Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, December 28, 2013

Mbeya jiji yapeta matokea darasa la saba..Ileje yashika mkia kimkoa.

HALMASHAURI ya jiji la Mbeya imeshika nafasi ya kwanza kimkoa kwa shule zake za msingi kufanya vizuri katika matokeo ya wahitimu wa elimu ya msingi mwaka huu huku wilaya ya Ileje ikishika mkia kwa kushika nafasi ya kumi. Hsalmashauri ya jiji imeongoza kimkoa kwa kupata wastani wa asilimia 65.5 ikafuatiwa na Rungwe yenye wastani wa 50.9,Wilaya ya Kyela imeshika nafasi ya tatu kwa wastani wa 46.4 huku wilaya ya Mbarali ikishika nafasi ya nne kwa wastani wa 43.6. Halmashauri ya Mbozi inashika nafasi ya tano ikiwa na wastani wa 42.8,Busokelo ikiwa ni halmashauri mpya inashika nafasi ya sita kwa wastani wa asilimia 42.7,Momba ikiwa ni halmashauri mpya pia ikashika nafasi ya saba kwa wastani wa asilimia 36.3. Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imeshika nafasi ya nane kwa wastani wa 35.6,nafasi ya tisa ikaangukia kwa wilaya yenye eneo kubwa sawa na asilimia 47 ya eneo lote la mkoa wa Mbeya wilaya ya Chunya iliyopata wastani wa asilimia 32.4 na Ileje ikashika mkia kwa kupata asilimia 30.8 ya ufaulu. Akitangaza matokeo kwa ujumla kwenye kikao cha Bodi cha Bodi ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa kuingia kidato cha kwanza,afisa elimu mkoa wa Mbeya Remigius Ntyama alisema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kiwango cha ufaulu kimeshuka ikilinganishwa na malengo ya kitaifa. Ntyama alisema mwaka 2011 kiwango cha ufaulu kimkoa kilikuwa asilimia 55,mwaka 2012 kikawa asilimia 30 na mwaka huu yamepanda kidogo kwa kufikia asilimia 44 japo hayajafikia malengo ya kitaifa ya asilimia 60 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa. Akifafanua zaidi juu ya matokeo ya mwaka huu afisa elimu huyo alisema waliofanya mtihani walikuwa 65,484 kati yao wakiwamo wavulana 30,367 na wasichana 35,117. Alisema waliofaulu kwa wastani wa kati ya alama 100 na 250 ni wahitimu 29,065 sawa na asilimia 44.38 ya waliofanya mtihani wakiwemo wavulana 14,246 na wasichana 14,419. Waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kulingana na vyumba vya madarasa vilivyopo ni 27,581 sawa na asilimia 94.89 kati yao wakiwemo wavulana 13,528 na wasichana 14,053 wakati waliosalia watachaguliwa baada ya mahitaji ya vyumba 59 kukamilishwa ambapo halmashauri ya jiji la Mbeya inaongoza kwa kuwa na uhaba wa vyumba 44 vya madarasa. Akizungumza wakati wa kufungua na pia kufunga kikao hicho,kaimu katibu tawala mkoa wa Mbeya Leonard Magacha aliwasisitiza wajumbe kutambua kuwa kila mmoja anayo nafasi ya kuhakikisha changamoto za elimu zinapatiwa ufumbuzi kwenye eneo lake.

Friday, December 27, 2013

Wanahabari wakiwa katika kubadilishana mawazo ya mwisho wa mwaka walipokutana na mhariri wa Lyamba Lya Mfipa.

Mhariri mkuu wa Lyamba Lya Mfipa Bw.Joachim Nyambo(Wa kwanza kulia) akifurahia jambo na wanahabari Husna Mlanzi wa Star TV na Radio Free Africa(RFA),Brandy Nelson wa Mwananchi,Amina Saidi wa Star TV na Moses Ng'wati wa Jambo Consept. Baada ya kicheko mazungumzo yaliendelea kama hivi

Tuesday, December 24, 2013

MBARALI WANAHITAJI ELIMU YA UFUGAJI BORA WA NGURUWE

Watoto wa Nguruwe wakinyonya huku wao na mama yao wakiishi katika mazingira yanayodhihirisha kuwa aliyewafuga hawajali na ndiyo sababu hakuwajengea banda bora na kuwafanya waishi kwenye tope namna hii. Nguruwe walioachwa wakizurura hovyo katika kijiji cha Simike wilayani Mbarali.Lyamba Lya Mfipa alikutana na hali hii alipotembelea kata hiyo jana.Uchunguzi unaonesha wafugaji wengi wa nguruwe wilayani Mbarali mkoani Mbeya hawana utaalamu wa ufugaji wa kisasa wa Nguruwe na mbuzi.

