Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, October 31, 2017

KWA NINI VIFO VYA WANAUME VINGI KULIKO WANAWAKE?

Na Joachim Nyambo.

“Matokeo ya Utafiti huu yanatuonyesha mahali tulipo na changamoto mbalimbali kuhusiana na ubora,utunzaji na utumiaji wa takwimu za vifo katika hospitali zetu.”

“Vile vile taarifa hii inaanisha vyanzo na sababu mbalimbali za vifo kwa wananchi tunaowahudumia katika Hospitali zetu.Ninaamini kuwa ripoti hii itaibua mjadala chanya na mawazo mapya ili kuboresha takwimu zetu za afya”

Yalikuwa maneno ya utangulizi ya mkuu wa wilaya ya Mbeya,Paul Ntinika alipomwakilisha Mkuu wa mkoa,Amos Makala kwenye ufunguzi waWarsha kuhusu sababu za vifo katika hospitali za Tanzania.Huu ni utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu nchini(NIMR)

Kwa mujibu wa Mtafiti mkuu kiongozi kutoka NIMR,Dk Leonard Moera utafiti huu ulifanyika Julai 2015 hadi Juni 2016.Malengo ya utafiti yalikuwa ni kuainisha matukio ya vifo katika hospitali za Tanzania ili kutambua ongezeko la maradhi yanayoathiri jamii na utafiti pia ulichunguza uwepo,upatikanaji na ubora wa takwimu za vifo hospitalini.

Dk Moera anasema utafiti huu ulihusisha Hospitali 11 ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda,Hospitali maalumu na Hospitali za wilaya ambapo katika ya Hospitali ambazo Takwimu hazikupatikana ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Chunya iliyopo mkoani Mbeya.

Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi,Kifua kikuu na Malaria kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,jinsia,wazee nawatoto ndiyo waliowezesha kufanyika kwa utafiti huu muhimu kwa Mustakabali wa Afya za watanzania.

Mkuu wa wilaya anasema,Kama ilivyoainishwa katika mpango mkakati wa Sekta ya Afya namba IV,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukua hatua Mahususi kuboresha mfumo wa utoaji wa Taarifa za Afya ili kukidhi mahitaji ya ufuatiliaji wa huduma za afya.Dhamira ya Serikali ni kutumia mfumo wa kielektrinoki katika ukusanyaji,uchanganuzi na matumizi ya takwimu

“Kwa utaratibu huu ni matumaini yetu tutaongeza ubora wa takwimu tunazozalisha katika mfumo wetu wa tarifa.Pamoja na hiloSerikali itatilia mkazo mafunzo ya watumishi na kuwakumbusha umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa katika kuainisha vyanzo vya maradhi na vifo.”anasema Ntinika.

Mkuu huyo wa wilaya hakusita kuimwagia sifa Ripoti ya Utafiti wa NIMRI akisema ni ya aina yake nchini kwakuwa inaainisha upatikanaji na viwango au sababu za vifo vilivyotokea katika hospitali za Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa maradhi yanayoongoza katika kusababisha vifo nchini ni Malaria,magonjwa ya mfumo wa kupumua,Ukimwi,upungufu wa damu na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu.”

“Hata hivyo vifo vifo vinavyotokana na Malaria,Ukimwi pamoja na Kifua kikuu vimepungua sana.Kwa mfano vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 47.Vilevile vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kwa asilimia 28 na Kifua kikuu kwa asilimia 26 kutoka mwaka 2006 hadi 2015”alisema Ntinika

Pamoja na kupungua huko,takwimu za utafiti huu zinaonesha kuwa bado Malaria ni ugonjwa unaoongoza kwa vifo vingi nchini huku ugonjwa wa Ukimwi ukishika nafasi ya tatu nyuma ya magonjwa ya mfumo wa kupumua.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka miaka hiyo kumi kati ya vifo 247,976 vilivyotokea Malaria iliongoza kwa asilimia 12.8, magonjwa ya mfumo wa kupumua asilimia 10.1,Ukimwi asiliamia 8.0,upungufu wa damu asilimia 7.8 na magonjwa ya moyo na mfumuko wa damu asilimia 6.3.Pia kumekuwepo na ongezeko kubwa la vifo kwa asilimia 128 vinavyosababishwa na magonjwa yanayoathiri kundi la watoto wachanga hasa wenye umri wa chini ya mwezi mmoja.

