RAIA wa Kenya na Mkurugenzi wa mkuu wa Kampuni ya
BAYLEM limited ya nchini Kenya John
Ogumbo amesema wakenya wanaowaonea wivu Watanzania kwa kupata rais mchapa kazi
na mwenye kuonesha uzalendo wa kweli kama ilivyokuwa kwa viongozi waasisi wa
mataifa ya barani Afrika.
Ogumbo aliyasema hayo alipoungana na viongozi wa
kampuni ya Hamiliton Medical kukabidhi msaada wa Mashine ya msaada wa Kupumulia
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 kwa hospitali ya Rufaa kanda ya
Mbeya.
Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa kinachozungumzwa
katika kila kona ya nchi ya Kenya na kwingineko wanakofanya shughuli za
usambazaji wa vifaa kwenye hospitali ni utendaji kazi wa Dk.John Magufuli.
Alisema watu wengi wanauona utendaji kazi wa rais
huyo kama wa mtu ambaye kamwe hakutarajiwa tena kuja kuonekana katika uongozi
wa ulimwengu wa sasa kutokana na viongozi wa mataifa mengi hivi sasa kuwa na
utendaji usioendana na matakwa ya wananchi wao.
“Mmepata kiongozi wa ajabu.Kila mkenya anashangaa,tunatamani
tungempata sisi.Kwakweli sisi wakenya tunawaonea wivu kwa kupata kiongozi huyu”
alisema Ogumbo.
Hata hivyo Ogumbo aliwasihi watanzania kuhakikisha
wanamuombea kwakuwa ni jambo lisilopingika kuwa kwa utendaji kazi wake ni wazi
atajiongezea maadui tena wale walio na uwezo wa kufanya jambo lolote kutokana
na uwezo wao kipesa.
Alisema watanzania pia wanapaswa kumpa ushirikiano
wa kutosha akisema kufanya hivyo kutawezesha taifa lao kupata mabadiliko
makubwa ya kimaendeleo katika kipindi cha miaka mitano tu na kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya kuigwa na kila mtu duniani.
Alisema iwapo watanzania watashindwa kuitumia fursa
ya uwepo wa Dk.Magufuli kwenye utawala watakuja kujijutia na kamwe hawatokuja
tena pata nafasi ya kubadili maisha yao na huenda ukawa mwisho wa kuendesha
mashindano ya kimageuzi ya maisha bora na mataifa mengine.
Akizungumzia msaada wa mashine ya kupumulia,alisema
kambuni hizo mbili ziliguswa baada ya kutembelea hospitali hiyo hususani katika
kitengo cha wazazi Meta na kujionea mashine zinazotumika bado zi za teknolojia
ya zamani.
Alisema mashine waliyokabidhi inao uwezo wa kuokoa
maisha ya mtoto aliyezaliwa kutoka ujauzito wa miezi mitano na inatumika pia
kwa watu wazima walio na uhitaji wa msaada wa upumuaji.
Kwa upande wake Meneja mauzo ukanda wa Afrika wa
kampuni ya Hamiliton Medical Gordon Blair aliahidi kuendelezwa kwa mashirikiano
yaliyopo baina ya taasisi za afya nchini na kampuni hizo lengo likiwa ni
kuwezesha utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa kanda ya
Mbeya Thomas Isdory alisema msaada huo utasaidia kupambana na changamoto ya
vifaa tiba huku akisema mashine za aina hiyo zinahitajika zaidi kutokana na
mwenendo wa utoaji huduma kwenye hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment