Na Joachim Nyambo.
OFISI ya Madini Chunya kwa sasa
inahudumia eneo lote la wilaya za Chunya mkoa wa Mbeya na Songwe mkoani
Songwe.Huduma ni pamoja na Utafiti,uchimbaji na biashara ya madini.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Madini
Mkazi wa wilaya ya Chunya Ndege Bilagi,Ofisi ina jumla ya watumishi 12
wanaogawanyika katika kada za mhandisi wa migodi mmoja,mjiolojia mmoja,Fundi
sanifu mmoja,mhasibu mmoja,madereva watatu,walinzi watatu,mwangalizi wa ofisi
mmoja na katibu mhitasi mmoja.Watumishi wane kati ya hao ni wa mkataba.
Ofisi hii inafanya kazi za Idara ya
Madini iliyo chini ya wizara ya nishati na Madini,inatoa taarifa yake ofisi ya
madini Kanda iliyopo jijini Mbeya.Pia inatoa taarifa katika taasisi nyingine za
serikali ikiwa ni pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya juu ya utekelezaji wa
shughuli mbalimbali za ofisi.
Ofisi inashirikiana na Halmashauri
katika kutekeleza majukumu yake kwani shughuli nyingi za uchimbaji
zinaingiliana na matumizi mengine ya rasilimali kama maji,misitu na ardhi.
“Baadhi ya shughuli zinazosimamiwa
na ofisi ni pamoja na Kusimamia na kuratibu mfumo wa leseni wa Online Mining
Cadastre Transaction Portal(OMCTP) kwa watumiaji wa leseni ikiwemo
kuwasajiri,kuwafundisha wachimbaji au wateja namna ya kuomba na kuingiza maombi
ya leseni kwa kutumia akaunti zao za barua pepe”anasema Bilagi.
Shughuli nyingine ni Kusimamia
uchimbaji wa awali(mdogo) wa madini ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za
ugani(Extension Service) kwa wachimbaji wadogo.Kukagua usalama wa maeneo ya
wachimbaji wadogo na wakubwa na Kutoa elimua ya uhifadhi wa mazingira kwa
wachimbaji wadogo,wa kati na wakubwa.
Nyingine ni kutoa elimu kuhusiana na
matumizi ya baruti na kusimamia au kuhakikisha kuwa sheria na matumizi ya
baruti vinatekelezwa kwa ufasaha.Kukusanya Maduhuli ya aina mbalimbali ya
serikali yatokanayo na shughuli mbalimbali za madini.
“Ofisi pia ainawajibika kukagua
shughuli za utafiti wa madini zinazofanywa na wenye leseni kubwa za utafiti wa
madini(prospecting licenses),kupokea taarifa za robo mwaka kutoka kwa watafiti
madini wenye leseni kubwa na kuzioanisha ili kubaini kama taarifa hizo
zinaendana na kazi iliyofanyika katika leseni husika”
“Kuna kusimamia shughuli za
uchimbaji mkubwa ili kubaini kama Sheria na kanuni zinafuatwa.Kufanya ukaguzi
wa shughuli zote za uchimbaji kwa lengo la kubaini ukiukwaji wa sheria,Kutoa
vibali vya kusafirisha madini na sampuli zenye madini nje na ndani ya nchi na
pia Kutoa vibali vya kuagiza Baruti,kukagua maghala ya kutunzia baruti”
“Kwa kifupi tunasimamia Sheria ya
Madini ya mwaka 2010,sheria ya Baruti ya mwaka 1963 pamoja na Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004” anasema Bilagi.
Uchimbaji mdogo wa madini
Bilagi anasema,Uchimbaji mdogo wa
madini unafanywa na watanzania pekee ambao lazima wawe na leseni za awali za
uchimbaji zijulikanazo kama Primary Mining Licenses(PMLs).Katika wilaya ya
Chunya uchimbaji huu unafanyika katika maeneo yaliyogawanywa kwenye kanda.