Kwa upande mwingine vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza na ajali vimeongezeka.Katika miaka ya hivi karibuni vifo kutokana na ajali vimeongezeka kwa asilimia 16,saratani asilimia 24,kiharusi asilimia,27 na kisukari asilimia 11.Na vifo hivyo vinaendelea kuongezeka.Kuna dalili kuwa magonjwa haya yataendelea kuongezeka katika siku za usoni.

“Hii ni ishara kuwa mafanikio yetu kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yanaadhiriwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza”anasema Ntinika.

“Kupungua kwa vifo kutokana na magonjwa makubwa ni dhahiri kuwa mikakati yetu katika magonjwa haya inafanikiwa.Hapa nawapongeza watumishi wote wa afya katika ngazi mbalimbali kwa mafanikiao haya makubwa”

“Lakini baada ya kupitia na kuichambua ripoti hii nimegundua kuwa watu wetu wanakufa kwa magonjwa yanayozuilika,ikiwa ni kweli kwamba Malaria,Ukimwi,magonjwa ya mfumo wa kupumua,magonjwa yasiyoambukiza na ajali huua maelfu ya watu wetu.Hii inatoa taswira kuwa tunayo kazi kubwa ya kufanya kuzuia vifo hivyo.Mikakati mseto inahitajika kupambana na magonjwa ya makundi yote hayo” anasema Ntinika.

Utafiti unaonesha vifo vingi vimetokea katika hospitali za Dar es salaam,Morogoro na Mwanza ambapo idadi kubwa ya vifo ilikuwa katika kundi la wanaume na mikoa iliyoongoza kwa kuwa na vifo vingi kwenye kundi la wanaume kuliko wanawake ni Mara,Kilimanjaro,Kigoma,Pwani,Ruvuma na Rukwa.

Hapa,Mtafiti mkuu kiongozi kutoka NIMR,Dk Leonard Moera anasema Uzembe wa kutowahi matibabu ni chanzo cha Wanaume nchini kukabiliwa na wimbi la vifo zaidi ya wananwake. Sababu ya vifo vingi vya wanaume ni utayari mdogo wa kundi hilo kwenda kuchunguza afya zao tofauti na ilivyo kwa wanawake.

“Wanaume ni wazito kwenda katika vituo vya tiba.Hata pale mtu anapojisikia tofauti ya mwili yaani maumivu ya kichwa au chochote mara nyingi ni watu wa kuhisi labda ni uchovu,na wakati mwingine utakwenda duka la madawa kutafuta dawa za kutuliza maumivu tu.Hivyo mpaka unakwenda kwenye kituo cha tiba tayari ugonjwa ulikwisha kuwa sugu mwilini hivyo kupona inakuwa vigumu”alisema Dk Moera.

Aliwasihi wanaume kubadili mitazao na kupenda kuchunguza afya zao mara kwa mara hasa kutokana na kuwa mfumo wa maisha yao ni wa kukumbana na misukosuko mingi katika mazingira tofauti yakiwemo yaliyo hatari.

Lakini utafiti pia unasema mikoa ya Mbeya,Iringa na Ruvuma bado inaongoza kwa vifo vitokanavyo na Ukimwi hali inayoonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU) ili kupunguza inadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Mkuu wa wilaya anasema Taarifa ya utafiti huu ni muhimu sana kwaajili ya kufanya maamuzi na kuandaa mipango kwa kutegemea ushahidi wa kitaalamu.Bila takwimu za uhakika si rahisi kujua ukubwa wa matatizo ma changamoto za utoaji huduma za afya.

