Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, February 27, 2015

WANAHABARI WANAHARAKATI WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA WANENA

 Mhariri mkuu wa blogu ya Lyamba Lya Mfipa Bw.Joachim Nyambo(Wa tatu kulia) akifuatilia jambo kwa makina wakati darasa likiendelea.
 Mmoja wa wanahabari washiriki wa mafunzo akichangia hoja.
Mwahabari mkongwe nchini Wence Mushi(Mbele) akiendelea kufundisha wana warsha katika hoteli ya Ruaha mjini Iringa.
 Kutoka kulia ni wanahabari kutoka Mbeya Thompson Mpanji,Esther Macha na mhariri mkuu wa Lyamba Lya Mfipa wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Bw.Mushi.

                      HABARI KAMILI TOKA IRINGA

KUTOPEWA kipaumbele kwa ofisi za maafisa jamii na maendeleo katika bajeti kumetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea kushamiri katika jamii.

Hayo yamebainishwa na wanahabari walioko kwenye mafunzo ya masuala ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika mkoani Iringa yakiwa yameandaliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake(Tamwa) ambapo washiriki wanatoka katika mikoa ya Mbeya,Iringa,Njombe na Ruvuma.

Wanahabari hao wamesema ofisi za maafisa ustawi wa jamii zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kutokana na halmashauri nyingi kutozipa kipaumbele ofisi hizo wakati wa upangaji wa bajeti.

Mmoja wa wanahabari hao Geofray Nihahi amesema wengi wa maofisda kutoa ofisi hizo wamekuwa wakilalamika kukosa fedha na ndiyo sababu hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na badala yake wamebakia maofisini ambako kimsingi hawana kazi zaidi ya kupiga soga.

Nihahi amesema uhaba huo wa fedha umesababisha maafisa hao kushinda kutekeleza majukumu waliyopewa ikiwemo utoaji elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia hivyo kusababisha vitendo vya ukatili kuendelea kukithiri.

Naye Cresensia Kapinga amesema ni wakati kwa wadau wa masuala ya kijamii kujiuliza kwa kila mmoja ni kwa namna gani ameweza kujitoa katika kuhakikisha anakomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii inayomzunguka na iwapo hajafanya basi atambue kuwa ana deni la kutekeleza hayo.

Kwa upande wake Tumaini Msowoya,amesema bado katika jamii kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia na pia ukatili dhidi ya watoto ambao baadhi ya wanajamii wanaufanya pasipo kujua kuwa wanakosea.

FAINALI NI JUMAMOSI HII FIKA KATIKA VIWANJA VYA TIA MBEYA


Wednesday, February 25, 2015

WANAFUNZI WATIMULIWA SHULE KWA KUSHINDWA KULIPA MICHANGO



ZAIDI ya wanafunzi 60 wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Seminari ya Kidugala, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), wamefukuzwa shule kwa madai ya kutolipa ada na michango mbalimbali.

Miongoni mwa michango ambayo wanafunzi hao wanadaiwa ni pamoja na mchango wa kununulia basi, mchango wa kambi wakati wa likizo ya mwezi wa sita, na mingineyo mingi.

Lyamba Lya Mfipa imeshuhudia wanafunzi wakihangaika kuwasiliana na wazazi wao, baada ya kushushwa Njombe mjini toka katika kijiji cha Kidugala, iliko shule hiyo ili watumiwe nauli.

“Tunahangaika kuwatafuta wazazi wetu walio mbali na Njombe ili watutumie nauli turudi nyumbani kwa sababu tumelipa ada kidogo, sio milioni 1.7 wanayoitaka walimu,mimi nimelipa Sh laki nane lakini nimefukuzwa,”alisema mmoja wa wanafunzi hao.


wazazi wa wanafunzi hao waliiomba serikali kuingilia kati tatizo la walimu wa shule hiyo kuwafukuza wanafunzi, na kuwatelekeza mijini jambo ambalo ni hatari. 

“Unapomfukuza mtoto bila kuwasiliana na mzazi unataka afanye nini, tunasikitishwa na jambo hili,” alisema Anitha Mgeni, mkazi wa mtaa wa Mgendela, Njombe mjini baada ya kuwapokea watoto watatu, akiwahifadhi nyumbani kwake ili wawasiliane na wazazi wao.

