Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, December 18, 2013

MFANYABIASHARA TUNDUMA AJERUHIWA KWA RISASI NA MAPANGA KISHA KUPORWA MAMILIONI

Polisi mkoani Mbeya inawasaka watu wanne wasiofahamika kufuatia watu hao kumvamia mfanya biashara ya kubadilisha fedha na kumjeruhi kwa risasi na mapanga na kisha kumpora fedha. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki alimtaja mfanyabiashara aliyevamiwa kuwa ni Alphonce Mwanjela(36) mkazi wa eneo la Sogea Makambini katika mji mdogo wa Tunduma uliopo wilayani Momba. Masaki alisema tukio hilo limetokea Desemba 16 majira ya saa 1:45 ya usiku katikika eneo la Sogea Makambini umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wa kubadili fedha ambaye hufanya shughuli zake katika mpaka wa kati ya Tanzania na Zambia.. Amesema akiwa anarudi nyumbani kutoka kazini, Mwanjela aliyekuwa amebeba fedha alivamiwa na kundi la watu wanne wasiofahamika na ndipo wakaanza kumjeruhi kwa kumkata mapanga kichwani na pia kumjeruhi kwa kumpiga risasi mguu wake wa kulia wakitumia bunduki inayodhaniwa kuwa ya aina ya ni Short Gun. Amesema baada ya kumjeruhi watu wao walimnyang’anya mfanyabiashara huyo fedha taslimu kiasi cha shilingi 5,200,000 fedha za kitanzania,dola 2,300 za kimarekani na Randi 10,000 za Afrika ya kusini. Kwa mujibu wa kaimu kamanda huyo,majeruhi alikimbizwa na wasamaria wema katika kituo cha afya cha Tunduma alikolazimika kulazwa na afya yake imetajwa kuendelea vizuri. Kufuatia tukio hilo,Masaki amesema msako mkali unaendeshwa na jeshi la polisi ili kuwabaini watu waliohusika na kutoa wito kwa watu au mtu yeyote aliye na taarifa juu ya mahali waliko kutoa taarifa katika mamlaka yoyote iliyopo jirani ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Amewataka pia wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara ya kubadili fedha katika mpaka wa Tunduma kuungana pamoja na kufungua duka la kubadili fedha litakalosajiriwa na kuweza kupewa ulinzi mzuri badala ya kuendelea kufanya shughuli hiyo kiholela na kuhatarisha maisha yao. Amewataka pia watu wanaotaka kubadili fedha zao kwenda katika tasisi zilizo rasmi akisema pia si rahisi kuweza kutapeliwa kama inavyofanyika kwa wale wanaokwenda kubadili kwa wafanyabiashara wasio rasmi wanaowakuta barabarani.

No comments:

Post a Comment