“Bila Takwimu sahihi,tutajikuta tunashughulika na matatizo yenye umuhimu mdogo na hivyo kutotumia rasilimali zetu ipasavyo.Ni muhimu Timu za menejimenti za mikoa za Afya na Hospitali zote kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti hii ili kuboresha takwimu katika hospitali zetu”alisisitiza Ntinika.

Kaimu Mkurugenzi wa wa NIMR Mbeya, Dk Nyanda Elius na Mganga mkuu Mkoa wa Rukwa,Dk Boniface Kasululu wanasema upo umuhimu mkubwa wa wadau wa afya kutumia Taarifa za utafiti huo katika utekelezaji wao wa kila siku.Ni taarifa zinazotoa Dira ya wapi Huduma za Afya kwa magonjwa mbalimbali nchini zinatokea,zilipo na mwelekeo kwa miaka ijayo.Mikoa na Hospitali zilizotumika kwa utafiti huu zinatoshelea kutoa viashiria vilivyopo kwenye maeneo yote nchini.

Ni wazi kuwa Bila uwepo wa Takwimu hakuna ufumbuzi wa jambo lolote,na ili takwimu zipatikane ni muhimu Utafiti ufanyike ili pia mtokeo yake yalete mapendekezo ya nini kifanyike.Lakini pia utafiti huu unaonesha kuwepo kwa utunzaji usiozingatia umakini katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma kama ilivyobainika kwa Hospitali kama ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Wazee Mbarali na kilio cha Sera ya mwaka 2003

 Wazee wilayani Mbarali wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali katika maandamano katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wazee duniani yaliyofanyika kiwilaya Oktoba 10 mwaka huu mjini Rujewa.
CHINI-Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Kivuma Msangi akizungumza na wawakilishi wa Wazee kutoka kata mbalimbali za wilayani hapo walioshiriki kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wazee duniani yaliyofanyika kiwilaya jana mjini Rujewa.Kulia kwake ni Katibu wa Balaza la wazee wilayani Mbarali,Hezron Kapwele.

Na Joachim Nyambo.

MWAKA 2003 ndipo Sera ya Wazee nchini ilipoundwa.Lengo la Sera hii ilikuwa ni kumjengea mzee mazingira bora katika mfumo wa maisha yake kupitia kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazomkabili.Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali ilitambua umuhimu wa Sera hii na ndipo ikaruhusu kundwa kwake.

Lakini Sera pekee haitoshi,pasipo uwepo wa sheria ni sawa na kuwa na jembe lisilo na mpini.Kamwe hauwezi litumia kulimia shamba.Hali hii ndiyo imekuwa ikiwasukuma wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii kukumbusha mamlaka husika ktunga sheria ya kuiwezesha Sera ya wazee kufanya kazi.Kwa kukosa sheria wazee wanakosa stahiki nyingi kwakuwa hawawezi kuzidai.

Hili ndilo pia lililoyasukuma pia Mabalaza ya wazee katika kata za Chimala na Ubaruku wilayani Mbarali mkoani Mbeya kukutana na kupaza sauti kwa pamoja wakiwawakilisha wazee wenzao nchini walipozungumza na vyombo vya habari siku chache kabla ya Oktoba Mosi mwaka huu.Walipaza sauti kabla ya kuifikia Oktoba Mosi kwakuwa ndiyo siku ya maadhimisho ya siku ya Wazee duniani.
Katika Kongamano la Pamoja lililoyakutanisha mabalaza hayo mawili ya wazee mjini Rujewa,washiriki walisema kutoundiwa Sheria,Sera ya wazee kumesababisha kundi hilo kukosa haki nyingi za msingi.

Miongoni mwa mambo waliyosema wanayakosa kutokana na Sera yao kukosa meno ni pamoja na Penseni kulipwa kwa ubaguzi kwa wastaafu wa Sekta zilizo rasmi huku waliolitumikia taifa kupitia Sekta nyingine wakiachwa.

