Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, October 30, 2013

WATANO WANUSURIKA KATIKA AJALI ZA MALORI

WATU watano wamenusurika kifo katika ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani Mbeya jana (oktoba 29) katika maeneo na nyakati tofauti. Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa 5:00 asubuhi katika kijiji cha Isyonje wilayani Mbeya ambapo gari lenye namba T 885 CBS aina ya Scania yenye tela namba T 319 CBU iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kuelekea nchini Malawi ikiwa na mifuko 600 ya Mbolea aina ya Urea iliacha njia na kupindika. Lyamba Lya Mfipa ilifika eneo la tukio na kushuhudia wakazi wa maeneo ya jirani wakijibebea mifuko ya Mbolea kwa kubeba kichwani na wengine pikipiki. Baadhi ya wakazi na polisi waliokutwa eneo la tukio na kuomba kutoandikwa majina yao kwakuwa si wasemaji walimtaja dereva kuwa ni George Mwanakulya ambaye hadi wakatio huo yeye na kondakta wake walikuwa wamekimbizwa hospitali ya rufaa Mbeya kwaajili ya matibabu. Ajali ya pili ilitokea majira ya saa 5:40 katika eneo la mlima wa Igawiro ambapo gari yenye namba T 320 BRQ na aina ya Scania na tela namba T 539 BRP ikiwa imebeba mzigo wa viazi mviringo liliacha njia na kupinduka na kusababisha majeraha kwa watu watatu akiwemo dereva lakini wote hawakufahamika.

MBEYA CITY,TANZANIA PRISONS ZAINGIZA MILIONI 31

MCHEZO wa ligi kuu Tanzania bara uliozikutanisha Mbeya City na Tanzania Prisons zote za mkoani Mbeya uliingiza jumla ya shilingi 31,67400. Akitangaza mapato hayo kwa waandishi wa habari,katibu wa chama cha soka mkoani Mbeya Haroub Suleiman alisema katika mchezo huo uliochezwa jumanne hii ndani ya uwanja wa Sokoine jijini hapa jumla ya watazamani 10,558 waliingia uwanjani kwa kiingilio cha shilingi 3000 kila mmoja. Seleman alisema mgawanyo wa mapato hayo ulifanyika kwa kila timu kuvuna kiasi cha shilingi 6,987,022 kila moja kodi ya ongezeko la thamani ikiwa ni shilingi 4,831,627. Alisema gharama za uwanja ilikuwa shilingi 3,552,723.42,gharama za tiketi shilingi 3,157,550.20,gharama za mechi 2,131,634 na kamati ya ligi shilingi 2,131,634. Mfuko wa maendeleo ya mpira ya Shirikisho la Soka nchini(TFF) ulivuna shilingi 1,065,817 huku chama cha soka mkoa yaani MREFA kikiambulia shilingi 828,968.79. Katibu huyo aliwashukuru mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo ambao ulimalizika kwa wenyeji wa mchezo Tanzani Prison kuambulia kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa wadogo zao wabishi wa ligi Mbeya City.

Tuesday, October 29, 2013

Mbeya City waichapa Tanzania Prisons 2-0

MCHEZO wa ligi kuu ya Tanzania bara kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons zote za jijini Mbeya umemalizika kwa wenyeji wa mchezo huo Prisons kuambulia kipigo cha goli 2-0. Ndani ya uwanja wa sokoine hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyokuwa imefanikiwa kulioana lango la mwenzake na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa bila kwa bila huku katika kipindi hicho timu zote zikiwa zimeonyesha uwezo sawa. Mabadiliko waliyoyafanya Mbeya City baada ya kuanza kwa kipindi cha pili ya kumtoa Alex Seth na kumwingiza Peter Mapunda yalionekana kuanza kuleta neema kwa timu hiyo baada ya Dakika ya 62 Mapunda kupachika bao safi akitumia mbwembwe zilizofanywa na mmoja wa walinzi wa Tanzania Prisons Julius Kiwan. Goli hilo lilionekana kuwapa wakati mgumu wajelajela kiasi cha wachezaji kuweza kupoteana uwanjani na ndipo dakika ya 69 Laurian Mpalile wa timu hiyo akajikuta anafanya madhambi eneo la hatari kwa kumvuta Deus Kaseke wa Mbeya City na mwamuzi Israel Nkonga kutoka Dar es salaam kuamuru ipigwe penati. Penati iliyopigwa kiufundi na Deogratius Julius iliiwezesha Mbeya City kujipatia goli la pili na kuiwezesha kuibuka na ushindi wa goli mbili 2-0 mbele ya ndugu zao Tanzania Prison.

Monday, October 28, 2013

AJALI MBAYA YAUA WATANO,22 WAJERUHIWA VIBAYA

WATU watano wamefariki dunia na wengine 22 kujeruhiwa vibaya baada ya Coasta walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka chanzo kikiwa ni mwendokasi uliofanya dereva kushindwa kuhimili. Ajali hiyo ilitokea leo (oktoba 28)majira ya saa sita mchana katika Mteremko wa Mlima Senjele uliopo mpakani mwa wilaya za Mbeya na Mbozi wakati coasta hiyo ikitokea Tunduma wilayani Momba kuja jijini Mbeya. Dereva wa gari hiyo yenye namba za usajili T 378 ADR aina ya Toyota Costa aliyefahamika kwa jina la Semu Mwakajwanga anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 60 na 70 alitoroka baada ya tukio na haijafahamika aliko. Akizungumza na waandishi wa habari,Muuguzi mkuu wa Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mbalizi ambako majeruhi wote walipelekwa, Sikitu Mbilinyi alikiri kupokea majeruhi 22 na kubainisha kuwa nane kati yao ni wanaume ambao hali zao zilikuwa zikiendelea vizuri kutokana na kutoumia sana ingawa walipata michubuko usoni na sehemu za mikono na miguu. Mbilinyi alibainisha kuwa kati ya majeruhi 10 wanawake walipokelewa wakiwa katika hali ya kuumia sana na kupatiwa matibabu ambapo kati yao wanne walipewa rufaa kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi kutokana na kuwa na majeraha ya kuumia vichwa na kuvunjika miguu. “Pia tumepokea majeruhi wanne ambao ni watoto wadogo ambao hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.Taarifa za eneo la tukio ni kwamba watu wanne walikufa papo hapo na mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano”alisema Mbilinyi Akizungumzia ajali hiyo,kondakta wa gari hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Ulimboka Noah(26) alisema chanzo cha ajali ni kutokana na gari kugoma kubadili gia gia ambapo dereva alivyojaribu kubadili ilishindikana ndipo alipojaribu kushuka nalo hivyo hivyo lakini kabla ya kufika darajani ilikuwa kama kitu kimelichota gari na kupinduka. Ulimboka alisema kutokana na jinsi lilivyopinduka gari hiyo inasemekana ni kutokana na kukatika kwa Propela Shafti ambayo ilijikita chini kisha kupindua gari au U- Bolt inaweza ikawa imeachia kwa kile alichosema eneo lilikuwa zuri na hakukuwa na kitu kilichogusa gari hadi likapinduka. Hadi tunakwenda mitamboni miili ya marehemu iliyohifadhiwa hospitali teule ya Ifisi na majeruhi walikuwa hawajatambuliwa majina na askari wa jeshi la polisi walikuwa wakiendelea kuchukua maelezo hospitalini hapo. PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA MBEYA YETU

MAHAFALI YA 14 YA KIDATO CHA NNE KATIKA SHULE YA SEKONDARI SOUTHERN HIGHLAND YALIVYONOGA

ILIANZA KWA VIPAJI MBALIMBALI KAMA INAVYOONEKANA HAPA KIKUNDI CHA KUCHEZA NYIMBO ZA AINA MBALIMBALI KIKITOA BURUDANIWAHITIMU WA KIDATO CHA NNE KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA SOUTHERN HIGHLAND YA JIJINI MBEYA WAKICHEZA KWA PAMOJA NA WAZAZI NA WAALIKWA WENGINE KWENYE MAHAFALI YA 14 YALIYOFANYIKA KWENYE UKUMBI WA MTENDA SOWETO JIJINI MBEYA

MAHAFALI YA SM IHANGA YANOGA

Wahitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Ihanga iliyopo katika mji mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali wakiwa katika mahafali ya nane ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo

BREAKING NEWSSSSSSSS

WATU WATATU WANAHOFIWA KUFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA COASTA ILIYOTOKEA HIVI PUNDE KATIKA KIJIJI CHA SONGWE WILAYANI MBEYA.....ENDELEA KUWA NASI KWA HABARI ZAIDI....

Sunday, October 27, 2013

AFA MAHAKAMANI AKISIKILIZA KESI YA MWANAYE

MAHAKAMA ya wilaya ya Rungwe juzi ilijikuta inasitisha kwa dakika kadhaa kusikiliza kesi baada ya mkazi wa kaya ya Masukuru wilayani hapa aliyefahamika kwa jina la Tiger Mwaigomole (70) kufariki dunia ghafla akiwa ndani ya chnumba cha mahakama wakati mashitaka yakiendelea. Mwaigomole alianguka ghafla mahakamani hapo na kufariki dunia alipokuwa akiendelea kufuatilia kesi ya kupigana na kujeruhi inayomkabili mtoto wake anayefahamika kwa jina la Gwakisa Tiger(40) iliyokuwa ikiendelea mahakamani hapo. Tukio hilo ambalo ni nadra sana kutokea,lilitokea majira ya saa 9 alasiri ndani ya Mahakama hiyo ambapo marehemu alifika mahakamani hapo akiwa na mwanaye aliyejulikana kwa jina la Lusajo Tiger wakiwa na lengo la kumwekea dhamana Gwakisa Tiger ambaye alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kwa kosa la kupigana na kujeruhi katika ugomvi uliotokea kijijini kwao. Kwa mujibu wa Lusajo wakati kesi ikiendelea mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Omary Kingwele, ndugu yao alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili ndipo marehemu alipoanza kutetemeka kwa madai kuwa anajisikia baridi kali sana. Alisema kutokana na marehemu kulalamikia baridi aliamua kumnunulia chai ya moto ili anywe na kupunguza baridi ambapo baada ya kufanya hivyo marehemu alikata roho muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai aliyokuwa amepelekewa huku akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama hiyo. Kutokana na tukio hilo askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo waliuchukua mwili wa marehemu na kuukimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana kwa ajili ya vipimo lakini hata hivyo mwili ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi ingawa ripoti ya kifo chake haikutolewa mapema. Wakati huo huo hukumu ya kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe na pia mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya hiyo, John Mwankenja inayowakabili Hakimu Mwakalinga na wenzie watatu huenda ikatolewa kesho(Oktoba 29). Uhakika wa kufika kwa ukomo wa shitaka hilo unatokana na mahakama kuu kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi kwa upande wa washitakiwa wote. Mwishoni mwa wiki jana Jaji Karua alisema baada ya kumaliza kusikiliza pande zote mbili atatumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kuandika hukumu ambayo anatarajiwa kuitoa jumanne hii kesi ambayo inasimamiwa na Mwanasheria wa Serikali Archiles Mulisa wakati washitakiwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.

WATANO WAUAWA KINYAMA CHUNYA

WATU watano wameuawa kikatili katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Chunya mkoani Mbeya moja likisababishwa na imani za kishirikina na la pili ikiwa ni wivu wa mapenzi. Tukio la kwanza lilitokea Oktoba 25 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku katika kijiji cha Mpona kata ya Totowe tarafa ya Songwe ambapo kikongwe na mkazi wa kijiji hicho Jampany Mhamali(78) akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea kwenye kilabu cha pombe za kienyeji alivamiwa na watu wawili wasiofahamika na kukatwakatwa mapanga kichwani na mkono wake wa kulia hadi kufa. Baada ya wakazi wa kijiji hicho kupata taarifa za mauaji hayo walijikusanya wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mawe na kuanzisha msako mkali kwa kufuata nyayo za viatu vya watu waliotuhumiwa kuhusika na baadaye wakafanikiwa kuwakamata watu hao ambao hawakufahamika majina na kuanza kuwashushia kipigo na kuwaua wote wawili. Hata hivyo wakati wakiendelea kupigwa watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji ya kikongwe Mhamali na kueleza kuwa wao walitumwa na Maneno Adamson maarufu kwa jina la Lyambo ambaye alikuwa akimtuhumu kikongwe huyo kuwa ni mchawi. Wanachi hao baada ya kuwaua watuhumiwa wawili walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa mtuhumiwa wa tatu akliyetajwa kuwaagiza watu hao lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kumkuta kwani alikuwa amekwisha toroka. Tukio la pili ni la kuuawa kwa kuteketezwa kwa moto kwa Adelina Philimon(45) mkazi wa kijiji cha Magamba wilayani hapa na Wasiwasi Mwashiombo(28) mkazi wa kijiji cha Ipoloto Wilayani Mbozi. Wapenzi hao ambao kiumri ni sawa na mama na mtoto wake waliteketea kwa moto baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kuchomwa moto na mtu aliyetajwa kwa jina la Zacharia Mwingila(39) mkazi wa Tunduma wilayani Momba. Chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi ambapo mtuhumiwa ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi alifikia hatua ya kuchoma moto nyumba baada ya kumkuta mpenzi wake akiwa amelala na mwanaume mwingine amjira ya saa tano za usiku wa oktoba 25 mwaka huu katika kijiji cha Magamba wilayani Chunya. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Robert Mayala alithibitisha kutokea kwa matukio hayo yote mawili na kuisihi jamii kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mikononi na pia kuishi kwa kuwatumhumu wakazi wenzao wakiwahusisha na imani za kishirikina.

