Kaimu mwanasheria wa halmashauri ya
jiji la Mbeya Chrispin Kaijage akigawa fomu za kiapo kama njugu nje ya ukumbi hali iliyosababisha hata wasiopaswa kuapishwa kuchukua fomu hizo.
Afisa mwingine wa halmashauri ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akiendelea kugawa fomu za kiapo.
Baadhi ya watu ambao hawakujulikana iwapo walikuwa wajumbe halali wa shughuli ya kuapishwa au la wakizisoma fomu za kiapo mara baada ya kugawiwa.
Wajumbe wakiwa wametawanyika mara baada ya kutoka nje ya ukumbi
Baadhi ya wajumbe wakimshangaa mwanasheria wa jiji kwa kitendo chake cha kugawa fomu za kiapo kama njugu nje ya ukumbi.
Haikujulikana mara moja maboksi haya yalikuwa na nini ndani.Yaliondolewa ukumbini mara baada ya wajumbe kukasirika na kuamua kutoka nje ya ukumbi.
HABARI KAMILI
KATIKA kile kinachodhihirisha uwepo
wa baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakisababisha serikali kuchukiwa na
wananchi kwa kuvurunda kwenye maeneo yao,kaimu mwanasheria wa halmashauri ya
jiji la Mbeya Chrispin Kaijage jana(Januari 5) alivuruga shughuli ya kuwaapisha
wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa.
Shughuli hiyo iliyokuwa ianze majira
ya saa tano asubuhi katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mbeya Day jijini
hapa,shughuli hiyo ilionekana kuanza kuingia dosari tangu mapema na hali hiyo
kuendelea hadi tunakwenda mitamboni.
Dosari ya kwanza ilianza pale
Kaijage aliporuhusu shughuli hiyo kugeuzwa na kuwa mkutano wa kisiasa ukiongoza
na mmoja wa viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) Baraka
Mwakyabula ambaye ni katibu mwenezi wa Chadema Mbeya mjini.
Chini ya mwanasheria huyo,Mwakyabula
alikabidhiwa ukumbi na kuendesha mkutano atakavyo kwani ndiye aliyeweza
kuchagua wajumbe aliotaka wasimame na kuuliza maswali yaliyoikuwa yakijibiwa na
mwanasheria wakati wajumbe wakisubiri viongozi wa halmashauri wafike
kuwaapisha.
Ni wakati huop ambapo baadhi ya
wajumbe walionekana kukerwa na kile kilichoendelea ukumbini hapo kiasi cha
kumtaka mwanasheria aharakishe kuwaleta viongozi wa halmashauri ili waapishwe
na kuondoka ili wakaendelee na shughuli zao nyingine.
Wajumbe walionekana kusononeshwa
zaidi kwa mwanasheria kuendelea kuruhusu shughuli ya kuapishwa ambayo ilikuwa
ikiendelea kuchelewa na kugeuzwa kuwa mkutano wa kisiasa kwani hata katika
kuteua wajumbe wa kuuliza mwongozaji alikuwa akionekana kutoa nafasi zaidi kwa
wajumbe kutoka vyama vya upinzani na kuwanyima fursa wanaotoka CCM.
Siasa hizo zilizokwenda sambamba na
kuchelewa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya jiji Musa Zungiza kulizidi kuingiza
dosari shughuli nzima kwani ilipofika majira ya saa nane kasoro wajumbe
walichukua uamuzi wa kuanza kutoka nje ya ukumbi na hapo kila mmoja akawa
anaongea kwa jazba maneno aliyoona yanafaa.
Wakizungumza kwa jazba nje ya ukumbi
wajumbe hao walisema Mkurugenzi wa Jiji na uongozi wa Halmashauri kwa ujumla umewadharau
na kuwanyanyasa kutokana na kutofuata muda waliokuwa wamewaandikia awali.
Mwakyabula ambaye pia ni mwenyekiti
wa Mtaa wa Mwanjelwa alimgeuka mwanasheria na kuungana na wajumbe wenzake
kulalamika akisema katika barua ya Halmashauri ya Jiji ya kuwaita kuapishwa
ilidai wanapaswa kufika eneo la tukio kuanzia majira ya saa tano asubuhi jambo
ambalo lilitekelezwa kwa wakati lakini wahusika hawakufika katika muda
ulioandikwa.
“Kitendo hiki ni kuonesha dharau kwa
wenyeviti na wajumbe.Haiwezekani wakatuita saa tano asubuhi lakini hadi hivi
sasa ni saa nane mchana hawajafika, hii ni fedheha kubwa hivyo tumekubaliana
zoezi hili liahirishwe kwa leo hadi siku nyingine watakapojipanga” alisisitiza
Mwenyekiti huyo.
Hata hivyo alisema licha ya
kuahirisha kwa shughuli hiyo ya kuapishwa lakini uongozi wa halmashauri ya Jiji
la Mbeya unapaswa kuwaomba msamaha wajumbe kwa kuwadharirisha pamoja na
kuwalipa posho ya siku hata kama zoezi halikufanyika.
Wakati hayo yote yakiendelea wajumbe
walikuwa wamegawanyika ambapo kundi kubwa walikuwa nje na wachache walisalia
ndani ya ukumbi wakiendelea kusubiri na hapo ndipo ilikuja dhana ya kuwa
waliobakia ukumbini ni wanaccm na baadhi ya wajumbe waliokuwa nje wakaanza
kusuka mpngo wa kuingia wawapige ili kuwalazimisha kutoka nje.
Wakati hayo yakiendelea,punde kaimu
mwanasheria alionekana akiwa katika lango kuu(Getini) na akaanza kugawa fomu
kiholela kwa wajumbe waliokuwa jirani hali iliyosababisha wajumbe wote
waliokuwa nje kukimbilia eneo la getini na kuanza kugawana fomu za kiapo kama
njugu.
Wapo wajumbe walioonekana kuchukua
fomu zaidi ya kumi na kuanza kuwagawia wenzao lakini wapo pia ambao walichukua
fomu kwa kiasi hicho na wakaonekana kutoka nje ya geti na kuelekea makwao
pasipo kueleza fomu hizo walikuwa wakizipeleka wapi.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya
wajumbe kuhoji ni kwa namna gani udhibiti wa fomu hizo umewekwa kwakuwa
kulikuwa na uwezekano mkubwa wa fomu kujazwa na mtu asiyestahili.
Kwa upande wake Kaijage, ambaye
alikuwa akiwasihi wajumbe kutulia lakini alishindwa kutoa ufafanuzi juu ya sababu
ya kuchelewa kwa viongozi waliopaswa kuwaapishwa Wenyeviti hao pamoja na
wajumbe wao.
Aidha alipoulizwa na waandishi wa
habari sababu za yeye kuanza kugawa fomu za kiapo kiholela pasipo kufuata
utaratibu huku akianzia barabarani alijibu kuwa yeye sie msemaji bali alifika
kituoni hapo kushuhudia zoezi la kuwaapisha viongozi hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Musa Zungiza, alipofuatwa ofisini
kwake,wanahabari walijibiwa kuwa alikuwa nje ya ofisi katika shughuli za
kuapisha wajumbe na wenyeviti kwenye kanda nyingine na alipotafutwa kwenye simu
yake ya kiganjani kujibu changamoto iliyojitokeza hakuweza kupokea.