Kanda ya Makongolosi kuna maeneo ya
Mkola,Mapele,Gepu,Ujerumani,Chipoka na Kilombero wakati Kanda ya Matundani vipo
vituo vya Kasisi,Kasakalawe,Itumbi Jeshini,Jobu Iti,Makatang’ombe,Idundu na
Bwawani.
Kanda ya Chunya kuna maeneo ya
Sinjili,Mlima Yasini,Mapogolo,Kiwanja,Mbugani,Itumba,Godima,Simba
Reef,Simbachai,Safari
Mine,Saitunduma,Simbadume,Majengo,Isenyela,Chalangwa,Nyatula,Mlimanjiwa,Kasanga
Madini,Kasanga Market,Soweto na Mamusapu.
Maeneo mengine kwenye ukanda huu ni
Mapapai,Ifumbo,Chikula,Kisu Mine,Magamba,Makoma,Mawelo,Mnyolima,Mwankonyonto,Shoga,Legezamwendo,Ilepuka,Chokaa,Mapunga,Majengo,Ihamba,Tukuyu,Sangambi,Izumbi
na Kikavu.
Anasema wilaya za Chunya na Songwe
zina wachimbaji wadogo wenye leseni za PMLs zipatazo 729.
Utafutaji wa Madini
Anasema Shughuli za Utafutaji wa
madini zinafanyika kwenye leseni zinazojulikana kama Prospecting Licences(PL)
katika maeneo yote ya wilaya ya Chunya
ili kubaini uwezekano wa kupata mashapo makubwa ya madini.
Ukanda huu wa madini unajulikana kwa
jina la kijiolojia kama Lupa Gold Fields ambao una madini ya dhahabu na madini
mengine ya Metali yaani Shaba,fedha,galena,chuma na mengineyo.Nje ya ukanda wa
Lupa Goldfields kuna madini mengine kama rare earth
elements(Metals),Magadi(Soda ash),madini ya vito na mengineyo.Wilaya hizi mbili
zina jumla ya leseni za utafutaji madini 179.
“Kuna kituo cha Kufundishia
wachimbaji wadogo cha Matundasi ASM kilichoanzishwa na serikali mwakaa 2005 ili
kutoa elimu kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo.Kituo hiki kipo eneo la Matundasi
ambapo mwaka 2008 kilibinafsishwa kwa mwekezaji kwa makubaliano na serikali ili
akiendeleze. Kwa sasa mradi huo unaendelea na shughuli za uchorongaji miamba
ili kubaini mashapo yatakayoweza kuanzisha mgodi darasa”anasema.
Uchimbaji Mkubwa
Uchimbaji mkubwa unafanyika katika
maeneo mbalimbali na kuna leseni zipatazo tano katika eneo linalisimamiwa na
Ofisi hii ya Madini ya Chunya.Kwa eneo la wilaya ya Chunya pekee kuna uchimbaji
mkubwa unafanyika eneo la kata ya Matundasi ambapo kampuni ya Sunshine Mining
Co Limited yenye leseni ya ucjenjuaji(processing licence) namba 00067/2013 na
imeomba Mining Licence kwa maeneo yake mawili.
“Kwa sasa kampuni hii imesimamisha shughuli zake ili kutengeneza
miundombinu ya bwawa la maji machafu(Tailing Storage Facility-TSF).Vilevile
tuna wachimbaji wengi wadogo ambao sasa mitaji yao na uchimbaji wao umekuwa
kutoka kwa wachimbaji wadogo hadi kufika kuwa wachimbaji wa kati.Mfano ni
Aidani Msigwa,Isack Msowoya na Elias Mwembe.”
