Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, February 14, 2016

MAISHA YA MATESO KIJIJINI KAPUNGA 2

Na Joachim Nyambo.

“SIWEZI kuisahau siku ya Julai 7 mwaka 2011 maishani mwangu.Maana ni siku yenye historia kubwa kwangu.Ni siku niliyojikuta siwezi tena kutunza heshima ya ndoa kwa wake zangu”  yalikuwa maneno yake Mwiguru Nguro alipozungumza nami mnamo Machi 2012.Ni siku nyingine tena nilipokitembelea kijiji cha Kapunga wilayani Chunya na kuzungumza na mkazi huyu.


Mwigulu ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 45 alikuwa ni muwe wa wake wawili.Kati ya wake hao mke mkubwa alikuwa amebahatika kuzaa watoto watatu na mke mdogo mtoto mmoja.Yeye pamoja na wake zake na watoto hao walikuwa wakishi katika kitongoji cha Mkanada kijijini Kapunga.

Kijiji wanachoishi ni kile ambacho wakazi wake walikuwa na mgogoro wa muda mrefu na kampuni ya Expot Trading kuhusiana na mpaka kama nilivyokusimulia kwenye toleo la kwanza la makala haya.Wakazi wa kijiji hicho walikuwa wakidai kijiji chao kipo kihalali lakini mwekezaji akipinga na kusema kijiji kiko ndani ya shamba lake.

Mvutano huo wa kimipaka ndiyo ulikuwa chanzo cha matukio mengi na malalamiko mbalimbali kwa pande zote.Tukio la Mwigulu ni miongoni mwa yale ya kinyama yaliyoelezwa na kijiji kuwa yamefanywa na mwekezaji kwa wakati huo.

Mwigulu ambaye ni mfugaji wa kabila la Kisukuma alisema tarehe hiyo asiyoweza kuisahau alikuwa na mwenzake waliyekuwa wakiendelea kulisha mifugo yao kama kawaida yao.Anasema siku hiyo walikuwa wakichunga ng’ombe wao karibu na shamba la mwekezaji.

Alisema wakati wanaendelea na shughuli hiyo ghafla mmoja wa watumishi wa kampuni ndogo ya Kapunga Rice Project iliyo chini ya Expot Trading Company aliyemtaja kwa jina moja la Gerry akiwa na walinzi walifika na gari ya kampuni na kuanza kuwafanyia vurugu.Lengo lao lilikuwa kuwakamata ng’ombe wao wakidai wameingizwa katika eneo la mwekezaji.

“Walijaribu kuwaswaga ng’ombe ili wawapeleke kambini kwao lakini sisi nasi tukawa tunawaaswaga wasiende huko.Baada ya mifugo yetu kuona inalaazimishwa na wasu isiyo na mazoea nayo baadhi ilianza kucharuka na ndipo mlinzi aliyekuwa na bunduki akapiga risasi na kumuua ng’ombe mmoja papo hapo na mwingine kumjeruhi”

“Hiyo haikutosha.Tukiwa tunaendelea kuikusanya mifugo yetu.Gerry aliingia kwenye gari na baada ya kuiwasha akaanza kunifuata nilipo kwa lengo la kunigonga.Nilijaribu kujitetea kwa kukimbia nikiikwepa gari.Mara ya kwanza alinikosa,yapili nikafanikiwa pia kukwepa laakini mara ya tatu sikuweza maana nilijikuta nimetumbukia kwenye kishimo kidogo na ndipo gari yake ikanigonga kiunoni.Inaonekana kwenye ngao ya gari yake kulikuwa na chuma kilichonichoma vibaya sehemu ya haja kubwa”

“Nilipata maumivu makali mno kiasi nikapoteza fahamu.Wasamariaa wema walinibeba na kunipeleka katika hospitali ya Chimala.Nilikaa hapo lakini baadaye ikaonekana huduma ninayopaswa kupewa haiwezi kupatikana hapo maana nilikuwa nimeumia vibaya”

Alisema kutokana kuhitaji huduma katika hospitali iliyo na uwezo zaidi ya hiyo ilimlazimu kwenda katika hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mbeya vijijini.Aliendelea na matibabu tangu Julai 18 hadi Septemba 7 mwaka 2011.

