Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, September 27, 2013

KASANGA WANYAKUA MILIONI MOJA YA MASHINDANO YA NGOMA ZA ASILI

KIKUNDI cha ngoma cha Kasanga maarufu kama Ing’oma cha wilayani Rungwe kimeibuka mshindi katika mashindano ya ngoma za asili yaliyoandaliwa na kampuni ya bia ya TBL kupitia kiwanda chake cha Mbeya. Mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya chuo cha uhasibu(TIA) jijini Mbeya yalishirikisha vikundi 26 vya Ngoma kutoka wilaya za Mbeya,Rungwe,Kyela,Mbozi,Njombe na Iringa. Kwa ushindi huo kikundi cha Kasanga kilijinyakulia kitisha cha fedha taslimu shilingi milioni moja na kikombe. Nafasi ya msindi wa pili ilikwenda kwa kikundi cha Lipango kutoka kata ya Isansa wilayani Mbozi ambacho kilizawadiwa fedha taslimu shilingi laki tano. Nafasi ya tatu ilikwenda kwa kikundi cha Mbeta kutoka Isyesye jijini Mbeya ambacho kilizawadiwa shilingi laki mbili wakati vikundi vingine shiriki vilipewa kifuta jasho cha shilingi 50,000 kila kimoja. Mkuu wa matukio wa kampuni ya TBL kanda ya Mbeya, Geophray Mwangungulu alisema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha wananchi kupenda ngoma za asili pamoja na utamaduni wao. Mwangungulu alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watanzania kusahau asili zao kutokana na ujio wa sayansi na teknolojia hatua inayohitaji wadau kufikiri namna nzuri ya kuwezesha utamaduni wa makabila ya kiafrika kudumishwa. Alitaja nyimbo na ngoma za asili kuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayoweza kuiwezesha jamii ya kiafrika kuzikumbuka na kudumisha mila zao katika kipindi hiki ambacho tamaduni za kimagharibi zinaonekana kuenea kwa kasi katika mataifa mengi duniani.

Wednesday, September 25, 2013

7 WAJISHINDIA PIKIPIKI ZA AMSHA MAISHA YAKO NA COCA COLA

Mmoja wa washindi wa promosheni ya Amsha maisha na Cocacola inayoendelea Bahati Mapula mkazi wa Ipinda wilayani Kyela akijaribu kuendesha pikipiki aina ya Honda yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 baada ya kukabidhiwa jana akiwa amembeba meneja wa kiwanda cha Cocacola Kwanza Gary Pay.Jumla ya pikipiki saba zilikabidhiwa kwa washindi huku washindi wengine wawili wakikabidhiwa fedha taslimu shilingi milioni moja kila mmoja na wengine wanne wakikabidhiwa laki tano kila mmojaMmoja wa washindi wa promosheni ya Amsha maisha yako na Cocacola inayoendelea mkazi wa Vwawa wilayani Mbozi Alfred Mpepela akipunga mkono kufurahia zawadi ya pikipiki aina ya Honda yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 baada ya kukabidhiwa.Kushoto kwake ni meneja wa kiwanda cha Cocacola Kwanza Gary Pay akifuatiwa na Meneja mauzo na masoko Jaynti Vekaria.Jumla ya pikipiki saba zilikabidhiwa kwa washindi huku washindi wengine wawili wakikabidhiwa fedha taslimu shilingi milioni moja kila mmoja na wengine wanne wakikabidhiwa laki tano kila mmoja

Saturday, September 21, 2013

T.PRISONS YATOSHANA NGUVU NA MTIBWA SUGAR.SHABIKI WAJIKUTA WAKO SOKOINE MBEYA WANASHANGILIA MECHI YA DAR ES SALAAM KATI YA MBEYA CITY NA SIMBA SC

