Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, December 30, 2015

MWILI WA MCHIMBAJI MWINGINE MGODI WA DHAHABU WAPATIKANA



HATIMAYE shughuli ya kutafuta miili ya wachimbaji wadogo waliofukiwa na kifusi kwenye mgodi wa dhahabu wa Mnadani kata ya Sangambi wilayani Chunya imemalizika jioni hii baada ya mwili wa mchimbaji wa pili kupatikana.

Mwili uliokuwa umesalia kwenye kifusi hicho ni wa mchimbaji Riziki Kalengo mkazi wa wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambapo hadi unaopolewa leo majira ya saa 11 kasoro za jioni ulikuwa na siku ya nne tangu wachimbaji hao wafukiwe na kifusi Disemba 27 mwaka huu wakiwa wawili.

Akizungumza na Lyamba Lya Mfipa kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio mara baada ya kupatikana kwa mwili huo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya,Bosco Mwanginde amesema mwili wa marehemu Riziki umepatikana kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na wadau mbalimbali wakiwemo wachimbaji na wakazi wa vijiji jirani.

Mwanginde amesema kutokana na miamba iliyokuwa imefunika shimo la mgodi huo katika kina kirefu,ilikuwa vigumu shughuli ya ufukuaji kifusi kuendelea kufanywa na mashine na hapo ndipo ikawalazimu wananchi kutumia zana za  kawaida zikiwemo chepe,majembe na sururu.

Amesema tayari miili yote ya marehemu wawili ukiwemo ule wa Wambura Makulu mkazi wa Musoma Mkoani Mara ulioopolewa siku ya jumanne imekabidhiwa kwa ndugu na jamaa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea makwao kwaajili ya maziko.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa,jina la Bwana na Libarikiwe!

No comments:

Post a Comment