Saturday, December 21, 2013

MADIWANI WATAKA TAARIFA YA MAUZO YA JEZI ZA MBEYA CITY

MADIWANI wa halmashauri ya jiji la Mbeya wameagiza taarifa za mapato na matumizi ya fedha zitokanazo na mauzo ya jezi za timu ya Mbeya City kuwekwa wazi. Madiwani walitoa agizo hilo jana kwenye kikao cha kawaida cha balaza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri eneo la uhindini. Madiwani hao walisema wamekuwa wakishuhudia jezi za Mbeya City zikiagizwa kutoka nje ya nchi na kuuzwa katika maeneo mbalimbali lakini hawajui fedha zinazopatikana zimekuwa zikitumika namna gani. Mmoja wa madiwani hao Frank Mayemba kutoka kata ya Itezi alisema kwakuwa timu ni mali ya wananchi kupitia Halmashauri yao ni lazima wananchi wapewe taarifa ya mapato ya fedha zitokanazo na mauzo ya jezi. “Jezi zina nembo ya halmashauri hivyo ni sehemu ya vyanzo vya mapato vya halmashauri yetu.Sasa tunapokuwa hatupewe taarifa kuwa halmashauri inmenufaika namna gani kwa kuuza jezi wananchi wanakuwa hawatendewi haki.Lazima tupewe taarifa ya mauzo ya jezi ili tubaini kama kuna ufisadi unaofanyika au la” alisisitiza Mayemba. Alisema balaza kupitia vikao vyake limekuwa likiishia kupewa taarifa za mishahara ya makocha,wachezaji na viongozi wengine wa timu lakini hakuna siku taarifa za mauzo ya jezi zimetolewa. Hata hivyo diwani huyo alisema huenda kasoro ya kutowekwa wazi kwa taarifa za fedha zitokanazo na mauzo ya jezi pamoja na michango ya wadau inatokana na mfumo wa muundo wa uendeshaji wa timu chini ya bodi hali aliyosema mfumo huo unapaswa kutazamwa upya. Kwa upande wake mstahiki Meya wa jiji la Mbeya Athanas Kapunga,aliahidi taarifa za mapato yatokanayo na mauzo ya jezi pamoja na michango kutoka kwa wadau kuletwa katika kikao kijacho cha balaza hilo.

Friday, December 20, 2013

MAUAJI YA KUTISHA YAFANYIKA NYUMBANI KWA DIWANI WA CCM

MAUAJI ya kinyama yamefanyika nyumbani kwa diwani wa kata ya Nkangamo wilayani Momba(CCM) baada ya mwanaye na mfanyakazi wa ndani kuuawa kikatili na watu wasiofahamika. Diwani aliyekumbwa na maswahibu hayo ametajwa kwa jina la Eston Kimwelu(55) mkazi wa mtaa wa Tazara katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba ambapo mauaji hayo yalitokea Desemba 19 mwaka huu saa 8:00 mchana nyumbani kwake. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki amewataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni mtoto wa diwani huyo Kalibu Kimwelu(6) aliyeuawa kwa kuchinjwa shingo kwa kisu wakati mfanyakazi wa ndani Sista Nyilenda(17) aliuawa kwa kunyongwa shingo kwa kutumia waya wa Luninga uliopo katika sebule ya nyumba ya familia hiyo. Masaki amesema wakati mauaji hayo yakitokea diwani Kimwelu alikuwa shambani kwake katika kijiji cha Kipaka huku mkewe Tumaini Yohana(29) katibu muhtasi wa halmashauri ya mji mdogo wa Tunduma wilayani hapa akiwa kazini. Amesema miili ya marehemu wote wawili ilikutwa katika sebule ya nyumba hiyo lakini pia bada ya kuchunguza ikabainika wauaji waliiba mabegi mawili yenye nguo yaliyokuwa katika chumba wanacholala watoto. Kaimu kamanda huyo amesema chanzo cha mauaji hayo bado kinachunguzwa ijapokuwa kinahusisha na mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia baina ya mke mdogo na mkubwa ambapo familia ya mke mkubwa imekuwa ikidai kutelekezwa na mumewe kwa kunyimwa mali yakiwemo mashamba. Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi linawashikilia watu watano wakiwemo watoto watatu wa mke mkubwa aliowataja kwa majina ya Enock(23) ,Gabriel(19) na Alex(16) na marafiki wa familia hiyo Mussa Ngoba(19) na Patrick Msigwa(18).