Kwa mara nyingine tena timu ya Tanzani Prisons ya mkoani Mbeya imejikuta ikuibanwa mbavu baada ya kulazimisha sare ya goli 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo baina ya timu hizo uliopigwa kwenye uwanja wa Sokoine. Mtibwa Sugar pasipo kuonesha udhaifu wa kuwa ugenini ndiyo waliotangulia kupata goli lao katika dakika ya 26 kipindi cha kwanza likifungwa na Shaaban Nditi kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Said Mkopi na goli hilo kudumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko. Kipindi cha pili Tanzania Prison wakaonyesha uhai zaidi ya ule wa kipindi cha kwanza kwa kucheza mpira ambao ulionekana kuanza kuwakuna mashabiki wachache waliofika uwanjani hapo na hatimaye mnamo dakika ya 53 Peter Michael akamalizika kazi nzuri iliyofanywa na Jimmy Shoji aliyempa pasi iliyojaa ufundi na kuiandikia timu hiyo goli la kusawazisha. Hata hivyo katika kipindi hicho Tanzania Prisons watapaswa kujilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi za wazi ilizopata ikiwemo ile iliyopatikana mnamo dakika ya 60 ambapo mshambuliaji Jeremiah Juma alibaki na mlinda mlango wa Mtibwa lakini akajikuta anapiga mpira ambao haukuweza kuleta madhara baada ya mlinamlango wa mtibwa kupangua shuti lake. Hata hivyo Mtibwa Sugar nao watapaswa kumshukuru mlina mlango wao Hussein Shariif kwani licha ya safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao kuwa butu pia alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira mingi hususani katika dakika za mwisho za mchezo ambapo Tanzania Prisons ilipiga kambi langoni kwake. Jambo lililokuwa kichekesho kikubwa uwanjani hapo ni kuona watazamaji wengi waliofika uwanjani wakionekana kujikita zaidi katika kusikiliza matangazo ya moja kwa moja ya mchezo kati ya Mbeya City ya jijini hapa na Simba ya Dar es salaam uliopigwa Dar es salaam na kujikuta mara kadhaa wakishangilia kila timu hiyo ilipotangazwa kufanya vizuri na kujisahau kama walikuwa uwanjani hapo kutazama mchezo wa Prisons na Mtibwa Sugar. Hadi kipenga cha mwisho cha mwamuzi Zhacharia Jackob kutoka mkoani Pwani kinapulizwa Tanzania Prisons moja ya Mbeya,Mtibwa Sugar moja.

Saturday, September 14, 2013

KILA MTU ANAHITAJI BURUDANI

DIWANI WA CHADEMA MBARONI AKITUHUMIWA KUFANYA MAPENZI NA MWANAFUNZI

DIWANI wa kata ya Kiwira wilayani Rungwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Laurent Mwakalibure(28) anashikiliwa na polisi akikabiliwa na tuhuma za kufanya mapenzi na mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya msingi Kiwira.

Friday, September 13, 2013

HOMA YA MCHEZO KATI YA MBEYA CITY NA YANGA YAZIDI KUPANDA.MULUGO AAHIDI MILIONI MBILI MBEYA CITY IKISHINDA

Joto la mchezo wa ligi kuu kati ya Timu za Mbeya City na Yanga ya Dar es salaam limeendelea kupanda huku kila upande ukiweka mbinu mbalimbali za ushindi kukabiliana na mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kesho alasiri Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songwe mkoani Mbeya ameahidi kitita cha sh. milioni mbili iwapo timu ya Mbeya City itaishinda timu ya Yanga ya Jijini Dar es salaam. Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari jioni hii Waziri Mulugo alisema kuwa mkakato wake ni kuhakikisha kuwa kila timu itakayowasili mkoani Mbeya inaondoka na kipigo katika michuano ya ligi inayoendelea. Alisema kuwa amedhamiria kuhakikisha timu za Mbeya zinazoshiriki ligi Kuu za Mbeya City na Prison na timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza Kimondo ya Mbozi zote zinapata ushindi mkubwa katika michezo mkoani Mbeya. ''Mbeya City ikiibuka na ushindi nitatoa milioni mbili taslimu kuipongeza, timu ya Prison nayo ikishinda nitatoa shilingi milioni mbili taslimu, nataka timu hizi ziwe mfano na nitahakikisha timu ya Kimondo nayo inapata mafanikio ili mwakani icheze ligi kuu,''alisema. Alisema kuwa dhamira yake ni kuona mkoa wa Mbeya ambao una vipaji vingi vya michezo kuwa katika ramani ya michezo kitaifa na katika dunia na kwamba kwa kutumia nafasi yake kama kiongozi wa serikali atahakikisha timu zote zinazokuja kucheza na timu za Mbeya zinafungwa.

