Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, April 12, 2016

Msaada MCC sawa na Unga usio nyumbani mwako!

Na Joachim Nyambo.


UNGA usio nyumbani mwako ni sawa na Majivu!Ni usemi wautumiao watu wa kabila la wafipa kutoka mkoani Rukwa ambao kwa lugha yao husema “Usu usi ung’anda umwako Itwi!



Maana ya Usemi huu ni kuwa kitu chcochote japo kiwe na uzuri wa namna gani,kama unakipata kutoka kwa jirani haupaswi kukitegemea kwa asilimia 100.Ukiwekeza matumaini yote ya kukipata kila siku basi utambue kuwa ipo siku utaadhirika.



Maana ya usemu huu hautofautiani na kinachoonekana kati ya Tanzania na Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia(MCC).Ni kwa miaka kadhaa Shirika hili limekuwa likiisaidia Tanzania fedha kwaajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na fedha kutoka MCC ni pamoja na barabara ya Tunduma-Sumbawanga na pia miradi ya Umeme vijijini.



Hivi karibuni  MCC imetangaza kusitisha msaada wa Dola za Marekani milioni 473 sawa na shilingi Trilioni moja kwa serikali ya Tanzania.Shirika hilo limezuia fedha hizo za maendeleo  kutokana na Tanzania kuitisha Uchaguzi wa marudio Zanzibar pamoja na kutumika kwa Sheria ya makosa ya Mitandao.



Chini ya Mpango wa Uwekezaji wa MCC-2,fedha hizo zilikuwa ziende katika kuboresha huduma za umeme,ikiwemo usambazaji wa nishati hiyo katika vijiji vingine zaidi nchini.Kupitia MCC Tanzania imeweza kupiga hatua katika matumizi ya umeme kutoka asilimia 10 ya wakazi mwaka 2005 hadi asilimia 46.Ongezeko hilo la matumizi ya umeme kwa watanzania sehemu kubwa limetokana na MCC-1.



Katika awamu ya kwanza Tanzania ilipokea kiasi cha Dola za Marekani milioni 698 ambazo zilitumika kwa ujenzi wa barabara za Tunduma-Sumbawanga,Tanga-Horohoro,Namtumbo-Songea hadi Mbinga.



Fedha hizo pia zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwaajili ya miji ya Dar es salaam na Morogoro na pia kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania bara.Zilitumika pia kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania visiwani na pia kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.



Ukweli ni kuwa msaada huu ulikuwa muhimu na umeleta mabadiliko makubwa nchini.Kuboreshwa kwa barabara katika maeneo yaliyokuwa yamesahaulika kamaa ile ya Tunduma-Sumbawanga kumefunguwa fursa nyingi za kimaendeleo.Ni wazi kwa mwananchi kama mkazi wa Rukwa unapomweleza suala la MCC kusitisha kuleta fedha nchini atasikitika kwakuwa ni mnufaika wa moja kwa moja.



Lakini fedha hizi ukweli si za watanzania.Ni sawa na unga wa kuomba kwa jirani.Hauwezi ukaupangia bajeti huku ukiwa na uhakika wa asilimia zote.Hata kama una imani na jirani anayekupa unga huo ni lazima pia ujue anakupa kutokana na kufurahi kwake,au kutosheka kwake.Siku akiona haukumfurahisha au unga wake hautoshelezi ni wazi atabadili mawazo.



Uamuzi huo wa jirani MCC kujiondoa katika miradi aliyokuwa akiifadhili Tanzania ni fundisho tosha kwa watanzania katika vita yao ya kukabili umasikini na kujiletea maendeleo.Msaada wa unga wa jirani sasa umekuwa majivu na yawapasa watanzania kutafuta unga wao ili wasijikute wanakula majivu.



Kukatishwa kwa msaada huu kumeonekana kuwa gumzo kubwa ndani na nje ya Tanzania.Wadau mbalimbali wameonekana kuwa na michango tofauti ya kimawazo juu ya uamuzi huu.Mitandayo ya kijamii imejaa maoni mbalimbali ya wachangiaji juu ya hoja hii.Wapo wanaoonesha woga wakisema sasa Tanzania itakuwa kwenye wakati mgumu na wapo wale wanaosema ni wakati wa kujipanga.