Monday, October 21, 2013

MWANDISHI ALIYEPIGWA RISASI AANZA KUFUNGUKA

MWANDISHI wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye hivi karibuni alikumbwa na madhila ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na mzazi mwenzie, ameanza kufunguka kidogo kidogo na kueleza kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea. Akizungumza kwa sauti ndogo na taratibu na gazeti hili kando ya kitanda alicholazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanahabari huyo alieleza kushangazwa na ujasiri na nguvu za aina yake ambazo zilimwezesha kutambaa na kujiburuza hadi eneo la karibu ya barabara ili kuomba msaada wa kukimbizwa hospitali. Ufoo ambaye alionyesha dhahiri kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazozingira tukio lake, alisema tayari alikuwa amewahakikishia polisi waliofika kumjulia hali hospitalini hapo kwamba alikuwa akisubiri afya yake iimarike kabla hajaeleza kwa kina kila anachokijua kuhusiana na tukio hilo. “Alifika hapa kunijulia hali na kuangalia maendeleo yangu afande Msangi na nikasema nitakuwa tayari kueleza kila ninachokijua baada ya afya yangu kuimarika. Nasikitika kuna watu wanasema mambo wakifikia hatua ya kutaka kuonekana wananifahamu vizuri kuliko hata ninavyojifahamu mwenyewe,” alisema akionyesha kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa kuhusu sakata lake. Ufoo ambaye alifikishwa hospitalini hapo Jumapili ya wiki iliyopita kutokana na kujeruhiwa kwa risasi na mwanaume aliyezaa naye mtoto mmoja alisema anamshukuru sana Mungu kwa uzima alionao sambamba na kuelezwa kupata faraja kubwa na kutiwa moyo na mwajiri wake, ndugu, jamaa na marafiki. Mwanahabari huyo ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi mwilini mwake siku chache zilizopita, amelazwa katika chumba cha peke yake ambacho ingawa kina seti ya televisheni alisema alikuwa haruhusiwi kuiangalia kwa ushauri na maelekezo ya madaktari. Huku akionekana wa chini ya uangalizi mwingine wa karibu na wa kudumu wa muuguzi ambaye muda wote wa mazungumzo haya alionekana kuwapo katika chumba hicho, Ufoo alisema alikuwa ana mapenzi makubwa kwa mzazi mwenzake huyo ambaye alipoteza maisha katika tukio hilo. “Nilimpenda sana Antheri. Alikuwa kijana mtaratibu na mpole sana. Najua kile kilichotokea ni shetani tu na binafsi nilishasamehe alfajiri ile ile baada ya tukio lile,” alieleza Ufoo ambaye pia alimpoteza mama yake mzazi katika mkasa huo. Ufoo ambaye mara kadhaa katika mazungumzo na gazeti hili alionekana kukunja uso akiashiria kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya bega katika mkono wake wa kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo alipopigwa risasi ya kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti muda mfupi baada ya Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake mzazi. Akijaribu kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi mwenzake huyo alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya kazi usiku huo huo wa tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Kabla ya kufika Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo hakuzieleza, alimkariri mzazi mwenzake huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa kujiua yeye na mtoto wao. “Hata sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka nyumbani Antheri alianza kwa kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na mtoto wetu,” alisema Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea na simulizi yake ya kusikitisha. Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema pamoja na kumwambia maneno hayo bado Mushi alimsisitiza kwamba waende kwa mama yake (Ufoo) baadae warudi kumchukua mtoto wao japo Ufoo hakusema walitaka kwenda wapi baada ya hapo. Alisema walipofika nyumbani kwa mama yake walikwenda moja kwa moja sebuleni na wakiwa wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na pale ghafla Mushi akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba; “Mama nimeishafanya maamuzi” Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka maneno hayo ghafla akaingiza mkono nyuma ya suruali alikokuwa ameweka bastola yake na kisha akaichomoa. Katika maelezo yake Ufoo alisema baada ya kuichomoa bastola hiyo mama yake naye alisimama na kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo hicho kilimfanya amiminiwe risasi mfululizo. Alisema kuona hivyo aliamua kukimbia kuelekea jikoni ambapo Mushi alimuona na kuanza kumiminia risasi ambayo moja ilimpata eneo la mkono wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana titi la kulia. Kwa mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya kunusuru maisha yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi nyingine kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni ambazo zilisababisha aanguke chini Akiendelea kusimulia, anasema ingawa alikuwa akivuja damu nyingi, na huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema wakati akitambaa aligeuka nyuma na akamuona Antheri akijielekeza bastola eneo la kidevu na alipofyatua risasi alianguka chini. “Nikiwa chini nilimuona Antheri akijipiga risasi kidevuni na akaanguka chini, sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani niliendelea kujiburuza ili kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo ALIVYOJIOKOA “Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”. Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja. “Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni. “Si rahisi kuamini, yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo. Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na akakubali. “Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda. “Wakati huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye pikipiki kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha. Lakini nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini. Alisema anakumbuka wakati walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya kupima uzito wa magari makubwa walikuta barabara ikiwa imejaa magari na yeye alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita hata nje ya barabara eneo la nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo kijana yule alilifanya. “Nilipofika eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza muuguzi niliyemkuta kwamba nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba asaidie kuokoa maisha yangu. Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha polisi (PF3) lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk. Dattan ambaye tunafahamiana” “Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na nikamweleza yaliyonipata na mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea dripu, na nikamsikia akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa hali niliyonayo kama wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo zingeweza kusababisha kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri hapo Tumbi. Kwa mujibu wa Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia daktari aliyekuwa akimhudumia akiomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili limchukue na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wito ambao ulijibiwa kwa maelezo kwamba lilikuwa halina mafuta. Majibu hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe kuletewa gari la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na muda mfupi baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa Muhimbili. Alisema wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa akipatwa na maumivu makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa ikipanda matuta ya barabarani na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza pumzi na kuishiwa nguvu.

