Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, March 21, 2016

WATATU WAUAWA KWA KUNYONGWA NA KUCHOMWA MOTO WAKIWA GUEST

WATU watatu wameuawa kwa kunyongwa na kisha miili yao kuchomwa moto katika Nyumba ya kulala wageni iitwayo Mexico Guest House iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya walikokuwa wamepanga vyumba vitatu tofauti.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Mbeya Ahmed Msangi waliouawa wametambuliwa kwa majina waliyoandika katika kitabu cha Mapokezi aliowataja kuwa ni wafanyabiashara Mariam Hassan aliyepanga chumba namba 15 na Abbas Yasini aliyepanga chumba namba 14 na mkulima Tatizo Adam aliyepanga chumba namba 103.

Kamanda Msangi amesema mnamo Machi 19 saa 10 jioni walifika wageni wane katika Guest hiyo kati yao watatu wakiwa wanaume na mwanamke mmoja ambapo walikodi vyumba vitatu na Marium aliingia katika chumba namba 15 akiwa na mwanaume mmoja ambaye hakuandika taarifa zake kwenye kitabu cha orodha ya wageni.

Amesema majira ya saa moja jioni watu hao ambao wote walisema wanatokea Songea mkoani Ruvuma walionekana wakitoka na baadaye waliporejea wakaingia na kukaa chumbani kwa Marium na kufanya maongezi huku wakinywa vinywaji.

Mnamo Machi 20 saa 1:30 asubuhi mtu mmoja aishiye jirani na nyumba hiyo aliona moshi ukitokea kwenye chumba namba 15 alichopanga Mariam na ndipo akawajulisha wahudumu wa gesti hiyo ambao baada ya kwenda kukagua walikuta miili ya watu watatu ikiwa imenyongwa na kasha kuchomwa moto.

Amesema hata hivyo inadaiwa kuwa mapema siku hiyo mwanaume aliyelala chumba namba 15 pamoja na marehemu Mariam ambaye hakuandika taarifa zake kwenye kitabu aliondoka gesti hapo akiwa amebeba ndoo ndogo na begi dogo ambapo aliaga kuwa yeye anasafiri lakini wenzake amewaacha wanaendelea kupumzika.

Kamanda Msangi alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi huku mmiliki wa gesti hiyo Sprian Mtengela anashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano huku akisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Kyela kwaajili ya utambuzi.


No comments:

Post a Comment