Na Joachim Nyambo,Mbeya.
MWANDISHI wa habari wa gazeti la Mtanzania,Gordon
Kalulunga Oktoba 24 mwaka huu aliwekwa kizuizini na kuhojiwa kwa muda wa masaa
manne katika kituo cha Polisi cha Mbalizi yalipo makao makuu ya Wilaya maalumu ya
kipolisi Mbeya vijijini.
Mwandishi wa habari hizi
aliyeambatana na Kalulunga walifika kituoni hapo majira ya Saa nane na Nusu mchana
ambapo awali majira ya saa tano asubuhi,afisa mmoja wa jeshi la polisi
alimpigia simu mwanahabari huyo akimtaka afike kituoni hapo kwaajili ya
kuhojiwa.
Kwa mujibu wa Kalulunga wakati
akipigiwa simu licha ya kuhoji kulikuwa na tatizo gani hata aitwe kituoni,afisa
aliyempigia simu hakumweleza kuna nini na badala yake akamweleza ni masuala ya
kiofisi yasiyoweza kuzungumzwa kupitia simu.
“Baada ya kupigiwa simu niliona
kabla ya kwenda ni vema niwajulishe ndugu,jamaa na rafiki zangu wakiwemo
wanahabari.Ndiyo sababu nimewaiteni ili ikiwezekana kwa walio na nafasi
niongozane nao wakajue kuna nini”alisema Kalulunga baada ya kukutana na
mwandishi wa habari hizi kabla ya kuelekea kituoni.
Zipo tetesi kutoka ndani ya jeshi
hilo kuwa awali maafisa wawili waliagizwa kumtafuta Kalulunga popote alipo ili
akamatwe na kufikishwa kituoni hapo lakini mmoja wa askari walioagizwa
alishauri mwanahabari huyo aitwe kwani hawezi kukaidi kufika.
Mara baada ya kuwasili kituoni
hapo,Kalulunga aliitwa katika chumba cha Ofisi za Upelelezi wa makosa ya jinai
huku akiruhusiwa kuingia na mtu mwingine mmoja ambaye ni mtu wake wa karibu ili
asikilize mahojiano hayo.
Kikao cha mahojiano kianza saa nane
mchana na kumalizika saa 12 jioni,ambapo mara baada ya kutoka Kalulunga alisema
amekumbana na tuhuma za kesi tatu miongoni mwa kesi hizo ikiwa ni kwa nini hivi
karibuni aliandika habari iliyoonesha mapungufu ya jeshi la polisi.
“Wamenihoji kuhusua habari ya tukio
la mtoto aliyesadikika kuzikwa ndani ya nyumba.Baadhi ya maswali ni pamoja na
kwa nini niliandika kuwa polisi waliogopa kuingia ndani ya nyumba hiyo”
“Suala la pili wamehoji ni kwa nini
kupitia mtandao wa kijamii wa Mbalizi Forum tuliweka mjadala wa risiti bandia
za faini zinazotolewa na baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani
wanapowakamata madereva wenye makosa”
Alisema kadhalika kesi ya tatu
ilihusu Mbalizi Forum kuruhusu mjadala wa uwepo wa baadhi ya askari
wanaoendekeza kupokea rushwa hususani wa kitengo cha usalama barabarani huku
pia wakimlaumu ni kwa nini kupitia mtandao huo yanayojadiliwa ni mabaya tu
yanayofanywa na jeshi la polisi lakini mazuri hayatajwi.
Alisema mara baada ya mahojiano
alichoambiwa na afisa aliyekuwa akimhoji ni kuwa jalada hilo litafikishwa juu
hivyo binafsi hakujua ni kupelekwa mahakamani au ala.