Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, February 27, 2012

BILALI APATA AJALI AKIUAGA MKOA WA MBEYA

MBUNGE wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mbeya,Hilda Ngoye na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Beatha Swai wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwamo kugonga pikipiki na kisha kupinduka mtaroni.
 
 Gari hilo yenye namba  STK 2429 mali ya serikaoli ya mkoa ilikuwa miongoni mwa zile zilizokuwa katika msafara wa kumsindikiza makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dk.Mohamed Gharib Bilali aliyekuwa akielekea mkoani Iringa baada ya kumaliza ziara ya siku tatu mkoani Mbeya.

Sunday, February 26, 2012

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA ZIARA YA MAKAMU WA RAIS DK.MOHAMED GHARIB BILAL MKOANI MBEYA

 Baadhi ya wakazi katika mji mdogo wa Tunduma waliojitokeza kumuona Dk.Bilal alipokwenda kufungua soko kuu la Tunduma
 Kutokana na ufinyu wa eneo ililazimu baadhi kupanda juu ya majengo ili wasipitwe na kile kilichokuwa kikiendelea katika eneo la soko
Ilikuwa nisawa na kuhatarisha maisha yao lakini hawakuwa na namna kutokana na umati mkubwa wa watu waliohudhuria
 Walikuwa karibu kabisa na nyaya za umeme lakini potelea mbali mpaka wafaidi kama wenzao
 Lakini kwa Mbeya vijijini hali ilikuwa Hivi
 Namna mbalimbali ya kushangilia ujio wa kiongozi wao wa kitaifa,
 Hawasemi kidumu chama chetu nooooo wanasema idumu serikali yetu izidi kutuletea mambo mazuri kijijini Kwetu
Je kuvaa nguo hizi kunamaanisha mapenzi ya kweli kwa chama kinachotumia rangi hizi ama ndiyo mtoko wa kwetu.Alijiandaa tu kwaajili ya kutoa burudani.Burudani ambayo ilionekana kupendwa na kila mmoja aliyefika eneo hili
Akiwa jijini Mbeya Dk.Bilal akaweka jiwe la msingi katika hosteli inayoendelea kujengwa

Saturday, February 25, 2012

DK.BILALI AKIWA MBEYA VIJIJINI


 Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mohamed Gharib Bilal akiweka jiwe la msingi katika kituo cha wakulima kilichopo katika kata ya  Tembela Mbeya vijijini
 Akikata Utepe kufungua jengo hilo
Hapa akizungumza na mtaalamu wa uhamilishaji katika kituo hicho

MARY MWANJELWA AKIRI KASI YA CHADEMA INAZIDI YA CCM

 MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Mbeya dk.Mary Mwanjelwa amekitaja chama cha demokrasia na maendeleo Chadema kuwa chama tishio kwa chama chake cha Mapinduzi CCM.
                        
Mbunge Mwanjelwa amesema Chadema ni chama kinachokuja kwa kasi hali inayotoa changamoto kwa wana CCM kujipanga ili kuendana na kasi za chama hicho iwapo inataka kuendelea kushika dola baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Aliyasema hayo katika nyakati na maeneo tofauti alipozungumza na wanajumuiya ya wanawake wanachama wa ccm UWT katika wilaya za Kyela na Rungwe zilizopo mkoani Mbeya.

“Ukweli ni kuwa pasipo kubadilika tutakuwa na wakati mgumu mno.Maana sasa tupo katika mfumo wa vyama vingi na chama kama Chadema mbio zake ni za kasi zinazitutaka tujipange kwelikweli kukilinda chama chetu ”
                    
Mwanjelwa pia alisisitiza kuwa makundi ndani ya CCM kwa kiasi kikubwa yamekiyumbisha chama na pasipo kuondokana nayo hali inaweza ikawa mbaya zaidi.

Aliwasihi wanachama wa chama hicho kuondokana na dhana ya makundi akisema wanachopaswa kukizungumza hivi sasa ni chama ili waweze kuwa na kauli moja itakayokirejeshea heshi yake na si kuendeleza malumbano yasiyo na tija.

