Naibu katibu mkuu wizara ya Maji mhandisi Ngosi Mwihava akitoa taarifa ya mradi wa tathmini ya maji.
MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amesema kupungua kwa maji ardhini ni miongoni mwa mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Kandoro aliyasema hayo alipofungua warsha ya siku
mbili ya kujadili taarifa ya Mpango wa
pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika bonde la maji
la Ziwa Rukwa inayofanyika jijini Mbeya ikihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka
mikoa ya Mbeya,Rukwa na Katavi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mara nyingi wakulima na
wafugaji wamekuwa wakigombania maeneo yaliyo na maji ya kutosha kwaajili ya
kulishia mifugo au kilimo.
“Haukuti watu wakipigana kwaajili ya jangwa,labda
kama kuna mafuta.Wanapigana kwakuwa kila mmoja anataka eneo lililo na unyevu
linalotesha nyasi.Sasa kadiri maji yanavyopungua ndivyo na migogoro hapa nchini
kati ya wakulima na wafugaji inaongezeka” alisema.
Alisisitiza halmashauri kuhakikisha zinakuwa na sheria
ndogo zitakazowezesha kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuyafanya yawe
endelevu kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.
Kandoro pia alisisitiza ushiriki wa wananchi kwenye
mipango mbalimbali ya utunzaji mazingira akisema wao ndiyo wahusika wakubwa
katika athari zozote zitokanazo na uharibifu unaoendelea kufanyika.
Alisema ni jambo la msingi kila mwananchi mahali
alipo atambue umuhimu wa utunzaji mazingira sambamba na kushiriki katika
mikakati inayowekwa na wadau wa masuala hayo.
Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wizara ya Maji
mhandisi Ngosi Mwihava alisema serikali imejipanga kuhakikisha tahtimini juu ya
uwepo wa maji katika mabonde ya maji zinafanyika ili kuwa na uhakika wa kiasi
hali cha maji kilichopo sambamba na matumizi sahihi.
PICHA KWA HISANI YA KENETH NGELESI
PICHA KWA HISANI YA KENETH NGELESI
No comments:
Post a Comment