HATIMAYE shughuli ya
kutafuta miili ya wachimbaji wadogo waliofukiwa na kifusi kwenye mgodi wa
dhahabu wa Mnadani kata ya Sangambi wilayani Chunya imemalizika jioni hii baada ya mwili
wa mchimbaji wa pili kupatikana.
Mwili uliokuwa umesalia
kwenye kifusi hicho ni wa mchimbaji Riziki Kalengo mkazi wa wilayani Mbozi
mkoani Mbeya ambapo hadi unaopolewa leo majira ya saa 11 kasoro za
jioni ulikuwa na siku ya nne tangu wachimbaji hao wafukiwe na kifusi Disemba 27
mwaka huu wakiwa wawili.
Akizungumza na Lyamba Lya Mfipa kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio mara baada ya kupatikana kwa mwili
huo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya,Bosco Mwanginde amesema mwili
wa marehemu Riziki umepatikana kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na wadau
mbalimbali wakiwemo wachimbaji na wakazi wa vijiji jirani.
Mwanginde amesema
kutokana na miamba iliyokuwa imefunika shimo la mgodi huo katika kina
kirefu,ilikuwa vigumu shughuli ya ufukuaji kifusi kuendelea kufanywa na mashine
na hapo ndipo ikawalazimu wananchi kutumia zana za kawaida zikiwemo chepe,majembe na sururu.
Amesema tayari miili
yote ya marehemu wawili ukiwemo ule wa Wambura Makulu mkazi wa Musoma Mkoani
Mara ulioopolewa siku ya jumanne imekabidhiwa kwa ndugu na jamaa tayari kwa
kuanza safari ya kuelekea makwao kwaajili ya maziko.
Bwana alitoa na Bwana
ametwaa,jina la Bwana na Libarikiwe!