Na Joachim Nyambo.
“Yapo mambo mengi yaliyonisukuma kuanzisha shule” Ni
sentensi aliyoanza nayo Anivene Lusubilo nilipozungumza naye.Huyu ni mmoja wa
wakurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya mchepuo wa kingereza ya Elisabene
iliyopo mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.Mkurugenzi mwenza ni mumewe
Frank Shitindi.
Ipo historia ndefu kwa familia ya wanandoa hawa hata
kufikia hatua ya kuwa na taasisi ya kutoa elimu ambayo sasa imekuwa manufaa kwa
jamii pia inayowazunguka na kwingineko nchini nchini.Ni familia yenye watoto
wane wote wakiwa ni mabinti.
“Msukumo wa kwanza nilianza kuupata kutokana na mimi
mwenyewe kupata elimu kwa kuungaunga sana.Hii ilitokana na wazazi wetu
kutotambua sana umuhimu wa elimu”
“Suala la pili ninaye binti yangu ambaye mara baada
ya kumaliza darasa la saba na kupata matokeo mabaya nilihangaika sana kupata
shule ya sekondari ya kumpeleka.Nilimpeleka shule tano binafsi lakini kila
alipofanya usaili alionekana kushindwa.Nilichokibaini ni kuwa alishindwa
kutokana na kuwa na uwezo mdogo wa lugha ya kingereza.Iliniumiza sana,nikawaza
halii kama hiyo ikoje kwa jamii inayonizunguka!” alisema Anivene ambaye ni
mtaalamu wa Kilimo katika halmashauri ya mji wa Tunduma.
“Watoto wote waliofaulu kwenye usaili uliofanyika
kwenye shule nilizompeleka mwanangu nilibainia walitokea katiak shule
binafsi.Nikaona walimu katika shule hizi wanajituma kutokana na kutetea ajira
zao hivyo mwanafunzi atapewa elimu inayostahili.Katika shule za serikali wapo
walimu wanaobweteka na kuona hana cha kupoteza mtoto anapokuwa na maendeleo
mabaya kitaaluma”
Anasema hapo alianza kufikiria kupeleka watoto wake
wote kwenye shule za michepuo ya Kingereza ili wasikumbwe na adha iliyomkuta
dada yao.Alimshawishi mumewe na walianza kuwekeza kidogo kidogo fedha kutoka
katika sehemu ya mishahara yao ya kila mwezi.
“Niligundua
gharama haikuwa kubwa sana kumsomesha mtoto katika shule hizi.Nilimshawishi
mume wangu kila mmoja wetu atenge shilingi elfu ishirini katika mshahara wake
wa kila mwezi.Tukajikuta tunaweza.Yule aliyekuwa darasa la nne na mwezie wa
darasa la kwanza tukawapeleka wote English Medium katika shule moja iliyopo
hapa mkoani kwetu lakini wilayani Mbozi.”
Anasema kuwapeleka watoto katika shule hiyo ya
mchepuo wa kingereza kukampa fundisho jingine ambalo lilizidi kumpanua mawazo
na kuzidisha nia ya kutafuta ufumbuzi.Mazingira aliyokutana nayo yakaonekana
kutomridhisha kama mzazi.
“Kwakweli pamoja na watoto kuendelea kusoma pale
sikuweza kuwa na amani kwakuwa kila tulipokwenda kuwasalimia watoto
hatukuridhishwa sana na mazingira tuliyokutana nayo.Masuala ya lishe,malazi na
pia mazingiara ya shule kwa ujumla.Tukaona kuna kila dalili za watoto
kuambukizana magonjwa kwa urahisi.Hapo tukaamua kuwahamishia katika shule moja
iliyopo jijini Mbeya.”
Wakati haya yakifanyika suala la uchungu wa mzazi
kuishi mbali na watoto wake nalo likajitokeza.Anivene akajikuta anakuwa mpweke
kwa watoto wake kuishi mbali nae.Akahisi watoto pia hawana imani kutokana na
kuishi kwao mbali na wapendwa wazazi wao.Akahisi kuna mambo muhimu wanayakosa.
“Hakuna siku niliyoumia kama nilipokuwa namwacha
mtoto wangu wa mwisho anakwenda kuanza darasa la awali.Kilikuwa kitoto kidogo
mno chenye miaka sita.Kilipoanza kulia nikajikuta na mimi nabubujikwa na
machozi.Nilikosa raha hata baada ya kuwa nimemwacha shuleni.Nilijua uangalizi
ni mzuri lakini nikawaza namba amekuwa akifurahi kila tuamkapo asubuhi.Nikaona
furaha yake sasa itakuwa imepotea na huenda hata masomo ikawa shida kwake.nilibeba
uchungu wa wanawake wote wa eneo hili”.
