Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, December 28, 2013

Mbeya jiji yapeta matokea darasa la saba..Ileje yashika mkia kimkoa.

HALMASHAURI ya jiji la Mbeya imeshika nafasi ya kwanza kimkoa kwa shule zake za msingi kufanya vizuri katika matokeo ya wahitimu wa elimu ya msingi mwaka huu huku wilaya ya Ileje ikishika mkia kwa kushika nafasi ya kumi. Hsalmashauri ya jiji imeongoza kimkoa kwa kupata wastani wa asilimia 65.5 ikafuatiwa na Rungwe yenye wastani wa 50.9,Wilaya ya Kyela imeshika nafasi ya tatu kwa wastani wa 46.4 huku wilaya ya Mbarali ikishika nafasi ya nne kwa wastani wa 43.6. Halmashauri ya Mbozi inashika nafasi ya tano ikiwa na wastani wa 42.8,Busokelo ikiwa ni halmashauri mpya inashika nafasi ya sita kwa wastani wa asilimia 42.7,Momba ikiwa ni halmashauri mpya pia ikashika nafasi ya saba kwa wastani wa asilimia 36.3. Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imeshika nafasi ya nane kwa wastani wa 35.6,nafasi ya tisa ikaangukia kwa wilaya yenye eneo kubwa sawa na asilimia 47 ya eneo lote la mkoa wa Mbeya wilaya ya Chunya iliyopata wastani wa asilimia 32.4 na Ileje ikashika mkia kwa kupata asilimia 30.8 ya ufaulu. Akitangaza matokeo kwa ujumla kwenye kikao cha Bodi cha Bodi ya Uchaguzi wa Wanafunzi wa kuingia kidato cha kwanza,afisa elimu mkoa wa Mbeya Remigius Ntyama alisema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kiwango cha ufaulu kimeshuka ikilinganishwa na malengo ya kitaifa. Ntyama alisema mwaka 2011 kiwango cha ufaulu kimkoa kilikuwa asilimia 55,mwaka 2012 kikawa asilimia 30 na mwaka huu yamepanda kidogo kwa kufikia asilimia 44 japo hayajafikia malengo ya kitaifa ya asilimia 60 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa. Akifafanua zaidi juu ya matokeo ya mwaka huu afisa elimu huyo alisema waliofanya mtihani walikuwa 65,484 kati yao wakiwamo wavulana 30,367 na wasichana 35,117. Alisema waliofaulu kwa wastani wa kati ya alama 100 na 250 ni wahitimu 29,065 sawa na asilimia 44.38 ya waliofanya mtihani wakiwemo wavulana 14,246 na wasichana 14,419. Waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kulingana na vyumba vya madarasa vilivyopo ni 27,581 sawa na asilimia 94.89 kati yao wakiwemo wavulana 13,528 na wasichana 14,053 wakati waliosalia watachaguliwa baada ya mahitaji ya vyumba 59 kukamilishwa ambapo halmashauri ya jiji la Mbeya inaongoza kwa kuwa na uhaba wa vyumba 44 vya madarasa. Akizungumza wakati wa kufungua na pia kufunga kikao hicho,kaimu katibu tawala mkoa wa Mbeya Leonard Magacha aliwasisitiza wajumbe kutambua kuwa kila mmoja anayo nafasi ya kuhakikisha changamoto za elimu zinapatiwa ufumbuzi kwenye eneo lake.

No comments:

Post a Comment