Na Mwandishi Wetu, Chunya.
HALIMASHAURI ya Wilaya
ya Chunya Mkoani Mbeya imewahakikishia wapenzi wa soka kuwa michezo ya Timu ya Ken
Gold iliyopanda ligi kuu wataishuhudia kwenye uwanja uliopo wilayani hapa kwakuwa mikakati imewekwa
kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona tayari
Shilingi milioni 200 imeytengwa na halimashauri hiyo kwaajili ya muendelezo wa
ujenzi wa uwanja huo wa michezo uliopo katika Kata ya Mbugani.
Akizungumza na
mwandishi wetu, Kambona alisema lengo la halimashauri ni kuona mradi wa ujenzi
wa uwanja wa michezo uliopo Kata ya Mbugani unaomilikiwa na Halmashauri hiyo
unakamilika kwa wakati kabla ya kuanza kwa ligi Kuu mwaka 2024/2025.
Alisema wanao uhakika
Ken Gold itautumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani kwakuwa mbali ya
kutenga fedha hiyo kupitia mapato yake ya ndani pia imeunda Kamati maalumu ya
wadau inayoongozwa na Ayoub Omary ili kusimamia kwa karibu mradi huo.
Kambona alisema sanjari
na mipango ya Kamati Halmashauri inatarajia kutenga fedha nyingi zaidi mwaka
ujao wa fedha ili kuuboresha zaidi uwanja huo na kuwa wa kisasa kwa kuwekwa
nyasi bandia.
Mkurugenzi huyo pia aliwashukuru
wadau wanaoendelea kutoa michango ya hali na mali akiwemo mwekezaji kwenye
Sekta ya Madini aliyemtaja kwa jina la David Mathayo aliyesema ametoa
tingatinga kwa ajili ya kushindilia uwanja.
Aliwataka wadau wengine
kuunga juhudi zinazofanywa na halimashauri ili kuhakikisha uwanja unakamilika
kabla ya mashindano ambapo wananchi wataongeza mapato yao kutokana na ujio wa
wageni kutoka nje ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Mmoja wa
wafanyabiashara na mkazi wa Kata ya Chokaa wilayani hapa, Boniphace Mwinuka alisema
hatua ya kupanda daraja kwa timu ya Ken Gold inaleta hamasa kubwa ya michezo
katika Wilaya ya Chunya kwani wengi wa wakazi walikuwa wakisafiri kwenda jijini
Mbeya ili kushuhudia michezo ya ligi kuu.
Mwinuka alisema miongoni
mwa faida zitakazopatikana kwa wakazi wilayani hapa iwapo ligi kuu itacheza
kwenye uwanja huo ni pamoja na wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni kupokea
wageni wengi pamoja na wajasiriamali na madereva wa Bodaboda kusafirisha abiria
kutoka maeneo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment