Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, January 26, 2012

MWANAFUNZI KIZIMBANI KWA WIZI

MWANAFUNZI wa sekondali ya Iramba mkoani hapa,Christina Nyingi(20) amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa kwa kosa la wizi wa mali yenye thamani ya shilingi milioni 2.

Awali, akisomewa mashitaka na wakili wa serikali Adolf Maganda Mbele ya hakimu mkazi Francis Kishenyi alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa novemba 28mwaka jana katika maeneo ya uhindini jijini hapa.

Maganda alieleza mahakamani hapo   kuwa mshitakiwa novemba 28 mwaka jana maeneo ya uhindini aliiba camera ya digital moja,simu  moja aina ya nokia,magauni mawili,chupa sita za pafyumu na mabegi mawili vyote vikiwa na thamani ya milioni 2 mali ya Mili Maboko.

Mshitakiwa alikana shitaka na kurudishwa rumande  katika gereza la Ruanda jijini hapa,baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kwamba kesi hiyo itatajwa tena febuari 8 mwaka huu.

Wakati huohuo Mkazi wa Manzese Darajani jijini Dar es salaamu amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kujifanya polisi.

Akisomewa  shitaka na wakili wa serikali Adolf Maganda mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa Kussaga Majinge alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa  januari 4 mwaka huu katika maeneo ya iyunga mkoani hapa.

Mshitakiwa alikana shtaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza Masharti  ya dhama, kesi hiyo itatajwa tena febuari 8 mwaka huu.
 Joachim Nyambo, Mbeya Januari 26 2012

Wednesday, January 25, 2012

WANAFAUNZI 1,302WASOTA KUANZA KIDATO CHA KWANZA MBARALIi

WANAFUNZI 1,302 hawajaanza masomo ya kidato cha kwanza wilayani hapa kufuatia uhaba wa vyumba vya madarasa unaozikabili shule za kata walizopangiwa.

Hali hiyo inatokana na wananchi katika kata hizo kugoma kuchangia ujenzi wa vyumba hivyo huku sababu ikitajwa kuwa ni baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kutafuna michango wanayokusanya huku vyumba vinavyohitajika kwa sasa vikiwa ni 32.

Hali hiyo imewekwa bayana na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali Keneth Ndingo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa maji uliopo mjini Rujewa.

Ndingo alisema kuwa upungufu huo wa madarasa ni changamoto kubwa  kwa wilaya na kutoa wito kwa kila kiongozi kuhakikisha anawajibika kutokana na nafasi yake kuhimiza ujenzi wa vyumba hivyo ili watoto waanze masomo.

Alisema  hakuna budi  kuweka mikakati madhubuti ili wanafunzi waliobaki waweze kuanza masomo na kwamba moja ya mkakati mkubwa ni  kuhamasisha uchangiaji kwa wananchi licha kukatishwa tamaa na viongozi wa vijiji na kata.

Alikiri wananchi wamekuwa wagumu kuchangia kutokana na kukata tama hali inayotokana na baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kufuja michango inayotolewa na wananchi ili iweze kusaidia  shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Hata hivyo mwenyekiti huyo hakuweka bayana ni maafisa watendaji na viongozi wa vijiji wangapi waliobainika kutafuna fedha za wananchi na pia ni hatua zipi za kishweria zilizochukuliwa dhidi yao wala kiasi cha fedha kilichobainika kutafunwa.


Saturday, January 21, 2012

Rungwe waunda kamati kufufua CHF

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya imeunda kamati ndogo ya watu 10 itakayoandaa mikakati ya kuhakikisha hamasa ya mfuko wa afya ya jamii CHF inatolewa kwa wananchi ili waweze kujiunga kwa wingi.

Mpango huo unatokana na wilaya kuwa ya kwanza kwa uhamasishaji huko katika miaka ya nyuma lakini kwa sasa inaonekana kushuka kwa kiasi kikubwa hali inayoonekana kusababishwa na kudorola kwa uhamasishaji.

Kamati hiyo iliundwa jana na mkuu wa wilaya Jackson Msome aliyekubaliana na wadau wengine waliohudhuria mkutano wa wakuu wa Idara za halmashauri hiyo wa kupata taarifa za maendeleo ya CHF na pia kujadili mradi mpya wa kuwasaidia wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF.

