Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, August 15, 2016

MBARONI KWA KUVAA SARE ZA JWTZ,KUMILIKI RISASI 10 ZA SMG





JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA.



 
                                                                                                  Ofisi ya Kamanda wa Polisi,                                                                                                                                                                                                                                                                                       Mkoa  wa  Mbeya,                                                                                   
Namba ya simu 2502572                                                                                   S. L. P. 260,
Fax - +255252503734                                                                                             MBEYA.
E-mail:-  rpc.mbeya@tpf.go.tz                                                                      

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 15.08.2016.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu na kumakata mali mbalimbali kama ifuatavyo :-

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 07.08.2016 hadi tarehe 13.08.2016 lilifanya misako mbalimbali katika maeneo ya Jiji la Mbeya. Misako hiyo ilifanyika maeneo ya Uyole, Isyesye, Ituha, Iyela, Airport, Kalobe, Nzovwe, Simike, Forest Mpya na Mwanjelwa. Katika Misako hiyo iliyolenga kukomesha vitendo vya wizi na uvunjaji nyumba wakati wa usiku  na mchana, mali na vitu mbalimbali vya wizi vilipatikana pamoja na watuhumiwa 10 kukamatwa kuhusika katika matukio hayo.

Mafanikio yaliyopatikana katika misako:

KUPATIKANA NA RISASI 10 ZA SMG

Mnamo tarehe 14.08.2016 majira ya saa 14:00 mchana huko maeneo ya Sae Jijini Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JOHAN MWASUMBWI (32) Mfanyabiashara na Mkazi wa Sae alikamatwa akiwa na risasi 10 za silaha aina ya SMG kinyume cha sheria.

KUPATIKANA NA SARE ZA JESHI [JWTZ]

Mnamo tarehe 14.08.2016 majira ya saa 14:00 mchana huko maeneo ya Sae Jijini Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JOHAN MWASUMBWI (32) Mfanyabiashara na Mkazi wa Sae alikamatwa akiwa amevaa sare za JWTZ aina ya Kombati [Shati na Suruali].

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.






Kupatikana kwa Gari moja na Bajaji: Katika misako hiyo Bajaji nne zilipatikana zenye namba za usajili MC 999 AKQ, MC 250 ARG, MC 274 AAK na moja iliyokuwa na namba 28 ubavuni  pamoja na gari moja yenye namba ya usajili T.501 CAB aina ya Toyota Noah rangi nyeupe.

Kupatikana kwa Mali za Wizi: Katika misako hiyo, mali na vitu mbalimbali vya wizi vilipatikana ambavyo ni:-
1.     Vyerehani vitatu moja aina ya Butterfly,
2.     Amplifier moja,
3.     Spika tatu kubwa,
4.     Laptop aina ya Samsung,
5.     Laptop aina ya HP G.56,
6.     Laptop aina ya HP 693,
7.     Redio aina ya Panasonic,
8.     Television Flat Screen aina ya Boss inchi 32,
9.     Monitor aina ya HP,
10. Mashine ya Kudarizi ya Umeme,
11. Viti vitatu vya Plastic,
12. Keyboard aina ya ACER na Mouse,
13. Deki aina ya Samsung,
14. Subwoofer moja aina ya Piano,
15. Computer isiyokuwa na jina,

Vitu vingine vilivyopatikana ni pamoja na Simu 10 za aina mbalimbali ikiwemo Tecno, Samsung na Itel, Chaja ya simu ya Smartphone, Earphone 08, Betri za simu 07, Makava ya simu, Flash Disk 03, Katoni za Soda 10, Kreti za bia tupu 06, Kreti za soda 08 na bidhaa mbalimbali za dukani ambazo ni mafuta ya kula, mafuta ya kujipaka mwilini, biskuti, juice, sabuni za unga.


Kukamatwa Watuhumiwa 10 wa Uhalifu: Aidha katika misako hiyo watuhumiwa 10 walikamatwa kuhusika katika matukio ya kupatikana na mali za wizi na kuvunja nyumba usiku na kuiba ambapo majalada ya uchunguzi yalifunguliwa. Watuhumiwa hao ni pamoja na
1. STEPHANO NAZMA (24) Mkulima na Mkazi wa Ituha
2. REGINA BENEDICT (16) Mkulima na Mkazi wa Kalobe
3. SHABANI DAFA (21) Dereva na Mkazi wa Airport
4. GODFREY NDUKWA (22) Mfanyabiashara na Mkazi wa Airport
5. JAMES ENOCK (20) Mkulima na Mkazi wa Airport.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni
6. FIDELIS NGOVANO (32) Mkulima na Mkazi wa Wilaya ya Mbarali
7. ISRAEL LIYAUMI (33) Mkulima na Mkazi wa Madibila Wilayani Mbarali 8. ZEBEDAYO KADUMA (35) Mkulima na Mkazi wa Uyole
9. RIZIKI ALFEO (17) Mkulima na Mkazi wa Ubaruku Wilayani Mbarali na 10. JOSHUA DAUDI (26) Mkulima na Mkazi wa Ubaruku Wilayani Mbarali.





Aidha katika zoezi hilo la Misako lilienda sambamba na ukaguzi wa nyumba za kulala wageni zilizopo katika maeneo ya Uyole, Isyesye, Ituha, Iyela, Airport ya Zamani, Kalobe, Nzovwe, Simike, Forest Mpya na Mwanjelwa. Hali kadhalika wamiliki na wahudumu katika Nyumba hizo za kulala wageni walipewa elimu ikiwa ni pamoja na kuandika majina ya wageni wote katika kitabu cha wageni pamoja na kuweka namba za wahudumu, wamiliki na viongozi wa Jeshi la Polisi kwenye milango kwa ajili ya dharura zitakazojitokeza kwa hatua zaidi.


WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii hasa vijana kuacha tabia ya kutaka kupata mali au utajiri kwa njia ya mkato na badala yake wafanye kazi halali ili wapate kipato halali. Pia anasisitiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa kufanya kazi hama biashara haramu, watumie fursa zilizopo Mkoa wa Mbeya kujitafutia ajira.

Imesainiwa na
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Wednesday, August 3, 2016

WAWILI MBARONI KWA KUHIMIZA OPARESHENI UKUTA

JESHI la polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili wakikabiliwa na tuhuma za kusambaza Ujumbe wenye kuashiria kuhatarisha amani ya nchi kupitia mtandao wa simu hatua inayohusishwa na  Tukio la Oparesheni Ukuta lililopangwa na Chama cha Demokrasia na maendeleo(Chadema) lifanyike Septemba mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari,wanaoshikiliwa ni pamoja na mkazi wa kata ya Isanga jijini Mbeya Moses Mwaifunga(28) na Meshaki Mgaya(28)mkazi wa Ileje mkoani Songwe.

Kadhalika kamanda Kidavashari amesema leo kuwa jeshi hilo linawatafuta watuhumiwa wengine Emma Kimambo na Moris Chanonga ambao amesema popote walipo wanapaswa kujisalimisha wenye katika vituo vya polisi vilivyopo jirani nao.

Anasema watuhumiwa hao wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema,wamehusika kusambaza jumbe mbalimbali unaoashiria kutokubaliana na agizo la serikali la kukataza kufanyika kwa uparesheni Ukuta kwakuwa Jumbe wanazosambaza zinashinikiza wafuasi wa chama hicho kutokata tama bali wajitokeze kushiriki oparesheni hiyo.

Anasema zipo baadhi ya jumbe ambazo watu hao wameonesha nia ya kufanya Oparesheni Ukuta hata kabla ya kuwadia kwa siku iliyokuwa ikitajwa na Chadema yaani Septemba Mosi huku pia nyingine zikionesha wamedhamiria kufanya uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo kuchoma ofisi za Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Kamanda Kidavashari anaonya wafuasi wa Chadema na wananchi wengine kuepuka kusambaza jumbe zinazoonekana kukiuka miiko na maadili ya Utaifa na pale wanapotumiwa kabla ya kuzituma kwa watu wengine wazifute au kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata sheria zilizowekwa na mamlaka huku akisisitiza kuwa hata maandiko matakatifu katika baadhi ya vitabu vya dini yanaeleza kuwa Kila Mamlaka inatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Tuesday, August 2, 2016

WAZIRI ATAKA MIZANI KWENYE NYAMA CHOMA

WAZIRI wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dk Charles Tzeba ameagiza wakala wa vipimo nchini(WMA) kuhakikisha mfumo wa matumizi ya vipimo vya Mizani unazifikia huduma za za kijamii zote ikiwemo nyama choma.

Dk Tzeba ametoa agizo hilo jana alipokuwa akifungua Maonesho ya Wakulima ya Nanenane kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kuhuduriwa na wadau kutoka Halmashauri za mikoa saba ya kanda hiyo.

Alisema miongoni mwa wateja wasionufaika na kile wanachonunua kutokana na kutojua ni kwa kiasi gani wamehudumiwa ni walaji wa nyama hususani zinazochomwa kwakuwa wauzaji hutumia njia ya kukadiria badala ya kuwapimia.

Alisema jambo la kushangaza ni kuwa wauzaji hao wa nyama choma huchukua bidhaa hizo kwenye bucha na machinjio zikiwa zimepimwa lakini wao hawataki kuwatendea haki wateja wao kwa kuwapimia kwa kipimo kinachotakiwa.

“Mteja wa nyamachoma anakadiriwa kwa vipande vya nyama anapewa bei,wakati muuzaji huyu wa nyama choma anaponunua dukani au machinjioni hakubali kutopimiwa.Hapa mteja anaibiwa”

“Lazima mteja ajue ni kiasi gani cha nyama amelipia kiasi cha fedha anachotajiwa.Suala la mazungumzo ya bei lije badae lakini tujue mteja anakula kiasi gani.Na hii yote inatokana na wakala wa vipimo kutotimiza wajibu wake” alisisitiza Tzeba.

Aliitaka WMA kuhakikisha inasimamia kwa uhakika mfumo wa matumizi wa vipimo vinavyotakiwa katika maeneo yote ikiwemo kwenye masoko ya bidhaa kama kuku,nyanya na vitunguu akisema bado mfanyabiashara ananeemeka kwa kuwanyoka wakulima na wateja wake.

Alisema serikali haiku tayari kuona vipimo vya makopo na ndoo vikiendelea kutumika bali kila mtanzania anapaswa awajibike kwa kuhakikisha kwenye eneo lake matumizi ya vipimo sahihi yanazingatiwa ili kuleta usawa katika uchumi.

Monday, August 1, 2016

VIJANA WAHUKUMIWA KWENDA JELA MAISHA KWA UBAKAJI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imewahukumu kutumikia kifungo cha maisha jela vijana wawili wakazi wa wilayani Chunya mkoani hapa kutokana na kosa la ubakaji wa mwanamke mmoja waliyembaka mbele ya watoto wake.

Kadhalika mahakama hiyo imewahukumu vijana hao wawili kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kutokana na kosa la Unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo siku ya tukio walimjeruhi mume wa mwanamke waliyembaka.

Vijana waliokumbwa na vifungo hivyo viwili kutokana na mashitaka mawili yaliyokuwa yakiwakabili ni Ngaru Joseph(32) na Pili Mneme Kapigi(30) wote wakiwa ni wakazi wa wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Awali ilielezwa mahakamani hapo na Mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi Mazoya Luchagula, Mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Alice Mkasela kuwa mnamo Julai 10 mwaka huu majira ya saa nane usiku nyumbani kwa mlalamikaji katika kijiji cha Ukwavila wilayani Mbarali washitakiwa walivamia na kuvunja mlango nyumba ya mkazi huyo aliyekuwa amelala na mke na watoto wao.

Luchagula alisema walipo fanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo washitakiwa hao walimjeruhi baba wa familia kwa kumkata na shoka kichwani  kisha wakapora fedha kiasi cha shilingi 580,000 wakachukua nguo zote za wanafamilia na kisha kumbaka mama wa familia mbele ya mumewe na watoto.

Mwendesha mashitaka huyo alisema wanafamilia hao kupitia mwanga wa taa ya sola waliweza kuwatambua watuhumiwa kabla wazazi hawajapelekwa hospitali ya misheni Chimala walikolazwa kwaajili ya matibabu.

Kufuati makosa hayo Luchagula aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine walio na tabia hizo wilayani hapa na kwingineko nchini.

Akito adhabu kwa washitakiwa,hakimu Mkasela aliyesema ameridhishwa na ushauhi uliotolewa mahakamani hapo na pande zote mbili alisema kwa kosa la kwanza la Unyangaji wa kutumia Silaha washitakiwa watakapswa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kwa kosa la pili la ubakaji watatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwao na watu wengine.

Awali washitakiwa waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu wakisema bado umri wao ni mdogo na wanategemewa na familia zao,maombi ambayo yalitupiliwa mbali na hakimu Mkasela.

TIB CORPORATE BANK YASAIDIA MILIONI 10 MADAWATI MKOANI MBEYA



Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akipokea mfano wa hundi ya sh..mil 10 kwa ajili ya mchango wa madawati mkoani Mbeya


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla akitoa neno la shukurani baada ya kupokea msaada wa fedha sh.mil 10 kutoka kwa Benki ya TIB

Mkurugenzi Mtendaji wa TIB Corporate Bank Frank Nyabundege akipena mkono na Katibu Tawala mkoa wa Mbeya Mariam Mtunguja mara baada ya kukabidhi msaada wa hundi ya sh. mil 10 kwa ajili ya madawati mkoani Mbeya, katikati ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa TIB Corparate Bank Frank Nyabundege mara baada ya kumkabidhi hundi ya Sh.mil 10 kwa ajili ya madawati mkoani Mbeya