MADIWANI WA CHADEMA WADAIWA KUTISHIA MAISHA YA MEYA

Baadhi ya madiwani na wafuasi wa Chadema wakijadiliano jambo nje ya jengo la ofisi za halmashauri ya jiji la Mbeya lililopo uhindini baada ya diwani mwenzao wa kata ya Ilomba Dickson Mwakilasa kuamuriwa na meya wa jiji la Mbeya Athanasi Kapunga atoke nje kwa kukiuka kanuni za kikao kubishana na meya huyo ukumbini na ndipo madiwani wenzake na wafuasi wa chama hicho wakaongozana naye kutoka hadi njeMEYA wa jiji la Mbeya Athanas Kapunga ameapa kuwafikisha katika vyombo vya sheria baadhi ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) waliotoa lugha za kutishia uhai wake leo kwa kumwambia wataonana yraiani kwakuwa kwenye kikao anatumia udikteta

Thursday, December 19, 2013

MAAFA YA KIMBUNGA CHA MVUA YENYE UPEPO MKALI YALIVYOITIKISA MBARALI.MKUU WA MKOA WA MBEYA AFANYA ZIARA KUWAFARIJI WAATHIRIKA.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiangalia jengo la kanisa la Tanzania Asemblies of God(TAG) lililopo katika kijiji cha Azimio Mswiswi wilayani Mbarali lililoezuliwa paa na kubomoka kuta kufuatia kimbunga cha mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha na kuleta maafa kijijini hapo desemba 17 majira ya saa 12 jioniMkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimfariji mmoja wa waathirika wa kimbunga mzee Abraham Mwakyusa anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 80 na 85 mkazi wa kijiji cha Azimio mswiswi kata ya Mahongole wilayani Mbarali ambaye alijeruhiwa sehemu ya paji lake la uso wakati paa la nyumba yake lilipoezuliwa na kimbunga kama linavyoonekana katika picha ya chini.Kwa mujibu wa mzee huyu ambaye watoto wake wote walikwisha fariki.Amekuwa akiishi katika nyumba hii tangu enzi ya utawala wa rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayajawahi kutokea maafa ya namna hii katika kijiji chao Mkuu wa mkoa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Azimio mswiswi kabla ya kuelekea katika kata ya Utengule usangu kijiji cha Simike alikozungumza pia na wakazi wa kijiji hicho ambacho pia kilikumbwa na maafa hayo MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Mbarali kupeleta timu ya wataalamu haraka iwezekanavyo katika kata zilizokumbwa na maafa ya kuezuliwa kwa paa za nyumba wilayani hapo. Lengo la kupeleka timu hiyo katika kata hizo na kufanya tathmini ya hasara iliyiopatikana na pia kutoa ushauri wa namna ya kuzisaidia kaya zilizokumbwa na maafa hayo yaliyotokea Desemba 17 mwaka huu majira ya saa 12 za jioni baada ya kunyesha kwa mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali. Akizungumza na wakazi wa kata mbalimbali zilizoathirika na maafa hayo yaliyosababisha pia vifo vya watu wawili waliosombwa na maji wakati wakitokea shambani,Kandoro aliwapongeza wakazi hao kwa kuonesha moyo wa ushirikiano wa kuzipa hifadhi familia zilizokosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa Hata hivyo amezitaka kaya zilizoathiriwa kuendelea na jitihada za kurejesha makazi yao katika hali ya awali kwa kujenga na kuezeka kwa kadiri wanavyoweza badala ya kubaki wakisubiri mpaka wataalamu wapiti na kufanya tatjmini wakilenga kupewa msaada. “Ni vema mkaendelea na ujenzi kwa kila mmoja uwezo wake unapoishia.Kama kuna msaada utakuja ukukute ukiwa unaendelea.Tutambue kuwa majanga haya yanapotokea hakuna anayekuwa na taarifa na lazima tukubaliane na yalitotokea” “Lakini pia niwakumbushe kuwa serikali haiji kujenga nyumba ya mtu hapa.Msaada ambao halmashauri yenu inaweza ikatoa ni kidogo sana kusaidia pale inapoona mmeshindwa kumalizia.Yawezekana ukawa mfuko mmoja wa saruji au hata kilo kadhaa za misumari.” Alisisitiza. Mkuu huyo wa mkoa alisema ujenzi usiozingatia utaalamu pia ni moja kati ya mambo yaliyopelekea upepo kuezua nyumba za wakazi hao kwa urahisi kwakuwa nyingi hazina nyenzo za kuwezesha paa kutoezuliwa. Uwepo wa mchwa katika eneo la bonde la usangu ni sababu nyingine aliyoitaja Kandoro kuwa chanzo cha kuezuliwa kwa mapaa kwani mbao katika nyumba nyingi zinaonekana kulika na si imara tena. Akizungumzia maafa hayo kwenye mkutano uliofanyika katika kata yake,afisa mtendaji wa kata ya Kongolo Twalib Mfumbilwa alisema madhara yaliyotokana na mvua hiyo yalivikumba vijiji vya Azimio Mswiswi na Azimio Mapula. Mfumbilwa alisema katika kijiji cha Azimio Mswiswi nyumba 37 ziliezuliwa paa na hivyo kusababisha hakiba za vyakula iliyokuwa ndani ya nyumba hizo pia kuharibika kwa kulowa na maji ya mvua. Kwa upande wa kijiji cha Azimio Mapula nyumba 46 ziliezuliwa paa na bati kuharibika,mazao yaliyopo mashambani kuharibika na pia mbuzi nane walikufa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba. Naye afisa mtendaji wa kijiji cha Simike kata ya Utengule Usangu alisema nyumba zilizoezuliwa ni 24 za kaya zenye familia za jumla ya watu 121,makanisa mawili,nyumba ya mwalimu wa shule ya msingi moja na ghala moja la masista wa shirika la Bikira Maria Simike ambapo kati ya nyumba hizo zote nane haziwezi kurudishiwa katika hali yake ya kawaida tofauti na kuanza ujenzi upya.