Msome amesema ili kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi ni lazima mikakati madhubuti iwekwe ikiwemo utoaji elimu kwa wakazi juu ya kuwa na bima itakayowahakikishia huduma ya afya pale wanapopata matatizo ya magonjwa.

Kamati iliyoundwa itakayokuwa chini ya mwenyekiti ambaye ni mganga mkuu wa wilaya hiyo Sungwa Ndagambwene ni pamoja na mwakilishi wa madhehebu ya kidini,ofisi ya michezo,vijana na utamaduni,ofisi ya maendeleo ya jamii,mratibu wa CHF wilaya,meneja wa CHF kanda pamoja na mwakilishi wa mashirika ama vikundi vya wananchi.

Mkuu wa wilaya alisema kamati hiyo itaandaa utaratibu mzima wa jinsi gani hamasa ifanyike ili siku moja wilaya iwe sehemu ya zile zinazotolewa mifano kwa kufanya vizuri tofauti na sasa ambapo mwamko unaonekana mdogo.

Awali akizungumzia sababu za wananchi waliokuwa wamejiunga na mfuko huo kujitoa,mnganga mkuu wa wilaya alisema baadhi walikatishwa tama na kasoro zilizobainika ikiwemo uhaba wa dawa jambo ambalo alisema hivi sasa limewekewa mikakati tofauti na kipindi hicho.

Alisema tatizo jingine lililopunguza idadi ya wanachama wa mfuko ni kujitoa kwa Rungwe Smallholders Tea Growers Association (RSTGA) iliyokuwa akiwalipia wakulima wanachama wakati ikipata faida lakini baada ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ikaelezwa hawapati tena faida.

Wednesday, January 18, 2012

Mbeya City kukipiga na Yanga,Simba na Azam

 
TIMU ya soka ya Mbeya City ya jijini Mbeya iliyopo katika ligi daraja la kwanza inaondoka alhamisi hii kuelekea jijini Dar es salaam kwaajili ya michezo ya kirafiki ikiwa ni katika kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo utakaoanza februari 5 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo(Januari 18) mkurugenzi wa halmashauri ya jiji Juma Iddy amesema ziara hiyo itaiwezesha timu kucheza jumla ya michezo sita ambapo kwa Dar es salaam pekee itacheza michezo mine.

Iddy amesema ikiwa Dar es salaam itacheza na timu tatu za ligi kuu ya Tanzania bara alizozitaja kuwa ni pamoja na mabingwa watetezi timu ya Yanga,Simba pamoja na Azam FC na timu moja iliyopo daraja la kwanza ambayo hakuwa tayari kuitaja.

Amesema baada ya michezo mine timu hiyo itaanza safari ya kurejea jijini Mbeya lakini ikiwa njiani itacheza na timu ya JKT Ruvu ya Pwani na Moro United na iwapo mazungumzo yatafanikiwa itacheza pia na Polisi Tanzania ya mkoani Dodoma.

Amesema timu hiyo kwa kukaa muda mrefu kambini anaamini itafanya vyema katika mzunguko ujao kama ilivyokuwa kwa ule wa awali ambapo hadi unamalizika Mbeya City ilikuwa na jumla ya pointi 13 ikiwa haijapoteza hata mchez o mmoja zaidi ya kutoa sare moja.

Wafanyabiashara wakubwa wanawadanganya wadogo suala la ushuru

Na Joachim Nyambo,Mbeya.

MKURUGENZI wa halmashauri ya jiji la Mbeya Juma Iddy ametoa ufafanuzi juu ya mambo yanayochochea migogoro ya wafanyabiashara wanaogomea ongezeko la ushuru katika masoko ya jijini humo.

Mgogo huo ulianza tangu Januari 16 mwaka huu baada ya wafanyabiashara katika soko la Soweto kugoma wakipinga ongezeko la ushuru walilotangazia na kusababisha soko hilo kufungwa kwa muda na umejkuwa ukizuka katika masoko mengine licha ya kuwepo kwa vikao vya mara kwa mara vinavyoukutanisha uongozi wa halmashauri na wafanyabiashara ili kufikia muafaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo(Januar18) ofisini kwake,Iddy amesema  mvutano huo unasababishwa na mitazamo binafsi walionao wafanyabiashara wanaomiliki vibanda ama maduka madogo wanaotaka waendelee kulipa shilingi 200 sawa na wale wanaouza nyanya na mchicha.