Miongoni mwa wazee hao,Hezron Pwela na Eliahidi Mchomvu walisema kutokana na mgawanyiko wa majukumu ndani ya taifa wastaafu wote inafaa walipwe pensheni kwakuwa kila mmoja alilitumikia taifa wakati ana nguvu kupitia ajira aliyokuwa nayo.

“Ikumbukwe kuwa wengi wetu hapa ni wale wale ambao tulilipa hata kodi ya kichwa kabla haijaondolewa.Lakini pia tulinunua bidhaa na mpaka sasa tunaendelea kununu na huko tunalipa kodi.Sasa kwa nini pensheni itolewe kwa aliyekuwa Serikalini pekee” alihoji mzee Mchomvu.

“Sote tuliijenga nchi,wengine kupitia kilimo,ufugaji,biashara,ufundi.Sote tulishiriki kulijenga taifa sasa tungependa kujua Rais wetu,wabunge wetu wanatufikiria vipi sisi wazee.Wazee pia tunawajibika kulea wajukuu na hata pale vijana wetu wanaposhindwa maisha huko mijini utasikia narudi kwa wazee wangu,hivyo sisi bado ni tegemeo la jamii” alisema Veronica Mkune.

Kwa upande wake mzee Joseph Meya aliikumbusha Serikali kutambua kuwa iwapo Kilimo kinatajwa kuwa Uti wa mgongo wa Taifa basi haina budi kutambua kuwa ni Sekta iliyo rasmi na yenye mchango mkubwa hivyo wastaafu wa sekta hiyo wanapaswa kuthaminiwa kama ilivyo kwa wale wa sekta za kiserikali.

“Sera tokea mwaka 2013 haijatungiwa sheria?Kama wazee tunapenda kujua Wabunge wetu,rais wetu wanatufikiriaje sisi wazee.Vijana wanafikia hatua ya kutuua kwa kuona tuna macho mekundu kutokana na kupikia kuni au vinyesi vya wanyama,hayo majiko ya gesi hatuyajui sisi” alisema Veronica Mkune.

Kilio hiki cha wazee hakikuishia katika Kongamano hili.Oktoba 10 ndipo kwa wilaya ya Mbarali wazee waliadhimisha siku yao ikiwa ni siku 10 zimepita tangu wenzao waadhimishe kidunia.

Katika maadhimisho haya yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ibara mjini Rujewa wilayani hapo wazee walizidi kupaza sauti zao.Safari hii wakaja na Suala la huduma ya Afya bure kwa wazee.Wanasema pamoja na kuwa hawaipati inavyotakiwa pale inapotolewa lakini bado kunachangamoto kubwa kwakuwa Matibabu bure ni huduma ambayo imebakia katika Zahanati na Vituo vya Afya pekee hatua inayoendelea kuwapa ugumu wa kupata huduma za afya kwa magonjwa sugu yanayowasumbua.

Akisoma Risala ya wazee,Katibu wa Balaza la wazee wilayani Mbarali,Hezron Kapwele alisema magonjwa mengi yanayowakabili wazee yanahitaji matibabu makubwa hivyo kwa huduma ya matibabu bure kuishia Zahanati na vituo vya Afya bado ni shida kwao.

“Magonjwa mengi yanayowasumbua wazee ni yale yanayotolewa huduma kwenye Hospitali kubwa ikiwemo za wilaya na Mikoa.Sasa wazee wanapokwenda kupata matibabu Zahanati au kituo cha afya wanaandikiwa waende kwenye ngazi za juu.Wakifika huko wanatakia walipie”

“Huduma kama za matibabu ya Mapafu,moyo,maini au figo si rahisi kuzipata kwenye zahanati zetu.Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma ili tuweze pia kupata huduma hizi kwenye hospitali za Rufaa”alisema Kapwele.

