Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, January 14, 2012

Khanga zakimbiza wajawazito Ileje


WILAYA ya Ileje mkoani Mbeya imetajwa kuwa miongoni mwa wilaya nchini zinazotisha kwa wanawake wajawazito kutojifungulia hospitali na vituo vingine vya afya licha ya kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito.

Hali hiyo ilibainishwa jana na meneja uwezeshaji wa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF Dk.Mathias Sweya katika mkutano wa kupanua uelewa kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje juu ya mradi wa kuwasaidia wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa NHIF na mfuko wa afya ya jamii CHF.

Dk Sweya alitolea mfano kwa kituo cha afya cha Sange kilichopo wilayani hapa ambapo katika mwaka 2011 wanawake 137 walihudhuria klinik kituoni hapo lakini kati yao ni 34 pekee waliojifungua hapo.

Alisema uchunguzi unaonesha kuwa kuwa gharama za vifaa vinavyopaswa kununuliwa kwa mama mjamzito zinachangia kwa kiasi kikubwa wanawake kutojifungulia kituoni hapo.

“Nilikwenda pale Sange nikauliza wao wanataka mama anayekwenda kujifungua aende na dishi pamoja na doti ya khanga mpya,lakini pale Isoko nikakuta wao wanataka aende na doti ya Khanga szilizo safi na si lazima ziwe mpya.Sasa nikapata maswali kwa Sange kama mwanamke hana uwezo nap engine baba aliingia mitini kabla hajanunua doti ya khanga mpya ni vigumu mjamzito akaenda hapo” alisema

Hata hivyo mmoja wa maafisa maendeleo Lucy Mwani akichangia hoja alisema yapo mambo mengi yanayopaswa kuchunguzwa ili kupata sababu ya wajawazito kutohudhuria kliniki ukiachilia mbali gharama akitaja baadhi kuwa ni pamoja na mila potofu.

Mwani alishauri kurejeshwa kwa Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya mama na mtoto (CSPD) akisema uliwezesha kupatikana kwa taarifa za haraka juu ya mama mjamzito na mwenendo wa maisha yake tangu dalili za mimba hadi kujifungua pamoja na changamoto anazokumbana nazo.

Mganga mkuu wa wilaya Dk.Yardi Simkoko alikiri wajawazito wengi kuhudhuria kliniki lakini inapofika siku ya kujifungua hawaendi maeneo husika na kutaja sababu kuwa ni pamoja na wanaume husika kujitoa,wanawake wenyewe kutokuwa wawazi kwa waume zao siku ya kujifungua inapofika.

Akizungumzia suala la wanaume kushiriki kwa karibu katika afya ya mama mjamzito,alisema bado wanaume wilayani hapa wapo nyuma katika jambo hilo hali inayolazimu sasa kuandaa mkakati wa kutoa kadi za mwaliko wa kliniki kwa wanaume.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Esther  Wakali amewataka wadau kwa pamoja kushirikiana ili kuwezesha miradi yote ya afya inayoletwa wilayani humo ili kuboresha viwango vya utoaji huduma kwa wananchi

No comments:

Post a Comment