Alisema wapo watu wanaoendelea kuyajenga makundi hayo badala ya kuketi na kujadili mikakati ya msingi lakini lengo la watu hao linaonekana ni kujijengea umaarufu wa kisiasa pasipo kujua mzizi wa kujijenga huko utatokana na uimara wa chama chao.

WANAWAKE CCM WATAKIWA KUGOMBEA UONGOZI

WANAWAKE wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Mbeya wamepewa changamoto ya kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama katika uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Katibu wa jumuiya ya wanawake wana ccm mkoani Mbeya Tabu Lugwesa alitoa hamasa hiyo wakati akizungumza na wanajumuiya hiyo katika wilaya za Kyela na Rungwe alipoambatana na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mbeya dk.Mary Mwanjelwa aliyekwenda kukabidhi msaada wa mashine za kutotoleshea vifaranga vya kuku.

Lugwesa alisema kwa miaka mingi wanawake ndani ya chama hicho wamekuwa hawajitokezi kuwania nafasi mbalimbali hali inayotokana na kutojiamioni kuwa wanao uwezo wa kuongoza na kukipa mwelekeo mzuri chama chao kama ilivyo kwa wanaume.

Aliwataka wanawake hao kubadilika kwa kuhakikisha wanachukua fomu na kugombea nafasi katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho ili wao pia waweze kutoa mchango wao kwa kukiongoza chama chao.

Alisisitiza kwa wale watakaogombea kutopakana matope kwakuwa inafaa ifike muda wa wao kusema inatosha wanawake kutajwa na jamii kuwa watu wasiopendana na kutakiana maendeleo.

“Tutasemwa wanawake hatupendani mpaka lini?Tubadilike tuwaonyeshe wanaotusema kuwa tunao uwezo wa  kushirikiana hasa katika hili la uchaguzi ili tuongeze wanawake wengi viongozi ndani ya chama chetu” alisema.

Hata hivyo aliwasihi kuhakikisha wanachagua viongozi walio na uwezo wa kukiongoza chama hususani wale wanaoweza kusimama mbele za watu na kujibu mapigo ya wapinzani akisema lengo la chama ni kupata viongozi wachapa kazi ili kijipange upya.

Alikemea tabia ya baadhi ya wanachama ambao wanapita kwa wenzao na kuanza kupotosha juu ya kanuni za uchaguzi zitakazofuatwa katika uchaguzi wa chama hicho mojawapo ikiwa ni wale wanaosema madiwani hawataruhusiwa kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi huo.

ZIARA YA MAKAMU WA RAIS MBEYA

Ndege ya Makamu wa Rais dk.Bilali ikitua katika uwanja wa ndege wa Mbeya tayari kwa ziara ya siku tatu mkoani Mbeya
Dk.Bilali akisalimia na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi aliyekuwa mmoja wa wenyeji waliofika katika uwanja wa ndege wa Mbeya kumlaki.HAPO CHINI NI

Friday, February 24, 2012

WAFANYABIASHARA SOKO LA SOKOINE JIJINI MBEYA WATISHIA KUGOMA ENDAPO JIJI HAWATAWAJENGEA CHOO

Wafanyabiashara wa soko la sokoine jijini mbeya wametishia kugoma endapo jiji halita wajengea choo kwani tangu wahamie sokoni hapo toka soko kuu la uhindini lilipoteketea kwa moto halmashauri ya jiji haijajenga choo na ushuru wa soko wanachukua kila siku na choo kilichopo ni cha mfanyabiasha wa kuuza pombe na supu uwanjani hapo na kina matundu mawili hivyo hakikidhi hali halisi ya wafanyabiashara hao takribani wanaofikia 800

Hiki ndicho choo kilichopo eneo hilo la soko chenye matundu mawili na kinahudumia zaidi ya watu 800

Thursday, February 23, 2012

HABARI KATIKA PICHA

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Husein Kandoro (Katikati ya waliokaa) akiwa na wanawake wajasiriamali wanaoshiriki semina iliyoandaliwa na shirika la viwango Tanzania TBS
Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania ilipotoa msaada wa mizinga ya kufugia nyuki kwa halmashauri za wilaya za mkoani Mbeya

AUAWA KWA KUENDESHA UBABE KIJIJINI

Mtu mmoja maefariki dunai mkoani Mbeya baada ya kupingwa na wananchi wenye hasira kali wakimtuhumu kuwanyanyasa wananchi wa kijiji cha Halambo Kata ya Halungu wilaya ya Mbozi mkoani hapa.
Tukio hilo limetokea kijijini hapo ambapo wananchi hao walimpiga hadi kumuua mkazi huyo aliyefahamika kwa jina la Imani Msinjili (23), kwa madai kuwa marehemu akilewa huwapiga wananchi hao na kuwaletea vurugu kubwa hali waliiona ni bughudha kwao.

