Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, December 19, 2013

MAAFA YA KIMBUNGA CHA MVUA YENYE UPEPO MKALI YALIVYOITIKISA MBARALI.MKUU WA MKOA WA MBEYA AFANYA ZIARA KUWAFARIJI WAATHIRIKA.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiangalia jengo la kanisa la Tanzania Asemblies of God(TAG) lililopo katika kijiji cha Azimio Mswiswi wilayani Mbarali lililoezuliwa paa na kubomoka kuta kufuatia kimbunga cha mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha na kuleta maafa kijijini hapo desemba 17 majira ya saa 12 jioniMkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimfariji mmoja wa waathirika wa kimbunga mzee Abraham Mwakyusa anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 80 na 85 mkazi wa kijiji cha Azimio mswiswi kata ya Mahongole wilayani Mbarali ambaye alijeruhiwa sehemu ya paji lake la uso wakati paa la nyumba yake lilipoezuliwa na kimbunga kama linavyoonekana katika picha ya chini.Kwa mujibu wa mzee huyu ambaye watoto wake wote walikwisha fariki.Amekuwa akiishi katika nyumba hii tangu enzi ya utawala wa rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayajawahi kutokea maafa ya namna hii katika kijiji chao Mkuu wa mkoa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Azimio mswiswi kabla ya kuelekea katika kata ya Utengule usangu kijiji cha Simike alikozungumza pia na wakazi wa kijiji hicho ambacho pia kilikumbwa na maafa hayo MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Mbarali kupeleta timu ya wataalamu haraka iwezekanavyo katika kata zilizokumbwa na maafa ya kuezuliwa kwa paa za nyumba wilayani hapo. Lengo la kupeleka timu hiyo katika kata hizo na kufanya tathmini ya hasara iliyiopatikana na pia kutoa ushauri wa namna ya kuzisaidia kaya zilizokumbwa na maafa hayo yaliyotokea Desemba 17 mwaka huu majira ya saa 12 za jioni baada ya kunyesha kwa mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali. Akizungumza na wakazi wa kata mbalimbali zilizoathirika na maafa hayo yaliyosababisha pia vifo vya watu wawili waliosombwa na maji wakati wakitokea shambani,Kandoro aliwapongeza wakazi hao kwa kuonesha moyo wa ushirikiano wa kuzipa hifadhi familia zilizokosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa Hata hivyo amezitaka kaya zilizoathiriwa kuendelea na jitihada za kurejesha makazi yao katika hali ya awali kwa kujenga na kuezeka kwa kadiri wanavyoweza badala ya kubaki wakisubiri mpaka wataalamu wapiti na kufanya tatjmini wakilenga kupewa msaada. “Ni vema mkaendelea na ujenzi kwa kila mmoja uwezo wake unapoishia.Kama kuna msaada utakuja ukukute ukiwa unaendelea.Tutambue kuwa majanga haya yanapotokea hakuna anayekuwa na taarifa na lazima tukubaliane na yalitotokea” “Lakini pia niwakumbushe kuwa serikali haiji kujenga nyumba ya mtu hapa.Msaada ambao halmashauri yenu inaweza ikatoa ni kidogo sana kusaidia pale inapoona mmeshindwa kumalizia.Yawezekana ukawa mfuko mmoja wa saruji au hata kilo kadhaa za misumari.” Alisisitiza. Mkuu huyo wa mkoa alisema ujenzi usiozingatia utaalamu pia ni moja kati ya mambo yaliyopelekea upepo kuezua nyumba za wakazi hao kwa urahisi kwakuwa nyingi hazina nyenzo za kuwezesha paa kutoezuliwa. Uwepo wa mchwa katika eneo la bonde la usangu ni sababu nyingine aliyoitaja Kandoro kuwa chanzo cha kuezuliwa kwa mapaa kwani mbao katika nyumba nyingi zinaonekana kulika na si imara tena. Akizungumzia maafa hayo kwenye mkutano uliofanyika katika kata yake,afisa mtendaji wa kata ya Kongolo Twalib Mfumbilwa alisema madhara yaliyotokana na mvua hiyo yalivikumba vijiji vya Azimio Mswiswi na Azimio Mapula. Mfumbilwa alisema katika kijiji cha Azimio Mswiswi nyumba 37 ziliezuliwa paa na hivyo kusababisha hakiba za vyakula iliyokuwa ndani ya nyumba hizo pia kuharibika kwa kulowa na maji ya mvua. Kwa upande wa kijiji cha Azimio Mapula nyumba 46 ziliezuliwa paa na bati kuharibika,mazao yaliyopo mashambani kuharibika na pia mbuzi nane walikufa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba. Naye afisa mtendaji wa kijiji cha Simike kata ya Utengule Usangu alisema nyumba zilizoezuliwa ni 24 za kaya zenye familia za jumla ya watu 121,makanisa mawili,nyumba ya mwalimu wa shule ya msingi moja na ghala moja la masista wa shirika la Bikira Maria Simike ambapo kati ya nyumba hizo zote nane haziwezi kurudishiwa katika hali yake ya kawaida tofauti na kuanza ujenzi upya.

No comments:

Post a Comment