Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, February 29, 2016

MOTO WATEKETEZA BWENI LA WANAFUNZI IYUNGA SEC




WANAFUNZI 95 katika shule ya sekondari ya wavulana ya Iyunga jijini Mbeya hawana mahali pa kulala kufuatia moto mkubwa kuteketeza Bweni lao leo (Feb 29) lililokuwa likifahamika kwa jina la Mkwawa.

Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo Edward Mwantimwa moto huo umezuka majira ya saa 4:00 asubuhi wakati wanafunzi  wakiwa darasani wakiendelea na masomo na baadaye Askati wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji walifika na kufanikiwa kuuzima ukiwa umeteketeza bweni lote.

Mwantimwa amesema pamoja na kutokuwepo kwa mwanafunzi aliyejeruhiwa moto huo umeteketeza vifaa mbalimbali vikiwemo vitanda,magodoro na nguo za wanafunzi 95 waliokuwa wakilitumia bweni hilo huku bweni jirani la Nyerere likiadhiriwa kidogo pia.

Akizungumzia chanzo cha tukio hilo,mkuu huyo wa shule moto amesema umetokana na hitilafu ya umeme kwenye soketi ambayo ipo karibu na mlangoni lakini hakubainisha iwapo soketi hiyo ilikuwa ikitumika wakati tukio likitokea.

Amesema kutokana na moto kuanzia katika eneo la mlango ilikuwqa vigumu kwa waokoaji kuweza kuingia ndani na kuokoa vitu vilivyokuwemo.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe Munasa amesema  sababu ya moto huo ni uchakavu wa miondombinu ya shule hiyo kongwe iliyojengwa tangu wakati wa utawala wa Mkoloni.

Munasa amesema kutokana na uchakavu wa majengo wanafunzi pamoja na watumishi shuleni hapo wanapaswa kuchukua taadhari katika utumiaji wa miundombinu hiyo hasa ya umeme, vyoo, na maji ambayo inaokena inauchakavu mkubwa.

Mkuu huyo wa wilaya amemtaka kaimu mkurugenzi wa halmaashauri ya jiji la Mbeya Dk Samwel Lazaro kununua vifaa  muhimu kwa mahitaji wa wanafunzi wakati mpango wa kukarabati jengo la bweni lililoungua ukiendelea kufanyiwa kazi.Thamani halisi ya hasara iliyopatikana bado haijafahamika.

Friday, February 26, 2016

HABARI NJEMA KWA WASOMAJI RIWAYA!





Kitabu Cha Riwaya ya kusisimua ya MASIKINI MIMI DEO KALIMANZIRA kinapatikana sokoni nchini kote.Tayari kimekwishawasili katika mikoa ya Mbeya,Rukwa na Katavi.Pata nakala yako sasa upate uhondo wa Riwaya hii ya kusisimua iliyotungwa na Leonard Mubali Mwandishi wa BBC.


Kitabu kimefika tayari maeneo ya Kahama,Kibondo,Ngara na Kasulu.Usambazaji unaendele unaendelea kulingana na makubaliano na mawakala kutokana na vigezo vilivyopo.

Thursday, February 18, 2016

MAISHA YA MATESO KIJIJINI KAPUNGA-4

Na Joachim Nyambo.

WAHENGA walinena hakuna lililo na mwanzo likakosa kuwa na mwisho!Mateso yaliyowasibu wakazi wa kijiji cha Kapunga sasa yamefikia ukomo.Miaka 10 ya misukosuko baina yao na mwekezaji kampuni ya Kapunga Rice inayoendesha shughuli zake chini ya kampuni mama ya Expot Trading ilikuwa mwiba kwa wakazi hawa.


Mgogoro baina ya pande hizo mbili umemalizika baada ya serikali kusikia kilio cha wananchi.Sasa mgogoro wa kimpaka uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 umemalizika kwa mwekezaji kuridhia kiasi cha hekta 1,870 za ardhi kurejeshwa kwa kijiji hicho.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Willium Lukuvi mapema mwezi jana alitangaza kurejeshwa kwa hekta hizo za ardhi kwa nyakati tofauti alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Kapunga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini.Alizungumzia pia jambo hilo alipokuwa kwenye kikao na madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.

“Rais John Pombe Magufuli ameamua kuwapa zawadi ya mwaka mpya wakazi wa Mbarali.Zawadi yenyewe ni kutekeleza kabla ya kutimiza siku mia moja za utawala wake ahadi aliyowaahidi wakazi wa Kapunga ya kutatua mgogoro wa kimpaka kati yenu na mwekezaji wa shamba la Kapunga aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu” alisema Lukuvi.

