya kubaki nao majumbani au kuwapeleka kwenye zahanati na Hospitali ya wilaya.

Msangi aliwahakikishia madiwani kuwa kwa idadi ya wagonjwa waliopo kwa wakati huo dawa zilizokuwepo zilikuwa zintosheleza lakini uhaba ungeweza kujitokeza iwapo ugonjwa huo utasambaa zaidi na kusababisha ongezeko kubwa la wagonjwa.
Hadi kufikia Agosti 30 zaidi ya watu 700 walikuwa wameripotiwa kuugua Kipindupindi tangu ugonjwa huo ulipobainika Agosti 2.Idadi ya waliokuwa wamekufa ilifikia nane.Watatu wa awali wakiwa walikufa kabla ya ugonjwa kutambulika,wanne walifia majumbani baada ya ugonjwa kutambulika na mmoja alikufa wakati akielekea Hospitali kupata matibabu.

Kwa mujibu wa Msangi hadi Agosti 30 idadi kubwa iliyokuwa imewahi kufikiwa ni ya wagonjwa 77 kwa siku.Lakini siku hiyo wagonjwa waliokuwepo ni saba hatua iliyoanza kuonyesha kuwa kulikuwa na kila dalili za kutokomeza ugonjwa huo.

Msangi alisema ugonjwa huo ulisambaa zaidi kutokana na maji ya mito iliyopo wilayani hapa kuwa na vimelea vya kipindupindu hatua iliyoilazimu halmashauri kushirikiana na wataalamu kutoka Idara ya maji kuyatibu maji kwa kutumia dawa mbalimbali kila wakati.

“Lakini pia kulikuwa na changamoto ya wananchi wenyewe kuwa na imani kuwa huenda kitu wanachokiita wao Kidudu mtu ndicho kinasababisha watu kuugua.Hawakutaka kuamini kuwa ni kipindupindu.Wapo waliothubutu hata kuhoji ni kipindupindu gani hiki hata hakiui baada ya kuona idadi ya watu wanaokufa ni ndogo ikilinganishwa na wakati mwingine wakati ugonjwa huu ulipowahi kulipuka”.alisema Msangi

Jioni ya siku hii nilipata wasaa wa kukutana na wakazi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Rujewa na nikasikia mengi.Upo uvumi uliosambaa ya kuwepo kwa mkazi mmoja waliyeadi amekuwa akimwaga kinyesi katika Mfereji wa maji yanayokwenda Shambani kwa mwekezaji wa Mbarali Estate.Mfereji ambao maji yake hutumiwa majumbani mwa wakazi wa miji ya Rujewa na ubaruku.Ikasemekana huyu ndiye aliyeueneza.Lakini ukweli wapo pia wakazi waliokuwa wakifua nguo zao kwenye mito iliyopo.

Jioni hii pia nilishuhudi mtu mmoja aliyejitambulisha kama mtaalamu wa afya.Huyu alikuwa akipita katika Baa na maduka ya vinywaji vya viwandani baridi na moto akigawa dawa alizoziita za kuzuia Kipindupindu yeye aliziita Anti Cholela.

Nikiwa na baadhi ya wakazi katika Baa moja iitwayo Igurusi Pazuri jirani na Stendi ya Mabasi ya Rujewa,mtu huyu ambaye wanaonekana kufahamiana naye japo walikuwa wagumu kutaja jina lake alipita na kutugawia vidonge vitatu kila mmoja wetu akisema ndiyo dozi kamili ya kuzuia.Viwili vikiwa vya kijini na kimoja cheupe.Nilipouliza mtaalamu mmoja akanambia vidonge hivyo ni Cypro na docsyren.

Kilichonishangaza mimi ni kuona dawa zikigawiwa hata kwa watu waliokuwa wakinywa pombe kama Bia,Konyagi na Value.Nikajiuliza dawa hii itanywewa wakati gani na watu hawa.Lakini mtoaji ambaye dhahiri naye alionekana kuwa aalikuwa ametumia kilevi kw asana tu hakuwa akitoa maaelekezo ya kutosha.Akaniacha hoi zaidi alipokuwa akiulizaa kama una mtu au watu nyumbani kwako pia unaweza kuwaachukulia.Nikajiuliza dozi hii ni sawa kwa watu wazima na watoto?Sikupata jibu.

Kwa wakati huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Francis Mtega alikiri kuwa makatazo ya awali ya upikaji holela vyakula na uuzaji pombe za kienyeji ulisababisha pia ugonjwa huo kuenea zaidi kwakuwa watu walilazimika kwenda kula na kunywa kiuficho katika maeneo yaliyo machafu wakihofia kukamatwa.

Mtega alisema kufuatia hali hiyo baadae,iliilazimu Halmashauri kuja na mpango mbadala wa kuhakikisha watoa huduma za vyakula na vinywaji wanazingatia kanuni za usafi ili waendelea kutoa huduma hizo kwenye maeneo yao kama kawaida.