Wednesday, December 18, 2013

MIUNDOMBINU DUNI YA SOKO BADO NI TATIZO KWA MATUNDA YANAYOZALISHWA KATIKA KATA YA KIWIRA WILAYANI RUNGWE

WANAWAKE WAKIWA KATIKA AJIRA YA KUKIMBIZANA NA MAGARI,KUPIGWA NA JUA NA HATA KUNYESHEWA NA MVUA WAKATI WAKITAFUTA SOKO LA MATUNDA KAMA WALIVYOKUTWA NA Lyamba Lya Mfipa LEO HII.Ni kwa muda mrefu wanawake hawa wamekuwa wakihatarisha afya na maisha yao kwa shughuli hii.

MFANYABIASHARA TUNDUMA AJERUHIWA KWA RISASI NA MAPANGA KISHA KUPORWA MAMILIONI

Polisi mkoani Mbeya inawasaka watu wanne wasiofahamika kufuatia watu hao kumvamia mfanya biashara ya kubadilisha fedha na kumjeruhi kwa risasi na mapanga na kisha kumpora fedha. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki alimtaja mfanyabiashara aliyevamiwa kuwa ni Alphonce Mwanjela(36) mkazi wa eneo la Sogea Makambini katika mji mdogo wa Tunduma uliopo wilayani Momba. Masaki alisema tukio hilo limetokea Desemba 16 majira ya saa 1:45 ya usiku katikika eneo la Sogea Makambini umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wa kubadili fedha ambaye hufanya shughuli zake katika mpaka wa kati ya Tanzania na Zambia.. Amesema akiwa anarudi nyumbani kutoka kazini, Mwanjela aliyekuwa amebeba fedha alivamiwa na kundi la watu wanne wasiofahamika na ndipo wakaanza kumjeruhi kwa kumkata mapanga kichwani na pia kumjeruhi kwa kumpiga risasi mguu wake wa kulia wakitumia bunduki inayodhaniwa kuwa ya aina ya ni Short Gun. Amesema baada ya kumjeruhi watu wao walimnyang’anya mfanyabiashara huyo fedha taslimu kiasi cha shilingi 5,200,000 fedha za kitanzania,dola 2,300 za kimarekani na Randi 10,000 za Afrika ya kusini. Kwa mujibu wa kaimu kamanda huyo,majeruhi alikimbizwa na wasamaria wema katika kituo cha afya cha Tunduma alikolazimika kulazwa na afya yake imetajwa kuendelea vizuri. Kufuatia tukio hilo,Masaki amesema msako mkali unaendeshwa na jeshi la polisi ili kuwabaini watu waliohusika na kutoa wito kwa watu au mtu yeyote aliye na taarifa juu ya mahali waliko kutoa taarifa katika mamlaka yoyote iliyopo jirani ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Amewataka pia wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara ya kubadili fedha katika mpaka wa Tunduma kuungana pamoja na kufungua duka la kubadili fedha litakalosajiriwa na kuweza kupewa ulinzi mzuri badala ya kuendelea kufanya shughuli hiyo kiholela na kuhatarisha maisha yao. Amewataka pia watu wanaotaka kubadili fedha zao kwenda katika tasisi zilizo rasmi akisema pia si rahisi kuweza kutapeliwa kama inavyofanyika kwa wale wanaokwenda kubadili kwa wafanyabiashara wasio rasmi wanaowakuta barabarani.