Mzazi huyo alidai kuwa shule hiyo ilijengwa na waumini wa KKKT kwa lengo la kuwasaidia watoto wa watu maskini, lakini kwa sasa imekuwa ikitoza ada kubwa kuliko matarajio ya waumini hao.

Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Kidugala, Jackson Ngilangwa alikiri wanafunzi wengi kudaiwa ada, na kwamba hakuwepo shuleni wakati wanafunzi hao wanafukuzwa.

Akizungumza kwa njia ya simu, Ngilangwa alisema michango na ada ambazo wanafunzi hao wanatakiwa kulipa ni ile ya msingi.
 “Mimi nipo kwenye semina sipo shuleni, ngoja niwasiliane na makamu mkuu wa shule kuona kwa nini amewafukuza wanafunzi hao,”alisema.

Thursday, February 19, 2015

UTEUZI WA WAKUU WA WILAYA

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda jana ametangaza wakuu wa wilaya wapya,wanaopumzishwa na wale wanaohamishiwa katika wilaya nyingine.
 
Katika uteuzi huo wa Rais ambao umefanywa kwa niaba yake na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, JK amewapiga chini wakuu wa wilaya 12 kutokana na sababu zilizoelezwa kuwa ni umri, afya na kuimarisha utendaji wa kazi serikalini.
Waziri Pinda  aliwataja waliotenguliwa kuwa ni pamoja na James Millya aliyekuwa Mkuu we wilaya ya Longido,Elias Lali aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Ngorongoro,Alfred Msovella aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kongwa ,Danny Makanga aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Kasulu,Fatma Kimario aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe.
Wengine waliotenguliwa  ni Evarist Kalalu aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Mufindi,Abihudi Saideya aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Momba Elibariki Kingu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga,Dk.Leticia Warioba aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Iringa Martha Umbulla aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kiteto,Khalid Mandia aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Babati na Elias Goroi.
Katika uteuzi huo wakuu wa wilaya 27 wameula ambao ni pamoja na Mtangazaji maarufu wa TBC Shaaban Kissu,(Kondoa)Mariam Mtima (Ruangwa),Dk.Jasmine Tiisike (Mpwapwa),Pololeti Mgema (Nachingwea),Fadhili Nkurlu (Misenyi),Felix Lyaniva (Rorya),Fredrick Mwakalebela (Wanging'ombe) na Zainabu Mbussi (Rungwe) .
Francis Mwonga(Bahi),Kiming'ombe Nzoka (Kiteto),Husna Msangi (Handeni),Emmanuel Uhaula (Tandahimba),Mboni Mhita  (Mufindi),Hashim Mgandilwa (Ngorongoro) ,Mariam Juma (Lushoto),Thea Ntara (Kyela) na Ahmad Nammohe (Mbozi)
Wengine ni aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi katika baadhi ya mikoa hapa nchini Zelothe Steven (Musoma),Pili Moshi (Kwimba),Mahmoud Kambona (Simanjiro) ,Glorius Luoga (Tarime),Zainabu Telack (Sengerema),Benard Nduta (Masasi),Zuhura Ally (Uyui) ,Paul Makonda (Kinondoni),Mwajuma Nyiruka (Misungwi) na Maftah Mohamed (Serengeti).
Aidha Waziri Pinda aliwataja wakuu wa wilaya 64 waliobadilishwa vituo vyao vya kazi kuwa ni  pamoja na Nyerembe Munasa (Arumeru hadi Mbeya), Jordan Rugimbana (Kinondoni hadi Morogoro), Fatma Salum Ally kutoka (Chamwino hadi Mtwara), Lephy Gembe(Dodoma hadi Kilombero) na Christopher Kangoye (Mpwapwa hadi Arusha).
Wengine ni Omar Kwaang’(Kondoa- Karatu), Francis Mtinga (Chemba-Muleba), Elizabeth Mkwasa (Bahi-Dodoma), Agnes Hokororo (Ruangwa –Namtumbo), Regina Chonjo kutoka (Nachingwea hadi Pangani), Husna Mwilima (Mbogwe- Arumeru na Gerald Guninita  (Kilolo – Kasulu).
Wengine waliobadilishwa vituo vya kazi ni Zipora Pangani  (Bukoba hadi Igunga), Kanali Issa Njiku  (Misenyi hadi Mlele), Richard Mbeho (Biharamuro hadi Momba), Lembris Kipuyo (Muleba hadi  Rombo), Ramadhani Maneno (Kigoma kwenda Chemba), Venance Mwamoto (Kibondo kwenda Kaliua), Gishuli Charles (Buhigwe kwenda Ikungi), Novatus Makunga (Hai kwenda Moshi) na Anatory Choya kutoka (Mbulu kwenda Ludewa).