Wakati huo wote alikuwa akijaribu kutafakari ni
kwanini watu wenye uwezo kwenye maeneo ya jirani hawajataka kuanzisha shule
kama hizo wanazozifuata mbali ili watoto waweze kusoma jirani na makwao?Mji wa
Tunduma una wakazi walio na vipato vizuri kutokana na wengi wao kuwa wafanyabiashara
wakubwa.Lakini hawakutaka kuwekeza katika suala la elimu.Wote wakawa wanapeleka
watoto mbali nao.
“Iliniuma sana lakini ikanibini kuja na wazo
jipya.Ili uweze kuanzisha shule yakupasa uwe na vigezo gani.Hapo ndipo
nilipoanza mchakato wa kufuatilia vigezo vinavyohitajika mpaka pale
niliporuhusiwa na serikali”
Anasema hapo ndipo alipoanza kujenga majengo kwenye
eneo lake lililopo katikati ya mji wa Tunduma ambako kwa sasa yapo madarasa ya
shule ya awali pekee.Mwaka 2012 baada ya kukamilisha majengo hayo nikaanza
kuwaza napataje walimu wa kuanza nao.Mtaji umeishia katika kujenga majengo na
kuboresha mazingira.
“Nilihitaji muda wa kujipanga zaidi mpaka kufikia
kuanza kuajiri na kupokea wanafunzi.Madhari niliyokuwa nimeweka yanayovutia
watoto kwa kuwepo na bembea siku moja yakaniponza.Siku hiyo watoto wawili wa
rafiki yangu waliokuwa wakisoma katika shule moja hapa mjini waligoma kwenda
shuleni kwao.Walimlazimisha mama yake awalete kwenye majengo yetu na wakasema
hawatokwenda shuleni kwao iwapo mama yao hatokubali ombi lao.”
“Mama yao alinipigia simu kuniomba awapeleke kwenye
majengo yetu nikamwambia haiwezekani sisi hatujaanza kufanya kazi hivyo
hatuwezi kuruhusu.Badaye alipoona wanamsumbua sana akanipigia tena simua
akanambia kwakuwa pale kuna walinzi anawapeleka hivyo hivyo ili wakashinde huko
wao wafurahi”
“Wakati akinambia hayo alikuwa tayari njiani
kuelekea huko.Sikuwa na namna zaidi ya kumkubalia.Nilimpigia mlinzi
akawafungulia geti na kuwaruhusu kuingia na mama yao akawaacha hapo.Mpaka nakwenda
niliwakuta wanaendelea kucheza wala hata hawakujali kuwa walikuwa peke yao”anasema.
Anasema hapo akawa na mtihani mpya.Ili mlazimu
atumie pesa yake ya mfukoni kuwanunulia chipsi kwenye kibanda kilichopo jirani
kwaajili ya chakula cha mchana.Baadaye mama yao aliwapitia watoto hao na kurudi
nao nyumbani.Kesho yake hali ilikuwa hivyo hivyo,watoto waligoma kwenda shuleni
kwao ikabidi waletwe shuleni hapo.
“Nikawa na kibarua kigumu.Watoto wa watu wanasinda
kwenye majengo yangu,hakuna mtu wa kuwasimamia,nikaona nina wakati
mgumu.Ilibidi nikutane na mzazi wao ili tulijadili jambo hili kwa pamoja.Ajabu
hakuwa na hofu kama yangu!Akanambia wewe unasubiri nini kutafuta walimu?akasema
tafuta mwalimu aanze kuwafundisha watoto mimi nitakutafutia wanafunzi wengine
kama unashindwa kuwatafuta”
“Nikaona mbona huyu simwelewi!Lakini nikaona huenda
huu ndiyo mwanzo wenyewe.Akanitafutia mwalimu mmoja anaitwa Sarafina.Sikuwa na
kwa kumweka ikabidi niishi nae nyumbani kwangu.Rafiki yangu akashawishi
wafanyabiashara wakaniletea watoto wengine wawili.Hapo nikawa na wanafunzi
wane.Kwakuwa usajiri wa shule tulikuwa
tumepata tayari hatukuwa na mashaka.”
