Na Joachim Nyambo.
NI miaka mitatu sasa imepita tangu
wakazi wa kata ya Masoko wilayani Mbeya walipochukua uamuzi wa kujenga shule ya
sekondari.Lengo la wakazi hawa ilikuwa kutekeleza adhma ya serikali ya kila
kata kuwa walau na shule moja ya sekondari.
Sekondari ya kata ya Masoko ijulikanayo
kama Shule ya sekondari ya Sasyaka ilianza kujengwa mwaka 2013 lakini mpaka leo
haijaanza kutumika.Kutoanza kufanya kazi kwa shule hii kunasababisha wanafunzi
wanaofaulu katika shule za msingi zilizopo kwenye kata ya Masoko kwenda kuanza
masomo ya sekondari kwenye shule za sekondari za kata za Shisyete na Ilembo.
Hii huwalazimu wanafunzi hao kwenda
kuishi mbali na wazazi wao katika vyumba vya kupanga au kulazimika kutembea
umbari mrefu wa zaidi ya kilometa 20 kwa siku kwenda na kurudi shuleni.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini
Oran Njeza anasema kilio kikubwa cha wakazi wa kata ya Masoko ni kukosekana kwa
shule ya sekondari.
Anasema kutokana na kukosekana kwa
sekondari,wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wamekuwa
wakilazimika kupangiwa shule zilizopo kwenye kata nyingine ikiwemo Ilembo hatua
ambayo huwalazimu kutembeza zaidi ya kilometa 10 kuzifikia shule hiyo hivyo kwa
siku wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 20 kwaajili ya kwenda na kurudi.
“Watoto wanawakati mgumu sana katika
kata hii.Wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 20 kwa siku.Hii inawalazimu
kutumia muda mwingi kutembea na muda mchache mno darasanai.” Anasema Njeza.
Anasema hali ni mbaya zaidi katika
kipindi cha mvua nyingi kwakuwa wanafunzi hufika shuleni wakiwa wamenyeshewa na
mvua na na vivyo hivyo wakati wa kurudi makwao na hivyo kushindwa kushiriki
vipindi darasani ipasavyo.
Wakazi wa kata hii wanasema
wamechoshwa na watotoa wao kwenda kusoma mbali na kata yao.Wamechoshwa na
athari ambazo zimekuwa zikiwakumba watoto hao na familia zao kwa ujumla.Familia
zilizo na watoto wa kike ndizo huathiriwa zaidi.
Fidelia Mwasenga ni mmoja wa wakazi
wa kijiji cha Masoko kilichopo kwenye kata hiyo,Anasema Kukosekana kwa
sekondari kwenye kata yao kunasababisha uduni wa elimu.Ndoto zao ilikuwa kuanza
kunufaika mapema na sekondari wanayoijenga.Sasa siku zinazidi kupita pasipo
matunda tarajiwa kuonekana.
“Sasa shule hii mimi inanikera
kwakuwa najiuliza ni kwa nini inachelewa kufunguliwa?Na hii tunaumia kutokana
na Mazingira ambayo watoto wanasoma.Ni mabaya sana,watoto wanapata mimba humo
njiani,Wengine hawaendi shule inavyostahili kwakuwa wanarubuniwa njiani.”
“Tumelia kwa muda mrefu.Imefikia
wakati mpaka wazazi wanakata tama ya kupeleka watoto wao shule kwakuwa kila
wanapojaribu kuwapeleka hawafikii malengo ya familia kwakuwa wanaishia
njiani.Tunaomba serikali itusikilize ifungue shule yetu” anaomba Fidelia.
Mkazi mwingine Donati Mwalinda
anasema walioathirika si watoto peke yao,wazazi pia wameathirika sana kwakuwa
hawaoni matunda ya michango wanayochangia katika elimu.
“Kwa mfano kipindi hiki cha
mvua,mtoto analowa njia nzima mpaka anafika shuleni.Akifika darasani amelowa
hata mahesabu hawezi kufanya kwakuwa akili haifanyi kazi.Atalazimika kulowa
tena wakati wa kurudi nyumbani mpaka anafika.Taayari kwa familia ni tatizo
kwani kwa kunyeshewa na mvua tayari anaweza kupata magonjwa na kuilazimu
familia kugharamia matibabu.”
“Tulijenga madarasa manne kwa wakati
mmoja mwaka huo huo 2013.Kazi nyingi tumefanya mapaka majengo ya shule hii
kufikia hapa unapoyaona.Kusomba tofali,kuchimba na kusomba mchanga kwa kichwa kutoka
mtoni zote tumefanya.Tukaambiwa tujenge kwanza jengo la utawala.Lakini matokeo
yake tumejenga mpaka jengo la utawala hawataki kufungua shule yetu” anasema mkazi
mwingine Obeid Mwashibanda.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wialayani
hapa Abihudi Fungamtama,anasema kilichocheleweshwa kufunguliwa kwa shule hiyo
ni kutokamilika kwa vigezo vinavyotakiwa.