Wengine ni Christine Mndeme (Hanang’ kwenda Ulanga), Jackson Msome (Musoma kwenda Bukoba, John Henjewele (Tarime kwenda Kilosa), Dk Norman Sigalla (Mbeya kwenda Songea), Dk Michael Kadeghe(Mbozi kwenda Mbulu), Cripin Meela (Rungwe kwenda Babati) na Magreth Malenga (Kyela kwenda Nyasa).
Aliwataja wengine kuwa ni Said Amanzi  (Morogoro kwenda Singida),Antony Mtaka (Mvomero kwenda Hai), Elias Tarimo (Kilosa kwenda Biharamulo), Francis Miti(Ulanga kwenda Hanang),  Hassan Masala(Kilombero kwenda Kibondo), Angelina Mabula (Butiama kwenda Iringa), Farida Mgomi (Masasi kwenda Chamwino), Wilman Ndile  (Mtwara kwenda Kalambo).
Pia aliwataja Ponsian Nyami (Tandahimba kwenda Bariadi),Mariam Lugaila (Misungwi kwenda Mbogwe), Mary Onesmo (Ukerewe kwenda Buhigwe), Karen Yunus  (Sengerema kwenda Magu), Josephine Matiro  (Makete kwenda Shinyanga), Joseph Mkirikiti (Songea kwenda Ukerewe), Abdula Lutavi  (Namtumbo kwenda Tanga), Ernest Kahindi (Nyasa kwenda Longido), Anna Nyamubi  (Shinyanga kwenda Butiama) na Rosemary Kirigini (Meatu kwenda Maswa).
Abdalla Ali Kihato (Maswa kwenda Mkuranga), Erasto Sima (Bariadi kwenda Meatu), Queen Mulozi(Singida kwenda Ulambo), Yahaya Nawanda kutoka Iramba kwenda Lindi, Manju Msambya (Ikungi kwenda Ilemela), Xaveli Maketta  (Kaliua kwenda Kigoma), Bituni Msangi (Nzega kwenda Kongwa) na Lucy Mayenga kutoka Uyui kwenda Iramba.
Majid Mwanga amebadilishwa kituo chake kutoka (Lushoto kwenda Bagamoyo), Muhingo Rweyemamu (Handeni kwenda Makete), Hafsa Mtasiwa (Pangani kwenda Korogwe), Dk Nassor Ali Hamid (Lindi kwenda Mafia), Festo Kiswaga(Nanyumbu kwenda Mvomero), Sauda Mtondoo(Mafia kwenda Nanyumbu), Seleman Mzee (Kwimba kwenda Kilolo), Esterina Kilasi (Wanging’ombe kwenda Muheza), Subira Mgalu(Muheza kwenda Karagwe) na Jacqueline Liana (Magu kwenda Nzega).
Pia aliwataja wakuu wa wilaya 42 waliobakishwa kwenye vituo vyao vya kazi kuwa ni Jowika Kasunga (Monduli), Raymond Mushi (Ilala), Sophia Mjema (Temeke), Amani Mwenegoha (Bukombe), Ibrahimu Marwa (Nywang’wale), Rodrick Mpogolo (Chato) Manzie Mangochie (Geita), Darry Rwegasira (Karagwe), Luteni Kanali Bnedict Kitenga (Kyerwa) na Constatine Kanyasu (Ngara).
Wengine ni Paza Mwamlima (Mpanda), Peter Kiroya (Kakonko), Hadija Nyembo (Uvinza), Dk Charles Mlingwa (Siha), Shaibu Ndemanga (Mwanga), Herman Kapufi (Same), Ephraimu Mbaga (Liwale), Abdallah Ulega (Kilwa), Joshua Mirumbe (Bunda), Deodatus Kinawiro (Chunya), Rosemary Senyamule (Ileje) na Galamhusein Shaban (Mbarali).
Wengine waliobaki ni Christopher Mgala (Newala), Barika Konisaga (Nyamagana), Sara Dumba (Njombe), Hanifa Karamagi (Gairo), Halima Kihemba (Kibaha), Nurdin Babu (Rufiji), Methew Sedoyeka (Sumbawanga), Idd Kimanta (Nkasi), Chande Nalicho (Tunduru)), Senyi Ngaga (Mbinga), Wilson Nkambaku (Kishapu) na Benson Mpesya (Kahama).
Wengine ni Paul Mzindakaya (Busega), Georgina Bundala (Itilima), Fatma Toufiq (Manyoni), Luten Edward Ole Lengai (Mkalama), Hanifa Selengu (Sikonge), Seleman Kumchaya (Tabora), Mboni Mgaza (Mkinga na Seleman Liwowa (Kilindi).
Kwa  mujibu wa Pinda  wakuu wa wilaya waliofariki ni  Kapteni James Yamungu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Serengeti,Anna Magoha aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Urambo na Moshi Chang'a aliyekuwa mkuu  wa wilaya ya Kalambo. 
Wakuu wa wilaya watano waliopandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa ni John Mongela aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Arusha amekuwa mkuu wa mkoa wa Kagera,Amina Masenza aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Ilemela amekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa,Dk.Ibrahim Khamis aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Moshi amekuwa mkuu wa mkoa wa Katavi ,Halima  Dendego aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Tanga amekuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara na Daud Ntibenda aliyekuwa mkuu wa wilaya amekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha. 