Alisema serikali imekubaliana na mwekezaji kurejesha kipande cha ardhi cha hekta 1,870 kwa wakazi wa kijiji cha Kapunga walichokidai kwa zaidi ya miaka kumi huku viongozi wengi wakiika kijijini hapo na kushindwa kufikia suluhisho la mgogoro.

Lukuvi alisema tatizo lilianzia mwaka 2005 wakati mwekezaji alipobinafsishiwa shamba kwani vipimo alivyopewa vilikuwa tofauti na uhalisia wa eneo lililokuwa likimilikiwa na serikali kama shamba la Kapunga.

Alisema tayari wamezungumza na kampuni husika iliyobinafsishiwa shamba hilo kwa mkataba wa umiliki wa miaka 99 ambayo tayari ilikwisha chukua mkopo benki kwa kutumia hati miliki ya ardhi hiyo.

“Tumekaa na kukubaliana,kiasi hiki cha ardhi kirejeshwe kwenu na mwekezaji amekubali.Ili kuwasaidia pia wawekezaji tumezungumza na watu wa benki waliyochukua mkopo na tumekubaliana kiasi cha mkopo kinachotokana na kiasi cha ardhi tunachokiondoa irejeshewe ili wasiendelee kumtoza mwekezaji” alisema Lukuvi hali iliyosababisha wakazi wa kijiji hicho kupiga mayowe na vigelegele kwa furaha.

“Awali hakukuwa makosa kwa serikali kulitumia shamba la Kapunga kwakuwa ardhi yote ni mali ya serikali.Nafco alikuwa mtoto wa serikali kwahiyo hakukuwa na tatizo kutumia ardhi hii.Makosa yalikuja kufanyika wakati shamba linabinafsishwa kwa kwekezaji.Hilo tumeliona na ndiyo sababu leo tumeridhia kurejesha ardhi yenu”

Lukuvi aliwaambia wakazi hao ambao muda wote akihutubia waliridhia kusimama wakinyeshewa mvua kuwa hekta hizo sasa ni mali ya kijiji chao na tayari wataalamu wa wizara yake wapo kijijini hapo na wanaendelea na utaratibu wa kutengeneza upya mipaka kati ya eneo la kijini na lile la mwekezaji ambalo sasa linabakiwa na hekta zisizopungua 5000.

Aliwataka wakazi wa kijiji hicho kutoa ushirikiano wa kina kwa wataalamu wanaofanya shughuli hiyo sambamba na kupendekeza umiliki wa ardhi iliyorejeshwa kwao ili watakao miliki wapewe hati miliki.

“Hakikisheni mnashiriki kuweka mipaka hii.Mshirikiane pia kuona namna gani inafaa kwa umiliki wa eneo hilo ili muweze kuwa na hati miliki.Hii itawezesha pia serikali kunufaika kwakuwa mtatakiwa kulipia kodi.Maana pasipo kuwa na hati ni wazi kuwa na serikali nayo inakosa haki yake”

Alipendekeza vijana kupewa kipaumbele wakati wa mgawanyo wa ardhi hiyo akisema kundi hilo ndilo linalokabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ardhi kutokana na ongezeko la wakazi.

“Siwezi kulazimisha kuwa wapewe vijana,lakini nashauri kipaumbele kikubwa kiwe kwao kwakuwa ni kundi lisilo na ardhi ya kumiliki.Wakati mkifanya mchakato wa kugawa au kutengeneza namna ya umiliki wa ardhi hii basi jaribuni na kulitafakari hili kwa kina”


Waziri huyo alionya kutokuwepo kwa upendeleo katika ugawaji na umiliki wa ardhi hiyo akisema yawezekana wajanja wachache wakataka kujinufaisha kupitiaa nyadhifa zao jambo alilosema likibainika litafuatiliwa kisheria.

“Tusije kusikia kuna mtu kapewa ardhi kutokanan na kitambi chake au nafasi yake.Mkasababisha wakubwa wachache wakaneemeka na walalahoi wakabaki wakiona kwa macho tu ardhi yao ikiwanenepesha wachache.Na ninyi maafisa tukisikia mna mgawo wenu hapa lazima tutachukua hatu.”alisisitiza Lukuvi.

Hatua hii ya kurejeshea kipande cha ardhi yao ni faraja kubwa kwa wakazi wa kijiji cha kapunga.Wanajua sasa ukomo wa mateso na manyanyaso umefika.Furaha yao inaongezeka mara dufu pale wanapowaza kuwa sasa kijiji chao kiko salama kwakuwa ilikuwa kiondolewe kwani kilikuwa kikitajwa kuwa sehemu ya eneo la mwekezaji.