Akiwa hospitalini hapo aliambiwa na madaktari kuwa mfumo wake wa uzazi ulikuwa umehaaribiwa hasa baada ya kuoza kwakuwa alichelewa kufanyiwa oparesheni.Alipaswa kufanyiwa oparesheni hiyo muda mfupi tu baada ya kugongwa lakini kutokana na kuchelewa baadhi ya mishipa ilikwisha anza kuoza.

“Niliambiwa kuwa baada tu ya kufikishwa katika hospitali ya Chimala nilipaswa kufanyiwa oparesheni hiyo na kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupona na hatimaaye kuwa na uwezo wa kusimamisha uume kama awali.Ina maana kule walipaswa kunisafisha na kisha kushona jeraha langu.Kutokana na kuchelewa kufanyiwa lilivunda na kuozesha baadhi ya mishipa hivyo nikaambiwa huenda nikapona lakini inaweza kuchukuaa muda mrefu kidogo”

“Katika kipindi hicho chote mhusika hakuwahi kunitembelea hata siku moja wala kuchangia gharama za matibabu yangu.Mpaka hivi sasa nazungumza na wewe hakuna chochote  ninachoweza kufanya.Si kazi wala tendo la ndoa maana kiuno change hakijapona natembea kwa msaada wa magongo na pia uume wangu hauwezi kusimama kama awali”.

Hata hivyo Mwiguru alinambia hajakata tamaa.Bado alikuwa na imani kuwa huenda akapona na siku moja akaendelea kutunza heshima katika ndoa zake.Aliwashukuru wake zake wote kwa kuendelea kumheshimu licha ya yeye kukosa uwezo wa kuwaridhisha kwa kuwapa haki yao ya msingi ya tendo la ndoa kwa wakati huo.

“Pamoja na matatizo yangu wameendelea kuwa na uvumilivu naamini ni kwakuwa wao pia wana subira wakiamini ipo siku nitapona naa kurejea katika hali yangu ya kawaida.Hakuna yeyote kati yao aliyenidharaau kwa kuisaliti ndoa yetu”

“Si kwamba wanakijiji wanamjengea majungu mwekezaji bali vitendo anavyowafanyia  haviwapendezi maana ni vya kinyama.Chukulia mfano kama sisi tulikuwa na makosa kwa nini asifuate njia zinazostahili.Vyombo vya sheria vipo ambavyo vingetuita na kutuwajibisha.Kwa nini ajichukulie sheria mikononi na kunipa ulemavu kama huu.Kwa nini aue mifugo yetu”.Anasema

“Kama mimi migogoro ya mashamba alio nayo na wanakijiji wenzangu wala hainigusi sana maana haihusishi eneo la makazi yangu wala mashamba yangu sasa kwa nini nianze kumjengea visa.Tatizo ni haya anayotufanyia.Kutufanyia unyama wa namna hii na pia kuuwa na kujeruhi mifugo yetu”

 “Sasa tunajiuliza hivi serikali ilimleta mwekezaji itusaidie wananchi au ndiyo ilimleta atuangamize.Maana anachokifanya si kutusaidia wanaKapunga bali kutuangamizaa.Si mimi tu amewahi kung’oa madaraja yanayotumiwa na wakazi wa kijiji hiki kuvuka kwenda eneo la Mpunga mmoja kuliko na mashamba yao.Alifanya shughuli hiyo usiku na mvua kubwa zikanyesha matokeo yake watu wameamka wanakwenda kuvuka wakijua daraja lipo wakasombwa na maji.Wapo waliopoteza maisha kwa kufa maji siku hiyo ”

Haya yalikuwa mateso mengine makubwa yaliyowakumba wakazi wa kijiji cha Kapunga kutokana na ardhi yao waliyoamua kumkabidhi Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya taifa lao.Hay pia yaliendelea kuzua hisia kwa wakazi hawa kutamani Baba wa taifa hili afufuke ili arejeshe ardhi yao kwakuwa sasa ilikuwa imegeuka Jehanamu kwao.

.................... ITAENDELEA KESHO...................

No comments:

Post a Comment