Imeelezwa kuwa majira ya saa tano asubuhi marehemu Msinjili alikuwa amelewa na kisha kuwapiga baadhi ya wananchi ndipo walipomkamata na kuanza kumpiga mpaka pale mauti yake yalipomfika katika eneo hilo la kilabu cha pombe alipokuwa marehemu akinywa.

Hata hivyo Jeshi la Polisi halikuweza kufika eneo la tukio mpaka jana Februari 23, mwaka licha ya kupewa taarifa na maiti iliendelea kuwepoeneo hilo.

Mwandishi wetu alipofanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Advocate Nyombi ili aweze kuthibitisha taarifa za tukio hilo hakuweza kupatikana mara moja.

Aidha kumekuwepo na tabia za baadhi ya wananchi mkoani hapa kuendelea na tabia za kujichukulia sheria mkononi licha ya Jeshi la Polisi na Viongozi wa madhehebu mbalimbali kuendelea kukemea vitendo hivyo viovu vinavyokiuka haki za binadamu.

Wakati huohuo wafanyabiashara wa Kijiji cha Mlowo bado wameendelea na mgomo wa kutolipa ushuru wa biashara na mazao wakidai wanahitaji kuonana na Mkuu wa wilaya ya Mbozi Mheshimiwa Gabriel Kimoro.
Habari na Ezekiel Kamanga.

Wednesday, February 22, 2012

DK.BILAL KUANZA ZIARA MKOANI MBEYA


MAKAMU wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu Mkoani Mbeya kesho kutwa (Feb 24).

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiwa mkoani hapaatak Dk.Bilal atakagua miradi 10 ya maendeleo ikiwemo ile itakayofunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi.

Kandoro alisema makamu huyo wa rais atawasili mkoani hapa majira ya saa 4:00 asubuhi na kulakiwa na mwenyeji wake katika uwanja wa ndege wa Jijini Mbeya.

Amesema baada ya ya kupokea taarifa ya mkoa katika Ikulu ndogo ataelekea wilayani Mbozi atakakozindua miradi miwili na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika kijiji cha Mlowo wilayani hapo.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni soko jipya la kisasa lililojengwa katika mji mdogo wa Tunduma na kuzindua matumizi ya teknolojia ya maabara rafiki katika shule ya Sekondari Vwawa.

“Siku ya pili ya ziara hiyo, Makamu wa Rais atakuwa kwenye wilaya za Mbeya na Mbarali ambako atatembelea miradi minne ya maendeleo katika wilaya hizo”.

“Miradi hiyo ni kuweka jiwe la msingi katika jengo jipya la kisasa la Chama cha kuweka na Kukopa (Saccos) cha Uwamu lililopo Uyole katika Jiji la Mbeya na kuweka jiwe la Msingi katika Hosteli ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya”

“Miradi mingine itakayofikiwa na Makamu wa Rais wilayani Mbarali kuwa ni kukagua ujenzi wa soko la mpunga lililopo Igurusi na kukagua ujenzi wa bwawa la umwagiliaji la Rwanyo”.

Kwa mujibu wa Kandoro, Dk. Bilal atahitimisha ziara yake katika halmashauri ya wilaya ya Rungwe ambako atafungua ofsisi ya umoja wa wakulima wadogo wa chai (RSTGA) Bulyaga, kufungua mradi wa umwagiliaji wa Kisegese na kutembelea shamba darasa la Kasyabone.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Dk.Bilal ataondoka mkoani Mbeya Februari 28 kuelekea mkoani Iringa kuendelea na ziara yake mkoani humo.

 Mwisho.