Alisema wafanyabiashara hao wanawashinikiza wale wadogo kwa kuwafukuza ndani ya masoko ili ionekane msimamo wa kupinga ongezeko la ushuru ni la wafanyabiashara wote jambo ambalo  halilengi kuwasaidia wanaozalisha faida ndogo ikilinganisha na wao.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,ongezeko la ushuru na bei za pango la vibanda na maduka linatokana na sheria ndogo mpya iliyopitishwa mwaka jana ikiwa imeridhiwa na wadau wote wakiwemo wafanyabiashara kupitia njia mbalimbali zinazostahili kufuatwa kabla ya sheria kupitishwa.

Amesema sheria hiyo inawataka wafanyabiashara wa bidhaa kama mbogamboga kuendelea kulipa shilingi 200 iliyokuwa ikitozwa kwa wafanyabiashara wote kwenye masoko tangu mwaka 2008,shilingi 300 kwa wanaomiliki vizimba na shilingi 500 kwa walio na vibanda ama maduka madogo ambao huza pia bidha aza viwandani.

Kwa upande wa miuondombinu inayolalamikiwa katika soko la Sido,mkurugenzi huyo amesema halmashauri haiwezi kuwekeza miundombinu ya muda mrefu kwakuwa eneo hilo si mali yake na mkataba wa wafanyabiashara kufanyia shughuli zao hapo utamalizima baada ya ujenzi wa soko la Mwanjelwa kumalizika na wafanyabiashara waliokuwepo awali kurejeshwa hapo.

Monday, January 16, 2012

Maghembe apata kigugumizi suala la kahawa mbichi,alazimika kuheshimu maamuzi ya halmashauri na serikali ya mkoa

Waziri wa Kilimo chakula na ushirika Profesa Jumanne Maghembe amemaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu wilayani Mbozi kuhusu ununuzi wa kahawa mbichi akisema maamuzi ya halmashauri na serikali ya mkoa kukataa ununuzi huo yanapaswa kuzingatiwa.

Profesa Maghembe ametoa tamko hilo leo (Januari 16) wilayani Mbozi katika mkutano ulioshirikisha wadau wa zao kahawa kutoka halmashauri nne za wilaya ya Mbeya vijijini,Ileje,Rungwe na Mbozi.

Mkutano huo uliokuwa na mvutano mkubwa baina ya pande pili ukiwema unaotetea na ule unaopinga ununuzi wa kahawa mbichi ulianza kwa taarifa za maendeleo ya kilimo cha zao hilo ambapo mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbasi Kandoro amesema ununuzi huo unamnyonya mkulima kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Eliki Ambakisye ameilaumu wizara kwa kuendelea kuufumbia macho mgogoro huo ili hali inatambua hakuna sheria wala kanuni ya zao hilo inayoruhusu ununuzi wa kahawa mbichi.

Akijibu hoja hizo na nyingine nyingi zilizotolewa na wajumbe Profesa Maghembe amesema wizara haiwezi kutupilia mbali maamuzi ya halmashauri pamoja na serikali ya mkoa hivyo iwapo vyombo hivyo havikubaliani na ununuzi huo lazima maamuzi yazingatiwe.

Saturday, January 14, 2012

Khanga zakimbiza wajawazito Ileje


WILAYA ya Ileje mkoani Mbeya imetajwa kuwa miongoni mwa wilaya nchini zinazotisha kwa wanawake wajawazito kutojifungulia hospitali na vituo vingine vya afya licha ya kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito.

Hali hiyo ilibainishwa jana na meneja uwezeshaji wa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF Dk.Mathias Sweya katika mkutano wa kupanua uelewa kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje juu ya mradi wa kuwasaidia wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa NHIF na mfuko wa afya ya jamii CHF.