Monday, October 14, 2013

WATOTO NA TEKNOLOJIA

Mtoto Nelson Joachim Nyambo akijaribu kumpigia mtu ambaye sikuweza kumfahamu simu kwa kutumia rimoti ya deki ya DVD.KAAZI KWELI KWELI

MOTO WATEKETEZA MKE NA MUME

MUME na mke wamefariki dunia kwa kuungua moto baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto. Wanandoa hao wamefahamika kwa majina ya Fadhir Said(45) na Lucy Said ambaye umri haufahamiki wote wakazi wa Ilemi jijini Mbeya. Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Mbeya Diwani Athuman tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku wa kuamkia leo(Oktoba 14) nyumbani kwao huko Ilemi. Kamanda Athuman alisema chanzo cha moto ulioteketeza nyumba hiyo yenye vyumba sita hakijajulikana na kuwa watoto wanne waliokolewa kabla ya kupata madhara. “Wananchi na polisi waliofika eneo la tukio walifanikiwa kuzima moto huo lakini ukiwa tayari umesababisha madhara ya vifo hivyo pamoja na kuteketeza mali mbalimbali ambazo thamani yake bado haijajulikana” alisema. Wakati huo huo jeshi hilo linamshikilia fundi magari mkazi wa kijiji cha Ilembo wilayani Mbozi Erick Kyando(32) baada ya kukamatwa akuiwa na noti bandia zenye thamani ya shilingi 100,000. Kamanda huyo alisema mtuhumiwa alikamatwa oktoba 13,saa 12 jioni katika mji mdogo wa Mlowo wilayani hapo akiwa na noti kumi bandia za shilingi elfu kumi kila moja zikiwa mpya. Mshitakiwa huyo alikamatwa wakati alipofika kwa wakala wa M-Pesa aitwaye Lydia Mwakipesile akitaka kuziweka katika akaunti yake.

