Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, February 18, 2016

MAISHA YA MATESO KIJIJINI KAPUNGA-4

Na Joachim Nyambo.

WAHENGA walinena hakuna lililo na mwanzo likakosa kuwa na mwisho!Mateso yaliyowasibu wakazi wa kijiji cha Kapunga sasa yamefikia ukomo.Miaka 10 ya misukosuko baina yao na mwekezaji kampuni ya Kapunga Rice inayoendesha shughuli zake chini ya kampuni mama ya Expot Trading ilikuwa mwiba kwa wakazi hawa.


Mgogoro baina ya pande hizo mbili umemalizika baada ya serikali kusikia kilio cha wananchi.Sasa mgogoro wa kimpaka uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 umemalizika kwa mwekezaji kuridhia kiasi cha hekta 1,870 za ardhi kurejeshwa kwa kijiji hicho.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Willium Lukuvi mapema mwezi jana alitangaza kurejeshwa kwa hekta hizo za ardhi kwa nyakati tofauti alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Kapunga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini.Alizungumzia pia jambo hilo alipokuwa kwenye kikao na madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.

“Rais John Pombe Magufuli ameamua kuwapa zawadi ya mwaka mpya wakazi wa Mbarali.Zawadi yenyewe ni kutekeleza kabla ya kutimiza siku mia moja za utawala wake ahadi aliyowaahidi wakazi wa Kapunga ya kutatua mgogoro wa kimpaka kati yenu na mwekezaji wa shamba la Kapunga aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu” alisema Lukuvi.

Alisema serikali imekubaliana na mwekezaji kurejesha kipande cha ardhi cha hekta 1,870 kwa wakazi wa kijiji cha Kapunga walichokidai kwa zaidi ya miaka kumi huku viongozi wengi wakiika kijijini hapo na kushindwa kufikia suluhisho la mgogoro.

Lukuvi alisema tatizo lilianzia mwaka 2005 wakati mwekezaji alipobinafsishiwa shamba kwani vipimo alivyopewa vilikuwa tofauti na uhalisia wa eneo lililokuwa likimilikiwa na serikali kama shamba la Kapunga.

Alisema tayari wamezungumza na kampuni husika iliyobinafsishiwa shamba hilo kwa mkataba wa umiliki wa miaka 99 ambayo tayari ilikwisha chukua mkopo benki kwa kutumia hati miliki ya ardhi hiyo.

“Tumekaa na kukubaliana,kiasi hiki cha ardhi kirejeshwe kwenu na mwekezaji amekubali.Ili kuwasaidia pia wawekezaji tumezungumza na watu wa benki waliyochukua mkopo na tumekubaliana kiasi cha mkopo kinachotokana na kiasi cha ardhi tunachokiondoa irejeshewe ili wasiendelee kumtoza mwekezaji” alisema Lukuvi hali iliyosababisha wakazi wa kijiji hicho kupiga mayowe na vigelegele kwa furaha.

“Awali hakukuwa makosa kwa serikali kulitumia shamba la Kapunga kwakuwa ardhi yote ni mali ya serikali.Nafco alikuwa mtoto wa serikali kwahiyo hakukuwa na tatizo kutumia ardhi hii.Makosa yalikuja kufanyika wakati shamba linabinafsishwa kwa kwekezaji.Hilo tumeliona na ndiyo sababu leo tumeridhia kurejesha ardhi yenu”

Lukuvi aliwaambia wakazi hao ambao muda wote akihutubia waliridhia kusimama wakinyeshewa mvua kuwa hekta hizo sasa ni mali ya kijiji chao na tayari wataalamu wa wizara yake wapo kijijini hapo na wanaendelea na utaratibu wa kutengeneza upya mipaka kati ya eneo la kijini na lile la mwekezaji ambalo sasa linabakiwa na hekta zisizopungua 5000.

Aliwataka wakazi wa kijiji hicho kutoa ushirikiano wa kina kwa wataalamu wanaofanya shughuli hiyo sambamba na kupendekeza umiliki wa ardhi iliyorejeshwa kwao ili watakao miliki wapewe hati miliki.

“Hakikisheni mnashiriki kuweka mipaka hii.Mshirikiane pia kuona namna gani inafaa kwa umiliki wa eneo hilo ili muweze kuwa na hati miliki.Hii itawezesha pia serikali kunufaika kwakuwa mtatakiwa kulipia kodi.Maana pasipo kuwa na hati ni wazi kuwa na serikali nayo inakosa haki yake”

Alipendekeza vijana kupewa kipaumbele wakati wa mgawanyo wa ardhi hiyo akisema kundi hilo ndilo linalokabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ardhi kutokana na ongezeko la wakazi.

