Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, March 29, 2016

Biashara ya Vileo na hatari ya ngono kwa mabinti Mbeya.

Na Joachim Nyambo.

BIASHARA ya vileo inazidi kushamiri siku hadi siku mkoani Mbeya kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini.Kushamiri kwa biashara hii kunakoendana na kupanuka kwake kunasababisha wafanyabiashara kubuni mbinu mpya kila kukicha.Lengo la ubunifu huu ni kuvutia wateja.

Mkoani hapa mji ulio na bishara kubwa ya vileo ni jiji la Mbeya.Maeneo kama ya Mwanjelwa,Kabwe,Soweto,Ilomba na Sae yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu yanaonekana kuwa na baa nyingi ikilinganishwa na maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.

Ingawa mkoa wa Mbeya unanafasi kubwa ya kuongoza kwa kuwa na makanisa mengi nchini,uwingi wa nyumba hizo za ibada bado haujafikiaa maeneo yanayouza vilevi.Yawezekana unapovuka kanisa moja kabla ya kulikuta jingine utakutana na baa,au Grocery zaidi ya tano mpaka sita.

Uwepo wa maeneo mengi ya kuuza mvinyo unatokana na jiji hili kuwaa moja ya maeneo nchini yenye kupata wageni wengi achilia mbali kipato kizuri cha wakazi wake.Wapo wageni ambao huingia jijini hapa kutoka mikoa mbalimbali nchini kila siku.Wapo pia wageni ambao huingia wakitokea nchi mbalimbali za jirani zikiwemo Zambia,Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Wengi wa wageni hawa ni wafanyabiashara ambao ama huingiza bidhaa kutoka makwao au kuja kuchukua zile zinazozalishwa mkoani hapa yakiwemo mazao ya chakula na biashara.Mazao hayo ni pamoja na Ndizi,Mahindi,Kokoa,Mpunga na Kahawa.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanabainisha kuwa Uwepo wa maeneo mengi ya starehe ni dalili za kukua kwa uchumi wa eneo husika.Hivyo kwa Mbeya kushamiri kwa biashara ya vilevi pia ni kiashiria cha kuwepo kwa uchumi imara na wenye kukua kila kunapokucha.

Lakini biashara ni matangazo!Hapo ndipo wamiliki wa baa,grosery na maeneo mengine ya starehe jijini hapa wamekuwa wakukuna vichwa kila mmoja akitafuta ubunifu utakaowezesha wateja wengi kukimbilia kwake.

Kuweka wahudumu wengi na walio warembo ni moja kati ya ubunifu ulioibuka katika siku za hivi karibuni jijini hapa.Wafanyabiashara za mvinyo wanasema njiaa hii inarahisisha zaidi kuwapata wateja kwakuwa hushawishika na uwepo wa warembo.

“Usione watu wanajaa namna hii ukajiuliza maswali mengi.Ni kweli wengine wanaweza kusema umetumia kizizi na wengine wakasema umeboresha mazingira yako vizuri.Lakini ukweli ni kwamba siku mabinti hawa wakipungua na mauzo yanapungua pia” alisema mmoja wa wafanyabiashara ya mvinyo katika maeneo ya Mwanjelwa aliyeomba kutotaja jina lake wala jila la eneo lake la biashara.

Mmiliki mwingine alisema kutokana na ushindani uliopo wanalazimika kuwafuata mabinti mbali kwakuwa wanaotoka jirani ni wasumbufu ahasa wanapopewa majukumu na mabosi wao.Hivyo inawalazima ama kutuma gari au nauli ili kuwafuata wahudumu.Hasara hutokea pale wanapofika na kulizoea jiji kwani huanza kurubuniwa na wenyeji na kuhamia sehemu nyingine.

Uchunguzi umebaini kuwa kivutio cha wahudumu hawa kwa wateja sit u kuwahudumia vinywaji.Ipo biashara ya ngono pia inayoendelea baina ya pande hizi mbili.Hiki ndicho hasa huwavuta wateja wengi kwenye baa hizi zilizo na warembo wengi.