WAWILI WAFA,18 WAJERUHIWA WAKIIBA PETROLI

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya baada ya kuungua na moto ulioripuka wakiwa wanajaribu kuiba mafuta aina ya petrol baada ya lori lililokuwa likisafirisha kupinduka.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa vyombo vya habari zinaeleza kuwa walipoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na mwanamke Maria Pajela(18) na Wiliam Pascal(38),wote wakazi wa kijiji  cha Idweli wilayani Rungwe.


Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Ahmed Msangi kupitia taarifa hiyo alisema  tukio hilo lilitokea jana(Feb18) majira ya saa tatu usiku katika kijiji cha Idweli, kata ya Isongole,  Tarafa ya ukukwe wilayani hapa.

 Kamanda Msangi alisema katika tukio hilo marehemu hao wawili kabla ya vifo vyao wakiwa na baadhi ya wakazi wengine wa kijiji cha Idweli walikuwa katika harakati za kuiba mafuta kutoka katika gari aina ya Scania  lenye namba za usajili T 891 AQZ likiwa na tela lenye namba T 821 ARF likitokea Dar es salaam kwenda nchini Malawi.


Amewataja majeruhi katika ajali hiyo ambao kati yao wanaume ni 13 na wanawake watano kuwa ni pamoja na Shukuru Kanzale (21),Nuru George (30), Asante Boniface(38), Joseph Jamson (18), Joseph Paschal(30), Siza Kanesa (22),Alex  Daud(35), Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37) na Samson Mbwila(29).


Wengine Veronica Elia (30),Dora Michael(35), Rabsen Ayub(26), Wasiwasi Spika (32), Asia Anon(20),Bahati Kyando (23),Christopher Erasto(32) na Melisa Sanane (50)wote wakazi wa kijiji cha Idweli.

Tuesday, February 17, 2015

Taarifa Sahihi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ0Kuhusu Kifo cha Askari Wake Huko Mbalizi


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya kifo cha Askari wake Praiveti Ahadi Mwaka Mwainyokole kilichotokea tarehe 4 Februari 2015 katika mji mdogo wa Mbalizi, Mkoani Mbeya.

Taarifa za mazingira ya kifo cha Askari huyo zimepotoshwa na baadhi ya Vyombo vya Habari na kusababisha mapokeo tofauti kwa wananchi.

Hali halisi ni kwamba, mnamo tarehe 4 Februari 2015 Askari huyo akiwa na Askari wenzake wanne (4) ambao ni Koplo Bedatu Benard Mloka, Praiveti Thani Hamisi Haji, Praiveti Mzee Buan Mzee na Praiveti Mohamed Juma walivamiwa na kundi la wahuni wakati wakitoka matembezini. Chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na Praiveti Rashid Maulid wa Kikosi chao kuibiwa samani kwenye nyumba aliyokuwa amepanga uraiani katika mji mdogo wa Mbalizi, Kitongoji cha Shigamba. Samani alizoibiwa ni pamoja na TV aina ya LG “flat screen” “Inch 20”, radio aina ya Sony moja, Deck aina ya Sangsung, flash moja, extension cable moja na fedha taslimu Tshs 30,000/=.