“Mwenye mamlaka ya kusajiri shule ni
Kamishna wa Elimu na Upo waraka maalumu uliotolewa unaoeleza kuwa ili shule
ifunguliwe lazima ikidhi vigezo ambavyo tumekuwa tukiwaelekeza wakazi wa kata
hii kuvitimiza”anasema Fungamtama.
“Moja unatakiwa kuwa na vyumba vya
madarasa angalau vya kutosha wanafunzi wa miaka miwili kwa maana ya kidato cha
kwanza na cha pili kwa mikondo miwilimiwili hivyo kunatakiwa kuwepo na madarasa
angalau manne.Lakini pia Miundombinu kwa maana ya Nyumba za walimu,maji na eneo
ambalo kwa kijijini ni hekta tatu.”
“Kwa shule hii kwa upande wa eneo
inalo la kutosha.Tatizo kubwa ni kwamba hakuna nyumba za walimu na pia maji
hayaklo jirani na shule.Pia hakuna samani kwa maana ya meza na viti.Jengo la
utawala halijakamilika na pia hakuna vyoo”
Afisa huyu anasema kutokamilika kwa
vigezo hivyo kwa kipindi cha nyuma kulitokana na kutojitoa kwa wananchi katika
michango mbalimbali ya ujenzi kama
ilivyohitajika.Uongozi wa kata hiyo ulihamasisha wananchi kutochangia ujenzi
huo ukisema serikali ina jukumu la kutekeleza jambo hilo tofauti na uongozi
uliopo hivi sasa ambao umeonesha nia ya kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye
mikakati ya kujiletea maendeleo.
“Kwa kasi ninayoiona hivi sasa nina
amini mwakani shule hii inaweza ikafunguliwa.Na sisi kama halmashauri kama
ilivyokuwa huko nyuma tutaendelea kushiriki kwa karibu kushauri ili ikamilike
kwa wakati ili angalau mwaka kesho shule iweze kupata usajiri” anasema afisa
huyo.
Lakini tama ya mbunge wa jimbo hili
ni kuona shule hii inafunguliwa haraka na watoto kuanza masomo shuleni hapo.Nia
ni kuwaondolea adha wanafunzi huku pia akisema atahakikisha ujenzi wa Hosteli
shuleni hapo unafanyika kwa haraka ili wanafunzi wa kike waishi jirani na shule
yao kuepuka vishawishi vya wanaume wa mitaani.
“Nilianza kuja shuleni hapa hata
kabla sijawa mbunge.Nikiwa Kamanda wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM)
nilifika mara kadhaa hapa hivyo natambua haja ya wakazi wa kata hii juu ya
sekondari.Nitahakikisha ninafanya kila linalowezekana kukamilisha jambo hili
kwa wakati”anasisitiza Njeza.
Nia ya mbunge huyu imejidhihirisha
hivi karibuni pale alipoandaa harambee ya kuchangia sekondari hii ya Masoko ili
kukamilisha ujenzi wake.Katika harambe hiyo iliyofanyika kwenye eneo la shule
husika Njeza alifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 30.
Miongoni mwa fedha zilizokusanywa
katikaa harambee hiyo ni pamoja na shilingi milioni 16 zilizotolewa na mbunge
Njeza huku halmashauri ya wilaya ikiahidi kuchangia shilingi milioni 6.2.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Masoko
Tumaini Mzumbwe kiasi cha shilingi milioni 71 kinahitajika ili kukamilisha
ujenzi wa sekondari hiyo.
Akizungumzia harambee hiyo,mbunge
Njeza aliyeambatana na wafanyabiashara rafiki zake kutoka mji mdogo wa Mbalizi
wilayani hapa ambao pia kila mmoja wao alichangia kwa kadiri alivyoweza,alisema
huo ni mwanzo na iwapo kuna jambo lolote atahitajika kuchangia hatosita.
“Lakini haya yote yatawezekana iwapo
tutashirikiana kila mmoja kwa namna anavyoweza.Tumekwishawambia wananchi kuwa
tusitarajie maendeleo kwa kutegemea nguvu ya jirani.Ni lazima tushiriki
kujiletea maendeleo na ndiyo sababu hata bajeti ijato ya serikali kuu inalenga
kujitegemea zaidi badala ya kubaki ombaomba”anasema Njeza.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbeya
Mwalingo Kisemba anasema ni kata mbili pekee zimebakia kwenye halmashauri yake
hazika shule za sekondari.Ipo kata ya Masoko ambayo ujenzi wa sekondari ya
Sasyaka unaendelea na kata ya Inyala ambako ujenzi wa sekondari ya Iyelanyala
unaendelea pia.
“Kwa kutimiza ujenzi wa sekondari
katika kata nyingine zote tunaamini tumepunguza deni kwa kiasi kikubwa hivyo
kutokana na ushiriki wa wananchi kwa sasa tutakamilisha na hizi mbili kwa
kipindi kifupi kijacho.Uwepo wetu tu hapa leo unaonesha nia yetu katika
kutekeleza jambo hili mapema” alisema Kisemba aliyehudhuria pia harambee hiyo.
Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa namba 0756 40 95 97 Email nyambojoachim@gmail.com
No comments:
Post a Comment