Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, December 28, 2015

WACHIMBAJI WADOGO WAHOFIWA KUFA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI

WACHIMBAJI wadogo wawili ambao majina yao hayajafahamika mara moja wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi kwenye machimbo bubu ya dhahabu yaliyopo eneo la mnadani kata ya Sangambi, wilayani Chunya.

Wakazi wa kata hiyo wanasema wachimbaji hao walifukiwa na fikusi wakiwa kazini Desemba 27, mwaka huu majira ya asubuhi.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya,Bosco Mwanginde alisema wachimbaji hao walikuwa sita na wakati wakiendelea na shughuli ya uchimbaji ndipo kifusi kiliwafukia wawili kati yao.

Mwanginde alisema awali kulikuwa na madai kwamba watu watatu ndio waliofukiwa na kifusi hicho, lakini baadaye ikathibitika kwamba waliofukiwa ni wawili kati ya hao sita.

Alisema mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, alimfikishia taarifa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, ambaye alifika jana(Desemba 8) eneo la tukio na kuongoza kazi ya kuokoa watu hao, akiwa pamoja na Mkuu wa wilaya ya Chunya, Elias Tarimo.

“Nilitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa, na nikaanza kufanya jitihada za kutafuta magari yenye mtambo wa kufukua (Tingatinga ).Ilikuwa vigumu kwakuwa gari za aina hiyo zilikuwa mbali.Nilifanikiwa kupata moja kutoka kwa Mehrab, ambalo ilikuwa mbali hivyo nayo imekuja leo (Jana) saa 12:00 asubuhi kazi ya kufukua kifusi ikaanza” alisema Mwanginde.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri, alisema hadi saa 11:00 jioni ya desemba 28 wakati akizungumza na Lyamba Lya Mfipa kwa njia ya simu,shughuli ya kufukua kifusi ilikuwa ikiendelea.

Hata hivyo Mwanginde aliwataka wachimbaji wilayani humo kuchukua tahadhari, wanapoingia kwenye mashimo ya migodi machimboni hapo hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Sangambi, Junjulu Mhewa, alisema alipata taarifa za vijana hao wawili kufukiwa na kifusi, ambapo alitoa taarifa kwenye uongozi wa wilaya, ambapo walifika eneo la tukio asubuhi lakini jitihada za kuwaokoa zilishindikana.

Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Ahmed Msangi, alisema taarifa za kufukiwa kwa wachimbaji hao, zilifahamika baada ya mmoja wa wachimbaji kuingia mgodini na kusikia sauti za watu wakiomba msaada wa kuokolewa na kubainisha kuwa shughuli ya kufukua kifusi inaendelea.

No comments:

Post a Comment