Wednesday, September 11, 2013

AJALI KIJIJI CHA KANONDO SUMBAWANGA

MAITI YA KICHANGA YAOKOTWA KWENYE KITUO CHA MAFUTA

MAITI ya mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja imeokotwa ikiwa imetelekezwa katika mji mdogo wa Tukuyu wilayani Rungwe. Maiti ya mtoto huyo mwenye jinsi ya kike imeokotwa jana(Septemba 10) mwaka huu majira ya saa nane mchana katika mtaa wa Bagamoyo nyuma ya kituo cha mafuta cha Caltex kilichopo mtaani hapo. Kamanda wa polisi mkoani hapa Diwan Athuman amesema leo kuwa mwili huo ulikuwa umeviringishwa kipande cha kitenge na kisha kuwekwa kwenye mfuko wa plastic maarufu kama Rambo. Kamanda Athuman amesema juu ya mfuko huo liliwekwa jiwe hali iliyodhihirisha mama wa mtoto huyo ambaye hajafahamika alimuua mwanaye baada ya kujifungua. Amesema jeshi la polisi linaendelea na msako ili mama wa mtoto huyo aweze kuchukuliwa hatua stahiki kutokana na tukio la kinyama alilotenda.

Tuesday, September 3, 2013

WAPENDEKEZA KUBORESHWA KWA BAADHI YA IBARA ZILIZOPO KWENYE RASIMU YA KATIBA MPYA YA TANZANIA

WAKAZI wialayni Sumbawanga mkoani Rukwa wamependekeza kufanyiwa marekebisho kwa ibara ya 72,ibara ndogo ya 5 na 6 sehemu ya A na B ya rasimu ya katiba mpya ambapo tume imependekea rais anapofariki nafasi yake ichukuliwe na mgombea aliyeshika nafasi ya pili kwa wingi wa kura katika matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani. Wakichangia maoni yao kwenye mdahalo wa kupitia na kujadili rasimu hiyo ulioandaliwa na asasi ya vikundi vya wakulima wadogo wilayani Humo(Umawawa) uliofanyika katika kata ya Kaengesa baadhi ya washiriki wamesema kuwa uwepo wa ibara hiyo unaweza kusababisha mshindi wa pili kwenye uchaguzi husika kufanya njama za kumuua rais kwa tamaa ya kushika madaraka baada ya kifo. Mmoja wa wachangia hoja hiyo Fulgency Songoro amesema amependekeza katiba kutoa fursa ya kufanyika kwa uchaguzi mpya iwapo itatokea rais aliyepo madarakani amefariki dunia akisema hiyo italeta usawa wa kidemokrasia kwa wananchi kutumia masanduku ya kura kuchagua kiongozi wanayemtaka. Songoro pia amependekeza,pamoja na kubaki ikulu wakati wa kampeni za uchaguzi,katiba pia isimpe fursa rasi ya kutoa tamko lolote linalohusiana na uchaguzi badala yake aendelee na majukumu yake kama kawaida.

Monday, September 2, 2013

MTOTO AGONGESHWA UKUTANI AFARIKI DUNIA

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani Mbeya akiwemo la mtoto kugongeshwa ukutani. Kifo cha mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Aines Zacharia mwenye umri wa miezi mine mkazi wa kijiji cha Ivuna wilayani Momba kilitokea Septemba mosi saa saba mchana alipokuwa akiendelea kupata matibabu katika kituo cha afya Kamsamba wilaya hapo. Kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa Barakael Masaki alisema awali kulikuwa na ugomvi kati ya mama wa mtoto huyo aliyemtaja kwa jina la Priscar Willson aliyekuwa amembeba mgongoni na mumewe Steven Cletus. Alisema kufuatia ugomvi huo Cletus alimsukuma mwanamke huyo na ndipo wakajikuta wanamgongesha mtoto ukutani na kumsababishia jeraha kubwa kichwani na ndipo mtuhumiwa alipokimbilia kusikojulikana na anatafutwa. Katika tukio jingine mtu aliyefahamika kwa jina moja la Oscar anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35 amefariki dunia baada ya kudondoka kutoka katika gari. Masaki alisema ajali hiyo ilitokea Septemba mosi saa 4:45 asubuhi maeneo ya Mabatini jijini Mbeya katika barabara ya Meta/stendi kuu na kutaja gari husika kuwa ni namba T 773 BNL iliyokuwa ikiendeshwa na Deston Kabissa(29) mkazi wa Sae jijini hapa. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya na kuwa dereva anaendelea kushikiliwa wakati uchunguzi zaidi juu ya ajali hiyo ukiwa unaendelea.