Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, April 29, 2012

CHUTCU WAFANYA MKUTANO WA 12

 Katibu tawala mkoa wa Mbeya akisoma hotuba ya mkuu wa mkoa huo Abbas Kandoro alipomwakilisha kufungua mkutano wa 12 wa chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Tumbaku wilayani Chunya(CHUTCU)
 

WAKULIMA wa zao la tumbaku wamehimizwa kuanza kujikita katika kilimo
cha mazao mbadala kutokana na zao hilo kuendelea kupigwa vita na
wanaharakati mbalimbali duniani.

Katibu tawala mkoa wa Mbeya Marium Mtunguja amesisitiza hayo kwenye
mkutano wa 12 wa chama kikuu cha ushirika wa wakulima wa tumbaku
wilayani Chunya(CHUTCU).

Mtunguja alisema kauli hiyo hailengi kukataza kilimo cha zao hilo bali
kuanza kuchukua tahadhari kwakuwa hakuna ajuaye nini yatakuwa matokeo
ya hoja zinazojadiliwa na kupiganiwa na wanaharakati wanaopinga
uvutaji wa sigara.

Aliyataja mazao yanayoweza kupewa nafasi na kuleta manufaa makubwa kwa
wakulima kuwa ni pamoja na ufuta unaostawi katika ardhi ya wilaya ya
Chunya,ufuta na alizeti.

Alisisitiza pia CHUTCU kuona uwezekano wa kuanzia chama cha kuweka na
kukopa (Saccos) ili kuwawezesha wanachama kuachana na mikopo iliyo na
riba kubwa kutoaka katika taasisi kubwa za kifedha.

Katibu tawala huyo aliwataka wanaushirika kuhakikisha wanaviimarisha
vyama vyao ili visishuke na kufa kama ilivyotokea kipindi cha miaka ya
nyuma badala yake wajiwekee mikakati ya kuviendelea na kuwa na nguvu
zaidi.

“Tuwe tunajiuliza ilikuwaje vyama vya ushirika vikafa.Sababu zipi.Ni
kutokana na uongozi mbovu uliojikita katika kuchukua mikopo mikubwa na
kuitumia vibaya kinyume na utaratibu sahihi.Sasa tusikubali kurudi
huko.Sasa tusonge mbele”.

Alibainisha kuwa kuendelezwa kwa vyama hivyo kutakuwa chachu ya
mafaniko kwa mtu mmoja mmoja na pia wilaya kwa kukuza uchumi
utakaowezesha kufanikishwa kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo hasa
elimu na makazi bora.


Kwa upande wake mwenyekiti wa CHUTCU Sebastian Mogela alikiri ushirika
kuendelea kuyategemea makampuni ni kuchelewa kupiga hatua kimaendeleo
akisema yapo kwaajili ya kufanya biashara yapate faida na si kutoa
misaada kwa wakulima.

Mogela alisisitiza umuhimu wa chama kikuu hicho kuwa na maofisa ugani
wake ili waweze kusimamia kwa karibu kilimo hicho na kuleta manufaa
zaidi kwa wakulima badala ya kuendelea kutumia wataalamu wa makampuni
yanayonunua tumbaku.

“Haiwezekani tukajitegemea kwa pembejeo pekee wakati wataalamu
wanaosimamia matumizi ya pembejeo hizo wanatoka kwingine.Lazima
usimamizi wake utalenga kuinufaisha kampuni yake na wala siyo sisi”.

No comments:

Post a Comment