Anasema baadaye waliopata mwalimu mwingine raia wa
Kenya.Lakini hakuweza kudumu shuleni hapo kwakuwa baadaye ilibainika hakuwa ametimiza
masharti ya kufanya kazi nchini hivyo aliondoka.Walilazimika kuendelea
kudunduliza walimu.
“Unajua tatizo kubwa tulilonalo hapa nchini ni
kupata walimu walio na uwezo.Si kwamba walimu hawapo!wapo wengi tu lakini uwezo
ni tatizo.Na hii ndiyo inasababisha shule zetu kuwa na ushindani mkubwa wa
kuwapata walimu wenye kuiwezesha taasisi yako kufanya vizuri”
Anasema kupenda kwake kujifunza kulimfanya azidi
kupanua wigo wa uelewa kila mara aliposafiri.Alipenda kutembelea shule
mbalimbali zinazotoa elimu sawa na ya shuleni kwake.Na kila jambo jipya
alilojifunza aliangalia namna ya kuliongeza kwenye taasisi yake.
“Kutokana na ugumu wa kupata walimu kuna wakati
ilinilazimu kwenda Dar es salaam na kukaa huko kwa majuma mawili nikiwatafuta
wanaoweza kuja kunisaidia.Hapo ndipo nilipokutana na mwalimu David Buyogela
ambaye sasa ndiye Mkuu wa shule.Nakumbuka ilikuwa mwaka 2013.Wakati huo pia
mpaka nafanya mazungumzo na mwalimu huyu nilikuwa naumwa na kabla sijarudi
ilibidi nifanyiwe upasuaji”
Kwakuwa mtazao wa familia hii ulikuwa ni kuwa na
shule ya awali na Msingi zilizokamilika,waliamua kutumia eneo walilokuwa nalo
nje ya mji kidogo litumike kwaajili ya kujenga shule ya msingi.Hapo ujenzi
ulianza na baada ya kuziona taasisi za kifedha zikakubali kutukopesha fedha.
Anivene anasema kujua namna ya kutawala imekuwa
chachu ya mafaniko kwenye taasisi yao kwani hadi sasa walimu na wanafunzi
wamezidi kuongezeka.Wapo wanaohamia wakitokea katika shule nyingine na pia wale
wanaoanza awali kila mwanzo wa mwaka wa masomo.
Mkuu wa shule mwalimu Buyogela anasema hivi sasa
shule ina jumla ya wanafunzi 255 kwa maana ya kuanzia darasa la awali hadi
darasa la tatu.Darasa la awali wapo 114
wasichana wakiwa 58 na wavulana 56,darasa la kwanza wako 71 wavulani 37
na wasichana 34.Darasa la pili waapo 54,wasichana 31 na wavulana 23 na darasa
la tatu wako 16 wasichana 11 na wavulana watano.
“Wapo watoto wanaohamia kutoka shule nyingine.Hawa
tunawasaili na kuona uwezo wao iwapo unaridhisha anaendelea na darasa alilokuwa
huko alikotoka na iwapo tutaona kiwango chake hakiridhishi tunaongeza na mzazi
au mlezi kumrejesha darasa moja.Lengo ni kumjengea uwezo kitaaluma aweze kwenda
sambamba na wenzie darasani” anasema Buyogela.
“Kama watumishi tumekuwa na jambo la kujivunia
kutokana na mahusiano mazuri baina yetu na mwajiri.Baadhi ya waajiri hawapedi
kupokea maoni ya wafanyakazi wao.Kwa hapa hali ni tofauti,tunasikilizwa na
tunajiona sehemu ya taasisi.”
Baadhi ya wanafunzi shuleni hapa Tecla Almasi,Moses
Ndaga na Jesca Korogwe wote wa darasa la tatu,wanasema mazingira ya utoaji
elimu yanayokwenda sambamba na kupata chakula yanawawezesha kupata fursa nzuri
ya kuwaelewa walimu wao.
Tecla na
Moses wanasema walihamia shuleni hapa wakitokea shule tofauti lakini tofauti na
walikotoka hapa wameongeza uwezo kitaaluma.Wanasema huenda mazingira ya walimu
kuwajali na uwepo wa miundombinu rafiki ya kufundishiwa imekuwa chachu ya
mafanikio yao tofauti na awali.
Uwepo wa uwekezaji shule ya Elisabene umekuwa chachu
ya maendeleo kwa watu mbalimbali.Zipo ajira zilizozalishwa kama za
walimu,madereva,wapishi,walinzi,watu wa usafi na utunzaji bustani,ujenzi wa
majengo,ufyatuaji tofali na nyingine nyingi.
