Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, June 28, 2012

MADAKTARI MBEYA WATIMULIWA

BODI ya hospitali ya Rufaa ya Mbeya imechukua uamuzi wa kuwatimua madaktari 54 waliokuwa katika mafunzo na wengi 18 wa kuajiriwa waliokuwa katika mgomo.

Mwenyekiti wa bodi hiyo kaimu mkuu wa mkoa wa Mbeya dk.Norman Sigalla alitangaza uamuzi huo leo hii (Juni 28) katika kikao kilichowakutanisha wajumbe wa bodi na waandishi wa habari.

Dk.Sigalla amesema bodi imefikia maamuzi hayo baada ya madaktari kushindwa kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kutofika katika kikao walichoitwa na pia kutojibu barua walizopewa na kutakiwa kujibu ni kwa nini wasiwajibishwe.

Amesema kutofika kazini kwa madaktari hao kwa siku tano mfululizo walivunja mkataba wao kwa mujibu wa kanuni za kudumu za utumishi wa umma toleo la mwaka 2009 kifungu namba F16,F 17 na F 27.

Amesema kwakuwa bodi ndiyo huingia mkataba na madaktari hao,imechukua uamuzi wa kuvunja mikataba nao na kuwarejesha kwa muajiri wao yaani waziri wa Afya na Ustawi wa jamii ili naye achukue hatua za juu zaidi.

Amefafanua kuwa wameshatoa agizo la kuwataka madaktari hao waliokuwa katika mafunzo kuondoka katika hosteli waliyokuwa wakiishi kwa gharama za hospitali ya rufaa.

Lyamba Lya Mfipa imefika katika hosteli ya madaktari hao saa  tisa alasiri na kukuta wakiendelea na harakati za kuhamisha mali zao kutoka katika hosteli hiyo na kuelekea mitaani.

Wakati huo huo mwenyekiti wa shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi (TUCTA) Nicholaus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Mbeya amelaani namna inayotumiwa na madaktari kutafuta suluhu ya madai yao.

Alisema yawezekana madai yao ni ya msingi lakini walipaswa kutumia njia ya mazungumzo na hasa kup[itia chama cha wafanyakazi cha TUGHE walicho wanachama na si chama cha kitaaluma wanachokitumia.

BREAKING NEWSSSSSSSSSSSSS

MADAKTARI WALIOGOMA KATIKA HOSPITALI YA RUIFAA MBEYA WATIMULIWA,HIVI SASA WANAHAMISHA MALI ZAO KATIKA HOSTEL WALIYOKUWA WAKIISHI

KWA HABARI ZAIDI ENDELEA KUWA NA LYAMBA LYA MFIPA................

Tuesday, June 26, 2012

KIAMA CHA MADAKTARI WALIOGOMA MBEYA

SERIKALI mkoani Mbeya imetishia kukatisha mikataba ya madaktari watakaoendeleza mgomo mpaka siku ya kesho(Juni 27) ikiwa ni siku tano mfululizo hawajaingia kazini.

Kaimu mkuu wa mkoa wa Mbeya Dk.Norman Fegi ameyasema hayo leo (Juni 26) katika kikao chake na waandishi wa habari ikiwa ni siku ya nne mfululizo tangu baadhi ya madaktari katika hospitali ya Rufaa kuanza mgomo.

Dk.Fegi amesema tangu kuanza kwa mgomo huo serikali ya mkoa kupitia mkuu wa mkoa ambaye kisheria ndiye mwenyekiti wa bodi ya hospitali inayoingia mkataba na madaktari wa mafunzo imeshawaandikia barua za kuwaita ili wafanye mazungumzo lakini jana(Juni 25) hawakufika.

Amesema baada ya kutofika huko mkoa ukawaandikia tena barua kwa kila mmoja wao kujibui ni kwa nini asiwajibishwe na kusisitiza kuwa iwapo mpaka siku ya tano hawatafika kazini mkoa utavunja mkataba na kuwarudisha kwa muajiri yaani wizara husika.

Amesema kwa sasa wamelazimika kuchukua baadhi ya madaktari kutoka vituo vya afya vilivyopo jijini Mbeya na ndiyo wanaendelea kutoa huduma hususani katika kitengo cha upasuaji cha hospitali ya Rufaa ambacho ndicho kimeathiriwa zaidi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa hospitali ya mkoa Dk.Eliuter Samky alisema madaktari waliogoma ni 45 waliopo katika mafunzo na 19 waliosajiriwa lakini wameajiriwa hivi karibuni lakini madaktari bingwa 19 wanaendelea na kazi kama kawaida.

