Na Joachim Nyambo.
JANUARI 12 hadi 14 mwaka 2012
zilikuwa tarehe nyingine za majonzi kwa wakazi wa Kapunga.Kwa kutumia ndege ya
kunyunyizia dawa mwekezaji wa katika shamba la Kapunga ambapo alimwaga sumu
katika mashamba ya wakulima wadogo yaliopo jirani na eneo lake.Zaidi ya wakazi 150
wa Kijiji cha Kapunga waliathirika na tukio hilo.
Meneja wa shamba hilo Walder
Vermaak, Afisa ugani Serger Bekker na Rubani wa ndege Andries Daffe walitajwa
kushiriki ukatili huo kwa kuharibu mazao ya wakulima hekari 489.5.Hii iliongeza
kilio na masikitiko makubwa kwa wakazi wa kijiji hiki.Wengi wakajiuliza hivi
kweli nia ya Baba wa taifa hili ilikuwa ni kuona wananchi tunatokwa machozi
katika ardhi yetu kila kukicha.
Licha ya kuharibiwa kwa mazao pia
wapo wananchi waliodhurika na sumu iliyonyunyiziwa kwenye mashaamba. Baadhi ya
wananchi walioathiriwa na sumu hiyo wakati ndege ikimwaga mashambani na
kushuhudiwa ni pamoja na Michael Shija, Severina Mbwilo, Elikana Nsemwa, Edward
Simkoko, Gaidon Peter Ngogo (54), Jailo Esau (22), Jackson Mwandemange
(52), Catherina Shipela (50), Edda Ngosha (35), Julius Isega(50), Ramadhan
Nyoni (52).Wengi kati yao walidhurika kwa kuharibika ngozi za miili yao
hususani miguuni na mikononi.Wengi pia walikumbwa na hili walipokuwa
wakishuhudia unyunyiziaji wa sumu hiyo.Hawakuwa na la kufanya ili kuzuia hili.
Shukrani kwa vyombo vya dola,vikaweza
kusikia kilio cha wananchi na kuchukua stahiki dhidi ya watuhumiwa. Meneja wa
shamba Walder Vermaak, Afisa ugani Serger Bekker na Rubani wa ndege Andries
Daffe wakafikishwa mahakamani.
Hatua ya kufikishwa mahakamani kwa
Mwekezaji wa shamba la la Kapunga Rice Project yaani Kampuni ya Export Trading
Group ikachukuliwa na wakazi wilayani hapa kama mwanzo wa kufikiwa muafaka wa
matukio yanayokiuka haki za binadamu ambayo walikuwa wakitendewa na mwekezaji
huyo.
Baadhi ya wakazi katika kijiji cha
Kapunga kilicho na jumla ya vitongoji saba wakanambia hatimaye serikali imeanza
kujionea mahusiano yasiyoridhisha baina ya mwekezaji na wakazi wa maeneo
jirani.Hata hivyo wakazi hao wakaiomba serikali kuyaangalia kwa kina malalamiko
mengine ambayo walikuwa wakiyawasilisha katika ngazi mbalimbali za serikali
wakimtupia lawama mwekezaji huyo lakini yalikuwa yakipuuzwa.
Mmmoja wa wakazi hao Elia Sanga
alisema kuwa kufikishwa mahakamani kwa mwekezaji huyo kunadhihirisha uongozi wa
serikali katika ngazi za Wilaya na Mkoa kuanza kuyafanyia kazi malalamiko ya
wakazi hao.
Februari 14 mwaka 2012 ndipo Mwekezaji
huyo apofikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbeya akishitakiwa kwa makosa
mawili tofauti.Kosa la kwanza ni kula njama ya kutenda kosa la kuharibu mali na
la pili kuharibu mali za wananchi kwa hila.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa
makosa hayo yaliyafanywa Januari 12 hadi 14, mwaka huu kwa kutumia ndege
ya kunyunyizia dawa ambapo alimwaga sumu katika mashamba ya wakulima zaidi ya
154 wa Kijiji cha Kapunga wilayani humo.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya
Hakimu wa mahakama hiyo Seif Kulita, Mwendesha mashitaka wa Serikali Griffin
Mwakapeje alisema kuwa washitakiwa hao akiwemo Meneja wa shamba hilo Walder
Vermaak, Afisa ugani Serger Bekker na Rubani wa ndege Andries Daffe walitenda
kosa hilo wilayani humo na kuharibu mazao ya wakulima hekari 489.5.
