Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, February 25, 2015

WANAFUNZI WATIMULIWA SHULE KWA KUSHINDWA KULIPA MICHANGO



ZAIDI ya wanafunzi 60 wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Seminari ya Kidugala, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), wamefukuzwa shule kwa madai ya kutolipa ada na michango mbalimbali.

Miongoni mwa michango ambayo wanafunzi hao wanadaiwa ni pamoja na mchango wa kununulia basi, mchango wa kambi wakati wa likizo ya mwezi wa sita, na mingineyo mingi.

Lyamba Lya Mfipa imeshuhudia wanafunzi wakihangaika kuwasiliana na wazazi wao, baada ya kushushwa Njombe mjini toka katika kijiji cha Kidugala, iliko shule hiyo ili watumiwe nauli.

“Tunahangaika kuwatafuta wazazi wetu walio mbali na Njombe ili watutumie nauli turudi nyumbani kwa sababu tumelipa ada kidogo, sio milioni 1.7 wanayoitaka walimu,mimi nimelipa Sh laki nane lakini nimefukuzwa,”alisema mmoja wa wanafunzi hao.


wazazi wa wanafunzi hao waliiomba serikali kuingilia kati tatizo la walimu wa shule hiyo kuwafukuza wanafunzi, na kuwatelekeza mijini jambo ambalo ni hatari. 

“Unapomfukuza mtoto bila kuwasiliana na mzazi unataka afanye nini, tunasikitishwa na jambo hili,” alisema Anitha Mgeni, mkazi wa mtaa wa Mgendela, Njombe mjini baada ya kuwapokea watoto watatu, akiwahifadhi nyumbani kwake ili wawasiliane na wazazi wao.

Mzazi huyo alidai kuwa shule hiyo ilijengwa na waumini wa KKKT kwa lengo la kuwasaidia watoto wa watu maskini, lakini kwa sasa imekuwa ikitoza ada kubwa kuliko matarajio ya waumini hao.

Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Kidugala, Jackson Ngilangwa alikiri wanafunzi wengi kudaiwa ada, na kwamba hakuwepo shuleni wakati wanafunzi hao wanafukuzwa.

Akizungumza kwa njia ya simu, Ngilangwa alisema michango na ada ambazo wanafunzi hao wanatakiwa kulipa ni ile ya msingi.
 “Mimi nipo kwenye semina sipo shuleni, ngoja niwasiliane na makamu mkuu wa shule kuona kwa nini amewafukuza wanafunzi hao,”alisema.

No comments:

Post a Comment