Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, October 28, 2013

AJALI MBAYA YAUA WATANO,22 WAJERUHIWA VIBAYA

WATU watano wamefariki dunia na wengine 22 kujeruhiwa vibaya baada ya Coasta walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka chanzo kikiwa ni mwendokasi uliofanya dereva kushindwa kuhimili. Ajali hiyo ilitokea leo (oktoba 28)majira ya saa sita mchana katika Mteremko wa Mlima Senjele uliopo mpakani mwa wilaya za Mbeya na Mbozi wakati coasta hiyo ikitokea Tunduma wilayani Momba kuja jijini Mbeya. Dereva wa gari hiyo yenye namba za usajili T 378 ADR aina ya Toyota Costa aliyefahamika kwa jina la Semu Mwakajwanga anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 60 na 70 alitoroka baada ya tukio na haijafahamika aliko. Akizungumza na waandishi wa habari,Muuguzi mkuu wa Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mbalizi ambako majeruhi wote walipelekwa, Sikitu Mbilinyi alikiri kupokea majeruhi 22 na kubainisha kuwa nane kati yao ni wanaume ambao hali zao zilikuwa zikiendelea vizuri kutokana na kutoumia sana ingawa walipata michubuko usoni na sehemu za mikono na miguu. Mbilinyi alibainisha kuwa kati ya majeruhi 10 wanawake walipokelewa wakiwa katika hali ya kuumia sana na kupatiwa matibabu ambapo kati yao wanne walipewa rufaa kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi kutokana na kuwa na majeraha ya kuumia vichwa na kuvunjika miguu. “Pia tumepokea majeruhi wanne ambao ni watoto wadogo ambao hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.Taarifa za eneo la tukio ni kwamba watu wanne walikufa papo hapo na mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano”alisema Mbilinyi Akizungumzia ajali hiyo,kondakta wa gari hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Ulimboka Noah(26) alisema chanzo cha ajali ni kutokana na gari kugoma kubadili gia gia ambapo dereva alivyojaribu kubadili ilishindikana ndipo alipojaribu kushuka nalo hivyo hivyo lakini kabla ya kufika darajani ilikuwa kama kitu kimelichota gari na kupinduka. Ulimboka alisema kutokana na jinsi lilivyopinduka gari hiyo inasemekana ni kutokana na kukatika kwa Propela Shafti ambayo ilijikita chini kisha kupindua gari au U- Bolt inaweza ikawa imeachia kwa kile alichosema eneo lilikuwa zuri na hakukuwa na kitu kilichogusa gari hadi likapinduka. Hadi tunakwenda mitamboni miili ya marehemu iliyohifadhiwa hospitali teule ya Ifisi na majeruhi walikuwa hawajatambuliwa majina na askari wa jeshi la polisi walikuwa wakiendelea kuchukua maelezo hospitalini hapo. PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA MBEYA YETU

No comments:

Post a Comment