“Wananchi waishio jirani na shule pia tunawapa maji
kutoka katika kisima kirefu tulichochimba hapa shuleni.Tunashiriki pia katika
shughuli za kijamii kwa kuchangia michango mbalimbali.Tunaamini jamii
inayotuzunguka ni sehemu yetu” anasema mkuu wa shule.
Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado kuna
changamoto zinazoikabili shule hii.Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na
mtoto kuletwa akiwa amechelewa kuanza shule,mzazi kutaka mtoto aingie darasa la
juu japo hana uwezo akiona kumrudisha darasa atapata hasara.Pia kutokuwepo kwa
hostel kunasababisha wanafunzi kukosa muda wa kutosha kupumzika akiwa katika
mazingira ya shule.
“Kama watumishi tunataraji utawala unafanyia kazi
suala la Usafiri wa watumishi,kujenga nyumba za wafanyakazi,Kujenga
hosteli,kupata fursa ya kujiendeleza kielimu,kushiriki semina za mara kwa mara
ili kujijengea uzoefu na pia kutuunganisha na taasisi za kifedha ili kupata
mikopo na pia mifuko ya kijamii”anasema Buyogela.
Mkurugenzi wa shule anasema changamoto za kiutawala
ni pamoja na wazazi kutolipa ada kwa wakati licha ya kuwa wazazi wengi wanao
uwezo mzuri kiuchumi,upatikanaji wa walimu,kutofikiwa kwa miundombinu ya maji
na maji katika eneo la shule ya msingi hivyo kulazimu kutumika kwa jenereta na
kisima cha kuchimbwa.Taasisi za kifedha kutoza riba kubwa kwenye mikopo.
“Tuna changamoto kubwa ya mtazamo hasi wa serikali
juu ya fedha binafsi,inaamini kuwa zinapata faida kubwa na hapo ndipo
tunapolundikiwa mzigo wa kodi lukuki zikiwemo za majengo,TRA,fedha za
ukaguzi,kulipia majengo.Hapa tunaona kama hakuna mahusiano mazuri baina ya
serikali na shule binafsi”
“Lakini kuna suala la wazazi kutowajibika na watoto
wao.Wapo ambao hawajawahi kufika hapa shuleni tangu watoto wao waanze kusoma
hapa.Hawaulizii maendeleo ya watoto wao na wala hawawaandai watoto wanapokuja
shule.Mtoto anakuja ukimuona tu utajua huyu anaumwa lakini unapompigia mzazi
anakuwa hajui lolote na amemruhusu aje shule siku hiyo.Mtoto mwingine utakuta
amekuja na nguo chafu ni kama hakutokea kwa mzazi.Hii yote ni kutokana na
wazazi kutowajali watoto” anasema Anivene.
Mkurugenzi huyu anasema matarajio ya taasisi hii ni
kujenga hosteli ili watoto waweze kukaa shuleni japo ni kwa wale
watakaopenda.Japo hii ni changamoto kwake kwani awali alipenda mtoto aje kusoma
na jioni aungane na familia yake.
Kuanzisha shule ya sekondari kutategemea mwenendo
mzuri wa mafanikio ya shule ya msingi.Japo ni muhimu kwakuwa itasaidia watoto
wanaomalisha shuleni hapo kuendelea na masomo ya sekondari wakiwa katika
mazingira waliyoyazoea tofauti na kwenda shule nyingine.
Mtazamo wa Serikali ya mkoa wa Songwe ni kuona
uwekezaji katika Nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu unaimarishwa.Hii
itasaidia jamii ya wakazi mkoani hapa kujikwamua na kuondokana na maadui
Ujinga,Maradhi na Umasikini pale watakapokuwa na elimu ya kutosha.
“Tunataka kuwaondoa wakazi wa mkoa wa Songwe kwenye
Unyonge.Wana fursa nyingi za uzalishaji mali lakini bado ni wanyonge na ili
kuwaondoa kwenye hali hii lazima tuwape elimu”alisema mkuu wa mkoa wa
SongweLuteni mstaafu Chiku Galawa alipozungumza na wanachama wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI).
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa,George Mbijima,alipokimbiza mwenge shuleni hapa alipongeza waasisi wa
shule ya Elisabene akisema jamii inapaswa kujikita katika uwekezaji wa
kujikomboa kutoka kwenye adui Ujinga.
No comments:
Post a Comment