Askari huyo alitoa taarifa Kituo cha Polisi tarehe 03 Februari 2015 na kupatiwa RB yenye Nambari MBI/RB/285/2015, sambamba na kutoa taarifa Polisi. Kituo hicho cha Polisi kilitoa askari mmoja ambae aliungana na askari Jeshi na wenzake na wakaenda eneo la relini ambako vijana wasio na ajira maalumu hushinda. Waliwakamata vijana saba, mmoja wa vijana hao alikimbia na kwenda kuwapa taarifa wenzao ambao hawakuwepo katika eneo hilo ambapo vijana sita walifikishwa kituo cha Polisi.

Ilipofika saa tatu usiku askari hao wakiwa katika matembezi ya kawaida walikutana na kundi la vijana wakiwa na silaha mbalimbali kama nondo na marungu ambao walianza kuwashambulia huku wakiwashutumu kuwa waliwapeleka wenzao Polisi.

Kwa kuwa kundi la vijana hao lilikuwa kubwa na likiwa na silaha zilizotajwa lilifanikiwa kuwajeruhiAskari hao akiwemo Praiveti Ahadi Mwainyokole ambae alijeruhiwa vibaya.
Askari hao walikwenda Polisi na wakachukuwa PF3 na kisha kwenda katika hospitali ya Jeshi Mbeya baadaye Praiveti Mwainyokole alifariki muda mfupi baada ya hali yake kutokuwa nzuri kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani hali iliyosababisha damu kuvia kwenye Ubongo.

JWTZ linasikitishwa na mauaji hayo yaliyofanywa kwa Askari wake, na mauaji ya askari wengine katika maeneo ambako vitendo kama hivyo vimetokea. Ikumbukwe kuwa JWTZ lipo kwa ajili ya usalama na ustawi wa wananchi, hivyo JWTZ linalaani vitendo viovu vinavyofanyika kwa askari wake na linatoa rai kwa vyombo vya sheria kuchukua mkondo wake.

Kimsingi JWTZ halina ugomvi na wananchi kwani kazi yake ya msingi ni kuwalinda ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo kwa utulivu na amani kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.

Imetolewa na
 Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga 

WANAFUNZI TUNDUMA WAFUNGA BARABARA KWA MUDA



 Wanafunzi kutoka shule mbalimbali mjini Tunduma Momba wakiwa barabarani kuandamana kwa kutaka serikali kujenga matuta katika barabara ya Mbeya Sumbawanga kutokana na mwanafunzi mwenzao kugongwa na kufa pamoja na wengine kujeruhiwa huku Polisi wakijaribu kuangalia hali ya usalama






 Mkuua wa wilaya ya Momba Abiud Saidea akiwasili eneo la tukio




                           HABARI KAMILI

WANAFUNZI wa shule Mbalimbali za  msingi wilayani katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba Mkoani Mbeya,wameandamana barabarani wakiishinikiza Serikali  kujenga matuta katika barabara inayo toka Mjini Tunduma hadi   Sumbawanga mkoani Rukwa kutoka na kutokea kwa ajari za mara kwa mara.

 Maandamano ya wanafunzi hao hayo yametokea leo asubuhi majira ya saa 3  ni baada ya Wanafuzi wawili kugongwa papo hapo na kusababisha mmoja kuaga dunia na wawili kuwa majeruhi katika ajari iliyo tokea jana katika maeneo ya Transforma mtaa wa Mwaka wilayani hapa. 


 Wakizungumza maeneo ya mandamano katika  umati wa wanafunzi wa shule hizo, huku wakiimba nyimbo  za kuishinikiza serikali kujenga  matuta eneo hilo ambalo limekuwa likisababisha ajari mara kadhaa.


 Wasema eneo la Transifoma  ni eneo ambalo mara kwa mara limekuwa likisababisha ajari kutokana na kukosekana kwa matuta ya  kuzuia mwendokasi  wa magari bila kujali kuwa ni kivuko cha wanafunzi.


 “Tunaitaka serikali kutujengea matuta eneo hili maana wanafunzi wengi wamepoteza maisha kwa kugongwa na magari ” alisema mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina  la Ally.

 Hata hivyo waliishinikiza seikali kwa kuitaka iharakishe kuchukua hatua hiyo mara moja ili kuepusha majanga hayo. 