Samky amesema wateja wote waliofika hospitalini hapo tangu kuanza kwa mgomo wameathirika kwa namna moja ama nyingine ikiwa ni kwakupata huduma isiyo katika kiwango ama muda wa kawaida au kisaikolojia.

Amesema tangu kuanza kwa mgomo huo haijatokea kifo lakini wagonjwa 250 wamefikishwa na kulazwa wakati wagonjwa wan je jumamosi walifika 53,jumapili 42 na jumatatu 283.

Amesema siku ya jumapili pia ilitokea ajali ya gari na majeruhi 16 wakafikishwa hospitalini hapo na wote walipata huduma japo si kwa kiwango kilichozoeleka siku zote.

Naye mganga mkuu wa mkoa dokta Seif Mhina alisema mgomo wa madaktari katika hospitali ya rufaa imeongeza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya mkoa hususani akina mama wajawazito waliokwenda kujifungua katika hospitali hiyo kitengo cha wazazi Meta na kukosa huduma ndipo wakaamua kukimbilia hapo.

Mhina amesema wajawazito wanaojifungua katika hospitali ya mkoa wameongezeka kutoka wawili hadi watano kwa siku na kufikia zaidi ya kumi huku wanaopata huduma ya upasuaji wakiongezeka kutoka mmoja kwa siku hadi kati ya watano na kumi.

NAPE AMRUSHIA DONGO LOWASA

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wametakiwa kutochagua viongozi kwa nafasi zao za kifedha wanazozitumia kurubuni wananchi kwa kutoa misaada mingi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye alitoa kauli hiyo leo(Juni 26) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya kauli inayoonekana kumhusu moja kwa moja aliyewahi kuwa Waziri mkuu Edward Lowasa ambaye hivi sasa anaonekana kukimbilia makanisani kwa kuchangia harambee mbalimbali.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo hususani ya kisiasa wamekuwa wakiitaja njia anayoitumia Lowasa kuwa njia ya kujisafisha na kujitengenezea nafasi nzuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Lakini Nape amesema wanaccm wanapaswa wautumie uchaguzi wa chama chao mwaka huu kuhakikisha viongozi wanaomwaga pesa nyingi kwa kutoa misaada wakidhani ni njia nzuri ya kuwashika wapiga kura wanatupwa nje ili kukisafisha chama chao.

Amesema kinachopaswa kufanywa na wanachama ni kuhakikisha wanachagua viongozi walio na uzalendo na chama chao na pia walio na uwezo wa uongozi ili kukijenga chama hicho badala ya kuwapa uongozi watu wanaonyooshewa vidole kila siku na wananchi.

Amewataka vijana hususani walio na elimu kujitosa kupigania uongozi wa chama hicho akisema hatua hiyo itakiwezesha kupata damu change na zilizo na nguvu ya kukiendeleza badala ya kukidumaza.  

Nnauye amekanusha pia kauli za baadhi ya watu wanaokejeli dhana ya Kujivua Gamba wakisema haijafanikiwa kauli aliyosema si kweli kwani dhana hiyo ilibeba mambo mengi ndani yake.

Amesema dhana hiyo ililenga kubadilisura ya chama kwa kuongeza damu change hali inayofanyika hivi sasa ambapo chama kimeanzisha mchakato wa kuwa nam mkoa maalumu kwaajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Amesema pia kuwawajibisha baadhi ya viongozi wasio na sifa tayari mikakati mbalimbali imefanywa na wapo baadhi ya watu walioachia ngazi mbalimbali pamoja na kuivunja kamati kuu iliyokuwa chini ya Yusuf Makamba.

“Kuna watu wamejivua uanachama mpaka ubunge tumeona leo hii mtu anasema dhana ya Kujivua Gamba haijafanikiwa mi nadhani ni uongo.Lakini pia baada ya chama kutoa muda kwa wahusika wajiwajibishe na hawakufanya hivyo sasa tuna vikao mbalimbali vinavyoendelea kpitia kamati za maamuzi na maadili.Huko nako tutatoka na maamuzi mengine” amesema.

Amesema pia katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka huu majina ya wagombea wanaokabiliwa na kashfa mbalimbali hayatarejeshwa hivyo ni vema wanachama hao wasijaze fomu kabisa.

