Na Joachim Nyambo.
WASWAHILI husema tembea uyaone!Huyasema haya
wakimaanisha unapotembea nje ya mazingira yako ya siku zote utayaona mapya
zaidi ya yale uyaonayo siku zote.Utayaona na kuyajua hata usiyowahi kufikiri
kuwa yapo katika dunia hii.
Hivi karibuni nimeungana na wahenga kutaka name niyajue
yaliyopo katika kijiji cha Igangwe kilichopo katika kata ya Mtanila wilayani
Chunya mkoani Mbeya.Hiki ni kijiji kilichotokana na oparesheni maalumu
zilizofanyika miaka ya 1970 ya kuvunja vijiji vidogo vidogo na kuunda vijiji
vikubwa.Kutoka jijini Mbeya mpaka kilipo kijiji hiki unatembea takribani
kilomita 150 kwa mwendo wa gari.
Nikiwa kijijini hapa mahali ambapo ndipo yalipo
makao makuu ya kata ya Mtanila nilipata wasaa wa kutembelea vitu mbalimbali
viki vikijikita kwenye masuala ya asili ya eneo na pia wakazi.Wakazi wa kijiji
hiki wengi wao ni wa kabila la Wanyekyusa na si Wabungu kama ilivyo kwa maeneo
mengi ya wilaya ya Chunya.Lakini wengi wa wakazi hao walihamia kijijini hapa kivutio
kikubwa kikiwa ni shuguli ya kilimo cha Tumbaku.
Nje kidogo ya kijiji ukiachilia mbali maeneo
yanayotumika kwa shughuli za kilimo,wapo wakazi ambao wao hujishughulisha na
ufugaji.Hawa ni watu wa makabila ya Kisukuma,Wazanaki,Barabaigi na wamang’ati.
Jambo la kwanza lililonishangaza kijijini hapa ni
kuona uoto wa asili uliostawi.Miti mbalimbali ya asili utaiona kijini hapa na sin
je ya kijiji kama ilivyo kwa vijiji vingine.Kinachofanyika hapa ni kila
mwanakijiji anayejenga nyumba yake kutokana mti wowote wa asili ulio nje ya jingo
lake analojenga.Atakata ule tu ulio ndani kwakuwa haiwezekani ndani ya nyumba
kukawa na mti.
Hii inakifanya kijiji hiki kionekana kuwa na nyumba
zilizo chini ya miti mkubwa ya asili na yenye kuleta kivuli kizuuri katika
karibia nje ya kila nyumba wenyeji wakisema kila mji.Haupati shida ya kufuata
kivuli mbali na nyumba uliyofikia au ulipo kwa wakati husika.
Uwepo wa uoto huu wa asili kijijini unapojumuiswa na
uoto wa kupandwa wa miti ya kisasa kama ya miembe unakifanya kijiji hiki
kuonekana katika hali ya kupendeza nay a ukijani kwa kipindi cha mwaka
mzima.Wakati mwingine majira ya usiku ukiwa safarini waweza ukakipita kijiji
hiki pasipokujua kama unapita mahali wanapoishi watu wengi.Hapa niliupenda
utaratibu wa utunzaji miti ya asili.
Misitu ya kijiji hiki haiishii tu kijijini.
Nje ya
kijiji kuna misitu minene zaidi.Vilima vilivyopambwa na miti ya asili ya aina
mbalimbali inalindwa na kutunzwa na kila mkazi wa kijiji hiki.
Takribani kilometa tatu kutoka kijijini upande wa
Magharibi kuna bonde kubwa la mto Lupa.Bonde hili lina historia ya kutisha
kidogo.Wakazi wa kijiji hiki wanasema miaka ya 1970 wakati wa kuanzisha kijiji
cha Igangwe walihamishwa kutoka maeneo mbalimbali walikokuwa wakiishi.Kwenye
bonde hili ndiko walikokuwa wakifuata maji kwaajili ya matumizi kwenye kambi
walizofikia.
Lakini wanawake waliofuata maji kwenye bonde hili
ililazimu wasindikizwe kwakuwa ni eneo lililokuwa pia na wanyama wengi wakiwemo
wakali kama simba.Mara kadhaa walikutana na simba waliokuwa wakijipumzisha kwenye
mawe yaliyopo ng`ambo ya mbuga hiyo.Yawezekana walikuwa wakifanya mawindo kwa
wanyama pia na kufuata maji katika eneo hilo.