MWANDISHI WA GAZETI LA UHURU APIGWA RISASI

Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo wilayani Momba mkoani Mbeya Shomi Mtaki amepigwa risasi baada ya kuvamiwa na majambazi shambani kwake katika kijiji cha Mpemba wilayani hapo. Mtaki ambaye alikuwa katika nyumba iliyopo shambani kwake alivamiwa usiku wa Octoba 10 na watu watano waliokuwa na silaha aina ya bunduki kisha kumlazimisha kutoa fedha. Wanablogu waliomtembelea shambani kwake walishuhudia majeraha aliyokuwa nayo Mtaki katika maeneo mbalimbali ya mwili wake ambapo alisema kuwa siku hiyo majira ya saa 9:00 usiku alisikia mchakato wa miguu nje ya nyumba yake na kwamba alipochungulia aliwaona vivuli vya watu wakiwa wamesimama karibu na trekta lake nje ya nyumba. Alisema kuwa alipowashitua watu hao walitamka wazi wazi kuwa wanataka fedha na muda huo huo akasikia kishindo kikubwa katika mlango wa kuingilia sebuleni ambapo wavamizi hao walikuwa wamepiga jiwe aina ya FATUMA kwa lengo la kuuvunja mlango ili waingie ndani. Alisema kuwa mara akasikia mlio wa risasi ikipigwa katika mlango wake na mara ukafunguka na vijana watatu waliingia sebuleni ambapo walichukua jiwe walilotumia kuvunja mlango wa sebuleni na kupiga katika mlango wa chumbani na kisha baadaye walimimina risasi katika mlango huo ambazo zilimpata katika mguu wa kushoto na kumjeruhi. Mtaki alisema kuwa yeye na mkewe walikuwa wakihangaika na kujaribu kujiokoa maisha yao ambapo mkewe aliposikia mlio wa risasi aliingia chini ya mvungu wa kitanda ili kujinusuru. ‘’Nilijiona nakikaribia kifo vijana walimimina risasi katika mlango wa chumbani zikanikuta mguuni na kunijeruhi vibaya, mlango ukafunguka wakaingia vijana watatu ambao hawakujiziba sura zao,’’alisema. Alisema kuwa mara baada ya kuingia walianza kumuamrisha atoe fedha, akawajibu kuwa hana fedha ndipo walipoanza kumpiga mgongoni huku wakitishia kumuua na kwamba wakati huo mkewe alikuwa amejificha katika mvungu wa kitanda. ‘’Wale wavamizi walianza kupekuwa vitu mbalimbali, wakachukua simu yangu ya mkononi ambayo mtu wa mwisho kuwasiliana naye alikuwa ni shemeji yangu ambaye ni Mwanajeshi,’’alisema na kuongeza. ‘’Wavamizi wale walichukua simu tatu, simu moja ikajipiga kwa bahati shemeji yangu aliipokea, akasikia vurumai iliyokuwa ikiendelea nyumbani na namna ambavyo tulivyokuwa tukijitetea ili tusiuawe, muda huo huo akaenda kutoa taarifa polisi,’’alisema. Alisema kuwa wavamizi hao waliingia katika mji wake majira ya saa 8:45 na kuendelea kuwepo pale hadi majira ya saa 9;00 usiku ambapo walichukua simu tatu, tv seat ya nchi 22, ving’amuzi viwili kimoja cha Startimes na kingine cha Zuku vyote vikiwa na thamani ya sh. Milioni 2. Alisema kuwa mara baada ya wavamizi hao kumaliza kukusanya vitu walivyoona vinafaa waliwaamrisha kuingia chumbani na wao wakatokomea upande wa mashariki na muda mfupi baadaye polisi walifika eneo la tukio wakatukuta mien a mke wangu tukiwa tumekumbatiana huku tukilia na kumuomba Mungu. KWA HISABNI YA MIRTANDAO MBALIMBALI

Thursday, October 10, 2013

WATATU WAAMSHA MAISHA YAO NA COCACOLA KWA KUJISHINDIA PIKIPIKI

Meneja mauzo na masoko wa kiwanda cha Cocacola kwanza cha mkoani Mbeya Vekaria Jayanti akimkabidhi mfano wa hundi ya kitita cha shilingi milioni moja Frank John mkazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa baada ya kubahatika katika promosheni ya Amsha maisha yako na Cocacola. MKAZI wa Chunya mkoani Mbeya Alex Mtweve na mkazi wa Soweto jijini hapa Jackson Mwamsonga ni miongoni mwa watu watatu waliojishindia pikipiki aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi milioni 2.5 kila moja katika promosheni ya Amsha Maisha yako na Cocacola. Mshindi wa tatu wa promosheni hiyo aliyejishindia pikipiki pia katika promosheni hiyo inayoendeshwa na kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola ni mkazi wa Songea mkoani Ruvuma Alex Manga. Meneja mauzo na masoko wa kiwanda cha Coca Cola Kwanza cha mkoani hapa Vekaria Jayanti alikabidhi pikipiki hizo jana kwa washindi katika hafla fupi iliyofanyika kwenye kituo kidogo cha mabasi cha Kabwe jijini hapa. Jayanti pia alikabidhi fedha taslimu kwa washindi wa viwango vya milioni moja moja kwa watu wawili na shilingi laki tano kila mmoja kwa washindi watatu. Waliokabidhiwa shilingi milioni moja kila mmoja ni mkazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa Frank John na mkazi wa Iringa Rahim Mwanuka. Waliojishindia shilingi laki tano kila mmoja na mkazi wa Mwanjelwa jijini hapa Daud Mwangomba,Edgar Sanga mkazi wa Kamsamba wilayani Momba na John Ngawanya mkazi wa Iringa. Akikabidhi zawadi kwa washindi,Jayanti aliwataka kuzitumia kuinua kipato cha familia zao ili malengo ya kampuni hiyo ya kuboresha maisha ya wateja wao yaweze kutimia. “Lengo la kampuni ni kuona maisha ya wateja wanaonunua vinywaji vyetu yanakuwa bora zaidi.Ndiyo sababu plomosheni yenyewe ikaitwa amsha maisha.Sasa ni vema mkatumia zawadi hizi kuboresha maisha ya familia zenu ili kampuni ijione imetimiza wajibu wa kuamsha maisha ya wateja wake” alisema Jayanti. Mmoja wa washindi wa pikipiki Alex Mtweve mkazi wa Chunya aliishukuru kampuni hiyo akisema imemwezesha kuachana na pikipiki ya mtu aliyokuwa akiendesha awali akisafirisha abiria maarufu kama bodaboda na sasa taendesha yak wake mwenyewe.

