WALEMAVU wa ngozi (Albino) wamesisitizwa kushiriki
zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika agosti 26 mwaka huu na
kudumu kwa muda wa siku saba.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya wakufunzi
watakaokwenda kufundisha makarani wa Sensa katika ngazi za tarafa za wilaya
mkoani Mbeya Mwalimu Sydney Mwamlima ambaye pia ni mlemavu wa ngozi ameyasema
hayo alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mafunzo yao ya
siku 12 kufungwa.
Mwalimu Mwamlima amesema kama ilivyo kwa shughuli
nyingine takwimu zitakazopatikana kupitia sense ya watu na makazi zitasaidia
serikali na wadau wengine katika kupanga mikakati ya kupambana na changamoto
zinazowakabili walemavu hao.
Amesema kumekuwepo na changamoto nyingi
zinazowakabili albino ikiwemo mauaji ya kinyama na kukatwa viungo kunakofanywa
na baadhi ya watu kutokana na imani za kishirikina hivyo jamii hiyo inaishi kwa
hofu kubwa.
Hata hivyo amesema ulinzi kwa jamii hiyo ni mdogo
hali aliyosema huenda pia inasababishwa na kutowepo kwa takwimu zinazoonesha
idadi yao ambazo zingeweza kusaidia katika kuweka mpango madhubuti ya kuwapa
huduma muhimu ikiwemo ulinzi dhidi ya maadui.
Amewataka albino wenzakekutojificha wakati wa kuhesabiwa
badala yake watoe ushirikiano wa kutosha kwa makarani watakaohusika na sense ya
watu na makazi kwenye maeneo wanayoishi.
“Ni vema tukajitokeza kuhesabiwa kwakuwa sisi kama
jamii yenye mahitaji maalumu pia takwimu zetu zinahitajika ili zisaidie wadau
mbalimbali kupanga mikakati itakayosaidia kutatua changamoto
zinazotukabili.Lakini pia sisi hatutengani na jamii nyingine hivyo ni vema
hesabu yetu pia ikaungana na watu wengine ili kuiwezesha serikali kutambua
idadi ya watu iliyo nao.” Alisisitiza mwalimu Mwamlima.
Naye afisa tawala wa wilaya ya Mbarali Moses Mashala
ambaye pia ni muhitimu wa mafunzo hayo amesema hamasa zaidi inahitajika kwa
wananchi hasa maeneo ya pembezoni ili watambue umuhimu wa kuhesabiwa.
Aliitaja wilaya ya Mbarali kuwa miongoni mwa maeneo
yanayohitaji uhamasishaji wa hali ya juu kutokana na jamii inayoishi katika
wilaya hiyo ambao wengi ni wafugaji wa makabila ya wasangu,wamasai na wasukuma
ambao ni mara chache kuhudhuria vikao na mikutano ya kuhamasisha masuala ya
msingi.
Kwa upande wake mshiriki mwingine Mary Swila mkazi
wilayani Momba amependekeza vyombo vya habari kuwezeshwa zaidi ili visaidie
katika kutoa elimu hususani katika maeneo ya pembezoni kama wilayani kwake
ambako watu wengi wanategemea vyombo hivyo.
No comments:
Post a Comment