“Halmashauri bado inaendelea na mikakati ya kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kwa kusimamia kanuni za usafi ambapo sasa watoa huduma za vyakula na vinywaji wasiozingatia maelekezo wanawajibishwa kupitia kikosi kazi maalumu kilichoundwa”alisema Mtega. 

Hali ilizidi kuwa mbaya,ugonjwa ukazidi kusambaa maeneo mengine hadi nje ya wilaya ya Mbarali.Septemba Mosi Serikali ya mkoa wa Mbeya ikalazimika kutangaza hali ya hatari.Mkuu wa mkoa Amos Makalla  alisema tayari Kipindupidu kimeripotiwa katika wilaya mbili.Akawataka wananchi kuchukua tahadhari kuzingatia kanuni za usafi kwakuwa baada ya kuripotiwa Mbarali mgonjwa mmoja  pia alibainika wilayani Mbeya.

Katika maeneo na nyakati tofauti,Makalla alisitiza wataalamu wa afya kuwajibika ipasavyo kutoa maelekezo kwa wananchi huku pia akiwataka wananchi watakaoona mgonjwa yeyote kuwa na dalili za kipindupindu kutoa taarifa haraka kwa mamlaka zinazohusika ili ufanyike uchunguzi mara moja.

Aliwataka wananchi kutopuuza suala la uwepo wa ugonjwa huo kwakuwa kutokana na muingiliano wa watu uliopo ni rahisi mno ugonjwa huo kusambaa maeneo mengine zaidi ya ulikobainika hivi sasa.Akasema Serikali inaendelea kuchukua jitihada za dhati kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ili kutoleta madhara zaidi kwa jamii ikiwemo kukwamisha shughuli za uzalishaji mali.

Naikumbuka pia Siku nilipokutana na mkazi wa Nonde jijini Mbeya aliyekuwa akiendelea kupata kinywaji katika moja ya vibanda vilivyopo eneo la Pamodz Uhindini.Japo hakutaka kutaja jina lake lakini alionesha kusikitishwa na hatua ya nyumba yake kuwekewa Karantini siku moja baada ya kubainika kuwepo na mgonjwa wa kipindu pindu.Huyu ni mtoto wa dada yake aliyekuja kumsabahi akitokea Chimala wilayani Mbarali.

“Kwa mara ya kwanza nyumba yangu iliwekewa Karantini,tukazuiwa watu kutoka wala watu wan je ya familia kuja.Binti yule aliyetokea Usangu Chimala huko alikuwa anatapika na kuharisha mpaka baadaye walipomhamishiwa kwenye kambi maalumu.Ilitisha sana majirani na rafiki zangu waliopata taarifa”alisikika mkazi huyo akisimulia watu aliokaa nao.

Ugonjwa huu ukazidi kuitikisa Mbarali.Jitihada za kupambana nao nazo zikaongezeka siku hadi siku.Silaha ya mwisho ikawa ni kuwashirikisha wazee maarufu hasa wa kimila.Kila hali ilipoonekana kuwa mbaya zaidi Serikali ililazimika kupiga marufuku uuzaji vyakula na vinywaji.Ilipoonekana nafuu ikaruhusu.

Oktoba 10 katika maadhimisho ya Siku ya wazee Duniani,ambapo kiwilaya waliadhimisha tarehe hiyo badala ya Oktoba Mosi,Halmashauri ya wilaya ikakiri kushindwa kudhibiti Ugonjwa wa kipindupindu hadi pale walipowashirikisha wazee wakiwemo viongozi wa Kimila.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri alisema kwa takribani miezi mitatu ugonjwa huo uliwasumbua na kuwafanya wataalamu kutolala usiku na mchana wakitumia utaalamu wao lakini hawakuweza kufua dafu.Msangi alisema baada ya kuwashirikisha wazee akiwemo kiongozi wa Kabila la Wasangu Chifu Melele wa sasa,kukawa na kila dalili za kukomeshwa kwa kipindupindu wilayani hapa.

“Wataalamu tumehangaika wee ,tumetumia utaalamu wetu lakini wapi!Tumewashirikisha hawa wazee hasa Chifu wetu Melele leo ninapozungumza tuna siku mbili hatuna hata mgonjwa mmoja wa kipindupindu wilayani kwetu”

“Tutazidi kuwashirikisha wazee kwakuwa tunatambua umuhimu wao.Wao wanayajua mambo mengi hivyo tukiwatenga tunaweza kuipoteza jamii yetu” alisisitiza Msangi.

Hatimaye hali imeonekana kuwa shwari,kwani hadi mwishoni mwa Oktoba hakuna mgonjwa mpya aliyebainika kuwa na ugonjwa huu.Hakika Mbarali hawatakisahau kipindupindu cha mwaka huu.

No comments:

Post a Comment