Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, October 31, 2017

Wazee Mbarali na kilio cha Sera ya mwaka 2003

 Wazee wilayani Mbarali wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali katika maandamano katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wazee duniani yaliyofanyika kiwilaya Oktoba 10 mwaka huu mjini Rujewa.
CHINI-Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Kivuma Msangi akizungumza na wawakilishi wa Wazee kutoka kata mbalimbali za wilayani hapo walioshiriki kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wazee duniani yaliyofanyika kiwilaya jana mjini Rujewa.Kulia kwake ni Katibu wa Balaza la wazee wilayani Mbarali,Hezron Kapwele.

Na Joachim Nyambo.

MWAKA 2003 ndipo Sera ya Wazee nchini ilipoundwa.Lengo la Sera hii ilikuwa ni kumjengea mzee mazingira bora katika mfumo wa maisha yake kupitia kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazomkabili.Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali ilitambua umuhimu wa Sera hii na ndipo ikaruhusu kundwa kwake.

Lakini Sera pekee haitoshi,pasipo uwepo wa sheria ni sawa na kuwa na jembe lisilo na mpini.Kamwe hauwezi litumia kulimia shamba.Hali hii ndiyo imekuwa ikiwasukuma wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii kukumbusha mamlaka husika ktunga sheria ya kuiwezesha Sera ya wazee kufanya kazi.Kwa kukosa sheria wazee wanakosa stahiki nyingi kwakuwa hawawezi kuzidai.

Hili ndilo pia lililoyasukuma pia Mabalaza ya wazee katika kata za Chimala na Ubaruku wilayani Mbarali mkoani Mbeya kukutana na kupaza sauti kwa pamoja wakiwawakilisha wazee wenzao nchini walipozungumza na vyombo vya habari siku chache kabla ya Oktoba Mosi mwaka huu.Walipaza sauti kabla ya kuifikia Oktoba Mosi kwakuwa ndiyo siku ya maadhimisho ya siku ya Wazee duniani.
Katika Kongamano la Pamoja lililoyakutanisha mabalaza hayo mawili ya wazee mjini Rujewa,washiriki walisema kutoundiwa Sheria,Sera ya wazee kumesababisha kundi hilo kukosa haki nyingi za msingi.

Miongoni mwa mambo waliyosema wanayakosa kutokana na Sera yao kukosa meno ni pamoja na Penseni kulipwa kwa ubaguzi kwa wastaafu wa Sekta zilizo rasmi huku waliolitumikia taifa kupitia Sekta nyingine wakiachwa.

Miongoni mwa wazee hao,Hezron Pwela na Eliahidi Mchomvu walisema kutokana na mgawanyiko wa majukumu ndani ya taifa wastaafu wote inafaa walipwe pensheni kwakuwa kila mmoja alilitumikia taifa wakati ana nguvu kupitia ajira aliyokuwa nayo.

“Ikumbukwe kuwa wengi wetu hapa ni wale wale ambao tulilipa hata kodi ya kichwa kabla haijaondolewa.Lakini pia tulinunua bidhaa na mpaka sasa tunaendelea kununu na huko tunalipa kodi.Sasa kwa nini pensheni itolewe kwa aliyekuwa Serikalini pekee” alihoji mzee Mchomvu.

“Sote tuliijenga nchi,wengine kupitia kilimo,ufugaji,biashara,ufundi.Sote tulishiriki kulijenga taifa sasa tungependa kujua Rais wetu,wabunge wetu wanatufikiria vipi sisi wazee.Wazee pia tunawajibika kulea wajukuu na hata pale vijana wetu wanaposhindwa maisha huko mijini utasikia narudi kwa wazee wangu,hivyo sisi bado ni tegemeo la jamii” alisema Veronica Mkune.

Kwa upande wake mzee Joseph Meya aliikumbusha Serikali kutambua kuwa iwapo Kilimo kinatajwa kuwa Uti wa mgongo wa Taifa basi haina budi kutambua kuwa ni Sekta iliyo rasmi na yenye mchango mkubwa hivyo wastaafu wa sekta hiyo wanapaswa kuthaminiwa kama ilivyo kwa wale wa sekta za kiserikali.

“Sera tokea mwaka 2013 haijatungiwa sheria?Kama wazee tunapenda kujua Wabunge wetu,rais wetu wanatufikiriaje sisi wazee.Vijana wanafikia hatua ya kutuua kwa kuona tuna macho mekundu kutokana na kupikia kuni au vinyesi vya wanyama,hayo majiko ya gesi hatuyajui sisi” alisema Veronica Mkune.

Kilio hiki cha wazee hakikuishia katika Kongamano hili.Oktoba 10 ndipo kwa wilaya ya Mbarali wazee waliadhimisha siku yao ikiwa ni siku 10 zimepita tangu wenzao waadhimishe kidunia.

Katika maadhimisho haya yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ibara mjini Rujewa wilayani hapo wazee walizidi kupaza sauti zao.Safari hii wakaja na Suala la huduma ya Afya bure kwa wazee.Wanasema pamoja na kuwa hawaipati inavyotakiwa pale inapotolewa lakini bado kunachangamoto kubwa kwakuwa Matibabu bure ni huduma ambayo imebakia katika Zahanati na Vituo vya Afya pekee hatua inayoendelea kuwapa ugumu wa kupata huduma za afya kwa magonjwa sugu yanayowasumbua.