Kapwele pia aliiomba Serikali kujenga mfumo utakaowezesha watoto yatima wanaoishi na wazee kuangaliwa kwa jicho la huruma hususani katika kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi ikiwemo Elimu.

“Lakini tunaomba mabalaza ya wazee yaundwe maeneo yote nay awe hai.Lakini iwapo kutakuwa na Pensheni jamii itawasaidia wazee hawa walau hata kufikia maeneo ya tiba kwa urahisi.Leo hii hata akipata tiba bure anafikaje kwenye kituo husika”

Mwanaharakati wa huduma za wazee maeneo ya pembezoni,Joseph Kadaga anasema kuna changamoto kubwa kwa familia za wazee walio na ulemavu tofauti huku wakiishi bila wategemezi wa karibu.

“Kuna familia tunazikuta huko vijijini Baba ni mlemavu wa masikio hasikii na mama ana ulemavu wa macho haoni.Watoto waliokuwa wakiwategemea walikwishafariki hivyo familia hii inabakia kuwategemea majirani pekee.Na wakati mwingine unakuta ulemavu umewapata uzeeni.Hapa tunaomba kwakweli mkono wa wadau hasa Serikali”anasema Kadaga mkazi wa kijiji cha Uhanila.

Mwanaharakati,Amina Mwiname anasema iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kutoa Penseni jamii kwa wazee wote hata Serikali ya Tanzania inaweza.Ni vyema ikawatizama wazee wote kwa jicho la huruma na kutambua mchango wao katika ujenzi wa Taifa walipokuwa na nguvu.

“Zanzibar walianza na Penseni jamii ya shilingi elfu ishirini kwa kila mzee na mwaka jana wameongeza na kufikia shilingi elfu hamsini kwa kila mzee.Tunaamini hata bara tunaweza tukiamua”anasema Mwiname.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Kivuma Msangi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Reuben Mfune kwenye maadhimisho hayo aliahidi kuendelea kushirikiana na jamii ya wazee katika masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mabaraza yao katika kila kata.

Msangi anasema kuimarika kwa mabalaza hayo kutawawezesha wazee kuwa na chombo cha kuwakutanisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kisha kuziwasilisha kunakohusika.

Mkurugenzi huyo pia aliahidi kukutana na Taasisi za kifedha na kujadiliana kwa pamoja uwezekano wa taasisi hizo kuanza kutoa mikopo midogo midogo na yenye masharti nafuu kwa wazee ili kuwawezesha kuendesha miradi mbalimbali ya kijasiriamali.


Mkurugenzi huyo anasema Halmashauri ya wilaya hiyo inatambua umuhimu na mchango wa wazee katika jamii yoyote.Ndiyo sababu mara kadhaa imekuwa ikiwashirikisha katika masuala mbalimbali muhimu ikiwemo yanayohitaji ufumbuzi.

Alitolea mfano katika jitihada za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hivi karibuni kwenye maeneo mbalimbali wilayani hapa.Anasema mpaka wanafanikiwa kudhdibiti ni wazee waliochangia kwa kiasi kikubwa hatua hiyo

Anasema kwa takribani miezi mitatu ugonjwa huo uliwasumbua na kuwafanya wataalamu kutolala usiku na mchana wakitumia utaalamu wao lakini hawakuweza kufua dafu.Baada ya kuwashirikisha wazee akiwemo kiongozi wa Kabila la Wasangu Chifu Melele wa sasa,kuna kila dalili za kukomeshwa kwa kipindupindu wilayani hapa.

“Wataalamu tumehangaika wee ,tumetumia utaalamu wetu lakini wapi!Tumewashirikisha hawa wazee hasa Chifu wetu Melele leo ninapozungumza tuna siku mbili hatuna hata mgonjwa mmoja wa kipindupindu wilayani kwetu”

“Tutazidi kuwashirikisha wazee kwakuwa tunatambua umuhimu wao.Wao wanayajua mambo mengi hivyo tukiwatenga tunaweza kuipoteza jamii yetu” alisisitiza Msangi.