Uzalishaji Madini na Ulipaji wa Maduhuli ya Serikali
Kwa mujibu wa sheria ya
madini,Wachimbaji wakubwa na wadogo wanapaswa kulipa kodi za serikali ambazo ni
Ada ya mwaka ya leseni,mrabaha wa asilimia nne kutokana na uzalishaji waa
madini,ada za kubeba baruti,ujenzi wa maghala ya kuhifadhia baruti.Hivyo serikali
kupata mapato kutokana na tozo hizo ambapo utaratibu ni kuwa fedha zinapaswa
kulipwa benki moja kwa moja.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha
2010/2011 hadi 2015/2016 Jumla ya Shilingi 1,888,642,319.66 zilikusanywa na
Ofisi ya Madini wilayani Chunya ikiwa ni Mrabaha wa
asilimia 4 wa madini aina ya dhahabu yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo wilayani
hapa katika kipindi hicho.
Bilagi anasema katika kipindi hicho
Jumla ya Gramu 821,113.16 za dhahabu zenye thamani ya jumla ya Shilingi
47,216,058,041.50 zilizalishwa katika migodi mbalimbali wilayani hapa hivyo
kuwezesha serikali kujipatia shilingi 1,888,642,319.66 ikiwa ni mrabaha wa asilimia 4.
Akifafanua zaidi,anasema katika
mwaka wa fedha 2010/2011 gramu 11,934.38 zenye thamani ya shilingi 668,325,550
zilizalishwa hivyo serikali ikajipatia mrabaha wa
shilingi 26,733,020.
Mwaka wa fedha 2011/2012 gramu
14,693.80 zilizalishwa zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi 822,852,600 hivyo
serikali ikajipatia shilingi 32,914,104.
Mwaka 2012/2013 zilizalishwa gramu
11,957.93 zenye thamani ya shilingi 669,643,800 hivyo serikali ikapata shilingi
26,785,752 na mwaka wa fedha 2013/2014 zikazalishwa gramu 68,508.93 zenye
thamani ya shilingi 3,836,499,900 na serikali ikajipatia shilingi 153,459,996.
Anasema mwaka wa fedha 2014/2015
zilizalishwa gramu 405,587.81 zilizokuwa na thamani ya jumla ya shilingi
22,712,917,481 na serikali ikajipatia shilingi 908,516,699.24 na mwaka
2015/2016 gramu 308,430.31 zilizalishwa zikiwa na thamani ya shilingi
18,505,818,710.50 na hivyo serikali ikajipatia shilingi 740,232,748.42.
Utengaji wa Maeneo kwaajili ya wachimbaji wadogo
Akizungumzia Utengaji wa Maeneo ya Uchimbaji
mdogo,Bilagi anasema Wizara ya Nishati na Madini ilitoa eneo la Itumbi B lenye
ukubwa wa Kilometa za mraba 12.78 ambapo baada ya kufanyiwa michoro zaidi ya
viwanja 300 vilipatikana.
Anasema pia kwa sasa Wizara imetenga
maeneo ya Mbugani na Chalangwa na mpango wa kuyagawa maeneo hayo utafanyika
mara baada ya Wakala wa Jiolojia Tanzania(GST) atakapofanya kazi ya Utafutaji
wa awali ili kubaini uwepo wa mashapo ya madini.
Changamoto zinazoikabili Ofisi
Kwa mujibu wa Bilagi Ofisi ya
Madini Chunya inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kimsingi zinakwamisha
utendajikazi.Changamoto hizi ni pamoja na Ukosefu wa rasilimali fedha za
kuendesha ofisi.Hii imesababisha kusimama kwa shughuli nyingi za nje ya
ofisi(field activities) kama ukaguzi kwa wachimbaji,watafutaji madini,kutoa
semina katika vijiji na pia kudhibiti wachimbaji haramu.
Umiliki na matumizi holela ya Baruti
ni changamoto nyingine inayohatarisha maisha ya wachimbaji wadogo wa
madini,familia zao na majirani wilayani Chunya.Bilagi anasema baadhi ya
wachimbaji wamekuwa wakitunza baruti majumbani mwao,madukani na baadhi husafiri nazo kwenye gari zao.
“Uhifadhi huu holela ni hatari kwa
maisha ya wachimbaji hao,familia na majirani zao kwakuwa inaweza kusababisha
mlipuko na kuwadhuru watu wanaokuwa jirani”.
Anasema changamoto nyingine iliyopo
ni baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali za vijiji kuingilia shughuli za
ofisi ya madini hasa pale wanapotoa vibali kwa wachimbaji kinyume cha sheria.Baadhi
yao wamekuwa wakaidi hata wanapoelimishwa na badala yake wamekuwa wakichochea
migomo kwa wananchi ili wasikubali kutii sheria ya madini ya mwaka 2010.
“Tuna changamoto pia ya baadhi ya
wanakijiji kujimilikisha maeneo ya kuchimb kwa kisingizio kuwa madini yapo
katika mashamba yao.Vile vile hali hii imesababisha baadhi ya wachimbaji
wanaomiliki leseni kisheria kushindwa kuchimba maeneo yao kwa kuhofia kufanyiwa
vurugu na wenyeji”
“Bado pia uchimbaji wa kuhama hama
unaendelea.Hii inasababishwa na wachimbaji wengi kutokuwa na mitaji ya kutosha
ya kufanya utafiti wa kugundua kama maeneo wanayoombea leseni yana mashapo ya
madini ya kutosha ili wachimbe” alisema Bilagi.
Kuwepo kwa Utitiri wa kodi na tozo
nyingi kwa wachimbaji wadogo nalo linatajwa kama changamoto kubwa.Baadhi ya
taasisi zinatoza kodi kubwa zinazoleta manung’uniko kutoka kwa wadau wa
shughuli za madini.Mfano watu wanaosaga mawe wanatakiwa kulipa TRA shilingi
700,000 kwa mwaka,wakilipe kijiji kuanzia kiasi cha shilingi 15,000 hadi 20,000
kwa mwezi na wanatakiwa walipe ushuru halmashauri ya wilaya.
Wachenjuaji wanalalamikia kodi ya
zimamoto ambapo hadi baadhi yao waliwahi kuwekwa mahabusu wakiamriwa kulipa
shilingi 5,000,000 kwa mwaka kama ada ya zimamoto huku wachimbaji wakiwa
hawapati huduma yoyote kutoka jeshi hilo.Kero kubwa ni namna taasisi husika
inavyoidai kwa njia ya shuruti kabla ya kuwaelimisha.
Bilagi anasema katika kutafuta
ufumbuzi wa baadhi ya changamoto,serikali kupitia ofisi ya madini wilaya
imeendelea kutoa Elimu kuhusu sheria ya Madini ya mwaka 2010 ili wananchi waweze
kutambua kuwa unapomiliki ardhi hauna ruhusa ya kumiliki madini yaliyopo bila
kufuata sheria.
Anasema pia Elimu inaendelea
kutolewa kwa wananchi na wachimbaji juu ya namna bora ya kumiliki na kutumia baruti
kwa mujibu wa Sheria ya Baruti ya mwaka 1963
Afisa huyo anasema Serikali ya awamu
ya Tano imedhamiria kuinua hali ya wachimbaji wadogo ili wasiwe wa kuhama hama
hivyo imeiwezesha wakala wa Jiolojia Tanzani(GST) ili wafanye utafutaji wa
awali wa mashapo yenye madini katyika maeneo mbalimbali nchini na Chunya ikiwa
ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele.
“Serikali ina mpango wa kujenga
kituo kingine cha kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika kata ya Mbugani ili
wawe na weledi wa uchimbaji wenye tija.Tunaendelea kutoa huduma ya kuandikisha
wananchi katika mfumo wa leseni wa OMCTP ili kila mchimbaji aweze kuomba leseni
bila ya kuwa na ulazima wa kufika ofisi ya madini”
Anasema kuhusu utitiri wa kodi Ofisi
ya madini Chunya ilikwisha wasilisha kwa Kamishna wa Madini.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla
alipotembelea shughuli za madini na kukutana na wadau wa Sekta hiyo aliahidi
kuendelea kupigania haki za wachimbaji wa madini ili kupunguza adha
zinazoikabili sekta hiyo wilayani hapa.
No comments:
Post a Comment