Mwakapeje alisema kuwa wawekezaji
hao wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume na sheria namba 226 (i) cha
marekebisho ya sheria ya mwaka 2002 la kuharibu mazao hayo ya Mpunga wa
wakulima wanaolima eneo linalojulikana kwa jina la Mpunga moja.
Baada ya mashitaka hayo, Hakimu
Kulita alpowauliza washitakiwa hao wote kwa pamoja walikana shitaka hilo ambapo
wakili aliyekuwa akiwatetea washitakiwa hao Ladislaus Rwekaza aliomba dhamana
kwa wateja wake na hatimaye mahakama ikaridhia kwa Masharti ya kila mtuhumiwa
kuwa na mdhamini mmoja mweye mali isiyohamishika isiyopungua Shilingi Milioni kumi.
Aidha Hakimu huyo alitoa sharti kwa
washitakiwa hao kuwa mbali na sharti la kuwa na mdhamini mmoja na mali
isiyohamishika pia watuhumiwa waliytakiwa kukabidhi hati za kusafiria na kwamba
hawapaswi kusafiri nje ya mkoa wa Mbeya na kama watahitaji kusafiri nje ya mkoa
wa Mbeya ni lazma wapate kibali cha mahakama hiyo ambapo washitakiwa walitimiza
masharti hayo.
Hapo ndipo washitakiwa hao
walidhaminiwa na Uwesu Msumi mkazi wa Jijini Dar Es Salaam ambaye aliikabidhi
mahakama hiyo hati ya nyumba yenye namba 229 Block J iliyopo Mbezi Jijini Dar
es Salaam, Christian Basil Mmas aliyekabidhi hati ya nyumba yenye namba 109
iliyopo Geza Ulole Jijini Dar es Salaam na Sunnil aliyetoa hati namba 254
iliyopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam pia na kesi ikaahirishwa hadi Machi 6,
mwaka huo ilipotarajiwa kutajwa tena.
Hata hivyo wakazi wa Kapunga
wanasema shitaka hilo limedumu kwa muda mrefu mahakamani pasipo
kumalizika.Waliwahi kushauriana na
uongozi wa kampuni husika kuona uwezekano wa kuliondoa shauri hilo mahakamani
ili wakae na kukubaliana nje ya mahakama.Hii ilitokana na nia iliyooneshwa na
mwekerzaji ya kukiri makosa ya kuharibu mazao.
Mbele ya waziri wa Ardhi,Nyumba na
Maendeleo ya makazi Willium Lukuvi Mapema Januari mwaka huu wakazi hao walisema
iwapo mwekezaji yuko tayari wanaweza kuliondoa shauri hilo mahakamani ili
walizungumzie nje.Wazo hilo lilinaonekana kukubalika pia na mwekezaji.
Akizungumza kwenye mkutano
aliowajulisha wakazi hao kurejeshwa kwa kijiji hekta 1,870
zilizoporwa awali na kuingizwa kwa mwekezaji,waziri Lukuvi alisema ni jambo
jema iwapo wataondoa shitaka mahakamani na kulizungumzia nje ya mahakama ili
kuweka wigo mpana wa kulijadili.Alimtaka mbunge wa jimbo la Mbarali Haroun Pirimohamed
kushiriki katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Kwa
upande wake Pirimohamed aliahidi kushirikiana na pande zote mbili sambamba na
mahakama kuondoa shitaka hilo mahakamani.Aliahidi kuhakikisha mgogoro baina ya
pande hizo mbili kumalizika nje ya mahakama akijigamba kuwa pande hizo zote
anazimudu.
“Babu
yangu aliwahi kunambia kuwa shitaka linapokuwa mahakamani ni sawa na watu
wawili wanagombania Ng’ombe mmoja ambapo mmoja kati yao anavuta pembe huku
mwenzie akivuta mkia lakini wote wawili wanajisahau kuwa wamemsahau mtu
katikati ambaye anamkamua ng’ombe huo pasipo kubughudhiwa” alisema Pirimohamed
kwenye mkutano uliowakutanisha waziri Lukuvi,Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas
Kandoro,Mkuu wa wilaya ya Mbarali Gulamhussein Kifu na watendaji wengine wa
mkoa na wilaya.
........................ITAENDELEA KESHO...................
No comments:
Post a Comment