MWANAFUNZI WA DARASA LA PILI AFA MAJI AKIOGELEA MTO CHUNYA

MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani hapa zimeendelea kuleta maafa kwa kuwezesha mito kujaa maji na kusababisha vifo vya watoto wanaoogelea. Ikiwa ni siku chache tu zimepita tangu mtoto mmoja aripotiwe kufa maji huko wilayani Mbarali alipokuwa akiogelea mtoni na wenzake,jeshi la polisi mkoani hapa limesema mtoto mwingine amekufa maji wilayani Chunya. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki amesema leo kuwa aliyekufa maji ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Chokaa wilayani Chunya aliyemtaja kwa jina la Ezekia Azigeti(10). Kamanda Masaki amesema mwanafunzi huyo alipoteza maisha Desemba 16 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni baada ya kuzidiwa na maji alipokuwa akiogelea katika mto Chunya. Aidha kaimu kamanda huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto mkoani Mbeya kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwa kuwakanya kwenda kuoga katika mito,mabawa au madimbwi ya maji. Amewataka pia wakazi kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa kufukia au kufunika na kuziba mashimo na visima vilivyo wazi ili kuepusha vifo vya watoto vitokanavyo na maji.

Sunday, December 15, 2013

WADAU WAJITOKEZA KUSHIRIKI KAMPENI YA SHARING IS MORE THAN GIVING

Mhariri mkuu wa Lyamba Lya Mfipa Bwana Joachim Nyambo(wa tatu kulia)akiwa na wanakikundi wa PMM GROUP alipotembelea kwenye viwanja vya Youth Centre linakofanyika zoezi la kupokea michango mbalimbali kupitia kampeni ya Sharing is more than Giving itakayopelekwa katika vituo vya watoto yatima na pia magerezani kwaajili ya wafungwa. Baadhi ya vitu vilivyokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali walioguswa na kampeni hii WAKAZI jijini Mbeya wamezidi kujitokeza katika viwanja vya ukumbi wa Youth Centre jijini hapa kushiriki katika kampeni ya Sharing is more than Giving kwa kupeleka vitu mbalimbali ikiwemo nguo na vyakula. Muungano wa PMM unaojumuisha Taasisi ya kuelimisha umma dhidi ya kupinga ugaidi na Maendeleo(PTA & HW trust Fund),Miss Mbeya 2013 Jacklin Luvanda na Maisha Group ndio ulioandaa kampeni hiyo ukilenga kukusanya na kisha kupeleza zawadi hizo kwa makundi yenye mahitaji ikiwemo watoto yatima na wafungwa magerezani. Baadhi ya vitu ambavyo vimewawasilishwa kwa waratibu wanaoendelea kupokea katika viwanja hivyo ni pamoja na sukari,nguo mbalimbali kwaajili ya mavazi na malazi,sabuni na fedha taslimu. Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kampeni hiyo na pia katibu wa PTA Arthur Kasiba amesema walifikia uamuzi huo baada ya kutembelea baadhi ya vituo vya kulelea watoto yatima na pia magerezani na kukuta jamii iliyopo huko inahitaji msaada wa hali na mali. Amewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuchangia kwa kadiri wanavyoweza na kutoa mwito kwa wengine kuzidi kuichangia jamii iliyo na mahitaji kutokana na kuwa katika mazingira mahumu. Jumapili hii jioni ndipo idadi ya vitu vilivyokusanywa itatangazwa katika hafla fupi itakayofanyika GR Hotel na pia vituo ambavyo misaada hiyo itapelekwa.Ikumbukwe kuwa mdau unaweza kuchangia hata nguo unayoona hauwezi kuivaa pengine kwakuwa inakubana au una nyingine na hivyo hauana haja ya kuilundika ndani.Tuungani kusaidia jamii zenye uhitaji