POLISI
Mkoani Mbeya, inawashikilia watu 13 wakiwemo viongozi wa Chama cha
walimu na walimu wenyewe kwa tuhuma za kuhusika na vurugu
zilizosababisha hasara zaidi ya shilingi milioni 100 wakati wa mgomo wa
walimu ulioanza juzi.
Kitendo
cha walimu hao kugoma kuingia darasani kilisababisha baadhi ya maeneo,
wanafunzi kufanya maandamano ya amani ya kudai haki ya kufundishwa
jambo ambalo linadaiwa kutumiwa vibaya na wahalifu kwani walitumia
nafasi hiyo kufanya uhalifu kwa kuiba mali za watu.
Wahalifu
hao walichoma ofisi za Halmashauri ya Mbozi ndani ya Mji mdogo wa
Tunduma na kuiba mali zilizokuwemo kama kompyuta 5 za ofisi, pikipiki
yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali.
Wahalifu
hao walivunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya
kubebea taka aina FAW SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo na
gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka
hiyo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani , aliwataja
watuhumiwa hao wanaodaiwa kuhusika na uhalifu na kusababisha hasara ya
shilingi milioni 117, 515,000 kuwa ni Mexon Mbilinyi, Akida Kondo,
Chalres Rupia, Athumani Mgala, Stela Garbert, Atiliyo Benard, Nikodemus
Exavely, Mashaka Amoni na James Kabuje.
Diwani,
alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika na uhalibifu
wa ofisi ya halmashauri ya mji mdogo wa tunduma ikiwa na kuiba mali
yenye thamani zaidi ya milioni 100 na kwamba wote kwa pamoja
wamefikishwa mahakamani leo.
Akizungumzia
suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu
alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha
wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Aliwataja
wahusika hao kuwa ni Mwalimu wa Patro Mangula na ni Katibu wa chama cha
walimu wilaya ya Kyela ambapo inadaiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa
akishirikiana na watu wengine kupita mashuleni kuhamasisha walimu
waliokuwa wanaendelea na kazi ya kufundisha wajiunge na mgomo.
Wengine
ni Mwalimu Emanuel Kyejo wa shule ya msingi Mbebe Wilaya ya Ileje na
mjumbe wa chama cha walimu wilaya ya Ileje, Anyakingwe Lwinga na mjumbe
wa chama cha walimu ambapo wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuhamasisha
walimu kugoma.
Aidha,
katika uhalifu wa Tunduma, Kamanada Diwani alisema kuwa polisi Mkoani
Mbeya kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuokoa Mabati 168,
Printa moja na mita mbili za maji, Bendera moja ya Taifa na photocopy
mashine.
Pia,
Kamanda Diwani alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi kwa nini askari
wake walitumia Bomu na risasi katika vurugu hizo ambapo alisema kuwa
Bomu hilo lilitumiwa kulitawanyisha kundi kubwa la watu lililokuwa
linazidi kuelekea kwenye ofisi za serikali pamoja na Taasisi za kibenki
na kwamba hakuna madhara yaliyojitokeza.
“Baadhi
ya watu wamekuwa wakiipotosha jamii kuwa askari walitumia bomu
kuwatawanya wanafunzi na ndio sababu za wananchi kuanzisha vurugu jambo
hilo si kweli kwani bomu lilitumiwa baada ya kundi la wahuni lililokuwa
likivamia ofisi na kuiba mali zilizomo ndani,”alisema.
Alisema,
wakati kundi hilo linafanya vurugu tayari wanafunzi walikuwa wamerejea
kwenye makao yao lakini kundi hilo la wahuni ndio lilikuwa likizidi
kujikusanya na kuendelea kufanya uhalifu huo huku baadhi wakiwa
wanaelekea kwenye eneo la Benki.
“Baada
ya walinzi wa Benki kuona kundi hilo linaikaribia benki askari walipiga
risasi mbili juu ili kuwatawanya na kwamba zoezi hilo lilisaidia
kuwarudisha watu hao waliokuwa na lengo la kufanya uhalifu katika benki
hiyo ,”alisema
Aidha,
Diwani aliitaka jamii kuondoa mawazo potofu kwamba huenda vurugu hizo
zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa jambo ambalo si kweli kwani jeshi
la polisi linaamini kuwa kundi hilo la uhalifu halina itikadi yoyote ya
siasa.
“Polisi
inawashikilia watu hao kwa tuhuma za uhalifu na ninaamini watu hawa ni
wahalifu hivyo watafikishwa mahakani kwa makosa ya uhalifu tu na wala
hakuna siasa,”alisema
Hata
hivyo aliwataka walimu pamoja na viongozi wa chama cha walimu kuacha
kuwahamasisha wezao kufanya mgomo kwani wao tayari walitangaza kugoma
na wamegoma hivyo kupita mashuleni na kuwakuta wezao wanafundisha na
kuwalazimisha kugoma ni uvunjifu wa amani hivyo hatua za kisheria
zitachukuliwa zidi yao.
HABARI NA PICHA KWA HISANI YA MBEYAYETU BLOGU
|