 Pia,kwa upande wa Wananchi wamesema kuwa ni haki yao kwa wanafunzi hao kudai haki yao na ukiangalia idadi ya watu waliogongwa  na magari katika eneo hili ni Wakubwa ni watu nane na watoto 10 kitu ambacho kinasadikika ni mwendokasi wa Madereva.

Akizungumza mbele ya umati wa wanafunzi diwani wa kata ya Tunduma Frank Mwakajoka aliitaka serikali  kuanza mara moja ujenzi wa matuta hayo ili kupunguza ajari za wanafunzi na watu wazima maeneo hayo.

“Tunaitaka serikali kuanza leo ujenzi wa matuta eneo la Transfoma maana tumechoka kupoteza maisha ya watu kwa ajari zinazo zuilika” amesema Mwakajoka.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Momba Abiudi Saidea amewata wanafunzi pamoja na wazazi kuwa watulivu wakati serikali ikitekeleza ujenzi wa matuta eneo hilo hatari , lililopoteza maisha ya watu wengi.

 Amesema ujenzi huo utaanza mara moja bila kuchelewa , na aliwahidi kuwa ameshaongea na uongozi wa Tanroad  wa makao makuu ya mkoa wa Mbeya ili waje wapime eneo hilo na kuanza ujenzi wa matuta hayo.

HABARI NA PICHA KWA HISANI YA MITANDAO MBALIMBALI YA KIJAMII

Friday, February 13, 2015

HATARI,KIONGOZI WA UVAMIZI VITUO VYA POLISI NCHINI AJIWEKA WAZI

                                        Kaisi Bin Abdullah akiwa amejiziba sura.
HATIMAYE kuvamiwa kwa vituo vya polisi na kuporwa silaha huku askari wake wakiuawa kikatili kumejulikana kunafanywa na nani kufuatia gazeti hili kunasa mkanda wa video wa mtu mmoja anayejiita Kaisi Bin Abdullah akijitapa kufanya hivyo kwa lengo la kukusanya silaha ili kulipa kisasi siku si nyingi!
Ijumaa liliunasa mkanda huo kutoka kwa mtu mmoja aliyekataa kujitambulisha kwa jina wala kusema anakotokea hapa nchini huku akisema: “Una maneno ya hatari sana, naogopa kujianika, nitauawa.”