Mkazi wa kijiji hiki Hamis Mwandura anasema historia
inaonyesha kuwa ukiachilia mbali wanyama kama swala na tandala ambao hadi leo
wanapatikana kwenye misitu inayozunguka bonde hilo,katika kipindi hicho,wanyama
wengine kama tembo,nyati,Twiga walipatikana kwa wingi.Ilikuwa suala la kawaida
pia kukutana na fisi,chui na nyoka wa aina mbalimbali na wa ukubwa tofauti.
“Ni eneo lililokuwa linatisha hata wakati sie
tunakua.Haikuwa rahisi kuja pasipo kujidhatiti kiulinzi na usalama katika eneo
hili”.anasema Hamisi ambaye kwa sasa mashamba yake hadi kuyafikia ni lazima
avuke bonde hilo.Lakini kwa miaka hiyo wazazi wake ndiyo walikuwa wakikumbwa na
mikasa ya wanyama hao.
Katika bonde hilo,chini kidogo ya eneo lenye mawe
yaliyokuwa mapumziko ya simba nikakutana na bwawa moja kubwa.Bwawa hili ni
maarufu kama Bwawa na Masimba.Kwa sasa maji ya bwawa hili linatumika kumwagilia
vitalu vya miche ya tumbaku kabla ya kwenda kuipandikiza mashambani.Bwawa hili
ni tegemeo kubwa kwa wakulima kwa nyakati za kiangazi kwa kuwa hutunza maji
mengi hata pale mto Lupa unapokuwa umekausha maji yake yote.
Kwa nini bwawa hili liliitwa Bwawa la Masimba?Ni
swali ambalo mtu yeyote angeweza kuuliza.Wenyeji wanasema bwawa hili kwa miaka
ya zamani haikuruhusiwa kulisogelea hovyo.Ni mahala palipotumika kwa matambiko.Hata
wenyeji wa eneo hilo na maeneo ya mbali waliokuwa chini ya himaya ya utawala wa
Chifu Kasaka walifanya tambiko hapo walipoona kuna mambo hayakwenda sawa.
“Hata Kasaka mwenyewe alikuwa akifanyia tambiko
hapa.Alikuwa kila akija hapa lazima mvua kubwa inyeshe na mto Lupa ukafurika
maji” anasema mwenyeji wangu akimaanisha Chifu Kasaka na si huyu Njelu Kasaka
wa sasa ambaye ni mwanasiasa.
Inasemekana katika kipindi hicho ndani ya bwawa hilo
kulikuwa na samaki mkubwa kuliko wote ndani ya mto Lupa.Alikuwa aina ya Kambare
mweusi.Huenda huyu ndiye aliyekuwa akiabudiwa wakati wa matambiko japo hakuna
aliye na uhakika juu ya hilo.
Kambare huyu alikuwa na uwezo wa kusafiri hadi nchi
kavu pale alipoamua.Safari za nchi kavu alizifanya nyakati za usiku kukiwa
kumetulia.Smaki huyu alifanya safari hizi pale alipoamua kutembelea mabwawa
mengine yaliyokuwa jirani wakati ambapo mto Lupa haukuwa na maji.
Inasemekana siku moja akiwa nje ya bwawa lake
hilo,alivamiwa na Simba mkubwa aliyekuwa mawindoni.Inaaminika na wakazi wa eneo
hili mapambano baina ya wawili hao yaani Simba na Samaki huyo mkubwa haikuwa
ndogo.Walipambana kwa muda mrefu.Simba akitumia nyenzo zake yaani kucha na meno
yake lakini Samaki akitumia mfupa wake mkubwa uliokuwa kwenye ubavu wake.
Fainali hiyo inaonekana iliishia kwenye ufukwe wa
bwawa ambapo siku iliyofuata zipo ishara nyingi za ajabu zilijitokeza na
kuwalazimu wakazi kwenda kwenye bwawa hilo kuona nini kilitokea hata kuwepo na
ishara za ajabu kama hizo.Walipofika pembezoni mwa bwawa walishangazwa na kile
walichokikuta.Walikuwa simba mkubwa aliyekufa na pia samaki akiwa amekufa.
Hapo ndipo bwawa hilo lilipobaddilishwa jina na
kuitwa Bwawa la Masimba.Ilikuwa simanzi kubwa kwa wakazi katika miaka
hiyo.Lakini pia huo ndiyo ukawa mwisho wa tumaini lao la kupata majibu ya
matatizo kwa kufanya maombi kwenye tambiko kupitia bwawa hilo.Hadi sasa kila
mmoja anajiendea kwenye bwawa atakavyo na kufanya atakayo japo bado ni eneo la
hatari hususani inapofika wakati wa mvua nyingi kwani viboko na mamba huonekana
kupenda kuishi humo na mabwawa mengine yaliyopo jirani.
Historia ya bwawa hili ilinifanya nizidi kufiatilia
kila nilichokiona kwenye bonde la mto Lupa,eneo la kijiji cha Igangwe.Kaskazini
mwa bwawa hili,takribani mita 150 nikaona miti mikavu iliyopangwa juu ya miamba
iliyochimbiwa chini.Binafsi nilihisi ni eneo flani linalotumika aidha kwa
kutega samaki au wanyama.Kwakuwa ni eneo lililo jirani na mashamba ya Tumbaku
nikajua labda hutumika pia kuanikia Tumbaku!
Juu Mwenyeji wangu Hamis Mwandura akirejesha miti kwenye eneo lake katika daraja la asili.Chini nikiendelea kuhoji juu ya matumizi ya daraja hili.
Ilimbidi mwenyeji wangu acheke kidogo. “Lile ni
daraja!Kama nilivyokueleza wakati wa mvua nyingi hauwezi kuvuka kirahisi huu
mto.Maji huwa mengi mpaka unalifikia daraja hili lazima uvulie nguo zako
kuleeeee!Karibia mita miambili”
“Kwa hiyo unapokuja huku darajani inamaana umefikia
katika maji ya kina kirefu sana.Sasa hapa kwakuwa ndiyo kunapokuwa na mkondo wa
maji ya kasi inatuwezesha kutumia daraja hili ambalo kimsingi nalo huwa
linakuwa limezama lakini mnaiona miti kwa ndani ya maji.Utafanya hivyo wakati
wa kuvuka kwenda shamba na wakati wa kurudi”
“Wakulima wanaovuka mto huu ni sisi tunaokwenda
katika mashamba yaliyopo maeneo ya Kiji,Shaurimoyo na Manyungu.Lakini pia kuna
watu wanaokwenda mpaka kijiji cha Ngwala wanaweza kupita huku lakini kwa
kipindi kama hiki ambacho mvua hazijanyesha kwa wingi na kuujaza mto Lupa.”
“Kwa sasa abiria wanaokwenda kijiji cha Ngwala
kupitia njia hii hutumia usafiri wa pikipiki ambao hulipia shilingi 15,000 kwa
kila mmoja kulipia usafiri huo.Kwa nyakati za mvua nyingi ni vigumu kutumia
usafiri huu kwakuwa kuvuka huu mto inakuwa vigumu” anasema Hamis.
Mwenyeji huyu anasema hatari iliyobakia katika mbuga
hiyo ni uvukaji wa mto wakati wa mvua nyingi.Anasema wapo watu waliowahi kufa
maji mtoni hapa.Ilikuwa katika vpindi tofauti lakini ni wakati mto huo
unapokuwa umefurika kiasi cha mbuga yote kujaa maji.
Mbuga hii imebarikiwa ndugu yangu.Niko katika eneo
hili hili nikaona matanuru mengi na makubwa ya tofali zilizochomwa.Mwenyeji
akanambia kwa sasa wanaitumia mbuga hii kama kiwanda cha kuzalishia
tofali.Anayetaka tofali mbichi atafyatua hapa na zitakuwa imara lakni akitaka
zilizo imara zaidi atafyatua na kuzichoma kabla ya kujengea.Lakini shughuli
zote hizi hufanyika wakati wa kiangazi.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tukihangaika wapi tupate
tofali imara.Hatukujua kama tuna utajiri kiasi hiki.Ni hivi karibuni tu
alihamia jamaa mmoja akitokea huko wilayani Mbozi.Ndiye aliyetufumbua macho na
ndiyo sababu unaona sasa kijiji kinapendeza kwa kujengwa nyumba bora.Hii ni
kutokana na tofali za hapa mbugani” anabainisha.
