JAMII nchini imehimizwa
kuongeza ushirikiano dhidi makundi ya watu walio na mahitaji maalumu hususani
walemavu kwakuwa kufanya hivyo kutawezesha uwepo wa jamii iliyo na ustawi na
yenye kujali maslahi ya kila mmoja.
Afisa ustawi wa jamii
mkoa wa Mbeya Bibi Stella Kategile amesisitiza hayo alipomwakilisha mkuu wa
mkoa huo Abbas Kandoro kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya walemavu
duniani,yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya yakiwa yameeandaliwa na Kituo cha Kulelea watoto wenye ulemavu cha Chird
Surport Tanzania(CST).
Katika maadhimisho hayo
yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa mpango wa Peleka rafiki zangu wote shuleni unaoendeshwa na CST,Bi.Kategile amesema
bado jamii ya walemavu imekuwa ikitengwa katika masuala mbalimbali hatua
inayosababisha jamii hiyo kujiona wanyonge na wasio na haki.
Kupitia hadhara hiyo,Bi
Kategile amesema kuna kila sababu ya jamii ya walemavu kushirikiana na makundi
mengine kwakuwa hakuna ajuae ulemavu utamfika lini.
Akizungumzia suala la
elimu kwa walemavu,Bi Kategile amesema kuna kila sababu ya kuendeleza mpango wa
elimu shirikishi kwenye shule zote ili kuwezesha watoto walio na ulemavu
kubadilishana uzoefu wa kivipaji na wenzao kwakuwa kila upande unajambo la kipekee
kwa kundi jingine
Kwa upande wake
mkurugenzi mtendaji wa CST Bibi Noela Shawa amesema Mradi wa Peleka rafiki
zangu wote shuleni hauwalengi watoto walio na ulemavu pekee bali pia wale
waishio katika mazingira magumu ambao wanaikosa haki ya kupata elimu kutokana
na mazingira wanayoishi.
Aidha Bi.Shawa amesema
miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi walio na ulemavu mashuleni,imekuwa
ikisababisha watoto wengi kushindwa kujiunga kwenye shule zilizopo jirani na
familia zao huku shule maalumu kwaajili ya watoto wa jamii hiyo zikionekana
kuwa mbali hivyo kusababisha baadhi ya wazazi kukata tamaa ya kuwapeleka
shuleni.
Desemba 3
ya kila mwaka,dunia huadhimisha siku ya Walemavu,lengo likiwa ni kuongeza
mapambano dhidi ya vizingiti vinavyokwamisha ustawi wa jamii hiyo pasipo kujali
aina ya ulemavu.
No comments:
Post a Comment