Unyonge utokanao na kutofahamu haki zao kisheria unatajwa kuwa chanzo cha wahudumu hawa wa kike katika baa nyingi mkoani hapa kugeuzwa watumwa wa biashara ya Ngono.

Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Community Media Organization(Tacomo),linasema limefanya uchunguzi na kubaini hali mbaya kwa wahudumu wa kike katika biashara ya ngono.

Mkurugenzi wa Tacomo, Gordon Kalulunga, anasema kumekuwepo na tatizo kubwa la wasichana wanaofanya kazi kwenye baa kukatiliwa kingono huku msingi mkubwa wa ukatili huo ukijengwa na waajiri wao.Hali hiyo imezidi kuwa mbaya na hatari kwa wafanyakazi hao lakini wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa kwa hofu ya kufukuzwa kazi na usalama wa maisha yao.

"Waajiri wakiwemo wamiliki wa baa na mameneja wamekuwa wakiwalazimisha wahudumu kufanya nao ngono kabla ya kuwapa ajira hizo.Lakini hata mara baada ya kuwaajiri huwalazimisha kufanya ngono na wateja wa baa hizo kwa makubaliano ya wateja hao kulipia kati ya shilingi elfu tano hadi elfu kumi kwa siku fedha iliyopewa jina maarufu la malipo ya kaunta.Malipo haya hayamhusishi binti anayekwenda kutumikishwa katika ngono bali itategemeana huruma ya mtu aliyekwenda naye akiamua kumlipa sawa na asipotaka pia haya” alisema Kalulunga.

“Kibaya zaidi ni kwamba tumebaini uwepo wa biashara ya binadamu ambapo kuna wahudumu wamekuwa mawakala wa kuwanunua wenzao mikoani kwa kuwalaghai kuwa waje Mbeya kufanya kazi za Hoteli na kulipwa fedha nyingi, ahadi ambayo haitimii kwani wakifika hapa wanaishia kutumikishwa kingono kwenye baa wanazoajiriwa" aliongeza Kalulunga.

Mkurugenzi huyo aliitaja mikoa ambayo wasichana wengi wanatolewa huko na kuletwa bmkoani Mbeya kutumikishwa kingono kuwa ni pamoja Singida, Iringa, Njombe na Ruvuma.

“Mkoa wa Singida unaongoza katika jambo hili.Tulichobaini ni kuwa wengi wanadanganywa kwa kuahidiwa mambo makubwa wakiwa makwao.Ndiyo sababu utakutana na mabinti wadogo wanaotoka kwenye mkoa huo wakifanya kazi za uhudumu katika baa za hapa mjini.Wapo pia wanaokuwa wametoroka mashuleni na kuja hapa”

“Ukweli wanapofika hawakutani nay ale walioahidiwa wakiwa nyumbani.Hujikuta wametumbukia kwenye hatari ya ulevi na ukahaba kwa kulazimishwa na waajiri wao”

“Wanajikuta kuhiari utumwa wa kuuzwa kwakuwa wanapofika hupewa chumba kimoja kwaajili ya kulala na kuhifadhi vitu vyao kama nguo.Haijalishi wako wengi kiasi gani.Wengine hupewa godoro na kitanda kimoja ili walale hapo.Wao huviita vyumba hivi Gheto.Siku pekee ambayo binti anaona analala vizuri ni pale anapobebwa na mwanaume kwenda kufanya naye ngono.Kwakuwa watalala wawili tofauti na Gheto anajiona mwenye bahati.Huenda pia akala chakula kizuri zaidi ya wanachokula wenzie Gheto” anasema Kalulunga.

Mkurugenzi huyo anasema ili kukabiliana na hali hiyo,Tacomo wameandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa wahudumu kwa kushirikiana na wadau wengine watakaoona kuna umuhimu wa jambo hili kufanyika, ili kuweza kutoa elimu kwanza ya kujitambua wahudumu hao ili kuwaondolea woga wa kutoa taarifa.

Aliwaomba wadau mbalimbali kuona umuhimu wa kushiriki katika mpango huo huku akivitaja vyombo vya habari kuwa mhimili muhimu utakaowezesha kuikomboa jamii ya wahudumu wa baa.

Kadhalika aliwataka wahudumu wa kike kwenye baa mkoani hapa,kujitokeza kwenye vyombo vya habari na sheria, kutoa malalamiko ya ukatili wa kijinsia hasa rushwa za ngono wanazofanyiwa.

Uchunguzi pia uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini uwepo wa uwezekano mkubwa wa wahudumu hawa kuambukizwa maaradhi kwa njia ya ngono.Wateja wengi huwanunuliwa pombe wahudumu wanaolenga kuondoka nao siku husika.Mara nyingi wawili wote hulewa na wanapofikia uamuzi wa kwenda kufanya ngono uhakika wa ngono salama unakuwa mdogo.

“Kama tunajikuta tumebeba mimba kutokana na wanaume hao hao tunaolewa nao iweje kwa magonjwa.Ni kweli upo uwezekano mkubwa wa kupata pia maambukizi kwakuwa wakati mwingine tunakosa namna ya kujitetea hasa pale mwanaume anapokuwa amekulipia kaunta na umekunywa bia zake” alisema mhudumu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jasmini japo alisema hilo ni jinalake la mjini tu.

“Inafikia wakati Yule anayepata wanaume wengi anaonekana mwenye bahati zaidi ya ninyi wengine.Atakula vizuri,atavaa vizuri,atasuka vizuri na atapendeza zaidi hata tunapokuwa tumeingia kazini.Anakuwa amejitengenezea mtaji mzuri wa kupata mwanaume mwingine aliye na fedha nyingi.Hivyo unapoanza shughuli hii kwa kumpata mwanaume mwenye nazo unakuwa umejipatia mtaji mzuri sana.”alisema dada huyo.

Histori pia inaonesha kuwa mabinti wengi huanza kutumia vilevi wanapowasili jijini hapa na kuanza kazi ya uhudumu.Wakiwa kwao hawatumii na hata ukiwauliza wanakwambia hawakuwahi kutumia kilevi chochote tangu kuzaliwa kwao.

Hatua hii inazua hofu ya kusafirishwa kwa magonjwa ya zinaa kutoka jijini hapa na kuyapeleka katika jamii wanazotoka mara wanapokwenda kwenye mapumziko.Wazazi wengi wa mabinti hawa sambamba na jamii zinazowazunguka wanaamini kuwa ni wafanyakazi katika mahoteli makubwa.Hii ni kwakuwa wengi wa wazazi hawa hawajafika jijini hapa kuona nini watoto wao wanafanya.

Uchunguzi unaonesha waahudumu hawa kulipwa mishahara midogo kutokana na uwingi wao.Anaebaki kutegemea mshahara ni wazi atabakia kuishi maisha magumu na kuwa ombaomba kwa wenzie.Wapo pia wahudumu ambao huwaomba mameneja kuwaruhusu wafanye kazi pasipo kuwalipa.Malipo yao hujilipa wenyewe kutokana na ubunifu wao.Mara nyingi hawa ni wakongwe kwenye biashara hii na wanaona kulipwa ujira kunasababisha waajiri kuwabana.

Halii hii ni changamoto kwa jamii,sit u wanakotoka mabinti hawa.Bali pia maeneo wanayofanyia shughuli zao.Ni wakati kwa mamlaka husika pia kulivalia njuga suala hili na kulitafutia ufumbuzi ili kuokoa kizazi hiki na kijacho.Nasema nihatari kwakuwa biashara hii inaendelea kukua kila siku.

No comments:

Post a Comment