NAPE NNAUYE AZURU CHUO CHA TEKU MBEYA


Monday, June 25, 2012

PROMOSHENI YA GAZETI LA SPOTILEO MBEYA

SAFARI ILIPOANZA KUTOKA OFISI ZA KAMPUNI YA TANZANIA STANDARD NEWSPAPER(TSN) MTAA WA ACASIA MAENEO YA UHINDINI
SHUGHULI IKAANZA KWA BURUDANI KATIKA ENEO LA ILEMI DARAJANI
SAFARI IKAENDELEA KATIKA MAENEO MENGINE IKIWEMO STENDI YA KABWE
WASHINDI WA KUJIBU MASWALI,KUCHEZA MUZIKI WAKAANZA KUPEWA ZAWADI
KWA MATUKIO ZAIDI KUHUSU PROMOSHENI HII KABAMBE ENDELEA KUTEMBELEA LYAMBA LYA MFIPA....................

88 MBARONI KWA UHARIFU MBEYA

WATU 88 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kwa kuhusika na matukio mbalimbali ya uharifu ikiwemo wizi wa mafuta aina ya diseli kwaajili ya kuendeshea mitambo katika ujenzi wa barabara kati ya Tunduma-Sumbawanga.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Athuman Diwani alisema watuhumiwa wa makosa hayo wamekamatwa katika oparesheni maalumu ya kupambana na uharifu iliyoanza Juni 8 mwaka huu na hayo ni matokea ya hadi usiku wa kuamkia leo (juni 25).

Kamanda Amesema katika matukio ya wizi wa diseli jumla ya lita 4,440 zenye thamani ya zaidi ya shilingi laki tisa zilikamatwa na tayari mahakama imeamuru mafuta hayo yarejeshwe yalikoibwa ili yakaendeleze shughuli za ujenzi wa barabara huku watuhumiwa nane wa wizi huo wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Lusekelo Paza,Anyemike Swile,Weiti Mwakatumbula,Michael Mwampamba,Mahona John,Erasto Mwaipaja,Seleman Nasoro na Hassan mrisho.

Amesema katika oparesheni hiyo pia zimekamatwa pikipiki tatu zilizoibwa akizitaja kuwa ni yenye namba T 584 BPU aina ya Star,T 301 BRU aina ya SanLG na T 489 BQU aina ya Sanya.

Mali nyingine ni bunduki mbili zilizotengenezwa kienyeji zinazotumia risasi za Shotgu,risasi nane,Televisheni mbili,kompyuta ndogo(Laptop) mbili,Printa moja,redio tatu,mbili aina ya Sub ufa na moja ya kawaida pamoja na simu nane za aina mbalimbali.

Hata hivyo amesema matokeo hayo mazuri yanatokana na ushirikiano mzuri ulioneshwa kati ya raia wema na askari wa jeshi hilo akisema wananchi walijitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa taarifa juu ya uwepo wa vitendo vya uharifu.

Amewaomba wananchi kuendeleza ushirikiano huo mzuri akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharifu na kuufanya mkoa kuwa na amani na utulivu.

Saturday, June 23, 2012

Meya atoa wiki moja vyoo vya soko la sokoine kujengwa


WATENDAJI  wa idara ya Biashara na Masoko katika halmashauri ya jiji la Mbeya wamepewa muda wa wiki moja kuhakikisha ujenzi wa vyoo katika soko la Sokoine jijini hapo lunakamilika.
 MEYA KAPUNGA (KUSHOTO)AKIFINGIANA NA MWEKA HAZINA WA JIJI
Agizo hilo limetolewa na Meya wa jiji hilo Athanas Kapunga wakati akikabidhi vifaa kwaajili ya ujenzi wa vyoo 12 vyenye thamani ya shilingi 500,776 vilivyotolewa na kampuni ya Marumaru ya jijini hapa.

Kapunga alisema alilazimika kutafuta msaada huo kufuatia wafanyabiashara katika soko hilo kulalamikia hali ya ukosefu wa vyoo na kutishia kutoendelea kulipa ushuru iwapo hawatojengewa vyoo.

“Mnamo Juni 11 mwaka huu wafanyabiashara hawa ambao awali walikuwa katika soko la Uhindini lililoungua waliiandikia halmashauri kuwa tangu wahamie Sokoine hakuna vyoo.Wakasema hatuwezi kuendelea kulipa ushuru wakati hakuna vyoo.Tukaona madai yao ni ya kweli”.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo alifanya ziara kutembelea soko hilo akiwa ameambatana na watendaji wa halmashauri na ndipo walipofikia uamuzi wa kuchukua baadhi ya vibanda vya maduka vilivyokuwa havijakamilika ili kuvitumia kwa ujenzi wa vyoo.