Sunday, February 19, 2012

UNYAMA ALIOFANYIWA MWANAFUNZI WA TEKU NA ASKARI

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha TEKU kilichopo jijini mbeya Daniel  Godluck Mwakyusa (31) aliuawa na Askari wa Jeshi la Polisi PC Maduhu tarehe 14/02/2012 katika sikukuu  ya wapendanao {valentine day].
Indaiwa Marehemu akiwa na wenzake wanne walikuwa katika starehe ya kawaida kama ilivyokuwa kwa wengine walioipa umuhimu siku hiyo.Wakiendelea na starehe yao pale Univesal Pub Uyole polisi waliokuwa doria walikuta vijana hao wakipata vinywaji ndipo waliwatuhumu kuwa ni majambazi ambapo PC Maduhu alimpiga marehemu risasi mbili kwa kutumia bunduki aina ya [SMG].
Inaelezwa kuwapia marehemu aliporwa fedha taslimu kiasi cha shilingi laki tatu pamoja na simu ya mkononiambayo haikufahamika mara moja aina na thamani yake
Kwa mujibu wa baba mzazi wa marehemu huyo  Bwana Pastory Mwakyusa amesema kuwa anasikitishwa sana na kitendo hicho  kilichotokea kwani mwanawe hakuwa na tabia ya wizi au ujambazi  hivyo ameliomba Jeshi la Polisi kueleza sababu ya kumuua mtoto wake.
Jeshi la Polisi lilitoa usafiri wa gari lenye nambari za usajili T 138 AFK aina ya Coster kwa ajili ya kusafirisha Mwili wa marehemu kwenda katika wilaya ya Kyela kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi wa  daktari kuthibitisha kuwa marehemu ameuwawa kwa risasi.
 
Swali ni je tangu lini jambazi,ama mwizi akagharamiwa na jeshi la polisi namna hiyo?

UBUNIFU ZAIDI KATIKA SHULE YA SANT MARY'S MBEYA

Wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Sant Mary's ya Mbeya wakiimba na kucheza wimbo wa Racing Up kwenye ibada ya kumshukuru mungu kwa ufaulu mzuri wa wanafunzi wa shule hiyo waliofanya mitihani ya kitaifa mwaka jana

MSHINDI NAMBA MOJA SHINDANO LA WANAHABARI MBEYA LA KUONJA BIA

Mshindi wa shindano la Beer Testing lililowashirikisha wanahabari mkoani Mbeya Sada Matiku akikabidhiwa zawadi zake

Kauli ya Dk. Harrison G Mwakyembe juu Ugonjwa wake hii hapa


Dk. Harrison G. Mwakyembe (Mb), NW-UJ
Dar es Salaam
18/02/12
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimelazimika leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi umesababishwa na nini! 
Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:

(i) Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa! 

(ii) Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza. 

(iii) Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!

(iv) ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa magazetini ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe. Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi? 

Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukidhibiti/ kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi na bila aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee kuombeana afya na uhai ili kutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania.

KUONJA BIA NAKO NI KAZI JAMANI ANGALIA

MSHINDI SHINDANO LA WANAHABARI MBEYA LA KUONJA BIA

Mshindi wa tatu katika shindano la kuonja bia lililofanyika mwishoni mwa wiki katika kiwanda cha TBL cha mkoani Mbeya Joachim Nyambo(Miliki wa mtandao huu) akikabidhiwa zawadi yake kutoka kwa Afisa mawasiliano na mahusiano wa kampuni hiyo Edith Mushi.Mshindi wa kwanza wa shindano hilo alikuwa Sada Matiku(Chanel Ten),wapili Patrick Cosisma(Highland Fm)

Friday, February 17, 2012

ZIARA ILIPOANZA KUTEMBELEA KIWANDA



MATUKIO ZAIDI YA WAANDISHI KATIKA KIWANDA CHA TBL MBEYA

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya wanaoshiriki shindano la Beer Testing linalofanyika hivi sasa katika kiwanda cha TBL cha mkoani hapa wakimsikiliza mmoja wa maofisa wa kiwanda hicho 

ZIARA YA WAANDISHI WA HABARI KATIKA KIWANDA CHA TBL MBEYA

 Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya wakipumzika baada ya kufika katika kiwanda cha bia cha TBL mkoani hapa.Lengo la ziara hii ni kushiriki shindano la kujaribu Bia (Beer Testing)
Afisa mawasiliano na mahusiano wa kampuni ya TBL Idith Mushi akiwakaribisha waandishi wa habari tayari kwa ziara ya kutembelea kiwanda na kushiriki shindano la Beer Testing