“Siwezi kulazimisha kuwa wapewe vijana,lakini nashauri kipaumbele kikubwa kiwe kwao kwakuwa ni kundi lisilo na ardhi ya kumiliki.Wakati mkifanya mchakato wa kugawa au kutengeneza namna ya umiliki wa ardhi hii basi jaribuni na kulitafakari hili kwa kina”


Waziri huyo alionya kutokuwepo kwa upendeleo katika ugawaji na umiliki wa ardhi hiyo akisema yawezekana wajanja wachache wakataka kujinufaisha kupitiaa nyadhifa zao jambo alilosema likibainika litafuatiliwa kisheria.

“Tusije kusikia kuna mtu kapewa ardhi kutokanan na kitambi chake au nafasi yake.Mkasababisha wakubwa wachache wakaneemeka na walalahoi wakabaki wakiona kwa macho tu ardhi yao ikiwanenepesha wachache.Na ninyi maafisa tukisikia mna mgawo wenu hapa lazima tutachukua hatu.”alisisitiza Lukuvi.

Hatua hii ya kurejeshea kipande cha ardhi yao ni faraja kubwa kwa wakazi wa kijiji cha kapunga.Wanajua sasa ukomo wa mateso na manyanyaso umefika.Furaha yao inaongezeka mara dufu pale wanapowaza kuwa sasa kijiji chao kiko salama kwakuwa ilikuwa kiondolewe kwani kilikuwa kikitajwa kuwa sehemu ya eneo la mwekezaji.

Mafanikio haya yenye kuonesha uwepo wa serikali sikivu na yenye kuwajali watu wake hayaishii kuwafurahisha wakazi wa Kapunga pekee.Wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari wanafurahia hatua hii.Hii ni kwakuwa walishiriki katika kutetea ardhi hiyo.Waliujulisha umma mateso waliyokuwa wakiyapata wakazi wa kijiji hiki kutoka kwa mwekezaji

Hata hivyo unapozungumzia mafanikio haya kamwe huwezi kuwasahau wada mbalimbali waliowezesha kuyafikia.Hawa ni pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile,aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mbarali,Luteni Cosmas Kayombo na wengine wengi.Mara kadhaa viongozi hawa walijaribu kutafuta suluhu ya mgogoro huu wakiwa wao wenyewe au kushirikiana na viongozi wa ngazi za juu.

Viongozi waliopo madarakani kama Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro na mkuu wa wilaya ya Mbarali Gullamhussein Kifu hawatosahaulika katika historia ya kijiji cha Kapunga.Wamekuwa mstari wa mbele na kuwezesha mgogoro huu kupatiwa ufumbuzi.

Uwepo wa rais Dk John Magufuli madarakani utabaki kukumbukwa na wakazi wa kijiji hiki.Aliwaahidi kutatua mzozo wao akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.Amewatekelezea ahadi hiyo akiwa hata hajatimiza siku 100 madarakani.Yeye anaiita zawadi ya mwaka mpya kwa wakazi wa Kapunga.

Wapo wakazi wengi waliokuwa wamekwishaanza kukata tama.Wakiamini mgogoro huo hautakuja pata ufumbuzi.Hii ni kutokana na kudumu kwa muda mrefu huku wakijionea danadana zilizokuwa zikipigwa na viongozi wengi waliofika kijijini hapo.

Wakazi wa kijiji hiki wanasema kurejeshea ardhi ni hatua ya kwanza.Wanahoji kwakuwa serikali imekiri makosa yalifanyika wakati wa kubinafsisha shamba la Kapunga ni nini hatma ya wananchi waliopata hasara kutokana na hasira za mwekezaji.

Katika mkutano wao na waziri Lukuvi wakazi hao walihoji ni nani anayepaswa kuwajibika kwa hasara walizopata.Wapo waliobomolewa nyumba zao na viwanja vyao vikatumika kujenga uwanja wa ndege wa mwekezaji,wapo waliobomolewa tofali walizokuwa wamefyatua na kuzichoma wakisubiri kujenga.Zipo familia zilizopoteza wapendwa wao kwa kusombwa na maji baada ya mwekezaji kubomoa madaraja.

Hili bado ni swali lisilopatiwa majibu.Kwa kuwa makosa yalifanyika wakati wa kuuza shamba wanakijiji wanaona ni wazi yupo mtu anayepaswa kuwajibika katika kulipa fidia ya hasara waliyoipata.Hii itaongeza ushirikiano baina yao na mwekezaji ambaye sasa anabakiwa na kipande cha ardhi kilicho halali.



Nawatakia kila la kheri wakazi wa Kapunga katika maisha yao mapya kwenye ardhi yao halali.Muhimu kwao ni kukumbuka ardhi waliyorudishiwa isije ikawaingiza kwenye migogoro mingine ya wao kwa wao.Umakini katika kupanga matumizi sahihi ya ardhi hiyo unahitajika.Ni wakati pia kwao kukaa na mwekezaji na kumaliza tofauti zao.Hii itadumisha udugu baina yao na kuishi maisha ya furaha wakiwa majirani wenye kupendana.

MWISHOOOO

No comments:

Post a Comment