Alisema vibanda vitatu vilivyokuwa vinajengwa kwaajili ya maduka vimechukuliwa na halmashauri na wamiliki watalipwa fidia kwaajili ya ujenzi wa vyoo hivyo.

Hata hivyo alisema kwakuwa ilikuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha ilikuwa vigumu kwa halmashauri kupata fedha mara moja na ndipo ikalmazimu kutembeza bakuli kwa wadau mbalimbali na ndipo kampuni ya Marumaru ikatoa msaada huo.

Alisema tayari amezungumza na mkurugenzi akamuhakikishia kuwa ametenga shilingi milioni kumi kwaajili ya ujenzi wa vyoo hivyo hivyo kinachotakiwa ni kuwalipa wahusika fidia na kuanza ujenzi mara moja.

Alisema mpaka ijumaa ya wiki ijayo ujenzi wa vyoo hivyo unapaswa uwe umekamilika na kuanza kutumika kwakuwa afya ni jambo la msingi kwanza kuliko hata kukusanya ushuru.

HAMASA YAKWAMISHA CHF MBEYA


HAMASA ndogo juu ya mfuko wa  afya ya jamii(CHF) imetajwa kuwa sababu kubwa ya wakazi mkoani Mbeya kutotambua umuhimu wa mfuko huo hivyo hawajiungi.

Hali hiyo imebainika katika semina elekezi kwa waratibu na waandishi wa habari mkoani Mbeya kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) iliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya mkoa.

Meneja wa NHIF kanda ya nyanda za juu kusini Selestin Muganga alisema hamasa bado hali inayosababisha wananchi kutojiunga na CHF kutokana na kukosa elimu juu ya mfuko huo.

Muganga alizitupia lawama halmashauri kwa kutolipa kipaumbele suala la utoaji elimu hiyo kupitia kwa waratibu wa mfuko huo na kusema viongozi wengi wa halmashauri hiyo wanazingatia miradi inayokuwa na maslahi ya moja kwa moja kwao na si ile inayolenga kuinufaisha halmashauri kama huo.

Alihimiza kuwepo kwa hali ya ushindani kwa kila wilaya juu ya mafanikio ya mfuko huo akisema hali hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa halmashauri zilizolala kuona zimebaki nyuma hivyo kuona aibu na muiga mfano wa wenzao wanaofanya vizuri.

Awali akifungua semina hiyo ya siku moja mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya Seif Mhina alihimiza hamasa ya CHF kutolewa katika msimu wa mavuno kama sasa wakati ambao wananchi wengi hususani wakulima wanakuwa na kipato kizuri madala ya masika.

Dokta Mhina alisema wananchi wanatumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya wana familia jambo linaloashiria kuwa elimu juu ya CHF haijawafikia hivyo hawatambui kuwepo kwa uwezekano wa wanakaya kupata matibabu kwa shilingi 10,000 tu kwa mwaka mzima.

“Mkielimisha hakuna mtu atakayebisha.Tatizo ni elimu bado haijawafikia Wananchi wanatumia pesa nyingi sana kwa matibabu ya kawaida tu.Tukiwahamasisha kuwa kaya zao zinaweza kutibiwa kwa shilingi 10,000 kwa mwaka mzima wataridhia tu” alisema

Alisema kujiunga kwa wingi kwa wananchi mkoani hapa kunaweza kusaidia pia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazoikabili huduma ya afya katika zahanati,vituo vya afya na hospitali zilizopo.

Aliutaja mkoa huo kuwa na kaya zipatazo laki sita ambazo zikijiunga zote na CHF zitawezesha kupatikana kwa shilingi bilioni sita na bima ya afya kupitia mpango wa Tele kwa tele ikichangia bilioni sita mkoa utakuwa na jumla ya shilingi bilioni 12 ukiachilia mbali fedha zitakazotoka serikalini ambazo ni za OC shilingi bilioni 2 na za kapu(Busket Fund) bilioni tano.

Alisema fedha hizo zinatosha kabisa kutatua changamoto zote zilizopo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa dawa kwa matumizi ya mwaka mzima,ununuzi wa vifaatiba na ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka NHIF kwa mkoani Mbeya zipo kaya 612,216 na kati ya hizo 17,988 sawa na asilimia 2.94 ndizo zilizojiunga na CHF ambapo wilaya ya Kyela iliyo na kaya 39,542 inaongoza kwa kuwa na kaya 4,447 zilizosajiriwa na Ileje iliyo na kaya 32,153 ni ya mwisho kwa kuwa na kaya 97 pekee zilizosajiriwa.