Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, January 6, 2015

UAPISHAJI WENYEVITI WA MITAA NA WAJUMBE ULIVYOINGIA DOSARI JIJINI MBEYA

 Kaimu mwanasheria wa halmashauri ya jiji la Mbeya Chrispin Kaijage akigawa fomu za kiapo kama njugu nje ya ukumbi hali iliyosababisha hata wasiopaswa kuapishwa kuchukua fomu hizo.

 Afisa mwingine wa halmashauri ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akiendelea kugawa fomu za kiapo.

 Baadhi ya watu ambao hawakujulikana iwapo walikuwa wajumbe halali wa shughuli ya kuapishwa au la wakizisoma fomu za kiapo mara baada ya kugawiwa.



 Wajumbe wakiwa wametawanyika mara baada ya kutoka nje ya ukumbi

 Baadhi ya wajumbe wakimshangaa mwanasheria wa jiji kwa kitendo chake cha kugawa fomu za kiapo kama njugu nje ya ukumbi.
 Haikujulikana mara moja maboksi haya yalikuwa na nini ndani.Yaliondolewa ukumbini mara baada ya wajumbe kukasirika na kuamua kutoka nje ya ukumbi.



                           HABARI KAMILI
KATIKA kile kinachodhihirisha uwepo wa baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakisababisha serikali kuchukiwa na wananchi kwa kuvurunda kwenye maeneo yao,kaimu mwanasheria wa halmashauri ya jiji la Mbeya Chrispin Kaijage jana(Januari 5) alivuruga shughuli ya kuwaapisha wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa.

Shughuli hiyo iliyokuwa ianze majira ya saa tano asubuhi katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mbeya Day jijini hapa,shughuli hiyo ilionekana kuanza kuingia dosari tangu mapema na hali hiyo kuendelea hadi tunakwenda mitamboni.

Dosari ya kwanza ilianza pale Kaijage aliporuhusu shughuli hiyo kugeuzwa na kuwa mkutano wa kisiasa ukiongoza na mmoja wa viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) Baraka Mwakyabula ambaye ni katibu mwenezi wa Chadema Mbeya mjini.

Chini ya mwanasheria huyo,Mwakyabula alikabidhiwa ukumbi na kuendesha mkutano atakavyo kwani ndiye aliyeweza kuchagua wajumbe aliotaka wasimame na kuuliza maswali yaliyoikuwa yakijibiwa na mwanasheria wakati wajumbe wakisubiri viongozi wa halmashauri wafike kuwaapisha.

Ni wakati huop ambapo baadhi ya wajumbe walionekana kukerwa na kile kilichoendelea ukumbini hapo kiasi cha kumtaka mwanasheria aharakishe kuwaleta viongozi wa halmashauri ili waapishwe na kuondoka ili wakaendelee na shughuli zao nyingine.

Wajumbe walionekana kusononeshwa zaidi kwa mwanasheria kuendelea kuruhusu shughuli ya kuapishwa ambayo ilikuwa ikiendelea kuchelewa na kugeuzwa kuwa mkutano wa kisiasa kwani hata katika kuteua wajumbe wa kuuliza mwongozaji alikuwa akionekana kutoa nafasi zaidi kwa wajumbe kutoka vyama vya upinzani na kuwanyima fursa wanaotoka CCM.


Siasa hizo zilizokwenda sambamba na kuchelewa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya jiji Musa Zungiza kulizidi kuingiza dosari shughuli nzima kwani ilipofika majira ya saa nane kasoro wajumbe walichukua uamuzi wa kuanza kutoka nje ya ukumbi na hapo kila mmoja akawa anaongea kwa jazba maneno aliyoona yanafaa.

Wakizungumza kwa jazba nje ya ukumbi wajumbe hao walisema Mkurugenzi wa Jiji na uongozi wa Halmashauri kwa ujumla umewadharau na kuwanyanyasa kutokana na kutofuata muda waliokuwa wamewaandikia awali.

Mwakyabula ambaye pia ni mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanjelwa alimgeuka mwanasheria na kuungana na wajumbe wenzake kulalamika akisema katika barua ya Halmashauri ya Jiji ya kuwaita kuapishwa ilidai wanapaswa kufika eneo la tukio kuanzia majira ya saa tano asubuhi jambo ambalo lilitekelezwa kwa wakati lakini wahusika hawakufika katika muda ulioandikwa.

“Kitendo hiki ni kuonesha dharau kwa wenyeviti na wajumbe.Haiwezekani wakatuita saa tano asubuhi lakini hadi hivi sasa ni saa nane mchana hawajafika, hii ni fedheha kubwa hivyo tumekubaliana zoezi hili liahirishwe kwa leo hadi siku nyingine watakapojipanga” alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo alisema licha ya kuahirisha kwa shughuli hiyo ya kuapishwa lakini uongozi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya unapaswa kuwaomba msamaha wajumbe kwa kuwadharirisha pamoja na kuwalipa posho ya siku hata kama zoezi halikufanyika.


Wakati hayo yote yakiendelea wajumbe walikuwa wamegawanyika ambapo kundi kubwa walikuwa nje na wachache walisalia ndani ya ukumbi wakiendelea kusubiri na hapo ndipo ilikuja dhana ya kuwa waliobakia ukumbini ni wanaccm na baadhi ya wajumbe waliokuwa nje wakaanza kusuka mpngo wa kuingia wawapige ili kuwalazimisha kutoka nje.

Wakati hayo yakiendelea,punde kaimu mwanasheria alionekana akiwa katika lango kuu(Getini) na akaanza kugawa fomu kiholela kwa wajumbe waliokuwa jirani hali iliyosababisha wajumbe wote waliokuwa nje kukimbilia eneo la getini na kuanza kugawana fomu za kiapo kama njugu.

Wapo wajumbe walioonekana kuchukua fomu zaidi ya kumi na kuanza kuwagawia wenzao lakini wapo pia ambao walichukua fomu kwa kiasi hicho na wakaonekana kutoka nje ya geti na kuelekea makwao pasipo kueleza fomu hizo walikuwa wakizipeleka wapi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wajumbe kuhoji ni kwa namna gani udhibiti wa fomu hizo umewekwa kwakuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa fomu kujazwa na mtu asiyestahili.


Kwa upande wake Kaijage, ambaye alikuwa akiwasihi wajumbe kutulia lakini alishindwa kutoa ufafanuzi juu ya sababu ya kuchelewa kwa viongozi waliopaswa kuwaapishwa Wenyeviti hao pamoja na wajumbe wao.


Aidha alipoulizwa na waandishi wa habari sababu za yeye kuanza kugawa fomu za kiapo kiholela pasipo kufuata utaratibu huku akianzia barabarani alijibu kuwa yeye sie msemaji bali alifika kituoni hapo kushuhudia zoezi la kuwaapisha viongozi hao.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Musa Zungiza, alipofuatwa ofisini kwake,wanahabari walijibiwa kuwa alikuwa nje ya ofisi katika shughuli za kuapisha wajumbe na wenyeviti kwenye kanda nyingine na alipotafutwa kwenye simu yake ya kiganjani kujibu changamoto iliyojitokeza hakuweza kupokea.

No comments:

Post a Comment