Thursday, February 16, 2012

BREAKING NEWZZZZZZZZZZZZZ POLISI WADAIWA KUUA

POLISI MBEYA WATUHUMIWA KUUWA KWA KUMCHOMA KIJANA NA SINGE KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI zaid endelea kutembelea blogu hii

23 WA TAIFA STARS WATAKAOIVAA MSUMBIJI

Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Kabla ya kuivaa Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezwa Februari 29 mwaka huu, kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki Februari 23 mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika kwenye uwanja huo huo.
 
Wachezaji wapya walioitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Februari 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni viungo Jonas Gerald (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
 
Kikosi kamili kinaundwa na makipa Shabani Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Juma Jabu (Simba), Stephen Mwasika (Yanga) na Kelvin Yondani (Simba).
 
Viungo ni Jonas Gerard (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe (Simba), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Abdi Kassim (Azam).
 
Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam), Nizar Khalfan (Philadelphia Union, Marekani), Mrisho Ngasa (Azam), Ally Badru Ally (Canal Suez, Misri), Uhuru Selemani (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).

WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATWA RUKWA

                       Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Mgnus Ulungi.
 MAOFISA wa Uhamiaji mkoani Rukwa wamewakamata wahamiaji haramu wawili akiwemo aliyekuwa mkimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi ambaye aliyerejea nchini na kuishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mpanda bila kibali.
Kamanda wa Uhamiaji wa Mkoa wa Rukwa, Wiulson Bambaganya amemtaja mhamiaji huyo haramu kuwa Desiree Sindaigaya (38), ambaye amekamatwa jana akiwa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Katumba baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Kamanda Bambaganya mhamiaji huyo haramu amerejeshwa leo nchini Burundi kupitia kijiji cha Manyovu mkoani Kigoma .
Kamanda huyo wa Uhamiaji amemtaja muhamiaji haramu mwingine kuwa Mohamed Sheikh Mohamed (44) raia wa Kenya mwenye asili ya nchi ya Somalia anadaiwa kuingia nchini na kuishi bila ya vibali vya kusafiria .

Inadaiwa Mohamed amekamatwa jana mchana katika eneo la Lwiche mjini Sumbawanga, baada ya kutoroka akiwa amedhaminiwa mjini Mpanda akihofia mkono mrefu wa Serikali kwa kuingia , kuishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria .


Kwa mujibu wa Kamanda Bambanganya, alipohojiwa mhamiaji haramu huyo amekiri kuingia nchini bila kuwa na kibali cha kusafiria na kwamba aliweza kuishi na kufanya kazi ya upishi kwa zaidi ya miezi mitatu katika hoteli moja mjini Mpanda, hadi hivi karibuni alipokamatwa kufuatia taarifa za siri kutoka kwa raia wema


Kamanda huyo wa Uhamiaji amesema kuwa muhamiahji huyo haramu anatarajiwa kufikishwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyopo mijini Sumbawanga .

VIINGILIO VYA MCHEZO WA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA KATI YA YANGA NA ZAMALEK YA MISRI VIMETAJWA.

 Mwakilishi wa kampuni ya Prime Time Promotions, Balozi Kindamba akionyesha mashine maalum ya kukagua tiketi zitakazotumika.
VIP A= 50,000
VIP B= 30,000
VIP C= 15,000
VITI VYA RANGI YA CHUNGWA (ORANGE) = 10,000
VITI VYA RANGI YA BLUE = 7,000
VITI VYA RANGI YA KIJANI (GREEN) = 3,000
 
 

BREAKING NEWZZZZZZZZZZZZZ BASI LA HAPPY NATION LAPATA AJALI

Basi la kampuni ya Happy Nation lililokuwa likitokea jijini Mbeya kwenda Dar es salaam leo limepata ajali baada ya kuanguka liliposhindwa kuumudu mteremko wa  TAZAMA, maarufu kama Pipeline. 