Baada ya kumaliza maswali yangu nikiwa katikati ya
mbuga,kwa mbaali upande wa pili nikaona kama kuna matanuri mengine,lakini
yaliyoezekwa.Sikuweza kufikiri mara moja kuwa zilikuwa nyumba kwakuwa
zilikwenda juu zaidi ya nyumba za kuishi.Hapo mwenyeji wangu akanambi twende
tufike utajionea mwenyewe.
Nilipofika ndipo nilipobaini hayakuwa matanuri ya
tofali kama yale ya mbugani,wala si nyumba za kuishi.Ni matanuri kwaajili ya
kukaushia tumbaku!Wenyeji wanaita mabani.Yapo ya kisasa nay a kizamani.Ya
kisasa hutumia pia majiko ya kisasa na hutumia kuni chache kuliko mabani ya
kizamani.Hivyo ya kisasa ni rafiki wa mazingira zaidi ya yale ya kizamani
kwakuwa miti inayokatwa kwaajili ya kuni hupungua idadi.
Pamoja na kuelekezwa namna tumbaku inavyokaushwa
kwenye mabani hayo baada ya kuvunwa shambani pia nikafundishwa namna ambavyo
tumbaku huhifadhiwa kabla ya kuuzwa.Lakini ndani ya mabani nikalazimika kuuliza
ni kwa nini sehemu ya njia za moto zimevunjwa,tena inaonekana si kwa bahati
mbaya ni makusudi.
“Hii ni kazi ya wawindaji.Wanalazimika kubomoa njia
hizi kwenye mabani kwakuwa wanapowinda wakitumia mbwa sungura hukimbilia kwenye
haya majiko.Kwa wakati huu ambapo hayatumiko wanyama wadogo kama sungura
huyatumia kama sehemu ya makazi na maficho anapohisi adui.Sasa wawindaji
wakibaini amekimbilia humu wanazima alikoingilia na ndipo wanakuja kumshambulia
humu ndani kwa kubashiri kwenye hizi njia za moto”alisema mwenyeji wangu.
Niliyaona mabani mengi kwakweli.Lakini niliamua
kuutembelea msitu wa asili wa kijiji pia.Huko nikakutana na matunda ya asili
kama yakiwamo nyefi kama wenyeji wanavyoyaita.Yalikuwepo pia matunda pori
mengine mengi,yanayoliwa na yasiyoliwa.Kwakuwa ni msimu wa mvua za mwanzo pia
nikafanikiwa kuuona uyoga pori mkubwa ambayo kwa huku ni toweo kizuri
sana.
Wenyeji walitupikia nasi tukafurahia kitoweo hiki kwa kula na ugali.Tukafurahia
kwa pamoja mazao yam situ wa asili.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Igangwe Gulila Mwakosya
anasema utunzaji endelevu wa misitu ya asili ni chachu ya mafaniko ya wakazi wa
kijiji hicho,kata ya Mtanila na watanzania wote kwa ujumla.Misitu hii inayo
faida kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.Ni katika msitu hu huo ambapo dawa
za asili pia hupatikana.Baadhi ya magonjwa yakiwemo ya matumbo hutibiwa kwa
mgonjwa kutumia dawa kutoka misitu hii.
“Ndiyo sabau hata sisi wakulima wa tumbaku
tunahimizana kuyalinda mazingira yetu.Tunapokata miti kwaajili ya mashamba na
pia kukaushia tumbaku tunahakikisha tunahimizana pia kupanda miti.Na kwa
mashamba tunayoacha kuyalima tunayatunza ili kurejesha uoto wa awali” anasema
Mwakosya ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha msingi cha wakulima wa Tumbaku
katika kijiji cha Igangwe(Igangwe Amcos).
Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Mtanila Venant Lymo
anasema lengo la serikali za vijiji vyote vya kata hiyo ni kuona misitu ya
asili inatunza kwa manufaa endelevu.
Yapo mengine mengi niliyojifunza kijijini
Igangwa,Nafasi haitoshelezi kuyaelezea.Lakini kwa hakika siku nilizokaa
kijijini hapa nilifurahia sana.Nikualike nawe utembelee kijiji hiki ukajionee!
UNAWEZA PIA KUIPATA MAKALA HII KUPITIA GAZETI LA HABARILEO LA NOVEMBA 20,2015.