Lakini maamuzi haya ya MCC yanakuja wakati serikali ya Tanzania chini ya rais Dk John Magufuli ikichukua hatua mbalimbali katika kuimarisha uchumi ili kuweza kuondokana na kutembeza bakuli na kuitwa ombaomba kwa mataifa wahisani.Tayari watanzani wameshuhudia jitihada kadhaa zinazofanywa na serikali ya Dk Magufuli katika kuimarisha uchumi wa taifa lao.



Miongoni mwa ambao yaliyokwishafanyika ni pamoja na udhibiti wa mapato katika bandari kuu ya Dar es salaam,Ufuatiliaji wa malipo halali ya kodi sambamba na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kwa kulipa mishahara wafanyakazi hewa.



Katika gazeti la habarileo la Machi 30 mwaka huu,Waziri wa Fedha na Mipango,Dk Phillip Mpango alikaririwa akisema serikali haishaangazwi na uamuzi wa MCC kwakuwa dalili zilikwishaanza kuonekana tangu Desemba mwaka jana.

“Tangu Desemba mwaka jana tulishasoma alama za nyakati na ndiyo sababu hatukuzijumuisha fedha za MCC-2 katika maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanayoendelea kwa mwaka ujao wa fedha.”



“Tulisoma kwenye mitandao matamshi ya viongozi wa mfuko huo ndiyo maana tukaamua kutozijumuisha fedha za MCC kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha,hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya kusitishwa kwa msaada huo”alikaririwa Dk Mpango.



Rais Dk Magufuli hata kabla ya kusitishwa kwa fedha za MCC amekuwa akikaririwa mara kadhaa na vyombo vya habari akihimiza matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo Tanzania pamoja na kila mwananchi kuwajibika katika kutoa kodi.



"Kila mmoja akifanya kazi, nchi haitahitaji wala kubembeleza misaada ya masharti kutoka nje kwa kuwa ni yenye neema, ina kila kitu na ikisimama imara na kila mmoja akatimiza wajibu wake, itakuwa ni nchi inayotoa msaada kwa nchi nyingine duniani". Anasema Dk Magufuli.



Dk Magufuli hatoi kauli hii baada ya kuingia madarakani tu.Hta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliomuingiza madarakani wa mwaka 2015 alikuwa akiyasema hayo.Alisikika mara nyingi akiwaambia wapiga kura kuwa kinachokosekana kwa Tanzania ni usimamizi imara wa rasilimali zilizopo.



Lakini pia kwa miaka kadhaa wanasiasa wakiwemo wa vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamikia mfumo wa usimamizi rasilimali wakisema ndiyo unaosababisha Tanzania kubakia ombaomba.Miongoni mwa vyama ambavyo viongozi wake wamekuwa wakililia mfumo wa usimamizi rasilimali ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema).



"Nchi hii tajiri sana lakini kutwa kucha kulialia msaada MCC millenium, watanzania leo hawapati umeme hadi tukaombe MCC wamekuwa wabunge kwetu? Ichaguenu Chadema hatutategemea wafadhili na masharti yao tutajenga nchi ya kujitegemea" yalikuwa maneno katika hotuba ya mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe baliyoitoa kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu Septemba 13,2015 katika Uwanja wa Nzega mkoani Tabora.



Kusitishwa kwa msaada huu wa wamarekani kunapaswa kuipa fundisho pia Tanzania kuwa taifa kubwa kama Marekani lina malengo yake hata linapokupa msaada.Wakati mwingine malengo yake yanaweza yasiendane na mipangilio ya Taifa linalopewa msaada na ndiyo sababu muasisi wa taifa Mwalimu Julius Nyerere alionya kuwepo na umakini katika kupokea misaada ya mataifa kama Marekani.



“Siku wamarekani wakinisifia nimefanya kazi nzuri nitajiuliza kuwa nimekosea wapi!" aliwahi kutamka Mwalimu Nyerere katika moja ya mikutano.



Kwa kauli ya mwalimu Nyerere kuna haja kwa Mtaifa yanayoendelea kupanua wigo wa fursa ya wadau wa kimaendeleo badala ya kusalia kwa taifa moja ambalo kila nchi change inaliangalia na kupiga magoti.Tanzania inapaswa kupongezwa kutokana na kuonesha nia ya kuanza kushirikiana na nchi kama Japani,China na Vietnam.

Mwisho.