WACHUMBIA NDIZI MASHAMBANI KUKIONA CHA MOTO

WACHUMBIAJI wa ndizi wilayani Rungwe wamepewa muda wa wiki mbili kuainisha madai yao kwa wakulima na kuyafikisha katika ofisi za watendaji wa vijiji kwakuwa sasa ni marufuku kufanyika kwa biashara hiyo. Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispini Meela amewataka wafanyabiashara waliochumbia ndizi kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwakuwa kuanzia Novemba Mosi mwaka huu biashara hiyo haitoruhusiwa tena wilayani hapa. Meela alitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Lugombo kata ya Lufingo wilayani hapa alipozindua muungano wa vikundi vidogo vya wakulima wa ndizi na kahawa bora(WANDIKARU). Alisema kwa muda mrefu wakulima wilayani hapa wameendelea kuwa masikini kutokana na kunyonywa kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwauzia mikungu ya ndizi change ikiwa bado mashambani hivyo wao wakulima kubaki wakiitunza kungoja ikomae wenye nayo waje kuivuna. Alisema haiwezekani kumsaidia mkulima wa ndizi wilayani hapa pasipo kufanya mamuzi magumu kama hayop hivyo sasa wafanyabiashara wachumbia ndizi imefika wakati wao kutafuta utaratibu mwingine na si waliouzoea. Alisema baada ya muda uliopangwa kupita itakuwa imekula kwa wafanyabiashara kwakuwa hakuna polisi,mahakama,wala mtendaji wa kijiji atakayepokea kesi ya kuchumbia nzidi na atakayepeleka kesi ya namna hiyo huyo atakamatwa. Alisema kuanzia sasa wakulima watapaswa kupeleka ndizi zao kwenye vituo vitakavyotengwa na vijiji na huko ndiko watakutana na wafanyabiashara watakaonunua kutoka kwao. Mkakati mwingine ni kufunguliwa kwa magulio maalumu ya kuuzia ndizi ambapo kwa halmashauri ya Rungwe limetengwa eneo la Karasha na halmashauri ya Busokelo eneo litakuwa Lwangwa. Awali mwenyekiti wa Wandikaru Lusekelo Mwakibete alisema muungano huo unatokana na vikundi 16 kutoka kata tofauti za wilayani hapa huku akibainisha ukosefu wa masoko maalumu vijijini kuwa moja ya changamoto inayochangia wafanyabiashara kuwarubuni wakulima kuwauzia ndizi mashambani.

Thursday, October 3, 2013

MWENGE WA UHURU WAKIMBIZWA HALMASHAURI YA RUNGWE

WAKAZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA WAKIPUNGA MIKONO KUUAGA MWENGE WA UHURU UKIELEKEZA MBIO ZAKE WILAYANI RUNGWE Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela(kulia) akipokea mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Mbeya dk.Norman Sigala tayari kuukimbiza katika halmashauri ya Rungwe na Busokelo zilizopo wilayani kwake Mmoja wa wakimbiza mwenge kitaifa Zamda John akimvisha mhitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Luanda Diana Dickson skafu ya wilaya ya Mbeya kabla ya yeye kuvishwa ya wilaya ya Rungwe