UWINDAJI wa panya (Kacheko
kwa lugha ya Kifipa) na wanyama wengine wadogo wadogo kwaajili ya kitoeo
umetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia kuchomwa kwa misitu katika kata
ya Sintali wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Mmmoja wa wakazi
wa kata hiyo Sabasi Severino Mafua ameeleza hayo alipokuwa akichangia mada
kwenye mdahalo wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi uliofanyika katika kata hiyo
jimbo la Nkasi kusini ulioandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali
wilayani hapa (Nkangonet) ukiwa umedhaminiwa na shirika la The Foundation For
Civil Society.
Mafua amesema kwa
sehemu kubwa kuchomwa kwa mapori kunakofanyika kwenye vijiji vya kata hiyo
kunatokana na wakazi kutafuta kitoeo aina ya panya na wanyama wengine wadogo
ambao unapochoma msitu ndipo urahisi wa kuwakamata ama kujua wanakojificha
unakuwepo.
“Wengi wanachoma
ili wapate kitoeo aina ya panya maana ni desturi ya wakazi wa kata hii na
wafipa kwa ujumla kula panya kama kitoeo.Na hata ukienda vilabuni utakuta
wamechomwa na wanauzwa kwa bei tofauti tofauti.Sasa wachimbaji wa panya hao
hulazimika kuchoma mapori ili iwe rahisi kuwakamata.Vivyo hivyo na tuwanyama
twingine tudogo tunatopatikana kwenye mapori na vichaka kama panya” anasema.