“Siwezi kutaja jina wala mahali ninapoishi, sitaki kupigwa picha, kama hamtaki niwapatie taarifa hii acheni niondoke,” alisema mtu huyo huku akinyanyuka kitini jambo lililowafanya wakuu wa dawati kukubaliana na matakwa yake na kuendelea na mahojiano.
Baadaye ilipatikana fursa ya kuuangalia mkanda huo; Bin Abdullah ametumia dakika 11: 03 kuzungumzia mambo mbalimbali lakini kubwa kuliko yote ni kuliponda Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuwakamata wenzao katika imani na harakati (zinazohifadhiwa kwa sasa) na kuwashikilia kwenye mahabusu mbalimbali nchini.
ALIANZA KWA KUSEMA
Bin Abullah ambaye kwenye mkanda huo amevaa nguo nyeusi kama ninja na miwani ya giza, alizungumza kwa kirefu, akitoa wito lakini mbele akasema:
“Tumeshaungana ili kupambana. Mkoa wa Mtwara zaidi ya wenzetu kumi na saba walikamatwa kwa makosa ya dhuluma, makosa ya kupanga, makosa ya ugaidi. Ishirini na moja wamekamatwa Zanzibar wako katika Gereza la Segerea (Dar). Wenzetu wengine kumi na nane wamekamatwa Mwanza wako katika Gereza la Kisongo, Arusha. Ndugu zangu, wenzetu wengine kumi na saba wameuawa Mtwara kwa amri ya ...(anamtaja waziri).”
ADAI WAMECHOKA NA SUBIRA
“Subira yetu imefika mwisho na tulichokuwa tunasubiri Mungu ameshatupa. Tunatoa ahadi kilichopo hivi sasa tunatoboa jahazi wote tuzame.”
WENZAO WAACHIWE HURU
“Tunatoa rai, wenzetu waliopo Gereza la Kisongo waachiwe huru. Hapa hatumtishi mtu yeyote yule.”
KUHUSU VITUO VYA POLISI
“Pili, agizo la Ernest Mangu IGP, umetangaza uliwenguni kwamba umewakamata wote waliovamia vituo vya polisi na umezikamata silaha zote. Ukweli ni kwamba unatetea tumbo lako. Hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa na wala silaha hazijakamatwa.
“Mungu ametukubali. Katika Kituo cha Polisi Ushirombo (Kilimanjaro) tumeweza kuvamia kituo, tukaweza kutoa roho za polisi na tukaweza kuchukua silaha, tunazo.“Tumevamia Kituo cha Polisi Ikwiriri (Pwani), tumeweza kuchukua silaha za kutosha, tumeweza kuchukua mabomu ya kutosha. Tunazo silaha tunasubiri muda zianze kufanya kazi.
“Ernest Mangu nakupa changamogto, hivi sasa tuna uwezo...(maneno yanahifadhiwa kwa usalama) wakati wowote ambao tunataka.”
HAKUNA UPINZANI?
“Tumeweza kuchukua silaha bila kuwa na silaha yoyote. Ndugu zetu wa Tanga wameweza kuchukua silaha wakiwa hawana silaha yoyote. Ikwiriri tumechukua silaha tukiwa hatuna silaha yoyote, mpaka sasa tumeshachukua roho tano za polisi.”
VITISHO VYA JUMLA
“Ndugu zangu, ...mlikuwa mkinisubiri nitoe tamko, natoa kauli rasmi...” alihitimisha Abdullah, huku vitisho vya jumla kwenye tamko lake vikiwahusu polisi, viongozi wa ngazi za juu serikalini pamoja na mikusanyiko ya ibada.
TAMKO NGUNGURI LA IGP
Baada ya video hiyo, Ijumaa lilimuibukia Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu na kuzungumza naye kuhusu mtu huyo na kumkabidhi video ambapo alisema:
“Nawashukuru sana kwa kuleta video hii, huu ndiyo ushirikiano unaotakiwa, nawaomba wananchi video za aina hii wazikatae kwa sababu ni kosa kuwa nazo na watu kadhaa wameshakamatwa kwa kuwa nazo.
“Sisi kama jeshi la polisi tunajua kuwa kuna watu wanadhani kufanya uhalifu kama huo kutawasaidia kutimiza matakwa yao, lakini ukweli ni kwamba polisi wapo imara na nina uhakika watuhumiwa watakamatwa kwa kushirikiana na raia wema.”
SHEHE MKUU AMKANA
Baada ya kuzungumza na IGP, Ijumaa lilimtafuta Shehe Mkuu Tanzania, Mufti Shaban Simba na kumsimulia kuhusu kuibuka kwa Bin Abullah na kutaka kujua pengine anamfahamu.
“Kwanza hizo taarifa hizo ndiyo nazisikia kutoka kwako. Hilo jina ulilonitajia (Bin Abdullah) sijawahi kulisikia labda muangalie kwa wenzetu upande wa pili.”
KUMBUKUMBU ZA NYUMA
Katika gazeti ndugu na hili, Uwazi, Toleo la Januari 28 mpaka Februari 2, mwaka huu ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari yenye kichwa; KUUAWA KWA POLISI IKWIRIRI; MAZITO YAIBUKA!
Katika habari hiyo, Uwazi lilichimba kwa kina kuhusu kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi Ikwiriri na kuuawa kwa askari wake wawili, Edger Jerald Mlinga (43) na Judith Timothy (32).
Watu hao waliodhaniwa ni majambazi walifanikiwa kupora bunduki 7, risasi 60 na mabomu kadhaa yaliyokuwa ndani ya kituo na kukimbia bila kukamatwa.
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi kwenye eneo la tukio walisema wana wasiwasi watu hao si majambazi bali ni kundi la kigaidi ambalo lina mkakati wa kukusanya silaha kwa ajili ya matumizi batili siku za baadaye, jambo ambalo limeanza kujionesha kupitia video iliyonaswa na Gazeti na Ijumaa.
KUTOKA DAWATI LA IJUMAA
Tunawaomba wananchi kwa ujumla kutokuwapa nafasi watu wa aina ya Abdullah wanaoeneza chuki kwa lengo la kuwagawa watu na kuleta machafuko, badala yake kila anayeashiria shari ni vema taarifa zake zikafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili amani ya taifa iendelee kudumu.
Aidha, tunalitaka jeshi la polisi pamoja na vyombo vya usalama kulichukulia kwa uzito tamko la mtu huyo anayedai kuwa ni kiongozi wa ugaidi, kumsaka na kumtia hatiani pamoja na wafuasi wake wote.