Dk Sweya alitolea mfano kwa kituo cha afya cha Sange kilichopo wilayani hapa ambapo katika mwaka 2011 wanawake 137 walihudhuria klinik kituoni hapo lakini kati yao ni 34 pekee waliojifungua hapo.

Alisema uchunguzi unaonesha kuwa kuwa gharama za vifaa vinavyopaswa kununuliwa kwa mama mjamzito zinachangia kwa kiasi kikubwa wanawake kutojifungulia kituoni hapo.

“Nilikwenda pale Sange nikauliza wao wanataka mama anayekwenda kujifungua aende na dishi pamoja na doti ya khanga mpya,lakini pale Isoko nikakuta wao wanataka aende na doti ya Khanga szilizo safi na si lazima ziwe mpya.Sasa nikapata maswali kwa Sange kama mwanamke hana uwezo nap engine baba aliingia mitini kabla hajanunua doti ya khanga mpya ni vigumu mjamzito akaenda hapo” alisema

Hata hivyo mmoja wa maafisa maendeleo Lucy Mwani akichangia hoja alisema yapo mambo mengi yanayopaswa kuchunguzwa ili kupata sababu ya wajawazito kutohudhuria kliniki ukiachilia mbali gharama akitaja baadhi kuwa ni pamoja na mila potofu.

Mwani alishauri kurejeshwa kwa Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya mama na mtoto (CSPD) akisema uliwezesha kupatikana kwa taarifa za haraka juu ya mama mjamzito na mwenendo wa maisha yake tangu dalili za mimba hadi kujifungua pamoja na changamoto anazokumbana nazo.

Mganga mkuu wa wilaya Dk.Yardi Simkoko alikiri wajawazito wengi kuhudhuria kliniki lakini inapofika siku ya kujifungua hawaendi maeneo husika na kutaja sababu kuwa ni pamoja na wanaume husika kujitoa,wanawake wenyewe kutokuwa wawazi kwa waume zao siku ya kujifungua inapofika.

Akizungumzia suala la wanaume kushiriki kwa karibu katika afya ya mama mjamzito,alisema bado wanaume wilayani hapa wapo nyuma katika jambo hilo hali inayolazimu sasa kuandaa mkakati wa kutoa kadi za mwaliko wa kliniki kwa wanaume.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Esther  Wakali amewataka wadau kwa pamoja kushirikiana ili kuwezesha miradi yote ya afya inayoletwa wilayani humo ili kuboresha viwango vya utoaji huduma kwa wananchi

Thursday, January 12, 2012

KKKT wataka Jamboleo iwalipe milioni 800


Na Joachim Nyambo,Mbeya.

KANISA la Kiinjili la Kilutheri KKKT dayosisi ya Konde limetoa siku saba kwa gazeti la Jamboleo kukanusha habari iliyochapishwa na gazeti hilo ikihusu kanisa kuwatimua wachungaji wawili kwa tuhuma za kujihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya nchini kupitia msamaha wa kodi kwenye uingizaji wa mizigo ya kanisa.

Siku hizo saba zimetolewa na kanila likitaka  gazeti likanushe habari hizo kupitia ukurasa wake wa kwanza na kulipa fidia ya shilingi milioni 800 kwa kuishushia hadhi yake mbele ya jamii na wadau wengine ambao wamepoteza uimani na kanisa hilo.

Kiongozi mkuu wa KKKT dayosisi ya Konde Askofu Israel Mwakyolire ametoa tamko hilo leo (Januari 12) alipokuwa akitoa msimamo wa kanisa kwa waandishi wa habari juu ya habari hiyo iliyochapishwa Januari mosi 2012 katika gazeti hilo.

Askofu Mwakyolire amesema kutotekelezwa kwa maagizo hayo katika muda uliopangwa kutoka siku ya tamko kutapelekea kanisa kufungua shitaka mahakamani ili kuiwajibisha kampuni.

Amesema pia kanisa linamtaka mwandishi wa habari hiyo (Dotto Mwaibale) kujieleza kusudio lake katika kutoa taarifa ya uongo yenye nia na kusudia la kulidharirisha kanisa ama sivyo pia atafikishwa mahakamani kwani hakuna mchungaji yeyote aliyefukuzwa wala kusimamishwa na kanisa.

Mwisho.

Na Joachim