Abiria waliopanda basi la kampuni ya Nganga Line wanasema watu wamejeruhiwa vibaya ila hakuna vifo. Basi hilo likiwa kwenye mwendo kasi lilitaka kulipita basi la Nganga, lakini kukawa na lori linapandisha mlima huo, ndipo dereva akalazimika kulirudisha nyuma ya basi la Nganga na kuligonga kwa nyuma na kupinduka. Abiria wa basi la Nganga wamesalimika wote. 
 
Habari zaidi endelea kutembelea blogu hii

Wednesday, February 15, 2012

MILA POTOFU CHANZO CHA KUFA WAJAWAZITO MPANDA

IMEELEZWA kuwa mila potofu na ukosefu wa elimu kwa jamii juu ya uzazi salama na wa mpango ni miongoni mwa sababu zinazochangia  ongezeko la vifo vya wajawazito wilayani Mpanda mkoani Rukwa.

Muuguzi mkuu wa wilaya ya Mpanda, Dk.  Pius Buzumalle alisema hayo jana wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa habari yaliyofanyika ofisini kwake, mjini hapa waliotaka kujua kiini cha baadhi vifo vya wajawazito wanaofikishwa katika hospita ya wilaya ya Mpanda.

Alisema kuwa bado jamii imekuwa ikiamini mila potofu zilizopitwa na wakati ambapo wajawazito wengi wamekuwa wakijifungulia kwa wakunga wa jadi ambao hawatambuliki na hawana utaalamu wa kutosha, hivyo  wamekuwa wakisababisha kutokea kwa vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

" utafiti unaonyesha kuwa Wapo wakinamama wenye tabia ya  kwenda kwa waganga wa kienyeji na kuwapatia dawa za miti shamba ambazo zimekuwa zikiwazuru wakati wa kujifungua, hivyo kuwaletea madhara makubwa ikiwamo kupoteza maisha yao na watoto" alisema Dk. Buzumalle.

Aliongeza kuwa pia kutokana ukosefu wa elimu ya uzazi salama kwa wakina mama wengi wajawazito imesababisha baadhi yao kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya na zahanati pindi wanapopata ujauzito hali ambayo imewasababishia kupata matatizo hayo.

Muuguzi mkuu huyo, ametoa maelezo hayo kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusiana na vifo vya akina mama wajawazito  wawili waliofariki katika hospitali ya wilaya ya mpanda hivi karibuni wakati wa kujifungua.

Ambapo amedai kuwa vifo vya akina mama hao vilitokana na sababu tofauti ikiwamo ya mmoja kuchelewa kufikishwa hospitalini na mwingine ambaye alifanyiwa uchunguzi baada ya kifo chake iligundulika kuwa kilitokana na kunywa dawa za miti shamba.

Dk. Buzumalle alieleza kuwa lengo la madaktari na wauguzi ni kuhakikisha kila mama mjamzito anayefikishwa katika hospitali ya wilaya ya mpanda na kwenye vituo vyote vya afya anajifungua salama na si tofauti na hivyo.

MWEKEZAJI SHAMBA LINALOSADIKIWA KUWA LA VIGOGO KIZIMBANI

Mwekezaji wa shamba la Mpunga la Kapunga Rice Project lililopo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kampuni ya Export Trading Group amefikishwa mahakama ya wilaya ya Mbeya kwa makosa mawili tofauti likiwemo kosa la kula njama la kutenda kosa la kuharibu mali na kuharibu mali za wananchi kwa hila.

Mwekezaji huyo amefikishwa mahakamani hapo Februari 14 siku ambayo watanzania waliungana na watu duniani kote kusherehekea siku ya wapendanao kwa makosa hayo yaliyoelezwa kuwa aliyafanya  Januari 12 hadi 14, mwaka huu kwa kutumia ndege ya kunyunyizia dawa ambapo alimwaga sumu katika mashamba ya wakulima zaidi ya 154 wa Kijiji cha Kapunga wilayani humo.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Seif Kulita, Mwendesha mashitaka wa Serikali Griffin Mwakapeje alisema kuwa washitakiwa hao aiwemo Meneja wa shamba hilo Walder Vermaak, Afisa ugani Serger Bekker na Rubani wa ndege Andries Daffe walitenda kosa hilo wilayani humo na kuharibu mazao ya wakulima hekari 489.5.

