Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, June 23, 2012

Meya atoa wiki moja vyoo vya soko la sokoine kujengwa


WATENDAJI  wa idara ya Biashara na Masoko katika halmashauri ya jiji la Mbeya wamepewa muda wa wiki moja kuhakikisha ujenzi wa vyoo katika soko la Sokoine jijini hapo lunakamilika.
 MEYA KAPUNGA (KUSHOTO)AKIFINGIANA NA MWEKA HAZINA WA JIJI
Agizo hilo limetolewa na Meya wa jiji hilo Athanas Kapunga wakati akikabidhi vifaa kwaajili ya ujenzi wa vyoo 12 vyenye thamani ya shilingi 500,776 vilivyotolewa na kampuni ya Marumaru ya jijini hapa.

Kapunga alisema alilazimika kutafuta msaada huo kufuatia wafanyabiashara katika soko hilo kulalamikia hali ya ukosefu wa vyoo na kutishia kutoendelea kulipa ushuru iwapo hawatojengewa vyoo.

“Mnamo Juni 11 mwaka huu wafanyabiashara hawa ambao awali walikuwa katika soko la Uhindini lililoungua waliiandikia halmashauri kuwa tangu wahamie Sokoine hakuna vyoo.Wakasema hatuwezi kuendelea kulipa ushuru wakati hakuna vyoo.Tukaona madai yao ni ya kweli”.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo alifanya ziara kutembelea soko hilo akiwa ameambatana na watendaji wa halmashauri na ndipo walipofikia uamuzi wa kuchukua baadhi ya vibanda vya maduka vilivyokuwa havijakamilika ili kuvitumia kwa ujenzi wa vyoo.

Alisema vibanda vitatu vilivyokuwa vinajengwa kwaajili ya maduka vimechukuliwa na halmashauri na wamiliki watalipwa fidia kwaajili ya ujenzi wa vyoo hivyo.

Hata hivyo alisema kwakuwa ilikuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha ilikuwa vigumu kwa halmashauri kupata fedha mara moja na ndipo ikalmazimu kutembeza bakuli kwa wadau mbalimbali na ndipo kampuni ya Marumaru ikatoa msaada huo.

Alisema tayari amezungumza na mkurugenzi akamuhakikishia kuwa ametenga shilingi milioni kumi kwaajili ya ujenzi wa vyoo hivyo hivyo kinachotakiwa ni kuwalipa wahusika fidia na kuanza ujenzi mara moja.

Alisema mpaka ijumaa ya wiki ijayo ujenzi wa vyoo hivyo unapaswa uwe umekamilika na kuanza kutumika kwakuwa afya ni jambo la msingi kwanza kuliko hata kukusanya ushuru.

No comments:

Post a Comment