Akisoma Risala ya wazee,Katibu wa Balaza la wazee wilayani Mbarali,Hezron Kapwele alisema magonjwa mengi yanayowakabili wazee yanahitaji matibabu makubwa hivyo kwa huduma ya matibabu bure kuishia Zahanati na vituo vya Afya bado ni shida kwao.

“Magonjwa mengi yanayowasumbua wazee ni yale yanayotolewa huduma kwenye Hospitali kubwa ikiwemo za wilaya na Mikoa.Sasa wazee wanapokwenda kupata matibabu Zahanati au kituo cha afya wanaandikiwa waende kwenye ngazi za juu.Wakifika huko wanatakia walipie”

“Huduma kama za matibabu ya Mapafu,moyo,maini au figo si rahisi kuzipata kwenye zahanati zetu.Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma ili tuweze pia kupata huduma hizi kwenye hospitali za Rufaa”alisema Kapwele.

Kapwele pia aliiomba Serikali kujenga mfumo utakaowezesha watoto yatima wanaoishi na wazee kuangaliwa kwa jicho la huruma hususani katika kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi ikiwemo Elimu.

“Lakini tunaomba mabalaza ya wazee yaundwe maeneo yote nay awe hai.Lakini iwapo kutakuwa na Pensheni jamii itawasaidia wazee hawa walau hata kufikia maeneo ya tiba kwa urahisi.Leo hii hata akipata tiba bure anafikaje kwenye kituo husika”

Mwanaharakati wa huduma za wazee maeneo ya pembezoni,Joseph Kadaga anasema kuna changamoto kubwa kwa familia za wazee walio na ulemavu tofauti huku wakiishi bila wategemezi wa karibu.

“Kuna familia tunazikuta huko vijijini Baba ni mlemavu wa masikio hasikii na mama ana ulemavu wa macho haoni.Watoto waliokuwa wakiwategemea walikwishafariki hivyo familia hii inabakia kuwategemea majirani pekee.Na wakati mwingine unakuta ulemavu umewapata uzeeni.Hapa tunaomba kwakweli mkono wa wadau hasa Serikali”anasema Kadaga mkazi wa kijiji cha Uhanila.

Mwanaharakati,Amina Mwiname anasema iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kutoa Penseni jamii kwa wazee wote hata Serikali ya Tanzania inaweza.Ni vyema ikawatizama wazee wote kwa jicho la huruma na kutambua mchango wao katika ujenzi wa Taifa walipokuwa na nguvu.

“Zanzibar walianza na Penseni jamii ya shilingi elfu ishirini kwa kila mzee na mwaka jana wameongeza na kufikia shilingi elfu hamsini kwa kila mzee.Tunaamini hata bara tunaweza tukiamua”anasema Mwiname.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Kivuma Msangi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Reuben Mfune kwenye maadhimisho hayo aliahidi kuendelea kushirikiana na jamii ya wazee katika masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mabaraza yao katika kila kata.

Msangi anasema kuimarika kwa mabalaza hayo kutawawezesha wazee kuwa na chombo cha kuwakutanisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kisha kuziwasilisha kunakohusika.

Mkurugenzi huyo pia aliahidi kukutana na Taasisi za kifedha na kujadiliana kwa pamoja uwezekano wa taasisi hizo kuanza kutoa mikopo midogo midogo na yenye masharti nafuu kwa wazee ili kuwawezesha kuendesha miradi mbalimbali ya kijasiriamali.


Mkurugenzi huyo anasema Halmashauri ya wilaya hiyo inatambua umuhimu na mchango wa wazee katika jamii yoyote.Ndiyo sababu mara kadhaa imekuwa ikiwashirikisha katika masuala mbalimbali muhimu ikiwemo yanayohitaji ufumbuzi.

Alitolea mfano katika jitihada za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hivi karibuni kwenye maeneo mbalimbali wilayani hapa.Anasema mpaka wanafanikiwa kudhdibiti ni wazee waliochangia kwa kiasi kikubwa hatua hiyo

Anasema kwa takribani miezi mitatu ugonjwa huo uliwasumbua na kuwafanya wataalamu kutolala usiku na mchana wakitumia utaalamu wao lakini hawakuweza kufua dafu.Baada ya kuwashirikisha wazee akiwemo kiongozi wa Kabila la Wasangu Chifu Melele wa sasa,kuna kila dalili za kukomeshwa kwa kipindupindu wilayani hapa.

“Wataalamu tumehangaika wee ,tumetumia utaalamu wetu lakini wapi!Tumewashirikisha hawa wazee hasa Chifu wetu Melele leo ninapozungumza tuna siku mbili hatuna hata mgonjwa mmoja wa kipindupindu wilayani kwetu”

“Tutazidi kuwashirikisha wazee kwakuwa tunatambua umuhimu wao.Wao wanayajua mambo mengi hivyo tukiwatenga tunaweza kuipoteza jamii yetu” alisisitiza Msangi.

No comments:

Post a Comment