DAWATI la jinsia
na watoto la jeshi la polisi wilayani Nkasi mkoani Rukwa linawashikiliwa watu
watatu wakazi wa kijiji cha mkole kwa kosa la kumlazimisha mtoto wao wa kike wa
miaka 18 kuolewa na Mwanaume wa miaka 72 baada ya kutoa mahali ya ng’ombe 8 na
shilingi 100,000.
Akizungumza binti
huyo( Jina linahifadhiwa) mbele ya dawati hilo alisema kuwa wazazi wake
walichukua mali kwa mzee Edward Muscat (72) Ng’ombe 8 Tshs,100,000 bila
kumshirikisha na kuamua kumlazimisha kwenda kuolewa
na mzee huyo ambaye kiuhalisia ni Babu yake.
Alisema kuwa yeye
baada ya kuambiwa na wazazi wake ya kuwa akaolewe na mzee huyo alikataa na
ndipo walipomlazimisha kwenda kwa nguvu kwa mzee huyo ambapo aliishi naye
kindoa kwa muda wa siku Nne na ndipo alipotoroka na kukimbilia polisi.
Alisema yeye kila
akirudi nyumbani wazazi wake hao umfukuza na kumalazimisha mtoto huyo kwenda
kwa mmewe huyo kwa madai kuwa walishapokea mali hivyo ni lazima aolewe na mzee
huyo.
Baba wa mtoto huyo
Mboje Saguda baada ya kumhoji juu ya tukio hilo akiwa mikononi mwa polisi
sambamba na mkewe alikiri kupokea mali hiyo kutoka kwa mzee huyo na kuwa wao
hiyo kwao ni mila wala siyo tatizo.
Na alidai kuwa
mtoto wao huyo licha ya kukataa kuolewa na mwanaume huyo ilikua ni lazima
aolewe ili kukidhi matakwa ya mila yao ya kabila la Wasukuma.
Mwenyekiti wa
dawati la jinsia na watoto wa wilaya Nkasi Anna Kisimba alisema wazee hao
wamekwenda kinyume na haki za binadamu na kuwa hivyo ni vitendo vya kikatili
dhidi ya mtoto wa kike na kuwa hivi sasa wanaandaa mashitaka ya kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa wote watatu ya kumdhalilisha mtoto wa kike.
Alisema wazee hao
mume na mke ikiwa ni pamoja na muoaji wametenda kosa la jinai kumlazimisha
binti mdogo kuolewa na Babu kwa lazima,na kuwa licha ya kwamba binti huyo kwa
umri aliofikia ni halai kuolewa lakini si katika mazingira ya kulazimishwa kwa
tamaa ya mali na kuwa suala la kuoa ama kuolewa ni la hiari hivyo ni lazima
kila mmoja akubali kwa dhati kutoka moyoni mwake.
Mkuu wa polisi (
OCD) wilayani Nkasi Cyprian Mushi alikiri jeshi lake kuwashikilia watu hao kwa
maana wazazi wa binti na muoaji kwa kwenda kinyume na haki za binadamu na kuwa
ni kitu ambacho hakikuballiki kuoana kwa kutofautiana umri kwa mbali kiasi hicho
hata kama wamekubaliana.
Amesema kuwa kosa
kubwa kwa watuhumiwa hao ni kitendo cha kumlazimisha binti ambaye kimsingi ana
maamuzi yake na hilo lote ni shinikizo litokanalo na tamaa ya mali iliyopelekea
kumdhalilisha binti huyo kijinsia,na kuwa upelelezi umekamilika kuanzia sasa
watafikishwa mahakamani kujibu yuhuma hizo.
Na Israel
Mwaisaka,Nkasi
No comments:
Post a Comment