MSANII
wa Muziki wa hip hop laini nchini David Michael Mlope maarufu kama Zola D ameibuka na kuwaponda
vijana wanaofanya mazoezi ya kutunisha misuli akisema wanahatarisha afya zao
kutokana na dawa wanazotumia.
Zola D ambaye pia ni mmoja wa
mabondia nchini alibainisha hayo alipozungumkza na waandishi wa habari
alipokuwa mkoani Mbeya ambapo alisema tabia ya Mapenzi ya jinsia moja ni
miongoni mwa matokeo ya Dawa wanazotumia watunisha misuli ili kutanua misuli
yao kwa haraka.
“Vijana wengi hivi sasa wanatumia
kwa wingi dawa za kutunisha misuli maarufu kama ‘doping’ ili waweze kutanua
misuli yao kwa haraka pale wanapohitaji.Kwa sababu zinazotajwa kuwa ni kutafuta
ajira kama vile ulinzi kwenye kumbi za starehe, ulinzi wa watu maarufu(bodyguard)
na wengine mashindano ya kunyanyua vitu vizito au wakiutafuta utanashati wanatumia
dawa hizi bila kujua madhara yake baadaye” alifafanua Zola D.
Alisema dawa hizo maarufu kwa jina
la Anabolic Steroids husaidia kutunisha misuli ndani ya muda mfupi lakini
madhara yake ni makubwa ambapo mtumiaji huweza kupata magonjwa ya kansa,
kupanuka kwa moyo na kupasua mishipa ya damu inayopelekea kupoteza maisha.
Alisema mbali na madhara hayo pia
vijana wengi hupoteza uwezo wa kufanya mapenzi jambo linalowapelekea
kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutokana na kupoteza nguvu za viungo vya
uzazi inayosababishwa na matumizi ya madawa hayo.
Alibainisha kuwa kutokana na madhara
hayo kwa vijana kupitia kampuni ya Tanzania Streetsworkout ameanzisha aina ya mazoezi ambayo hayahusiani na kwenda gymu
wala kunyenyua vitu vizito mazoezi ambayo yanamlenga kila mtu bila kujali umri
wala jinsia
Alisema mazoezi ni tiba ya magonjwa
mengi hivyo ni muhimu kila mtu akaona umuhimu wa kufanya mazoezi ambayo sio
lazima kunyenyua vitu vizito ilikuwa na misuli mikubwa bali ni kujenga utimamu
wa mwili ili kujiepusha na magonjwa.
Aliongeza kuwa aina hiyo ya mazoezi wanayofundisha
wao ni yale ambayo hufanywa nyumbani, chumbani, ofisini na hata barabarani
ambapo kila mtu anaweza kufanya mazoezi kwa dakika tatu na kuendelea kadri
atakavyojipangia lakini matokeo yake ni makubwa kutokana na mabadiliko
anayoyapata.
Alisema kwa sasa kupitia kampuni
hiyo,wanazunguka nchi nzima lengo likiwa ni kuhamasisha vijana,wazee na watoto
kuacha kutumia dawa za kutunisha misuli na badala yake wajikite kwenye mazoezi
ya kawaida ili kujenga afya zao na hatimaye kujikita katika uzalishaji mali.
No comments:
Post a Comment