Mafanikio haya yenye kuonesha uwepo wa serikali sikivu na yenye kuwajali watu wake hayaishii kuwafurahisha wakazi wa Kapunga pekee.Wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari wanafurahia hatua hii.Hii ni kwakuwa walishiriki katika kutetea ardhi hiyo.Waliujulisha umma mateso waliyokuwa wakiyapata wakazi wa kijiji hiki kutoka kwa mwekezaji

Hata hivyo unapozungumzia mafanikio haya kamwe huwezi kuwasahau wada mbalimbali waliowezesha kuyafikia.Hawa ni pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile,aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mbarali,Luteni Cosmas Kayombo na wengine wengi.Mara kadhaa viongozi hawa walijaribu kutafuta suluhu ya mgogoro huu wakiwa wao wenyewe au kushirikiana na viongozi wa ngazi za juu.

Viongozi waliopo madarakani kama Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro na mkuu wa wilaya ya Mbarali Gullamhussein Kifu hawatosahaulika katika historia ya kijiji cha Kapunga.Wamekuwa mstari wa mbele na kuwezesha mgogoro huu kupatiwa ufumbuzi.

Uwepo wa rais Dk John Magufuli madarakani utabaki kukumbukwa na wakazi wa kijiji hiki.Aliwaahidi kutatua mzozo wao akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.Amewatekelezea ahadi hiyo akiwa hata hajatimiza siku 100 madarakani.Yeye anaiita zawadi ya mwaka mpya kwa wakazi wa Kapunga.

Wapo wakazi wengi waliokuwa wamekwishaanza kukata tama.Wakiamini mgogoro huo hautakuja pata ufumbuzi.Hii ni kutokana na kudumu kwa muda mrefu huku wakijionea danadana zilizokuwa zikipigwa na viongozi wengi waliofika kijijini hapo.

Wakazi wa kijiji hiki wanasema kurejeshea ardhi ni hatua ya kwanza.Wanahoji kwakuwa serikali imekiri makosa yalifanyika wakati wa kubinafsisha shamba la Kapunga ni nini hatma ya wananchi waliopata hasara kutokana na hasira za mwekezaji.

Katika mkutano wao na waziri Lukuvi wakazi hao walihoji ni nani anayepaswa kuwajibika kwa hasara walizopata.Wapo waliobomolewa nyumba zao na viwanja vyao vikatumika kujenga uwanja wa ndege wa mwekezaji,wapo waliobomolewa tofali walizokuwa wamefyatua na kuzichoma wakisubiri kujenga.Zipo familia zilizopoteza wapendwa wao kwa kusombwa na maji baada ya mwekezaji kubomoa madaraja.

Hili bado ni swali lisilopatiwa majibu.Kwa kuwa makosa yalifanyika wakati wa kuuza shamba wanakijiji wanaona ni wazi yupo mtu anayepaswa kuwajibika katika kulipa fidia ya hasara waliyoipata.Hii itaongeza ushirikiano baina yao na mwekezaji ambaye sasa anabakiwa na kipande cha ardhi kilicho halali.



Nawatakia kila la kheri wakazi wa Kapunga katika maisha yao mapya kwenye ardhi yao halali.Muhimu kwao ni kukumbuka ardhi waliyorudishiwa isije ikawaingiza kwenye migogoro mingine ya wao kwa wao.Umakini katika kupanga matumizi sahihi ya ardhi hiyo unahitajika.Ni wakati pia kwao kukaa na mwekezaji na kumaliza tofauti zao.Hii itadumisha udugu baina yao na kuishi maisha ya furaha wakiwa majirani wenye kupendana.

MWISHOOOO

Monday, February 15, 2016

DKT.MAGUFULI ATEUA MABALOZI WATATU,WAMO MIGIRO NA CHIKAWE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi walioteuliwa kuwa ni Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Mheshimiwa Mathias Meinrad Chikawe na Dkt. Ramadhan Dau.

Vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja walioteuliwa kuwa ni:Naibu Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam. Kamishna Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Mstaafu Suleiman Kova.

Naibu Kamishna wa Polisi Albert Nyamuhanga ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki. Kamishna Nyamuhanga anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.

Naibu Kamishna wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia. Kamishna Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni. Kamishna Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Paul Moses Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kabla ya Uteuzi huu Dkt. Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk Management) katika Benki Kuu ya Tanzania. Dkt. Kipilimba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Dikson Maimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Teuzi zote zinaanzia leo tarehe 15 Februari, 2016

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
15 Februari, 2016