Mwakapeje alisema kuwa wawekezaji hao wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume na sheria namba 226 (i) cha marekebisho ya sheria ya mwaka 2002 la kuharibu mazao hayo ya Mpunga wa wakulima wanaolima eneo linalojulikana kwa jina la Mpunga moja.

Baada ya mashitaka hayo, Hakimu Kulita alpowauliza washitakiwa hao wote kwa pamoja walikana shitaka hilo ambapo wakili anaowatetea watuhumiwa hao Ladislaus Rwekaza aliomba dhamana kwa wateja wake na hatimaye mahakama ikaridhia kwa Masharti ya kila mtuhumiwa kuwa na mdhamini mmoja mweye mali isiyohamishika isiyopungua Shilingi Milioni kumi.

Aidha Hakimu huyo alitoa sharti kwa watumumiwa hao kuwa mbali na sharti la kuwa na mdhamini mmoja na mali isiyohamishika pia watuhumiwa waliytakiwa kukabidhi hati za kusafiria na kwamba hawapaswi kusafiri nje ya mkoa wa Mbeya na kama watahitaji kusafiri nje ya mkoa wa Mbeya ni lazma wapate kibali cha mahakama hiyo ambapo washitakiwa walitimiza masharti hayo.

Baada ya Masharti hayo watuhumiwa walidhaminiwa na Uwesu Msumi mkazi wa Jijini Dar Es Salaam na kukabidhi hati ya nyumba yenye namba 229 Block J iliyopo Mbezi Jijini Dar es Salaam, Christian Basil Mmas aliyekabidhi hati ya nyumba yenye namba 109 iliyopo Geza Ulole Jijini Dar es Salaam na Sunnil aliyetoa hati namba 254 iliyopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam na kesi hiyo itatajwa tena Machi 6, mwaka huu.
Baadhi ya wananchi walioathiriwa na sumu hiyo wakati ndege ikimwaga mashambani na kushuhudiwa ni pamoja na Michael Shija, Severina Mbwilo, Elikana Nsemwa, Edward Simkoko, Gaidon Peter Ngogo (54), Jailo Esau (22), Jackson Mwandemange  (52), Catherina Shipela (50), Edda Ngosha (35), Julius Isega(50), Ramadhan Nyoni (52)

CCM IRINGA KULIKONI?

JE 2012 NI MWAKA WA CCM NA VITIMBI?
Siku chache baada ya kamanda wa vijana wa CCM mkoani Mbeya Stephen Mwakajumilo kumwaga sumu ya maneno katika jimbo la Mwakyembe Iringa nako CCM ina Mambo.

Habari zisizo rasmi tunaambiwa wakati kesho chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kinakusudia kufanya mkutano wake wa Halmashauri kuu ya mkoa ,wajumbe wa mkutano huo wameonyesha kutofautiana na katibu wa CCM mkoa Bi.Mary Tesha na kupanga kutumia mkutano huo kumweka kitimoto ama kumkataa .

Habari kutoka ndani ya chama hicho mkoani hapo zinadokeza kuwa moja kati ya vikwazo vya CCM kuendelea kukataliwa na wakazi wa Iringa ni kutokana na katibu huyo kufanya kazi kivyake vyake na kutowajali watendaji wengine.

Yasemekana kuwa hata wafanyabiashara na wadau mbali mbali waliokuwa wakichangia chama kwa sasa toka afike katibu huyo wameanza kurudi nyuma na kuwa zipo dalili za CCM mkoa wa Iringa kushindwa vibaya katika chaguzi kutokana na katibu huyo kujijali yeye zaidi kuliko chama na kuomba CCM Taifa kujaribu kufuatilia utendaji kazi wa katibu huyo wa mkoa ambaye wamemfananisha na mfanyabiashara

Tuesday, February 14, 2012

TUPO KIKAZI ZAIDI

Mmiliki wa Blogu hii Joachim Daniel Nyambo(Wa pili kutoka kulia) akiwa na waandishi waandamizi wenzake,Wa kwanza kulia ni Solomon Mwansele(Uhuru na Mzalendo),Kutoka kushoto ni Moses Ng'wati na Hosea Cheyo wa TBC